Maisha ya nabii


C. KUINGIA KATIKA CHAMA CHA KUSAIDIA WANYONGE



Yüklə 0,69 Mb.
səhifə3/15
tarix10.12.2017
ölçüsü0,69 Mb.
#34382
1   2   3   4   5   6   7   8   9   ...   15

C. KUINGIA KATIKA CHAMA CHA KUSAIDIA WANYONGE
Tumekwisha kuona katika sura zilizopita ya kuwa Bwana Abu Talib alishika mahali pa baba yake. Makureshi waliyaridhia haya na akakaa katika ushekhe wake juu ya Makureshi wote. Lakini hakuweza kupata hishima kama ya baba yake, wala hakuweza kuchuma nguvu za kuweza kumfikilishia makamo hayo. Akawa ni mkubwa kwa jina tu ila kwa baadhi ya koo za Kikureshi. Lakini koo zilizokuwa na jeuri na nguvu hakuweza kuzitia katika mikono yake, kama alivyoweza baba yake Bwana Abdul Muttalib. Kwa hivyo zilikuwa zikifanya jeuri kubwa katika mji wa Makka, zilizokuwa jeuri zaidi katika koo hizo ni ukoo wa Bani Umayya na Bani Makhzum. Mwenye chake hakuwa na chake mbele yao, nguvu ndiyo haki, mwenye kujitetea kwa silaha ndiye aliyekuwa akiweza kushusha pumzi kwa raha, ama maneno ya njia hayakusaidia kitu, koo mbili hizi zilikuwa na watu wengi waliokuwa matajiri na mashujaa.
Lakini jeuri yao ilipopindukia mipaka, na watu wakachoshwa na udhalimu wao, mara ulianza mnongono wa kufungua chama kitakachozikusanya baadhi ya koo za Kikureshi zikabiliane na zile koo mbili jeuri na nyenginezo zitakapotaka kufanya jeuri yake. Katika mwaka wa 12 baada ya kufa Bwana Abdul Muttalib – katika mwezi wa mfunguo pili mwaka 590 – Bwana Zubeyr baba yake mdogo Mtume (s.a.w.) aliwaalika wakubwa wa kila kabila la Kikureshi na akawapa shauri la kufungua chama kitakachoweza kuwazuilia madhalimu watakapotaka kudhulumu. Katika koo 12 kubwa za Kikureshi zilizokusanywa siku hiyo hazijakubali shauri hii ila koo 5 tu. Nazo ni:-
1) Bani Hashim. Kabila ya baba yake Mtume (s.a.w.) .

2) Bani Zuhra. Kabila ya mama yake Mtume (s.a.w.) .

3) Bani Taym. Kabila ya Sayyidna Abubakr.

4) Bani Asad. Kabila ya Bibi Khadija, mke wa kwanza wa Mtume (s.a.w.) .

5) Bani Muttalib. Kabila ya Imam Shafi.
Wakaagana wakutane siku nyengine watengeneze makusudio na sharti za chama hicho. Baada ya siku mbili tatu walikutana na wakakubaliana makusudio yao, makusudio yenyewe yalikuwa ni:-
1) Kuwasaidia wasiojiweza wakiwa katika kabila hizi tano au hawamo, Makureshi au si Makureshi.
2) Kumsaidia kila mwenye kudhulumiwa na kufanya kama inavyoyumkinika kurejeshewa haki yake.
Katika mikutano yote hiyo Mtume (s.a.w.) alikuwa akihudhuria na akitoa mashauri yake, lakini alikuwa kijana wa miaka 20 tu, Mtume (s.a.w.) alikuwa akifurahi sana kila anapokumbuka kuwa yeye alikuwa mwanachama katika chama hicho.
Makureshi walikidharau sana chama hicho na wakakidhani kuwa hakitafanya kitu kwa hivyo wakakita chama cha mafidhuli yaani “Wenye kujitia katika mambo yasiyowahusu na wasiyoweza kuyafanya”. Lakini hakijakuwa chama ufidhuli kama walivyokidhani, bali kilikuwa cha vitendo, kikakamilisha kila kilichoazimia kukifanya, ikapatikana salama kidogo katika mji wa Makka, mwenye chake akajijua kama ana chake.


D. WAKE ALIOWAOA
Mtume (s.a.w.) aliporejea katika safari yake ile ya Sham, Bibi Khadija alifurahi sana kwa faida aliyoipata, hakupata kuona faida kubwa kama hiyo tangu alipoanza kupeleka misafara yake Sham, akahakikisha barabara zile sifa alizokuwa akizisikia, akaona kuwa huyo ndiye mtu atakayemfaa katika mambo yake. Vile vile alipata kuhadithiwa zamani na mtoto wa baba yake mdogo ambaye aliyefuata dini ya Kinasara, kuwa imekaribia kuletwa Mtume wa Kiarabu katika mji wa Makka. Na ilivyokuwa hakuna mtu yoyote katika mji wa Makka mwenye sifa nzuri na za ajabu namna zile ila yeye tu, alikata bibi huyu kuwa yeye ndiye atakayekuwa Mtume. Mtumwa wake pia alimsimlia mambo haya ya ajabu aliyoyaona kwa Mtume (s.a.w.) katika safari zao, na yale maneno aliyokuwa akiambiwa na Mapadri wa Sham.
Bibi Khadija aliona kuwa itakuwa bora sana akiweza kuolewa na mume huyu mtukufu. Akachukuwa fedha akampa shoga yake – Bibi Nafisa – ampelekee Mtume (s.a.w.) na amtake aje ampose kwa baba yake kwa mahari hayo. Mtume (s.a.w.) alifurahi sana kwani amekwishatimia miaka 25 na hakuwa na hali ya kuweza kuoa, akenda akawapasha habari baba zake nao pia wakafurahi, wakatoka wote pamoja kwenda kumposea bibi huyu. Bwana Abu Talib ndiye aliyetoa hutuba ya kuposa. Baba yake Bibi Khadija akafurahi sana, na akakubali jambo hilo, baada ya kumshauri mwenyewe Bibi Khadija, Mtume (s.a.w.) alitoa mahari yake Ngamia 40.
Wakati ule Bibi huyu alikuwa keshatimia miaka 40, na Mtume (s.a.w.) alikuwa na umri wa miaka 25 tu , vile vile alikuwa amekwisha olewa na waume wawili na kuzaa nao watoto watano. Ama kwa Mtume (s.a.w.) ilikuwa ndicho chuo chake cha kwanza, wake wote aliowaoa Mtume (s.a.w.) ni 11 lakini waliomkalia eda ni 9 tu, na haya ndiyo majina ya wake wote:-
1. Bibi Khadija bint Khuwaylid: Kureshi katika kabila ya Bani Asad. Yeye ndiye mkewe wa awali, alimuoa katika mwaka 595, na akafa mwezi wa January mwaka 620. Kwa tarehe ya Kiislamu alikuwa amekufa Mfunguo mosi mwaka wa 10 wa kuja Utume. Basi alikuwa ameishi naye kwa muda wa 25, mpaka alipokufa bibi huyu ndipo alipoowa mke mwengine, wakati huo Mtume (s.a.w.) alikuwa ni mwenye umri wa miaka 50. Watoto wote aliozaa Mtume (s.a.w.) walizaliwa na bibi huyu, ila kitinda mimba chake tu1, ndiye aliyezaliwa na mama mwengine. Yeye ndiye Mwislamu wa kwanza baada ya Mtume (s.a.w.), naye ndiye mwanamke wa pili mtukufu katika uma huu wa Nabii Muhammad (s.a.w) Ama mwanamke wa awali aliye mtukufu katika uma huu ni mwanawe – Bibi Fatma – .
2. Bibi Sawda bint Zam’a: Kureshi katika kabila la Bani Amri bin Luay. Baada ya miezi miwili tangu kufa Bibi Khadija Mtume (s.a.w.) alimuoa Bibi huyu katika mwaka wa 10 wa kupewa Utume, Mfunguo tatu. Kwa tarehe ya kizungu ilikuwa Machi 620. Bibi huyu alisilimu zamani pamoja na mumewe, na akenda nchi ya Uhabushia pamoja naye, huko mumewe alikufa, naye akarejea Makka ndipo alipoolewa na Mtume (s.a.w.) ili amtoe ukiwa wa ujane, ingawa Bibi huyu alikuwa mtu mzima. Amekufa Bibi huyu mwaka 54 A. H. – 674. Yeye ni wa tisa katika wenye fatwa nyingi miongoni mwa wake zake Mtume (s.a.w.) .
3. Bibi Aysha bint Abubakr: Kureshi katika kabila ya Bani Taym. Alizaliwa katika mwaka wa 4 wa kuja Utume. Akaolewa na Mtume (s.a.w.) Mfunguo mosi, 2 A. H. – Januari 623. Alikuwa mwanamke mwenye kupenda ilimu sana, kwa hivyo alikuwa akihifadhi maneno mengi ya Mtume (s.a.w.) Hata Mtume (s.a.w.) alisema kuwaambia baadhi ya Masahaba wadogo: “Pokeeni mengi yanayohusu dini yenu kwa hiki kijanakike chekundu”. Alipokufa Mtume (s.a.w.), alikuwa ni mwanamke wa miaka 19, na juu ya hivyo Hadithi zilizopokelewa kwake alizozihifadhi kwa Mtume (s.a.w.) ni 2,220. Naye ndiye wa kwanza mwenye Fat-wa nyingi katika wake zake Mtume (s.a.w.). Na ndiye wa pili katika Masahaba waliopokea Hadithi nyingi kwa Mtume (s.a.w.). Mtume (s.a.w.) hakupata kuoa mwanamke kijana ila huyu, naye ndiye mwanamke wa 3 katika wanawake watukufu wa uma huu. Amekufa Bibi huyu mwaka 57 A.H. – 677.
4. Bibi Hafsa bint Umar bin Al-Khattab: Kureshi katika kabila la Bani Adiy, alikuwa ni mwanamke mkali sana, hata alipokufa mumewe hakupata mume mwingine wa kumuoa ingawa baba yake aliwaomba marafiki zake wote wamwoe, lakini hapana aliyeridhia kwa kuogopa ukali wake, hata alipokuja kumsikia Mtume (s.a.w.) ndipo Mtume (s.a.w.) alimwoa. Alimwoa mwezi wa Shaaban 3 A.H – Nov. 624 A.D. Hadithi zilizopokewa naye ni 60. Huyu ndiye bibi aliyekuwa na msahafu wa asili ambo misahafu yote imenakiliwa katika msahafu huo. Amekufa mwaka 48 A.H – 668. Yeye ndiye wa nne mwenye Fatwa nyingi katika wake zake Mtume (s.a.w.) na alikuwa akijuwa kuandika.
5. Bibi Zaynab bint Khuzayma: Mwarabu katika kabila la Bani Hawazin, kabila ya mama yake Mtume (s.a.w.) wa kunyonyesha, wengi katika kabila hii walikuwa hawakusilimu bado, Mtume (s.a.w.) akaoa huko ili apate kuchanganyika nao. Alimwoa mfunguo mosi 4 A.H – June 625 A.D. Bibi huyu alikaa na Mtume (s.a.w.) muda wa miezi miwili tu kisha akafa.
6. Bibi Hindi bint Abi Umayya: Kureshi katika kabila ya Bani Makhzum. Yeye ni mtoto wa kambo wa shangazi lake Mtume (s.a.w.) hasa, Bibi Atika bint Abdul Muttalib. Alikuwa mtu mzima alipoolewa na Mtume (s.a.w.), mumewe alikufa akamwachia watoto wengi wala hao hawakuwa na jamaa wa Kiislamu, jamaa zao wote walikuwa makafiri bado, Mtume (s.a.w.) alimwoa katika mwezi wa mfunguo Pili 4 A.H – Feb. 626. huyu ndiye mke aliyekuwa akifuatana naye sana vitani. Wanavyuoni wamepokea Hadithi 328 kwake. Amekufa 61 A.H – 681. Yeye ni wa pili mwenye Fatwa nyingi katika wakeze Mtume (s.a.w.) na ndiye wa pili mwenye Hadithi nyingi katika wao.
7. Bibi Zaynab bint Jahsh: Mwarabu katika kabila ya Bani Asad bin Khuzayma lakini mama yake ni shangazi lake Mtume (s.a.w.), aliyekuwa akiitwa Bibi Umayma bint Abdul Muttalib, alimwoa kwa sababu alikuwa ni mwanamke mwenye kuachwa, maana hapo zamani mwanamke aliyeachwa alikuwa akidharauliwa sana, wala hakuwa akipata mtu kumwoa tena, kwa hivyo Mtume (s.a.w.) alimwoa ili kuondosha ada hii mbaya. Alimwoa katika mwezi wa mfunguo tano 5 A.H – Juni 626 A.D. Hadithi zake ni 11 na ni wa 8 katika wenye Fatwa nyingi katika wao. Alikufa 20 A.H – 641. Alikuwa hodari wa kufanya vitu na kutoa sadaka kwa pesa anazopata.
8. Bibi Juwayriya bint Al-Harith: Mwarabu katika kabila ya Bani Mustalik – tumbo katika Khuzaa –. Kabila hii ilipigana na Mtume (s.a.w.) na ikashindwa, watu wengi wakatekwa pamoja na huyu mwanamke ambaye yeye alikuwa ni mtoto wa “Shekhe” wa kabila ile, alikuja baba yake kumkomboa kwa Mtume (s.a.w.) na akapewa bure bila ya kikomboleo chochote. Lakini pale pale Mtume (s.a.w.) akamposa kwa baba yake, na baba yake akafurahi sana, akamwoza kwa mahari ya Dirham 500, na pale pale akasilimu pamoja na jamaa zake wote waliokuwepo pale, mateka wote wakaachiliwa huru na ngawira yote ikarejeshwa, akawa bibi huyu baraka kwa watu wake na kwa Waislamu wote. Alimwoa mwanamke huyu katika mwezi wa Shaaban, 5 A.H.– Decemba 626 A.D. Hadithi zilizopokewa kwake ni 7. Bibi huyu alikufa mwaka 56 A.H – 676. Yeye ni wa sita mwenye Fatwa nyingi katika wakeze Mtume (s.a.w.) .
9. Bibi Ramla bint Abi Sufyan: Kureshi katika kabila la Bani Umayya. Alikuwa mtoto wa Abi Sufyan “Shekhe” wa watu wa Makka wote na adui mkubwa wa Mtume (s.a.w.), lakini bibi huyu alisilimu zamani pamoja na mumewe Ubaydullah bin Jahsh na wakenda wote katika nchi ya Uhabashia, baada ya miaka kupita yule mumewe aliingia katika dini ya Kinasara, lakini yeye alisalia katika dini ya Kiislamu, Mtume (s.a.w.) alipeleka mtu kwenda kumposea na kumleta Madina. Akaja Madina katika mwezi wa Mfunguo nane 7 A.H – Agosti 628 A.D. Baba yake alikuwa hana budi kuja kumtazama alipokuwa akipita Madina katika safari zake, na kila mara mwanamke huyu alijitahidi kumlinganishia baba yake baina ya wema wa Uislamu na ubaya wa ukafiri, hata katika mwaka wa 8 A.H ilipotekwa Makka bwana huyu alisilimu mara moja. Bibi hyu alikufa mwaka 44 A.H. 664 A.D. Wanavyuoni wamepokea Hadithi 65 kwake. Yeye ndiye wa tano mwenye Fatwa nyingi katika wakeze Mtume (s.a.w.) .
10. Bibi Safiyya bint Huyay: Yahudi mtoto wa mfalme wa Bani Nadhir, alitekwa katika vita vya Khaybar, na Mtume (s.a.w.) akamwandikia na akamwoa, ili apate kufungana mkono na Mayahudi, lakini haukuweza kupatikana urafiki wowote kwa watu hao. Alimwoa katika mwezi wa Mfunguo tisa, 7 A.H – Sept. 628. Hadithi 10 zimepokelewa kwake. Alikufa mwaka 51 A.H – 671. Yeye ni wa tatu katika wakeze Mtume (s.a.w.) wenye Fatwa nyingi.
11. Bibi Maymuna bint Harith: Mwarabu katika kabila la Bani Hawazin. Yeye ndiye mke wa mwisho. Alikuwa mwanamke wa miaka 51 alipoolewa na Mtume (s.a.w.). Alimwoa katika Mfunguo pili 7 A.H – Feb. 629. Bibi huyu alikuwa ndugu wa kwa mama na Bibi Zaynab bint Khuzayma, mke wa tano wa Mtume (s.a.w.) na alikuwa mama mdogo wa Bwana Khalid bin Walid mkubwa wa majeshi ya Makureshi, wakati huu Mtume (s.a.w.) alimpatia wasaa jamadari huyu, akamfahamisha vilivyo dini ya Uislamu, haikupita miezi 2 baada ya kuolewa mama yake ila Bwana Khalid alisilimu pamoja na jamadari mwenzake, Bwana Amr bin Al’As. Wakawa majemedari wa majeshi ya Kiislamu, baada ya kuwa majamadari ya makafiri, juu ya uzee wake mwanamke huyu aliweza kuhifadhi maneno mengi ya Mtume (s.a.w.). Zimepokewa kwake Hadithi 76. Bibi huyu alikufa mwaka 51 A.H – 671. Yeye ni wa saba mwenye Fatwa nyingi katika wakeze Mtume (s.a.w.) .
Hawa ndio wake wote aliowaoa Mtume (s.a.w.) wala hajapata kuwa nao pamoja zaidi kuliko wake tisa, kuna watu wengine wanaodai ya kwamba Mtume Muhammda (s.a.w.) alikuwa ni mtu wa kupenda starehe sana na kufuata matamanio ya nafsi yake, alama ya hayo ni huku kuwa na wake tisa wakati mmoja! Lakini tukifikiri kidogo tutaona kabisa Mtume (s.a.w.) hakuwa na sifa hiyo, kwani kila mwenye kuwa na sifa ya kupenda kuoa huoa wake vijana wanaopendeza, hawaoi wanawake wazee waliokurubia kwenda kwa mikongojo. Tumekwisha kuona kuwa Mtume (s.a.w.) hajapata kuoa mke kijana ila Bibi Aysha tu. Wake wote aliowaoa walikuwa watu wazima waliokwishakuolewa chuo kimoja au viwili ua zaidi. Bali wengine walikuwa wamekwisha kupindukia miaka 50 walipoolewa na Mtume (s.a.w.). Nani ulimwenguni aliyetaka kustarehe na wanawake akaoa wanawake wa miaka 50 au zaidi? Hapana! Basi kwa hivyo tunafahamu ya kwamba Mtume Muhammad (s.a.w.) hakuoa wake hawa kwa ajili ya kustarehe, la! bali aliwaoa kwa sababu hizi. Alioa:-
1. Wake zake wengine – kama Bibi Aysha – kwa ajili ya kufunga urafiki baina yake na baina ya msaidizi wake mkubwa katika kutangaza dini, Sayyidna Abubakr.
2. Wake zake wengine – kama Bibi Hafsa – kwa ajili ya kumwonea huruma na kumwondoshea majonzi baba yake kwa kuwa watu wote aliowataka wamwoe mwanawe walikataa.

3. Wake zake wengine – kama Bibi Ramla bint Sufyan – kwa ajili ya kumlipa kitendo chake kizuri kile cha kusalia Uislamuni katika nchi ya ugeni, ingawa mumewe kaiacha dini hiyo, na jamaa zake wote wanaabudu masanamu.
4. Wake zake wengine – kama Bibi Zaynab bint Jahsh – kwa ajili ya kuondosha ile dasturi yao mbaya ya kumnyanyasa na kutomwoa mwanamke aliyeachwa.
5. Wake zake wengine – kama Bibi Zaynab bint Khuzayma na Bibi Safiyya na wote wengine waliosalia – kwa ajili ya kutangaza dini katika zile kabila zao kubwa ambazo wakati huo zilikuwa bado hazikusilimu. Hakuoa hata mke mmoja katika kabila ambazo watu wake wote wamekwisha silimu, kama kabila mbili za Ansar – Aus na Khazraj – Lau kuwa kweli akitaka kustarehe na wanawake angalioa wanawake vijana wazuri awatakao, katika kabila hizi za Kiansari na nyingi nyenginezo ambazo zilikuwa zikimtii zaidi kuliko Mfalme yoyote ulimwenguni. Lakini alikuwa akiwaoa kwa ajili ya kutangaza dini.
E.WATOTO NA WAJUKUU WA MTUME (S.A.W.)
Mtume (s.a.w.) kazaa watoto saba tu, sita kwa Bibi Khadija na wa saba kwa suria wake, baada ya miaka mingi tangu kufa Bibi Khadija. Watoto wenyewe ni hawa:-
1. Bwana Qasim: Amemzaa baada ya miaka miwili tangu kumwoa Bibi Khadija, wakati huu Mtume (s.a.w.) alikuwa kijana wa miaka 27. Aliishi muda wa miaka miwili tu kisha akafa. Mtume (s.a.w.) alikuwa akiitwa “Abul Qasim” kwa ajili ya mtoto huyu.
2. Bibi Zaynab: Kamzaa naye ni kijana wa miaka 30, ulipokuja Utume alikuwa keshaolewa na mtoto wa mama yake mdogo, aliyekuwa akiitwa Bwana Abul As bin Rabii bin Abdul Uzza bin Abdishams bin Abd Manaf – katika Bani Umayya – Bwana huyu hakusilimu ila katika mwaka 7 A.H Wala mkewe huyu hakupata nafasi ya kuhama pamoja na baba yake alipokwenda Madina. Hakuja Madina ila katika mwezi wa pili baada ya vita vya Badr. Huyu mumewe alitekwa katika vita hivyo. Na Mtume (s.a.w.) alimshurutiza kumrejesha mwanawe ili awe ndiye kikomboleo chake, muda wote huo alikaa Madina bila ya mume, mpaka aliposilimu mumewe, Mtume (s.a.w.) alimrejesha kwa mumewe huyu wakakaa raha mustarehe, alizaa naye watoto 2 kabla ya kuhamia Madina. Nao ni:
(a) Bwana Ali: ambaye alikuwa nyuma ya Mtume (s.a.w.) juu ya farasi wake baadhi ya wakati siku walipoiteka Makka. Alikufa kabla hajabalighi.
(b) Bibi Umaama: ambaye aliolewa na Sayyidna Ali alipokufa bibi Fatma, mwenyewe Bibi Fatma kawausia haya.

Huyu Bibi Zaynab alikufa katika mwaka 8 A.H – 629. Naye ni mwanamke wa mika 31.


3. Bibi Ruqayya: Alizaliwa alipokuwa Mtume (s.a.w.) miaka 33. Sura yake ilikuwa nzuri sana hakuwa yoyote katika ndugu zake aliyekuwa akilingana naye kwa uzuri, umekuja Utume naye ni mtoto wa miaka 8, lakini keshafungishwa ndoa na mtoto wa Abu Lahab, aliyekuwa akiitwa Utba. Kwa hivyo akikaa huko huko nyumbani kwa Abu Lahab, na nyumba yake ilikuwa imeshikamana na nyumba ya Mtume (s.a.w.), hata ulipokuja Utume, na Abu Lahab na mkewe wakawa maadui wakubwa wa Mtume (s.a.w.), wazee hawa walimwamrisha mtoto wao amwache Bibi Ruqayya. Akamwacha naye akarejea kwao, na wakati huu naye ni mwanamke wa miaka 10 na kitu.
Akaolewa na Sayyidna Uthman bin Affan. Hata wakati walipohama baadhi ya Masahaba kwenda katika nchi ya Mahabushia, alikwenda pamoja naye, akachukua mimba huko akazaa mtoto mwanamume. – Bwana Abdalla – kisha wakarejea Makka, na wakahama kabla ya Mtume (s.a.w.) wakenda Madina. Mtume (s.a.w.) alipofika Madina aliwakuta wakukuu, hata mwezi wa Ramadhan 2.A.H – Jan. 624, alishikwa na ugonjwa wa tetekuwanga akafa, Mtume (s.a.w.) anarejea katika vita vya Badr yeye na jeshi lake akawakuta watu makaburini wanamzika. Akasikitika sana kwani ndiye mwanawe wa awali kufa mtu mzima, alikuwa kijana wa mika 21 na kitu. Na siku zile zile yule mwanawe Bwana Abdalla akafa.
4. Bibi Ummu Kulthum: Amezaliwa ulipokua umri wa Mtume (s.a.w.) miaka 36. Yeye kama dada yake, Bibi Ruqayya — alikua amefungishwa ndoa na mtoto mwingine wa Abu Lahab – Utayba. Akaachwa vile vile kama alivyoachwa nduguye, lakini alikuwa mtoto wa miaka 8 tu. Hata alipokufa ndugu yake – Bibi Ruqayya – aliolewa na Sayyidna Uthman, akaingia nyumba ya dada yake, katika mwezi wa mfunguo nane 3 A.H.-Aug.624. Lakini hakuzaa kabisa. Katika mwezi wa Shabani 9 A.H.-Oct. 630 – naye alishikwa na ugonjwa akafa. Baada ya kwisha kuzikwa; na kurejea makwao, Mtume (s.a.w.) aliwasikia watu wakisema ya kuwa Sayyidna Uthman ana kisukumi; kwa hivyo alisimama akasema; “Mwozeni Uthman lau ningelikua na mwengine asieolewa ningemwoza.” Sayyidna Uthman anaitwa “Dhun-Nurayn.” Kwa ajili ya kuoa watoto hawa wawili wa Mtume (s.a.w.).
5. Bibi Fatma: Alizaliwa na umri wa Mtume (s.a.w.) ni miaka 39. Alikuwa na sifa za utukufu nyingi zaidi kuliko ndugu zake wote. Mtume (s.a.w.) alikuwa akimpenda mno kwa ajili ya sifa hizo. Alipokuwa akisafiri, nyumba ya mwisho aliyokuwa akiingia kuiaga ni nyumba ya mwanawe huyu, na vile vile nyumba yake ndio nyumba ya kwanza anayoingia anaporejea safarini. Katika mwezi wa 3 baada ya kwisha vita vya Badr. Mtume (s.a.w.) alimwoza Sayyidna Ali bin Abi Talib. Siku hizo Sayyidna Ali alikua na miaka 21 na nusu, na yeye Bibi Fatma ni miaka 15 na nusu. Alizaa naye watoto sita – watatu wanaume na watatu wanawake –. Lakini walioishi wakawa wakubwa ni watano tu. Walio mashuhuri zaidi ni:
(a) Sayyidna Al Hasan: Amezaliwa mwezi wa Ramadhani 3 A.H.-Dec. 624 — na akafa1 Mfunguo sita mwaka wa 50 A. H.— 670.
(b) Sayyidna Al Huseyn: Amezaliwa mwezi wa Shabani 4 A. H.—Nov. 625; na ameuawa mwanzo wa Mfunguo nne mwaka wa 61 A. H.—681.
Watoto hawa walimshabihi sana Mtume (s.a.w.) kwa sura. Hasa Bwana Al Hasan, na vile vile kwa tabia, Mtume (s.a.w.) alipokuwa akikaa nao humweka Al Hasan juu ya paja la kulia na Al Huseyn juu ya paja la kushoto na akisema: “Hawa ndio maua yangu; hawa ndio watakaoendeleza nasaba yangu.2

Bibi Fatma ndie peke yake aliyeishi katika watoto wa Mtume (s.a.w.) mpaka kufa kwake na alikufa baada yake kwa miezi sita. Alikufa mwezi wa Ramadhani 11 A. H.—Dec. 632 yeye ndiye mwanamke bora kuliko wanawake wote katika umma huu.


6. Bwana Abdalla: Kazaliwa mwaka wa pili wa kuja Utume; akafa wakati ugomvi wa dini uliposhika nguvu. Alipokufa Makureshi walisema, “Muhammad amekua kibubutu; hana mtoto wa kiume wa kulihuisha jina lake” Mungu akamshushia sura 108 (Al Kawthar) ambayo ilimpa habari kuwa yeye atapewa kheri nyingi, na jina lake halitokufa milele.
7. Bwana Ibrahim: Huyu ni mtoto wa suria wa Kiqibt (Copt) ambaye aliletwa na Liwali wa nchi ya Misr katika mwaka 7 A.H. wakati huo watoto wake wote wanaume walikuwa wamekwisha kufa. Akamweka usuria kwa kutaraji atazaa naye. Akazaa naye mtoto huyu katika mwezi wa mfunguo tatu 8 A. H.—April 630. Lakini alikufa baada ya miezi 15 tu, – katika mwezi wa mfunguo sita, 10 A. H.— 631
Mtume (s.a.w.) alisikitika sana kwa kifo chake na akalia machozi; lakini bila ya kusema maneno yoyote kwa kutoa sauti! Watu wakasema; “Jua limepatwa kwa ajili ya mtoto wa Mtume (s.a.w.)” Mtume (s.a.w.) aliposikia aliinuka akasema: “Jua na mwezi ni viumbe katika viumbe vya Mwenye -ezi-Mungu. Havipatwi kwa ajili ya kufa yoyote wala kuhuika yoyote”.
F. BABA WADOGO WA MTUME (S.A.W.) NA MASHANGAZI ZAKE
Watoto wa Bwana Abdul Muttalib 19 – 13 wanaume na 6 wanawake. Lakini waliokuwa ndugu baba na mama na baba yake Mtume (s.a.w.) ni wanaume 3 na wanawake 5, nao ni hawa:


  1. Bwana Abu Talib: Baba yake Sayyidna Ali.




  1. Bwana Zubeyr: Aliyekuwa akimlea Mtume (s.a.w.) pamoja na Bwana Abu Talib.




  1. Bwana Abdul Kaaba: Kafa kabla ya baba yake.




  1. Bibi Baydhaa: Bibi yake Sayyidna Uthman bin Affan mzaa mama yake. Na mama yake huyo akiitwa Bibi Arwa bint Kurayz.




  1. Bibi Aatika: Mama wa Bibi Hind bint Abi Umayya1, mke wa sita wa Mtume (s.a.w.).




  1. Bibi Barra: Mama wa Bwana Abu Salama – mmoja katika Masahaba wakubwa na wa mwanzo – katika kusilimu, kuhama na kwenda katika nchi ya Mahabushia na kwenda Madina.




  1. Bibi Umayma: Mama yake Bibi Zaynab bint Jahsh – mke wa saba wa Mtume (s.a.w.), na ndiye mama wa Bwana Abdalla bin Jahsh, mmoja katika Majamadari wa Kiislamu zama za Mtume (s.a.w.).




  1. Bibi Arwa: Katika baba zake wadogo wote walisilimu watu wote wakajua ni wawili tu: Bwana Hamza na Bwana Abbas, na katika Mashangazi zake ni Bibi Safiyya na vile vile Bibi Aatika na Bibi Umayma na Bibi Arwa kama wanavyosema baadhi ya wanavyuoni.


G. WAJOMBA ZAKE MTUME (S.A.W.) NA MAMA ZAKE WADOGO
Hana wajomba wala mama wadogo1.
H. KUJENGWA AL KAABA
Mtume (s.a.w.) alipokuwa miaka 35 Al Kaaba ilifanya nyufa kubwa, na ikakaribia kuvunjika. Makureshi wakafanya shauri ya kuvunja na kuijenga yote upya. Al Kaaba ilikuwa haina sakafu, lakini wakati huo waliazimia kuijenga sakafu ya mawe. Waliigawa kazi hii kwa koo mbali mbali, kila ukuta mmoja katika kuta tano ulikuwa na ukoo wake makhsusi wa kuujenga.

1. Nusu ya ukuta wa Kaskazini na ukuta wote wa Mashariki – ambao ndio wenye mlango – ulikuwa ukijengwa na Bani Abd Manaf na Bani Zuhra, katika Bani Abd Manaf zinaingia zile koo tatu tukufu za Makureshi – Bani Hashim Bani Umayya na vile vile unaingia ukoo wa Bani Muttalib – .
2. Nusu ya ukuta wa Kaskazini na ukuta wote wa Magharibi ulikuwa ukijengwa na Bani Asad, Bani Adiy na Bani Abdid Dar.
3. Ukuta wa Kusini waliachiwa Bani Makhzum na kabila zote za Makureshi zilizosalia.
4. Sakafu ya Al Kaaba waliachiwa Bani Jumah na Bani Sahm.
Lakini Hajarul Aswad lilipokuwa likitaka kuwekwa mahali pake baina ya ukuta wa Kusini na Mashariki, hapo ndipo walipogombana. Kila ukoo ulitaka mkubwa wao aliweke. Ugomvi ukashika nguvu – kila ukoo ukakaza upande wake ukiona kuwa ndio wenye kustahiki –. Kazi ikazuilika muda wa siku tano – panangojwa vita tu –, tumbo litakaloshinda ndilo liweke jiwe la Hajarul Aswad.
Kila wenye akili walikuwa hawataki vitokee vita vya wenyewe kwa wenyewe. Basi siku moja hawa Makureshi wenye ugomvi walipokuwa wamekaa kwenye Al Kaaba pamoja na bwana mmoja mtu mzima sana wa Kibani Makhzum1, walimtaka shauri bwana huyo naye alisema: “Jambo lililobora ni kuwa yoyote atakaeingia katika Al Kaaba sasa hivi katika mlango wa Bani Abdid Dar tumkubalie hukumu yake yoyote atakayoisema juu ya kuliweka jiwe hili” waliokuwepo wote hapo walikubali shauri hii, mara kwa bahati nzuri aliingia Mtume (s.a.w.) – alikuwa hakupata Utume bado –, na hapo wote wakasema kwa umoja wao: “Hadhal Amin – Huyu yule mwaminifu – na sote tumemkubali” Mtume (s.a.w.) akalichukuwa lile jiwe akalitia katika shali yake, akamwita kila mkubwa wa ukoo kisha akawaamrisha walichukue kitikiti mpaka mahali pake. Hapo Mtume (s.a.w.) akalipokea akaliweka yeye kwa mkono wake na kwa radhi yao wote.

Yüklə 0,69 Mb.

Dostları ilə paylaş:
1   2   3   4   5   6   7   8   9   ...   15




Verilənlər bazası müəlliflik hüququ ilə müdafiə olunur ©muhaz.org 2024
rəhbərliyinə müraciət

gir | qeydiyyatdan keç
    Ana səhifə


yükləyin