B. KWENDA KULIPA UMRA WALIYOZUILIWA KUIFANYA NA MAKURESHI
Tumekwisha kuona ya kuwa Mtume (s.a.w.) alizuiliwa na Makureshi asihiji mwaka ule, na akatakiwa ende zake na watu wake na arejee mwaka wa pili. Mtume (s.a.w.) tuliona aliridhia shauri hii. Hata mwaka wa pili ulipotimia, Mtume (s.a.w.) alitoka katika mwezi wa Mfunguo pili mwaka wa 7 A. H. (February 629) na watu 2,000 – wanawake na wanaume na watoto – ili kwenda kulipa Umra. Wakauingia mji wa Makka kwa zile shuruti walizozitaka Makureshi pasina kukhalifu hata moja.
Alipoanza kuikabili Al Kaaba, na akaona Makureshi wamekusanyika chungu penye Al Kaaba, Mtume (s.a.w.) aliogopa sana Makureshi wasije wakafanya khiana, wakawashambulia, nao hawana silaha za kutosha. Pale pale Mtume (s.a.w.) akawafanyia ishara Masahaba zake ya kuwa wakati watakapoizunguka Al Kaaba mara 7 waizunguke kwa mwendo wa mbio na wa nguvu, ili wapate kuwatisha Makureshi, Masahaba wakatii vilivyo amri hii. Maamirijeshi wa Kikureshi, walipowaona Masahaba wanatufu namna hii, walisema: “Loo! Hawa ibada yao inaonyesha nguvu namna hii! Je kupigana kwao kutakuwaje leo? Haya natutawanyike” Mabwana wakubwa wa Kikureshi wakatawanyika wakenda zao, wakauacha mji wa Makka mtupu muda wa siku 3, wasigite wala wasiukanyage muda wote huo, ili wasije wakawaona adui zao. Mtume (s.a.w.) na Masahaba zake wakafanya ibada zao kwa raha na nyoyo kutua. Hata siku yane wakaondoka wakarejea kwao Madina baada yakufanya Umra (Hija ndogo), kwani wakati ulikuwa si wa Hija.
SURA YA KUMI NA MBILI
KUWAPELEKEA BARUA WAFALME WALIOKUWA KARIBU NA BARA ARABU
KUWAPELEKEA BARUA WAFALME WALIOKUWA KARIBU NA BARA ARABU
Alipokwisha kutulia na watu wake wakapumua roho zao kwa ile sulhu ya Hudaybiya iliyoahidi kuzuilia vita kwa miaka 10 – Mtume (s.a.w.) aliona ni shauri nzuri sana kuwaandikia barua Wafalme wa zama hizo na kuwataka kuingia katika dini ya Kiislamu. Kwa hivyo akafua mhuri wake wa kupigia chapa kila barua atakayowapelekea hao na wengine, kwani alipewa habari kuwa Wafalme hawakubali kupokea barua za mtu asiye kuwa na mhuri wake makhsusi. Chapa ya mhuri huo ulikuwa “Muhammad Rasulu Llah.”
Baada ya kutengeza mhuri huo Mtume (s.a.w.) alichagua Masahaba mahodari waliokuwa wakizijua vyema nchi za hao alioazimia kuwapelekea barua. Wafalme wenyewe wanaojulikana kwa hakika kuwa wamepelekewa barua hizo ni kumi:
1. HIRAK (HERACLIUS) MFALME WA DOLA YA KIRUMI
Alipelekewa barua hii wakati alipokuja Palestine kuzuru mji wa Baitil Maqdis (Jerusalem) kwa ajili ya kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyewapa nguvu wakawashinda Maajemi (Persians), na wakawaondoa katika nchi ya Asia Minor baada ya kuwa hawa Maajemi wamezihozi nchi hizo kwa Warume kwa muda wa miaka 10. Barua hii ilipelekwa katika mwaka 7 A.H. (628) aliyeipeleka ni Bwana Dihya bin Khalifa. Mfalme huyu aliipokea barua hii kwa uzuri, akaisomesha na akaifahamu madhumuni yake, lakini hakusilimu, bali katika mwaka wa pili 8 A.H. (629) alizatiti jeshi kubwa kuja kuwapiga Waislamu. Jeshi hili lilikutana na Waislamu katika mahali palipokuwa pakiitwa Muuta, na Waislamu wengi walikufa na Majamadari wao 3 aliowachagua Mtume (s.a.w.) waliuawa pia.
Baada ya kuuawa Majamadari hawa, wapiganaji wakamchagua Bwana Khalida bin Al Walid awe Amirijeshi. Bwana huyu alipiganisha kwa uhodari mkubwa hata akajipatia jina hili analotajikana nalo mpaka sasa. Tangu siku hiyo ndipo alipoanza kupewa Ujamadari wa vita na Mtume (s.a.w.) na kupewa jina la “Simba wa Mungu.”
2. KISRA IBARWIZ (CHOSROES EPARWIZ)
Mfalme wa Dola ya Kiajemi siku hizo, alipelekewa barua hii na Bwana Abdalla bin Hudhafa. Kupewa tu barua hii, huyo Kisra aliichana bila ya kuisomesha, na akaamrisha afukuziliwe mbali huyo aliyeileta. Mtume (s.a.w.) kupata habari hii, alikasirika sana akasema: “Na yeye Ufalme wake utachanikachanika kama alivyoichana barua yangu.”
Maneno haya ya Mtume (s.a.w.) hayakuanguka chini, kwani haikupita miaka 3 tangu kufa Mtume (s.a.w.) ila Ufalme wa Kiajemi ulianza kurithiwa na Waislamu, mpaka leo haukurejea tena, ingawa waliweza kuurejesha Ufalme wa nchi yao yote (Persia) tangu muda wa zaidi ya mika 1000 mpaka sasa.
3. NAJASH AS-HAM
Mfalme wa Dola yote ya Kihabushia ya siku hizo ambayo ilikuwa kubwa zaidi kuliko hii ya zama za Haile Selassie huyu, kwani nchi ya Somalia na baadhi ya Nubia zilikuwa ndani ya Dola hiyo. Mfalme huyu ndiye yule yule ambaye Mtume (s.a.w.) alimpelekea baadhi ya Masahaba zake wakakae katika nchi yake wakati Mtume (s.a.w.) alipokuwako Makka bado. Mpaka wakati huu wa kupelekwa barua hii wengi katika Masahaba hao walikuwa bado wapo kuko huko Uhabushia. Barua hii ilifikishwa kwenye mji wa Aksum, ambao ndiyo uliokuwa mji mkubwa wa Dola ya Kihabushia siku hizo. Aliyepewa kuifikisha barua hii ni Sahaba mmoja aliyekuwa akiitwa Bwana Amr bin Umayya. Mfalme huyu kuipata barua hii aliifanyia hishma kubwa, na akafurahi nayo sana, akaitafutia mahali pazuri kabisa akaitia. Baadaye akamwandikia barua Mtume (s.a.w.) ya kumjibu, alimjibisha akamwambia: “Mimi na mwanangu na baadhi ya watu wa nyumbani kwangu tumekubali kuifuata dini hiyo, lakini siwezi kuwalazimisha raia zangu walio makasisi wa dini yangu ya zamani. Siku watakapoitakidi ukweli wa dini hii – kama tulivyoitakidi – wataifuata mara moja.” Baada ya kwisha kuandika alimpa yule mjumbe aipeleke, na akampa mjumbe huyu zawadi nzuri – zake yeye na za kumpelekea Mtume (s.a.w.) – .
Baadhi ya Mashaba waliokuweko huko walimfuata bwana huyu aliyeleta barua wakarejea Madina. Miongoni mwa waliomfuata siku hiyo ni Bibi Ramla bint Abi Sufyan – ndugu yake Bwana Muawiya bin Abi Sufyan – Bibi huyu aliposwa na Mtume (s.a.w.) na yeye yupo katika nchi ya Uhabushia kwa kufuatana na mumewe – Ubeydila bin Jahsh – kwa ajili ya kukimbia mateso ya Makureshi. Baada ya kukaa siku nyingi huko na kuingiana na makasisi wa Kimasihi bwana huyo alipenda kuacha dini hii ya Kiislamu na kuifuata hiyo dini ya Kimasihi. Basi akafanya alivyopenda bila ya kupingwa na yoyote katika jamaa zake, ama yule mkewe alikataa katakata kutoka katika dini yake ya Kiislamu bali alingangania kutukutu, ingawa mumewe alijitahidi kumchochea ili aiache hiyo dini ya Kiislamu. Mtume (s.a.w.) alipopata habari hii alifurahikiwa mno na bibi huyu ambae jamaa zake wote walikuwa katika dini ya Kikureshi ila yeye na mumewe, na sasa ijapokuwa mumewe amekwisha mwacha mkono katika dini hii – yeye ameikakamia vilivyo – Kwa ajili ya kumlipa kitendo chake hiki kizuri na kumwondoshea majonzi na upweke Mtume (s.a.w.) alimposa akamwoa, na hali ya kuwa yeye yupo katika nchi ya Mahabushia na Mtume (s.a.w.) yupo Madina. Bibi huyu hakupata wasaa kuja Madina ila alipokuja Bwana huyu na barua ya Mtume (s.a.w.).
Mtume (s.a.w.) alikuwa na furaha tatu siku aliporejea Bwana Amr bin Umayya. Alikuwa na furaha yake ya kuwashinda Mayahudi katika vita vya Khaybar; akapata furaha ya pili kwa kufikiwa na Masahaba zake waliokuwa Uhabushia, na akapata furaha ya tatu kwa kuwa Mfalme wa nchi hiyo amekubali kufuata dini ya Kiislam na kuacha dini yake ya asili.
Ulipatikana urafiki mkubwa baina ya Mtume (s.a.w.) na Mfalme huyu. Hata siku moja katika mwaka 9 A. H. (630) Mtume (s.a.w.) aliletewa habari na Jibril ya kuwa mchana huo Najash As-ham amekufa. Mtume (s.a.w.) alihuzunika sana, na akawaita watu wake waje msikitini wamsalie rafiki yao mkubwa tangu zamani - wamsalie Salatul Maytil Ghaib.
4. MAKAUKIS (PKAUCHIOS)
Liwali aliyewekwa na Warumi kuitawala nchi yote ya Misr. Lakini yeye mwenyewe hakuwa Mrumi, bali alikuwa mzalendo anayetokana na Maqipti – wakazi wa asili wa Misr –. Alikuwa mtu mkubwa sana na mwerevu kabisa ndipo akapata cheo hiki kikubwa mno. Hawa Maliwali wa kiwanamji walikuwa wakikaa karibu na mahali ambapo umejengwa huu mji wa Cairo baadae. Ama bwana mkubwa kabisa wa Kirumi yeye alikuwa akikaa katika mji wa Alexandria, na amri zilizokhusu uaskari zilikuwa chini ya mkono wake.
Aliyepewa utumwa wa kumpelekea barua hii ni Bwana Hatib bin Abi Baltaa. Baada ya kwisha kuisomesha barua hii na kuifahamu madhumuni yake Liwali huyu alimdadisi barabara huyu Bwana Hatib kwa kila habari za Mtume (s.a.w.). Miongoni mwa maneno aliyomwambia ni haya : “Ee Hatib! Kitu gani kilichomzuilia Mtume wenu – kama kweli yeye ni Mtume – kumwomba Mungu wake ampe nguvu za kuwashinda watu waliokuwa wakimtaabisha na kumtesa, hata ikampasa kutoka katika nchi ya wazee wake tangu asili yao? Kwa nini asimwombe Mungu wake akawapa maadui hao cha kuwapa? Hii ni alama ya kuwa yeye hana hadhi yoyote kwa Mungu.” Bwana Hatib alimjibu akamwambia: “Ee Bwana Liwali Hukiri kuwa Nabii Isa Mtume wa Mungu? Mbona yeye naye hakutaka kwa Mwenyezi Mungu awashushie balaa pale pale wale waliomhusuru na wakataka kumwua?” Liwali alicheka akasema: “Ahsante bingwa uliyeletwa na bingwa.” Bali alimwita karani na akamwamrisha aiweke ile barua katika mkakasi mzuri wa pembe kama alivyofanya yule Mfalme wa Mahabushia.
Baada ya kwisha kuiweka barua hii, Liwali alimwambia Bwana Hatib: “Mimi siwezi kufuata Mtume huyu, kwani raia zangu hawatakubali kunifuata, na mimi sitaki kukosa ukubwa wangu! Lakini chukua zawadi hizi umpelekee Mtume wenu na mwambie udhuru wangu huu. Nawe fanya upesi wende zako kabla haijatangaa habari yako kwa watu wangu, wasije wakenda kinyume na mimi” Zawadi zenyewe alizompa kumpelekea Mtume (s.a.w.) ni hizi :
-
Baadhi ya vitambaa vya nguo.
-
Nyumbu mkubwa mwenye nguvu.
-
Punda mzuri mweupe sana.
-
Farasi “aliyeitwa akaitika”.
-
Baadhi ya chupa za asali ya mtaa wa Binha, mtaa maarufu mpaka leo kwa asali yake nzuri.
-
Shanuo la kani la kuchania nywele.
-
Kitana kizuri cha kupunia ndevu na kulazia nywele.
-
Mkasi mdogo wa kukatia kucha.
-
Marwedi ndefu ya kupakia wanja machoni.
-
Kioo kidogo cha kujitazamia.
-
-13.Wajakazi 3 ambao 1 akiitwa Maria, 2 akiitwa Sirin na 3 akiitwa Kisar na vinginevyo.
Huyu Maria Mtume (s.a.w.) alimweka usuria. Akamzalia mtoto mwanamume ambaye alimpa jina la Ibrahim. Ama huyu Sirin Mtume (s.a.w.) alimpa Shair wake mkubwa, Bwana Hassan bin Thabit. Mjakazi huyu alimzalia bwana wake mtoto ambaye alikuwa Shair kama baba yake. Yule mjakazi watatu Kisar, Mtume (s.a.w.) alimpelekea Sahaba mmoja aliyekuwa akiitwa Bwana Abu Jahm. Baada ya kumweka usuria naye alimzaa Bwana Zakariyya aliyekuwa Naib wa Liwali wa Misr.
5. HAWDHA BIN ALI AL HANAFY
Mfalme wa nchi ya Najd – nchi iliyoko Mashariki ya Hijaz –. Mfalme huyu alikuwa katika mji wa Al Yamama – mji mkubwa wa nchi ya Najd –. Sahaba aliyepewa barua yake kuipeleka ni Bwana Salit bin Amr. Baada ya kwisha kumpa zawadi kidogo mjumbe huyu, Mfalme huyu aliandika barua akamjibisha Mtume (s.a.w.) ya kuwa yeye hawezi kusilimu mpaka Mtume (s.a.w.) ampe ahadi kwanza ya kuwa atakuwa mshirika wake katika Ufalme atakao upata. Mtume (s.a.w.) asimjibishe lolote kwani Mtume (s.a.w.) alikuja kutangaza dini, si kutafuta Ufalme.
6. MUNDHIR BIN SAWA AT TAMIMY
Liwali wa visiwa vya Bahreyn. Aliyepewa kumpelekea barua hiyo ni Bwana Al Alaa bin Al Hadhramy. Liwali huyu alisilimu pale pale, akaacha dini yake ya asili – dini ya Dola ya Kiajemi ya siku hizo – , na yeye alikuwa kama Liwali chini ya utawala wa Dola hiyo. Sehemu kubwa ya watu wake pia walimfuata katika dini hii. Wengine katika hawa walikuwa na dini ya Kiyahudi, wengine walikuwa na dini yao ya Kiarabu ya masanamu.
7. HARITH BIN ABI SHAMI AL GHASSANY
Liwali wa Sham, aliyekuwa chini ya amri ya Kirumi. Aliyepewa barua kumpelekea katika mji wa Damascus ni Bwana Shujaa bin Wahb. Baada ya kuisoma tu aliichana vipande vipande, akavirusha hewani. Kisha akamwambia Bwana Shujaa: “Kamhubiri rafiki yako kwa haya niliyoyafanya, na umwambie akae tayari kungojea jeshi nitakalomletea ambalo hakupata kuona mfano wake. Barua yake na ya yule mfalme wa Warumi zilipelekwa wakati mmoja. Na wakawa shauri moja kumpiga Mtume (s.a.w.).
8. HARITH BIN ABDI KULAL AL HIMYARY
Mfalme wa baadhi ya pande za Yaman, aliyempelekea barua hiyo ni Bwana Muhajir bin Umayya. Mfalme huyu alimjibu vizuri Mtume (s.a.w.), na akambainishia ya kuwa yeye amesilimu na anatumai kuwa wengi katika watu wake watasilimu kwa zama za karibu. Na akawapelekea Wafalme wengine wa Yaman, na wakati huo Hadhramaut ikihisabika ni sehemu ya Yaman.
9 - 10. JAYFAR BIN JULANDA NA ABDI BIN JULANDA AL AZDY
Ndugu wawili Wafalme waliokuwa wakitawala Oman zama za Mtume (s.a.w.). Wafalme hawa walikuwa wa kabila ya Bani Azd. Nchi ya Oman ilivyokuwa ipo mbali na nchi ya Hijaz. Wafalme wake walikawia sana kupelekewa barua hizi za Mtume (s.a.w.), mpaka katika mwisho wa mwaka wa 8 A.H. – 630 – ndipo Mtume (s.a.w.) alipowapelekea Barua katika mkono wa Bwana Amr bin Al As. Bwana huyu alimwendea Bwana Abdi kwanza kwani ndiye aliyekuwa akisifiwa kwa upole na ubaridi. Baada ya kuamini yeye ndipo alipofuatana naye kwenda kwa mkubwa wake Bwana Jayfar. Bwana mkubwa huyu alimdadisi vyema Bwana Amr. Alimuuliza tarehe1 ya Mtume (s.a.w.) tangu kuzaliwa kwake mpaka siku hiyo na watu gani watukufu walioacha dini zao wakafuata dini hiyo mpya. Bwana Amr baada ya kumtajia watukufu hao na baada ya kuyakinisha bwana huyu ukweli wa maneno ya Bwana Amr, alisilimu pale pale na watu wake wote waliokuwa katika mji wa Suhar – mji mkubwa wa nchi ya Oman siku hizo –. Kisha watu wa miji mengine nao wakafuata.
Bwana Amr baada ya haya hakuondoka akaenda zake, bali alikaa kuwafundisha dini na kutazama namna gani mambo yake yalivyopitishwa. Katika muda huu wa kuwapo Bwana Amr huko Oman pamoja na wale Wafalme wawili, yule mkubwa alifanya bidii kubwa kuwataka kila waliokuwa chini ya mamlaka yake wafuate dini hii mpya, aliwapelekea barua za kuwafahamisha Uislamu na kuwataka wasilimu – na wasilimishe kila Maliwali wake waliokuwa katika nchi za kusini – kama nchi za Wamahara na wengineo na waliokuwa kaskazini. Maliwali wote hawa walileta jawabu nzuri za kubainisha kuwa wao wamesilimu na kila aliopo nchi yao kwa kishindo kikubwa1.
Baada ya siku nyingi kidogo kupita Bwana Amr alipata habari ya kuwa Mtume (s.a.w.) amekufa. Akapatwa na majonzi makubwa, hata asiweze tena kukaa Oman, akaazimia kwenda zake Madina. Bwana Abdi – yule Mfalme mdogo – na baadhi ya mabwana wakubwa wa Kioman walifuatana na Bwana huyu mpaka Madina.2 Huko walimkuta Sayyidna Abu Bakr ndiye Khalifa. Khalifa huyu aliwatukuza sana watu wa Oman na akawashukuru mno kwa wema wao waliomfanyia Bwana Amr tangu kufika kwake huko Oman3, mpaka kurejea kwake. Baada ya kukaa huko kidogo na kujuana na mabwana wakubwa wa Kisahaba, mabwana hawa wa Kiomani walirejea kwao nao wamejaa mambo mengi mazuri ya dini ya kawafunza watu wao. Na wajukuu wa Mfalme huyu Bwana Abd – Bwana Suleyman bin Abdallah bin Abd, na ndugu yake , Bwana Saad – wao na wenzao waliokuja pande hizi kiasi cha mwaka 75 A.H (695). Ndiyo waliolimbusha Uislamu huku, hata mwisho ukatapakaa hivi.
SURA YA KUMI NA TATU
KUSILIMU BARA ARABU YOTE
KUSILIMU BARA ARABU YOTE
A. KWENDA KUITEKA MAKKA
Tumekwisha kuona ya kuwa Mtume (s.a.w.) aliandika mkataba na Makureshi wasipigane kwa muda wa miaka 10, na vile vile ya kuwa kila mmoja katika wao wasipigane na muitifaki wa mwenziwe. Bani Khuzaa wakawa waitifaki wa Waislamu, na Bani Bakr wakawa waitifaki wa Makureshi.
Baada ya miaka miwili kutimia vilitokea vita baina ya hawa Bani Khuzaa na Bani Bakr. Sababu yake ni hii:-
Siku moja kijana wa Bani Bakr alikaa mahali na wenziwe, akawa anakwimba nyimbo za kumtukana Mtume (s.a.w.), na wenziwe wa Kibani Bakr wanacheka, pale pale alitokea kijana wa Kibani Khuzaa akawakuta katika kutukana kwao huko. Kijana huyu akamkataza mwimbaji asiendelee na nyimbo zake hizi za ufidhuli, yule mwimbaji asikubali, bali alimtolea utovu wa adabu mkubwa. Kijana huyu wa Kibani Khuzaa akahamaki, akampiga yule mwimbaji kichwani kwa mkia wa ngamia, kichwa kikapasuka akawa anatoka damu.
Pale pale vikaanguka vita baina ya Bani Khuzaa na Bani Bakr. Baada ya kupigana kwa muda mrefu walitokea mabwana wakubwa wakapatanisha na vita vikanyamaza. Lakini wale Bani Bakr walikubali sulhu ile kwa ncha ya ulimi tu, kwani waliondoka wakubwa wao wakaenda kwa mabwana wa Kikureshi wawaazime silaha, na wawape baadhi ya mashujaa wao wachanganyike nao katika kuwashambulia Bani Khuzaa usiku – bila kuwa na mshindo wowote – Makureshi wakawapa silaha na wakawachagulia wakali katika mashujaa wao wakawapa. Miongoni mwa mashujaa hao ni mabwana hawa:-
-
Safwan bin Umayya.
-
Ikrima bin Abu Jahl – mtoto wa Abu Jahl – na
-
Suhayl bin Amr – yule mkubwa wa Makureshi katika kufunga ule mkataba wa Sulhu ya Hudaybiya – .
Mabwana hawa walijificha kwa Bani Bakr, mpaka usiku wakatoka pamoja nao wakawashambulia Bani Khuzaa kwa ghafla wakawaua watu 23, na wakachukua baadhi ya mali. Bani Khuzaa walikwenda mbio na wake zao na watoto wao mpaka kwenye msikiti wa Makka wakajitia, hapo ndipo walipopata salama.
Asubuhi ilipopambazuka tu alitoka Shairi na mkubwa wa Bani Khuzaa – Bwana Amr bin Salim – pamoja na mabwana wengine 40, wa Kikhuzaa mpaka Madina kwa Mtume (s.a.w.). Akaingia msikitini, akamkuta Mtume (s.a.w.) kakaa na Masahaba wake, akatoa salamu, kisha akasimama akamsemesha Mtume (s.a.w.) kwa mashairi haya.
Rabi ninafikilisha ** Kwa Nabii Muhamadi
Kureshi wamepitisha ** Jeuri kubwa ya hadi.
Watu wengi wamefisha ** Na mali wamefisidi.
Basi tunakukumbusha ** Ahadi tulopeana.
Metwingilia ghafula ** Usiku bila habari.
Hawajatupa muhula ** Nasi tukawa tayari.
Tukawa hatuna hila ** Ila tulidahadari.
Basi tunakukumbusha ** Ahadi tulopeana.
.
Bwana habari ni hizi ** Bani Khuzaa twalia.
Twapukutika machozi ** Kwa yaliyo tufikia.
Nawe ndiye mwokozi ** Tumekuja kukwambia.
Basi tunakukumbusha ** Ahadi tulopeana.
Mtume (s.a.w.) akawajibu: “Mtanusuriwa, Amr! Mtanusuriwa, Amr!” Pale pale Mtume (s.a.w.) akaamrisha iandaliwe Jihadi kwenda kupigwa Makureshi waliowaua watu 23 katika waitifaki wa Mtume (s.a.w.). Pale pale akawapelekea wajumbe wakubwa wa kabila nyengine za Kiarabu zilizokuwa zimesilimu, ili na wao walete majeshi yao wachanganyike na Muhajir na Ansar. Haukupita muda mrefu ila majeshi ya kabila hizo yalianza kumiminika Madina. Kabila zenyewe ni hizi:-
1. Bani Aslam 2. Bani Ghifar
3. Bani Muzayna. 4. Bani Juhayna.
5. Bani Asad. 6. Bani Sulaym.
7. Bani Kaab.
Hata asubuhi ya Ijumaa mwezi 10 Ramadhan mwaka 8 A.H (January 630.) Mtume (s.a.w.) alitoka kwenda kuipiga Makka na jeshi la watu 10,000. miongoni mwa hao Muhajir walikua 700 na Ansar 4,000 na 5,300 ni katika hayo majeshi ya kabila za Kiarabu zilizokuja kumsaidia Mtume (s.a.w.).
Mtume (s.a.w.) aliyagawa majeshi haya sehemu 4, na kila sehemu ilikuwa na mkubwa wake. Amir jeshi wa Kiansar alikuwa Bwana Saad bin Ubada. Amir wa Kimuhajir alikuwa Bwana Zubeyr bin Al Awwam. Yale majeshi ya Waislamu wengine yaligawika sehemu mbili – sehemu moja ikawa chini ya Bwana Abu Ubayda, sehemu ya pili chini ya Bwana Khalid bin Al Walid .
Njiani Mtume (s.a.w.) alikutana na baadhi ya Makureshi waliokuwa wanahama Makka wanakuja Madina kusilimu. Miongoni mwa hao ni ndugu yake – Bwana Abu Sufyan bin Harith bin Abdul Muttalib – Bwana huyu alikuwa akimtukana mno Mtume (s.a.w.) na Uislamu kwa mashairi yake ya usafihi, lakini Mtume (s.a.w.) akamsamehe yote aliyoyafanya, kwani Uislamu unafuta kila dhambi zilizotangulia1. Na miongoni mwa aliyokutana nao ni shemeji yake, na mtoto wa shangazi lake – Bwana Abdalla bin Abi Umayya –. Alikuwa ni ndugu wa Bibi Ummu Salama Hind bint Abi Umayya, ambaye alikuwa katika jeshi hili la kwenda kupiga Makka. Bibi huyu alimwombea sana ndugu yake huyu hata Mtume (s.a.w.) akamwelea radhi.
Bwana huyu alikuwa akimuudhi sana Mtume (s.a.w.) kwa kumtaka – kufundisha watu wengine – wamtake namna kwa namna za miujiza. Miongoni mwa mambo aliyowafundisha watu wamtake Mtume (s.a.w.) ni haya yaliyotajwa katika Sura ya Subhana tangu Aya ya 90 mpaka 93:
Walisema hatutakuamini mpaka utuchimbulie katika ardhi (yetu hii) chemchem (yenye maji mengi)
(Aya ya 90).
Au ujipatishie (sasa hivi) bustani ya mitende na mizabibu, uchimbue ndani yake mito kuichimbua 1
(Aya ya 91).
Au utuangushie mbingu – kama ulivyodai –vipande vipande, au umlete Mungu na Malaika makundi kwa makundi
(Aya ya 92).
Au ujipatishie (sasa hivi) nyumba ya dhahabu (tupu) au upande mbinguni, wala hatutasadiki kupanda kwako mpaka utushushie – na huku tunakuona unavyoshuka – daftari (yenye shahada ya Mungu na Malaika wake ya kuwa wewe ni Mtume (s.a.w.) 2
(Aya ya 93).
Mwisho kabisa alikutana na baba yake mdogo, Bwana Abbas bin Adil Muttalib pamoja na watu wa nyumbani kwake wote. Mtume (s.a.w.) akawaamrisha wanawake na watoto wende Madina na akamchukua baba yake mdogo na kila aliyekuwa mtu mzima, akenda nao Makka.
Hata wakati wa Laasiri walipofika mtaa wa Batn Mar. Mtume (s.a.w.) aliwamrisha wajenge mahema mengi wapumzike hapo usiku kucha. Masahaba wakafanya kama walivyoamrishwa na Mtume (s.a.w.). Hata usiku ulipoingia aliwaamrisha wawashe mioto (nyoto) ili kuwaonyesha Makureshi kuwa wao ni wengi. Bwana Abbas alifanya hofu kubwa na huzuni kubwa juu ya Makureshi kwa kuona jeshi kubwa lile limezatiti barabara. Mshipa wa Kikureshi ukampiga. Akamfikiri rafiki yake Ubu Sufyan bin Harb, na mabwana wengine wa Kikureshi. Mara akamwambia Mtume (s.a.w.): “Ya Rasulallah Makureshi jamaa zako. Jeshi hili likiwavamia litawamaliza wote, hawatakuwapo tena Makureshi. Nakuomba unipe ruhusa nende Makka usiku huu huu nikamchukue mkubw wao, Abu Sufyan ili aje afanye sulhu kabla hamjawashambulia kwa jeshi hili” Mtume (s.a.w.) akampa ruhusa na akampa nyumbu wake mwenyewe aliyekuwa kampanda ampande.
Bwana Abbasa hakuwahi kufika Makka mara alikutana na Abu Sufyan na bwana mwengine aliyekuwa akiitwa Bwana Hakim bin Hizam bin Khuwaylid – mtoto wa kaka yake Bibi Khadija – Bwana Abbas aliwaambia kubwa na dogo la jeshi la Mtume (s.a.w.), na wao wakaona shauri nzuri hiyo ya kusilimu kabla ya kupigana. Mabwana hawa wakafuatana na Bwana Abbas mpaka kwa Mtume (s.a.w.). Mtume (s.a.w.) akamwamrisha Bwana Abbas akalale nao mpaka asubuhi. Asubuhi akaja nao mpaka kwa Mtume (s.a.w.). Mtume (s.a.w.) akamwambia Abu Sufyan: “Ee Abu Sufyan! Bado tu hukwisha kutambua ya kuwa miungu yenu si ya haki?” Akajibu: “Nimekwishajua kwani wangekuwa miungu kweli wengetusaidia leo kumshinda Mungu wako wa haki” Akamwambia tena: “Bado huyakinishi ya kuwa mimi ni Mtume?” Akamwambia: “Ama hili nina shaka nalo bado lakini sasa na tuseme habari ya kusalimu amri kwanza” Mtume (s.a.w.) akamwambia: “Nenda Makka ukanadi kwamba wakati litakapoingia jeshi letu kila atakayekuwa nyumbani kwako au nyumbani kwa Hakim bin Hizam kasalimika, na kila atayeingia nyumbani kwake akafunga mlango kasalimika, na kila atakayekwenda kukaa kwenye msikiti mkubwa wa Makka naye kasalimika pia” Abu Sufyan na Hakim wakaondoka na utumwa huu wakenda zao Makka kuwapasha habari watu wao. Watu wa Makka wakadawaa, wasijue la kufanya, kweli imedhihiri uongo umejitenga.
Hata asubuhi ya Jumaatatu mwezi 20 Ramadhan, Mtume (s.a.w.) aliamrisha jeshi lake liondoke liingie mji wa Makka. Lakini aliwafahamisha majamadari wote barabara ya kuwa wasifanye mapigano yoyote bali waingie kwa salama – pasipo kumfinya hata mtu ukucha wala kuchukua chake – Akamwamrisha jamadari Khalid aingie kwa upande wa Kusini kwa njia inayoitwa Kudaa, na jamadari Saad aingie kwa upande wa Magharibi, na jamadari Abu Ubayda aingie kwa upande wa Mashariki, na yeye na Muhajir na jamadari wao Zubeyr wakaingia kwa upande wa Kaskazini kwa njia inayoitwa Kadaa. Majeshi haya yakaingia mpaka kwenye msikiti wa Makka, pasina jambo lolote kutokea. Lakini Bwana Khalid bin Al Walid alikutana na jeshi la vijana wa Kikureshi waliokataa kusalimu amri. Wakalipinga jeshi lake lisiingie. Basi kwa hivyo wakatiana mikononi. Haikupatikana njia ila walipoua Makureshi 23, na waliosalimu amri wakakimbia.
Mtume (s.a.w.) aliingia mji wa Makka naye yupo juu ya ngamia, na nyuma yake kampandisha mtoto wa huru wake – Bwana Osama bin Zayd bin Haritha – akatufu juu ya ngamia wake yule, na watu wanamfuata. Alipokwisha aliingia yeye na watu wake katika kuyavunja masanamu yaliyokuwa juu ya nje ya Al Kaaba.
Baadaye Mtume (s.a.w.) alimtuma Sahaba mmoja aliyekuwa akiitwa Bwana Uthman bin Talha ende kwa mama yake akachukue ufunguo wa Al Kaaba, kwani ufunguo ulikuwa ukishikwa na watu wa ukoo wao – Ukoo wa Bani Abdid Dar – Bwana huyu alimrai mno mama yake hata akakubali kuutoa kwa salama, kwani mzee huyu alikuwa hakusilimu bado. Ulipoletwa ufunguo, Mtume (s.a.w.) alifungua akaingia ndani ya Al Kaaba akasali rakaa mbili halafu akatoka nje, akasimama juu ya kizingiti cha chini cha Al Kaaba, akahutubu kubainisha amri na makatazo ya dini ya Kiislamu. Kisha akasema: “Enyi Makureshi! Mungu amekwisha kukuondosheeni jeuri za kijinga na kujitapa kwa ajili ya nasaba. Watu wote wanatokana na Adam. Na Adam kaumbwa kwa udongo. Hana fadhila Mwarabu juu ya kuwa Mwarabu wala mwekundu juu ya mweusi, wala mweupe juu ya mwekundu” Kisha akasoma Aya hii ya 13 ya Sura ya 49 (Suratul Hujurat).
Enyi watu! Hakika sisi tumekuumbeni (nyote) kwa mwanamke na mwanamume na tumekujaalieni mapote1 (mbali mbali) na kabila (mbali mbali) ili mjuane (tu), (lakini) mtukufu wenu kwa Mungu ni yule anayemcha Mungu zaidi2
(Aya ya 13)
Kisha akasema: “Enyi Makureshi, mnaonaje? Mnadhani nitakufanyeni nini leo” Suhayl akajibi: “Tunasema kheri na tunadhani kheri. Wewe ni ndugu mtukufu na mtoto wa ndugu mtukufu” Mtume (s.a.w.) akasema: “Mimi nasema kama alivyosema ndugu yangu Nabii Yusuf: ‘Hapana kulaumiwa leo. Mungu atakughufirieni3, Inshaallah’ haya nendeni zenu kafanyeni mambo yenu”.
Baada ya kumaliza Mtume (s.a.w.) hutuba yake, Sayyidna Abubakr akenda akamleta baba yake mbele ya Mtume (s.a.w.) ili aje kusilimu naye, Mtume (s.a.w.) akamwambia Sayyidna Abubakr: “Yanini kumtaabisha? Lau ungalinambia kabla ningalikwenda mimi nyumbani kwake” Bwana huyo alikuwa mzee sana wakati huo, kila unywele uliokuwa juu ya mwili wake ulikuwa mweupe. Alipokwisha kusilimu Bwana huyu, Mtume (s.a.w.) alimwita Bwana Uthman bin Abi Talha aliyeleta ufunguo kutoka kwa mama yake. akatwa ule ufunguo wa Al Kaaba akampa akamwambia: “Utwaeni enyi Bani Abdid Dar ufunguo wenu na ukae kwenu, kina Bani Abdid Dar”. Basi mpaka leo hii ufunguo wa Al Kaaba unashikwa na Bani Abdid Dar kama ulivyokuwa kabla ya Uislamu.
Baadaye Mtume (s.a.w.) alikwenda kuwatolea hutba wanawake waliokuwa wamekusanyika mahali pamoja wanamngojea. Mkubwa wa wanawake wote wa Makka wakati huo alikuwa Bibi Hind bint Utba – mke wa bwana mkubwa wa Kikureshi Bwana Abu Sufyan na mama wa Bwana Muawiya bin Abi Sufyan – Bibi huyu alikuwa amejifunika gubi gubi ili asijulikane na Mtume (s.a.w.), kwani alikuwa kafanya mambo mengi mabaya juu ya Waislamu. Moja katika hayo ni kule kumpasua tumbo ami yake – Sayyidna Hamza – na akalitafuna ini lake, kisha akamkata vipande vipande. Mtume (s.a.w.) alianza hutba yake akasema hivi: “Enyi wanawake mliokusanyika hapa. Msiabudu Waungu wengine tena ila Mungu mmoja wa haki” Bibi Hind akajibu: “Hatuna shughuli nao, kwani lau wangekuwa wanafaa kitu wangetufaa leo” Mtume (s.a.w.) akaendelea: “Wala msiibe” Bibi Hind akauliza: “unaonaje? Mwanamke akiwa mumewe bakhili hampi cha kumtosha, ana dhambi akimuibia kidogo? Mtume (s.a.w.) akamjibu la1” Kisha akaendelea: “Wala msizini” Bibi Hind akadakiza akasema: “Tangu lini mwanamke muungwana kuzini? Wewe unatukataza tusiyoyafanya”. Mtume (s.a.w.) akaendelea: “Wala msiue watoto wenu”. Bibi Hind akasema: “Lau tungalikuwa tunawaua ungaliwapata wapi wewe kuwaua katika vita vyetu baina yako na sisi?”2 Mtume (s.a.w.) alipoona mno tena wala hamjui nani alimwambia: “Wewe ni Hind nin?” Bibi Hind akajibu: “Ndiye mimi” Mtume (s.a.w.) akamwambia: “Tumekusamehe yote uliyotufanyia zamani. Yaliyopita yamepita”. Bibi Hind akainuka akasema: “Wallahi! Nimehudhuria hapa, na hapana mtu yoyote ninayemchukia mno ulimwenguni, na ninaye mtakia kila baa imfikie kuliko wewe. Na sasa naondoka hapa, na hapana ninayempenda mno na kumtakia kheri imfike kuliko wewe”.1 Mtume (s.a.w.) akajibu: “Na kila siku yatazidi mapenzi yako kwetu”. Baada ya hutuba yake hii, wanawake walitawanyika wakenda majumbani mwao.
Mtume (s.a.w.) akaamrisha kujengewa hema zake katika mtaa wa Hajun, hema moja ilikuwa ya mkewe. Bibi Hind bint Umayya na nyengine ya mkewe Bibi Maymuna bint Al Harith, akakaa mahali hapo muda wa siku 18. baadae akaondoka yeye na majeshi yake wakenda zao. Kwa muda huu aliokuwako Makka, kila siku alikuwa akitoa vikosi vya watu kwenda miji iliyokuwa karibu na Makka ili kuvunja masanamu yaliyokuwako huko.
Alipoazimia kuondoka alimchagua awe Liwali wa Makka kijana mdogo mzalendo wa Kibani Umayya alikuwa kasilimu siku zile zile na ambaye alikuwa kijana wa miaka 18 tu. Kijana huyu alikuwa akiitwa Bwana Attab bin Asid bin Abil As bin Umayya, mshahara aliyoahidiwa kupewa na Mtume (s.a.w.) ni dirham 354 kila mwaka, yani dirham moja kila siku (takriban senti 60)2. Na akamwacha kijana mmoja wa Kiansar ambaye alikuwa akipata miaka 26 tu ndiye awafundishe dini watu wote waliokuwako Makka. Bwana huyu ingawa alikuwa kijana mdogo, lakini alikuwa hodari mno ajabu, na alikuwa akipendwa sana na Mtume (s.a.w.). Jina lake lilikuwa Bwana Muadh bin Jabal.
Dostları ilə paylaş: |