Maisha ya nabii



Yüklə 0,69 Mb.
səhifə4/15
tarix10.12.2017
ölçüsü0,69 Mb.
#34382
1   2   3   4   5   6   7   8   9   ...   15

SURA YA NNE

KUPATA UTUME NABII MUHAMMAD (S.A.W)
KUPATA UTUME NABII MUHAMMAD (S.A.W)
Tumekwisha kuona kuwa Mtume (s.a.w.) hakupata kufanya jambo lolote katika mambo waliokuwa wakiyafanya makafiri, wala hakuwa akihudhuria sikukuu zao tangu kufahamu kwake. Alikuwa akipenda kukaa peke yake. kufanya haya kulikuwa kukimwonyesha raha kubwa kuliko kutoka mbele za watu akaona yale mambo yao mabaya aliyokuwa akiyachukia. Kila usiku ukicha naye alikuwa akizidi kuyachukia. Lakini alikuwa hajui la kufanya.
Hata alipotimia miaka 38 hakuweza tena kustahamili kuona zile ibada za masanamu na tabia mbovu walizokuwa nazo wenziwe, ilivyokuwa hana la kufanya katika kuyazuiya yale, alifanya shauri kuuacha mji wa Makka na kwenda maporini kukaa. Akapata pango zuri katika Jabal Hira Kaskazini ya Makka, inapata meli 3 toka huko Makka. Akawa akikaa huko kwenye Jabal Hira kwa muda wa wiki nyingi, kisha hurejea Makka kuja kumtazama mkewe, wanawe na jamaa zake wengine, na vile vile kwa ajili ya kuchua chakula kinapokuwa kimekwisha. Wakati mwengine akikaa siku nyingi sana huko maporini hata humpasa mkewe Bibi Khadija kwenda kumsikiliza na mara nyengine alikuwa akifuatana naye, pamoja na watoto wao mpaka maporini. Alidumu juu ya hali hii muda wa miaka miwili na kitu.
Hata siku moja – katika mwezi wa Ramadhani mwezi 17, Jumaatatu katika mwaka wa 40 unusu wa umri wake – Mtume (s.a.w.) alimuona mtu kamsimamia mbele yake bila ya kumuona wapi katokea, akamwambia: “Soma” Mtume (s.a.w.) akamjibu: “Mimi sijui kusoma kwani sijapata kujifundisha kusoma” akaja akamkamata akambana, akamwambia tena: “Soma” Mtume (s.a.w.) akamjibu jawabu yake ile ile, hata mara ya tatu akamwambia: “Soma – Iqraa Bismi Rabbik - ” akamsomea sura hiyo ya 96 mpaka kati yake, kisha Mtume (s.a.w.) akaisoma kama alivyosomewa. Hii ndiyo sura ya kwanza kushuka katika Qurani, ingawa haijawekwa mwanzo.
Mara yule mtu (Malaika) akaondoka machoni mwake – asimwone kenda wapi. Na Mtume (s.a.w.) naye akarejea kwake – khofu imemshika – . Alipofika nyumbani, Bibi Khadija alidhani ana homa, akamfunika maguo gubi gubi na akakaa mbele yake akimsikiliza anavyoweweseka. Hata homa ilipomwachia alimweleza Bibi Khadija yote yaliyomtokea, na Bibi Khadija akamtuliza moyo wake, akamyakinishia ya kuwa hapana lolote baya litakalomzukia. Mara Bibi huyu akaondoka akenda kwa jamaa yake – Bwana Waraqa bin Naufal – akampa habari yote iliyompata mumewe. Naye akamwamrisha amwite, na Mtume (s.a.w.) akenda akamweleza habari yake yote. Bwana Waraqa akamwambia: “Huyo ndiye Jibril aliyemshukia Nabii Mussa na Nabii Isa. Basi jibashirie kuwa wewe ni Mtume (s.a.w.) wa Umma huu!! Nami natamani kuwa hai nikuone unavyosimama kuwatengeneza jamaa zako, Inshaalla nitakuwa mkono wako wa kulia!” wakarejea kwao na khofu yote imemtoka. Baada ya kuazimia kuwa hatakwenda tena kule pangoni. Pale pale akaondoka akenda pangoni mwake ili aonane naye tena, ingawa alikaa huko muda mrefu. Siku ile ya kupata Utume inawafiki mwezi wa December 610.
Huyu Bwana Waraqa hakuwa akiabudu dini ya masanamu bali alikuwa akifata dini ya Kimasihi1, alipokuwa akisoma vitabu vya dini hii aliona kwamba kutatokea Mtume mwengine ndiyo maana alipohadithiwa habari ile iliyompata Mtume (s.a.w.), mara moja akatambua kuwa huyo mtu aliyemjia Mtume (s.a.w.) ni Jibril ambaye hamjii mtu yoyote ila Mtume tu.
A. NAMNA ZA KULETWA WAHYI
Waisalamu wanaitakidi kuwa Quran ni maneno ya Mungu, na vile vile Taurat ya Nabii Mussa, Injili ya Nabii Isa na Zaburi ya Nabii Daud, vyote hivi pia ni vitabu vyenye maneno ya Mwenye ezi Mungu. Lakini Mungu haonekani kwa macho wala hayupo mahala makhsusi, basi vipi hawa Mitume wamepata maneno haya? Jawabu yake ni hii. Wao huyapokea ima:-
1. Kwa Jibril – Malaika mkubwa kuliko Malika wote wa Mwenyezi Mungu1. Au.
2. Mwenyezi Mungu huwaumbia sauti, wakaweza kusikia maneno yake mwenyewe khasa, kama alivyosikia Nabii Musa. Au.

3. Mwenyezi Mungu huwatia itikadi kubwa katika nyoyo zao wakafahamnu kuwa inatakiwa kwao kufanya au kusema jambo makhsusi, basi hulisema au hulifanya. Au.
4. Huwa kwa kuotesha usingizini kuwa afanye kitu fulani au kujiona anafanya kitu fulani, kama alivyojiona Nabii Ibrahim kuwa anamchinja mwanawe, kwa hivyo akaondoka kwenda kumchinja.
Kwa hivyo maneno yote wanayotamka Mitume huwa miongoni mwa namna za Wahyi, kama alivyosema Mungu katika sura ya 53 (An Najm) Aya ya 4 :
Hayakuwa maneno yake (Nabii Muhammad) ila ni Wahyi
Huyu Jibril alipokuwa akiwajia ima:

  1. Huwajia kwa sura ya Kibinaadamu. Au

  2. Kwa sura ya kiumbe chenye mbawa. Au

  3. Husikiwa sauti yake na kishindo chake tu bila kuonekana.

Mitume mingine hupewa namna moja mbili katika namna hizi za Wahyi, na wengene hupata zote au namna moja tu.
B. KUAMRISHWA KUFUNDISHA DINI
Baada ya siku kidogo kupita tangu siku ile aliyopewa habari kuwa atakuwa Mtume (s.a.w.) na baada ya kurejea tena kule pangoni mara siku moja alimdhihirikia tena yule Malaika, na akamsemeza kwa maneno yaliyoko katika Suratil Muddaththir, tangu mwanzo wake mpaka Aya ya 71. hii ndiyo sura ya pili iliyoshuka ulimwenguni, ingawa imewekwa mahali pa sura ya 74.
Aliamrishwa katika sura hii ainuke afundishe watu dini ya haki na akataze ibada ya upotofu waliyokuwa nayo, aliamrishwa kusubiri kwa taabu zote zitakazompata mbele, lakini hakubainishiwa namna ya kufundisha kwenyewe – mmoja mmoja kwanza? Kwa siri? Au wote kwa pamoja bila ya kificho? – Alitumia akili yake, akaona bora kuwafundisha kwa siri mmoja mmoja. Akayafikiri pale pale majina ya atakaowaanza awali, nao ni wale aliokuwa akijuwana nao zaidi na waliokuwa hirimu zake au wadogo kuliko yeye. Alijuwa ya kuwa hii tu itakuwa kazi kubwa isiyokuwa na mfano, seuze kwenda kuwabainishia mabingwa wa Kikureshi waliotopea katika ibada ya masanamu kuwa hiyo si ibada kitu. Mtume (s.a.w.) aliona mzigo mkubwa katwikwa na akafanya khofu kubwa asije akashindwa njiani.
Akamfikiri Bwana Waraqa bin Naufal ambaye alikuwa amekwisha kufa siku zile akafikiri ile ahadi aliyompa kwamba atakuwa mkono wake wa kulia wakati atakaposimama kuwatangazia dini jamaa zake. Mara akawaza shauri nyengine, akarejea kwa mkewe Bibi Khadija, akamsimlia habari hii, pale pale bibi huyu akamwamini akawa ndiye mtu wa awali kabisa kushehedusha shahada ya Uislamu, basi Muislamu wa mwanzo kabisa ni mwanamke, uso wake ulikuwa mabruki, hakuwa ndiye mbwi ndiye n’go,1 bali amekuwa ndiye mfunguzi wa mfuatano wa Uislamu, hata leo wako Waislamu zaidi kuliko 400, 000, 000 duniani2.
Sasa nitawataja Waislmu wa mwanzo kabisa kwa mpango wa kusilimu kwao mmoja baada ya mmoja, lakini sitawataja wale wasiokuwa mashuhuri sana.
C. WAISLAMU WA AWALI KABISA
1. Bibi Khadija bint Khuweylid: pamoja na watoto wake aliyowazaa na Mtume (s.a.w.) na aliyowazaa kwa waume zake wawili wa mwanzo. Wale aliowazaa na Mtume (s.a.w.) baadhi yao walikuwa wadogo bado, hawajui ukafiri wala Uislamu. Lakini alivyosilimu mama yao ndiyo kama wamesilimu wao, kwani wataondokea juu ya Uislamu tu. Mtume (s.a.w.) aliamrishwa kufundisha dini siku ya Jumaatatu, na bibi huyu alisilimu siku hiyo hiyo akafanya ibada na Mtume (s.a.w.) usiku ule ule kabla ya mtu yoyote ulimwenguni! Huyu ndiye aliyefuzu kweli kweli.
2. Sayyidna Ali bin Abi Talib bin Abdil Muttalib: alikuwa akilelewa na Mtume (s.a.w.), alipomuaona Mtume (s.a.w.) na Bibi Khadija usiku ule wanafanya mpya aliwauliza, “Hii ni ibada gani?” Mtume (s.a.w.) alimfahamisha na akamtaka awe pamoja nao, lakini yeye alikataa kwanza akasema “Mpaka nende nikamshauri baba yangu” Mtume (s.a.w.) akamkataza kuitoa siri ile nje. Mara asubuhi ya usiku ule ule kijana huyu akaja kwa Mtume (s.a.w.) akampa habari kuwa yeye yu pamoja nao, akawa ndiye Islamu wa pili duniani, aliposilimu alikuwa kijana wa miaka 10 hivi.
3. Bwana Zaydi Al Haritha Al Kalbi: Huru wa Mtume (s.a.w.) na mwanawe wa kupanga, alikuwa akikaa pamoja na Mtume (s.a.w.), na akasilimu – kama Sayyidna Ali – mchana wa Jumaane, alisilimu yeye na mkewe Bibi Ummu Aymana – Yaya wa Mtume (s.a.w.) – .
4. Sayyidna Abubakr Siddiq: Rafiki mkubwa sana wa Mtume (s.a.w.) toka udogo wao, aliyekuwa akionekana kutwa kucha kabla hajenda zake pangoni, hakuwako Makka siku alipoamrishwa Mtume (s.a.w.) kufundisha dini, alikuwa amekwenda Yaman katika biashara zake, baada ya siku tatu akafika, na alipokuja kumtazama Mtume (s.a.w.) alipewa habari ile, saa ile ile akasilimu bila ya kushangaa, kwani alikuwa akijua kwa yakini kuwa rafiki yake hasemi uwongo, alisilimu yeye na mama yake – Bibi Salma bint Sakhr – na mkewe mdogo – Bibi Ummu Ruman na watoto wake wakubwa – Bibi Asmaa na Bwana Abdulla.
5. Sayyidna Uthman bin Affan: Mzalendo wa Kikureshi na katika kabila ya Bani Umayya, na tajiri mkubwa katika matajiri wa Kikureshi, na bibi yake mzaa mama yake ni shangazi lake Mtume (s.a.w.). Alikuwa katika watu waliokuwa wakitajikana na mwenendo mwema na fikra nzuri sana, kwa hivyo alipoendewa tu na akafahamishwa uzuri wa dini ya Kiislamu mara alifuata. Akawa ni katika wenye kuisimamia dini kwa hali na mali.
6. Bwana Zubeyr bin Awwam bin Khuweylid: Mtoto wa ndugu yake Bibi Khadija mama yake ni Bibi Safiyya bint Abdul Muttalib, shangazi lake Mtume (s.a.w.), alisilimu yeye na mama yake Bibi Safiyya.
7. Bwana Abdulrahman bin Auf bin Abd Auf bin Harith bin Zuhra: Jamaa wa mama yake Mtume (s.a.w.). Mama yake – Bibi Shaffa bint Auf bin Harith bin Zuhra – ndiye aliyekuwa mkunga wa Mwana Amina bint Wahab bin Abd Manaf bin Zuhra wakati alipomzaa Mtume (s.a.w.) –. Mama huyu alikuwa mara nyingi akimhadithia mwanawe ajabu zilizotokea siku aliyozaliwa Mtume (s.a.w.). Kwa hivyo mara aliposikia Utume wake alisilimu yeye na mwanawe huyu na jamaa zake wengine. Yeye alikuwa katika matajiri wakubwa wa Kikureshi.
8. Bwana Said bin Zayd: Mtoto wa baba yake mdogo Sayyidna Umar bin Al Khtattab, alisilimu yeye na mkewe – Bibi Fatma bint Al Khattab – kabla hajasilimu Sayyidna Umar.
9. Bwana Saad bin Abi Waqqas bin Wuhayb bin Abd Manaf: Jamaa sana na mama yake Mtume (s.a.w.), Mtume (s.a.w.) alikuwa akimwita mjomba, na akimtukuza sana, alikuwa mmoja katika mashujaa wakubwa wa Kiislamu.
10. Bwana Talha bin Ubeydillah: Baba yake na babu yake Sayyidna Abubakr ni ndugu, alikuwa katika wafanyaji biashara wakubwa.
11. Bwana Arqam bin Abi Arqam: Kwake ndipo palipokuwa mahali ambapo Waislamu wakikusanyika kufanaya ibada zao kwa siri. Na Waislamu wengi wengineo, na wengi katika hao walikuwa katika matajiri na watukufu wao mbele ya Makureshi ila si majeuri wao tu, si mafakiri wa Kikureshi kama wanavyosema watu wengine.
D. KUTANGAZA DINI KWA SIRI
Tumeona ya kuwa Mtume (s.a.w.) alichagua watu wa kuwaambia Ujumbe wake1, hakuondoka mara moja tu akanadi kuwa yeye ni Mtume, karibu wote wale waliokuwa rafiki zake walimwamini wakamfuata, na kila mmoja katika hao akawa anawalingania watu wengine anaowaona wanaelekea kufuata, wakasilimu watu si haba, lakini bila ya kujulikana na yoyote wasiokuwa wao wenyewe kwa wenyewe, walidumu juu ya haya kwa muda wa miaka mitatu, walikuwa wakikutana na kufanya ibada zao nje ya mji, hata waliposikia minong’ono ya kuwa wameonekana, waliacha kwenda huko maporini na wakatafuta nyumba ya kuweza kukusanyika wenyewe kwa wenyewe bila ya kuonekana. Bwana Arqam akatoa nyumba yake ndiyo iwe mahala pa kukusanyikia kwao, nyumba hii ilikuwa karibi na Jabal Safaa, na mpaka leo ipo alama yake, huko ndiko wakifanya mikutano yao na ibada yao, ilikuwa ni kusali raka nne tu kwanza – mbili asubuhi na mbili jioni kama walivyokuwa wakiabudu watu waliomfuata Nabii Ibrahim katika karne ya 21 kabla ya kuzaliwa Nabii Issa – na walikuwa wakifunga siku moja katika mwaka mzima, siku yenyewe iliyokuwa wajibu kufunga ni mwezi 10 Mfunguo nne, huku kusali rakaa nne tu mchana kutwa kulibadilishwa mwezi wa 12 wa kuja Utume kwa kuamrishwa kusali raka 17, mbili Alfajiri, nne Adhuhuri, nne Laasiri, tatu Magharibi na nne Isha, na katika mwaka wa pili wa Al Hijra iliamrishwa kufunga mwezi mzima wa Ramadhan badala ya siku ile moja.
E. KUDHIHIRISHA DINI
Baada ya miaka mitatu aliteremshiwa Aya ya 94 katika Suratil Hijr iliyomwamrisha kudhihirisha Dini1, pale pale Mtume (s.a.w.) aliondoka nyumbani kwake akenda akapanda juu ya Jabal Safaa akapiga kelele, akawa anazita kabila za Kikureshi zote zilizoko Makka, mara tu walaposikia mwito wake, kila mmoja aliacha kazi yake akaufuata ukulele ule, muda si muda jabali lote lilizungukwa nao darmadar, naye Mtume (s.a.w.) yupo juu yake anawaona, hata walipokuja wote, Mtume (s.a.w.) aliwaambia: “Mnajua kuwa mji wenu huuu haupigwi na kabila yoyote? Kabila zote za Kiarabu zinatutukuza kwa ajili ya hii nyumba yetu tukufu ya ibada. Lakini mnaonaje nikikwambieni kuwa: ‘Naona jeshi la mafarasi linakuja kukushambulieni, mtanisadiki?’ Makureshi wakajibu “Ndiyo tutakusadiki” Akawaambia tena: “Vipi mtanisadiki nanyi hamjaona na baada ya kuwa na yakini kuwa mji wenu hautapigwa maisha na kabila yoyote? Maana Waarabu wote watainuka kuipiga kabila hiyo kabla ya kufika huku” Wakajibu wote kwa pamoja: “Tutakusadiki kwa sababu wewe ni Al Amin2 hatujapata kusikia la uwongo kwako muda wa miaka yote hii tuliyokaa pamoja nawe. Kwa hivyo tutakusadiki kwa kila utakalotwambia” Mtume (s.a.w.) akasema: “Basi nisadikini kuwa mimi ni Mtume wa Menyezi Mungu nimekuja kukufikisheni Dini ya haki”.
Mara pale pale baba yake mdogo – Abu Lahb – aliyadakiza maneno yake akamwambia: “Umehasirika Muhammad! Hishima yote tuliyokuwa tukikupa sasa umeikosa, ondokeni mwacheni mpuuzi huyu!” Mtume (s.a.w.) akavunjika moyo sana akashuka akenda zake kwa mkewe akampa habari yote ile na namna Abu Lahb alivyomvunja mbele za watu. Mwenyezi Mungu alimletea sura ya kumliwaza na ya kumwonyesha kuwa Abu Lahb atakuwa mtu wa Motoni. Sura ya Tabbat Yadaa Abi Lahb.


SURA YA TANO

KUTESWA KWA WAISLAMU

KUTESWA KWA WAISLAMU
Kila waliokuwa hawana habari ya Uislamu waliisikia siku hii aliposimama Mtume (s.a.w.) juu ya Jabal Safaa na akadhihirisha mbele ya watu wote kuwa yeye ni Mtume, amekuja kutengua ile dini yao na kufundisha dini nyengine. Watu waliokuwa wanadadisi pale pale waliondoka kuwatafuta hao Waislamu na kuwauliza hakika ya dini yao hiyo na vipi inatafautika na dini yao ya asili, wakati huo watu wengi kidogo walikuwa wamekwisha silimu, na mara walianza kueleza dini hiyo kwa kila wenye kuwauliza, wakasilimu waliojaaliwa uongofu na wakakakamia katika masanamu yao wale waliokuwa wakaidi, wakazidi kuyapenda na kuyatukuza kuliko zamani, ili wapate kuwaudhi waliosilimu. Lakini kila mchana ulipopambazuka na idadi ya Waislamu ilizidi, hata wale wakubwa wa kikafiri walipohisi hatari ya Uislamu juu ya dini yao waliazimia wauzuie kwa nguvu kama hautazuilika kwa salama. Mara wakajikusanya na wakaazimia wasiwe na chembe ya huruma katika nyoyo zao juu ya hao walioacha dini yao, mambo waliyoazimia kufanya ni:-


  1. Kufanya kila inavyoyumkinika kuzuia watu wasisilimu.

  2. Kumwadhibu adhabu kubwa kila aliyesilimu.

  3. Kama hayumkiniki kuadhibiwa, adharauliwe na kila mtu, asipewe ile hishima aliyokuwa akipewa.

  4. Kama ni mfanyaji biashara, watu wasinunue biashara yake wala wasimwuzie.

  5. Na kama ni yatima asipewe pesa zake. – Kwa hivyo mayatima wengi na hao wengine waliogopa kusilimu na waliosilimu walikosa pesa zao na itibari yao –.


A. WAKUBWA WA KUWATESA WAISLAMU

Waliokuwa wakiwatesa zaidi Waislamu ni hawa:-



  1. Abu Lahb: Baba yake mdogo Mtume (s.a.w.).




  1. Ummu Jamil bint Harb: Mke wa huyu Abu Lahb. Mungu amemtaja mwanamke huyu katika Quran kwa jina la Hammalatal Hatab1.




  1. Abu Jahl: Mjomba wake Sayyidna Umar bin Khattab, Mtume (s.a.w.) alikuwa akisema: “Kila umma una Firauni wake, na Farauni wa umma huu ni Abu Jahl” Jina lake khasa ni Abul Hakam – Babe akili – mwenye akili kubwa, lakini Waislmu wakamgeuza wakamwita Abu Jahl – baba la upumbavu2 –.




  1. Sayyidna Umar bin Al Khattab: Lakini mwisho wake alisilimu na akawa Khalifa wa pili wa Kiislamu.




  1. Uqba bin Abdi Muayt: Bwana wa Kibani Umayya, na baba wa kambo wa Sayyidna Uthman bin Affan.




  1. Hakam bin Abil As: Baba yake mdogo Sayyidna Uthman, alimtaabisha sana Sayyidna Uthman aliposilimu. Lakini yeye mwenyewe alisilimu mwisho wake, na yeye ndiye baba wa Wafalme wa Kibani Umayya wote, ila watatu wa mwanzo tu.




  1. Walid bin Al Mughyra: Bwana mkubwa wa Kibani Makhzum na tajiri mkubwa kabisa wa Kikureshi, alikuwa na hishma kubwa ambayo hakuwa nayo yoyote wakati huo. Neno lake ndilo neno, alikuwa hana jina ila “Rrajul Adhim” – yaani yule mtu mtukufu - Mali ya mayatima wengi yalikuwa mkononi mwake, kwa hivyo alipata njia ya kuwazuilia mayatima wengi wasisilimu kwa kuogopa wasije wakakosa mali yao. Lakini mwanawe mdogo – Khalid bin Walid – alisilimu baadae, akawa jamadari mkubwa wakati wa Mtume (s.a.w.) na baada yake. Na vile vile watoto wake wengine.




  1. Asi bin Wail: Baba yake Bwana Amr bin Al As – jamadari mkubwa wa Kiislamu na ndiye aliyeitoa Misr katika mikono ya Warumi.




  1. Umayya bin Khalaf: Akimwadhibu yoyote yule aliyesilimu katika ukoo wake, na wengi wengineo wasiokuwa hawa, ambao itachukua dakika nyingi kuwataja licha kuwaandika.


B. WATU WALIOADHIBIWA SANA KWA AJILI YA DINI YAO

Watu walioadhibiwa sana kwa ajili ya dini yao ni hawa:-


1. Sayyidna Abubakr: Mara tu Mtume (s.a.w.) alipodhihirisha kwa watu Utume wake, Sayyidna Abubakr alikwenda msikitini akatoa khutba juu ya Uislamu. Hakushtukia ila watu wote waliokuwa hapo wanampiga, baada ya kuanguka chini, aliinuka Utba bin Rabia akampiga kwa viatu mpaka akazimia, hakupata fahamu ila walipokuja jamaa zake wakamchukua kitikiti mpaka kwake, akasalia ndani baadhi ya siku, hawezi hata kujinyanyua kitandani.
2. Bwana Bilal: Alikuwa mtumwa wa Umayya bin Khalaf, – Adui mkubwa wa Waislamu –. Huyu Umayya alikuwa akimfunga kamba za mikono na miguu na ya shingo, na akiwambia watoto wamburure njiani kama wadudu chungu wanavyoburura nyuki aliyekufa, mara nyingi alikuwa akimshindisha na akimlaza na njaa, kisha humchukua siku ya pili yenye jua kali, akenda naye akamlaza chali, utupu juu ya mchanga wa moto, na akamwekea jiwe la moto juu ya kifua chake, na akamwambia “Utasalia vivi hivi mpaka ufe au uache dini ya Muhammad” Bwana Bilal alikuwa hasemi ila “Ahad Ahad” yaani “Naabudu Mungu mmoja tu wa haki” akawa anataabishwa vivyo hivyo mpaka akakombolewa na Sayyidna Abubakr kwa kumbadilisha na mtumwa wa kikafiri pamoja na mkewe na mtoto wake na pamoja na pesa nyingi juu yake.
3. Bwana Abu Fukayha: Alikuwa akitaabishwa na mtoto wa Umayya kwa namna ile ile ambayo Umayya akimtaabisha Bwana Bilal.
4. Bibi Zinira: Abu Jahl alikuwa akikiunguza chuma motoni kisha akimgandamiza nacho machoni mpaka akawa pofu.
5. Bwana Khabbab: Alikuwa mtumwa wa mwanamke katili kweli kweli, alikuwa akinyolewa nywele kisha akichomwa kwa bapa la chuma chenye moto juu ya kichwa, akawa madonda matupu kichwani.
6-8. Ammar bin Yasir na Baba yake na Ndugu yake: Walikuwa wakibabuliwa kwa majani ya mtende kila siku, hata wakajaa madonda mwili mzima, na 2 katika hawa wakafa, akasalia Bwana Ammar tu.
9. Mama yake Bwana Ammar: Alifungwa baina ya ngamia wawili – mguu mmoja huku na wa pili huku – tena wakaendeshwa mbio njia mbali mbali, na huyu mwanamke akachanika pande mbili.
10. Bwana Amir bin Fuhayra: Aliadhibiwa hata akarukwa na akili.
11. Bibi Lubayna: Sayyidna Umar – kabla ya kusilimu kwake – alikuwa akimpiga bakora wee hata mpaka achoke mwenyewe.
Wapo wengi wasiokuwa hawa, na wengine waliteswa kwa mateso ambayo hayafai kutajwa kitabuni.
C. WALIOREJEA KATIKA UKAFIRI KWA AJILI YA ADHABU ZILIZOWAKUTA

Wengine mashaka yalipowazidi – walirejea kwenye dini yao ya zamani – lakini si wengi. Miongoni mwa waliorejea ni hawa:-



  1. Abu Qeys: Mtoto wa Walid bin Mughyra.

  2. Ali: Mtoto wa Umayya bin Khalaf, aliyekuwa akimtaabisha Bilal.

  3. Harith bin Rabia: Babu yake alikuwa katika mabwana wakubwa wa Makka.

  4. As bin Munabbih: Mtoto wa mtu mkubwa sana wa Makka na ni jamaa mno na Umayya bin Khalaf.

Ilikuwa hapana ukoo wowote wa Kikureshi na Waislamu kidogo sana kuliko ukoo wa Umayya bin Khalaf, na yote haya yalikuwa kwa ajili yake, wengine walirejea kwa dhahiri yao tu, na ndani yao walikuwa Waislamu, hata mji wa Makka ulipotekwa ndipo walipodhihirisha kuwa wao walikuwa Waislamu tangu zamani, na Mtume (s.a.w.) na badhi ya Masahaba walikuwa wakijua.


D. NASAHA WALIZOTOA MAKURESHI KUMPA MTUME (S.A.W.)
Makureshi walipoona ukatili wao katika kuadhibisha Waislamu haukufidisha kitu katika kuuzuia Uislamu, waliona kuwa itakuwa bora wakenda kwa Mtume (s.a.w.) wakaonane naye uso kwa uso na wampe nasaha zao, basi wakaondoka wakubwa wa Kikureshi wakenda kwa Mtume (s.a.w.), msemaji wao alikuwa Utba bin Rabia – Babu yake Bwana Muawiya kwa upande wa mama yake – Akasema kumwambia Mtume Muhammad (s.a.w.): “Unajua kuwa hapana mwarabu yoyote aliyewaletea baa watu wake zaidi kuliko wewe? Umetutawanya mbali mbali baba hapatani na mtoto, wala mtoto hapatani na mjomba. Kaka hana huruma juu ya dada yake, wala dada hana huruma juu ya mdogo wake, basi tumekuja tuyatengeneze mambo haya, na tuondoshe huu ugomvi ulioko baina yetu. Tumekuja kukudhihirishia mambo 5, ukiyakubali utastarehe wewe na watu wako, na tutapumzika sisi vile vile. Mambo yenyewe ni haya:-


  1. Kama wewe unafanya kwa ajili ya kutaka mali, basi twambie kiasi gani unataka mara moja tutachanga tukupe nawe uwache haya.

  2. Au ukiwa unataka ufalme juu yetu tutakutawalisha sasa hivi mbele ya watu wote.

  3. Au ukiwa unataka Ushekhe tu hili ni jepesi zaidi, tutakupa Ushekhe juu ya koo zote za Kikureshi, zisikate lolote bila ya amri yako.

  4. Au kama unataka mwanamke mzuri sana, basi sisi sote tumeridhia uchague mwanamke umtakae katika ukoo wowote wa Kikureshi na katika kabila yoyote ya kiarabu.

  5. Au kama ni mgonjwa – umepatwa na jini – twambie tukakutafutie kila mganga mpaka achomoke jini huyu. Kwani mwenye jini hukomolewa.

Mtume (s.a.w.) akawajibu1: “Yote hayo mliyoyasema hayakuwepo moyoni mwangu wala mimi sina shughuli nayo, mimi nimeletwa nije nikufundisheni dini ya haki na malipo yangu nitapata kwa Mwenyezi Mungu, sitaki kitu kwenu nyinyi ila kuniachia kufikisha utumwa wa Mola wangu” Unaonaje lau kuwa si Mtume (s.a.w.) wa kweli si mara moja angekubali shauri hii, akastarehe yeye na akapumzisha watu wake? Alikuwa anajua kwa yakini kuwa wangelimfanyia kila alilolitaka. Pana shahada kubwa ya kuonyesha ukweli wake zaidi kuliko hii?


E. RAI WALIZOZITOA MAKURESHI KUMPA BWANA ABU TALIB

Wale wakubwa wa Kikureshi walipoona nasaha zao hazikufidisha kitu, walimwendea Bwana Abu Talib kwa umoja wao, kama walivyomwendea Mtume (s.a.w.) wakambwambia hivi: “Abu Talib wewe ni mtu mkubwa kwetu na mwenye kusikilizwa maneno yako. Wewe ndiye mkubwa wa dini yetu, na umeona namna gani mwanao anavyoiponda dini hiyo, basi tunakuomba umzuie kutangaza hiyo dini ya uzushi, au tuache tumfanye tutakavyo, kwani wewe ni kama sisi katika kuionea uchungu dini hii ya wazee wetu”. Bwana Abu Talib akawajibu jawabu nzuri na akawaahidi kuwa atamsemesha kwa hayo.


Zilipopita siku nyingi bila ya kuona chochote kuzuilika walimjia tena mara ya pili wakamwambia: “Abu Talib hukumzuia mwanao na sisi hatuwezi kusubiri tena juu ya haya, basi khiari moja katika mawili:

  1. Ima umzuie kutangaza huo uzushi wake, au.

  2. Tutakupiga vita pamoja naye na kila atakayekusaidia.

Bwana Abu Talib akaona taabu kupigwa vita na watu wote, kwa hivyo akawapa ahadi kubwa kuwa atamsemesha mwanawe, akamwendea Mtume (s.a.w.) amweleze maneno yote waliyomweleza Makureshi na akamwambia: “Mwanangu! usinitwike mzigo nisioweza kuuchukua” Mtume (s.a.w.) alipomsikia baba yake mdogo anasema vile machozi yalimlengalenga, akamwambia: “Baba! kama umeshindwa kunisaidia basi, lakini mimi nitaendelea kutangaza amri ya Mungu mpaka Mungu afanye anavyotaka. Wallahi! Hata kama lau wangeliweza kunitilia jua katika mkono wangu wa kulia na mwezi katika mkono wangu wa kushoto ili niache jambo hili nisingeliacha ila akitaka mwenyewe Mwenyezi Mungu” Bwana Abu Talib akamfanyia huruma kubwa na akamwambia: “Fanya unavyotaka Wallahi sitaacha kukunusuru, nitakufa pamoja na wewe”
Huyu Bwana Abu Talib alikuwa mtungaji mashairi kwa hivyo alimwambia maneno hayo kwa mashairi. Tafsiri yake ni hii:-
Mimi Wallahi najua * dini yako ni ya kweli

Ila mimi nachelea * maneno ya mafedhuli

Mjasiri sitakuwa * ‘kiwacha dini asili

Na patanenwa “Ajabu * mtu kufwata mwanawe”

Sasa mwanangu inuka * eleza zako amri

Hapana wa kukushika * kwa yako una hiari

Labuda nikishafika * mwanandani wa kaburi

Hapo sina la kufanya * jisimamie mwenyewe.


Yüklə 0,69 Mb.

Dostları ilə paylaş:
1   2   3   4   5   6   7   8   9   ...   15




Verilənlər bazası müəlliflik hüququ ilə müdafiə olunur ©muhaz.org 2024
rəhbərliyinə müraciət

gir | qeydiyyatdan keç
    Ana səhifə


yükləyin