Maisha ya nabii


Waamrishe mtu mmoja ampige upanga wa shingo, amwulie mbali. Au. 4



Yüklə 0,69 Mb.
səhifə7/15
tarix10.12.2017
ölçüsü0,69 Mb.
#34382
1   2   3   4   5   6   7   8   9   10   ...   15

3. Waamrishe mtu mmoja ampige upanga wa shingo, amwulie mbali. Au.
4. Wachague kijana mtukufu katika kila tombo la Kikureshi, kisha wampe kila mmoja katika hao upanga mkali, watake wakusanyike alfajiri moja makhsusi wampige wote kwa pamoja, ili lawama iangukiae kabila zote za Kikureshi, hapo Bani Hashim hawatakuwa na la kufanya1, ila kupokea diya2 yake tu.
Mkutano huu ulifanyika mwezi 25 Mfunguo tano, mwaka 13 May 622. Mtume (s.a.w.) akatoka Makka usiku wa mwezi mosi Mfunguo sita, usiku walioweka kumwulia.

SURA YA NANE


KUHAMIA MTUME (S.A.W.) MADINA
KUHAMIA MTUME (S.A.W.) MADINA
A. KWENDA KWA MTUME (S.A.W.) MWENYEWE MADINA
Katika mchana ule ambao usiku wake waliazimia wale vijana wa Kikureshi kumwua Mtume (s.a.w.) alikuja Jibril akamweleza Mtume (s.a.w.) habari ya Makureshi, na akamwambia atoke usiku ule ule ende Madina kama walivyokwenda Masahaba zake, pale pale Mtume (s.a.w.) akaondoka akenda kwa Sayyidna Abubakr akamwambia kuwa safari imekwishawiva usiku wa kadiri ya saa nane atampitia wende zao.
Yeye Mtume (s.a.w.) na Sayyidna Abubakr walikuwa wamekwisha weka tayari kila kitu cha safari, na wamekwisha kupanga njia za kupita, na pango la kujificha siku za kutafutwa. Walikuwa wamekwisha kununua ngamia wawili wastahamilivu na wepesi wa mwendo, wakampa mtu akae nao mpaka watakapowahitajia. Sayyidna Abubakr alimwamrisha mchungaji wa mbuzi wake – Bwana Amr bin Fuhayra – awe akiwaletea maji na maziwa kwenye hilo pango watalokuwapo, mchungaji huyu alikuwa ni mtumwa wa Sayyidna Abubakr na alikuwa Mwislamu wa kweli kweli, tena akampeleka mwanawe mkubwa mwanamke1 – Bibi Asmaa – kwenye hilo pango, na akamwambia awe akiwaletea chakula kwa siri usiku watakapokuwa wamekwisha kwenda huko. Bibi Asmaa alikuwa katika wanawake wa mbele kusilimu. Alisilimu aliposilimu baba yake na akaolewa na Bwana Zubeyr bin Awwam, baadae alimwamrisha mwanawe mdogo aliyekuwa akiitwa Abdalla awaletee habari yoyote inayowakhusu wao watakapokuwa pangoni2, kadhalika aliagana na Bedui mmoja aliyekuwa anajuana naye sana awapeleke Madina kwa njia zilizokuwa hazitumiwi na yoyote. Aliagana naye kumpa kiasi cha shillingi 300. Bedui huyu alikuwa akikaa muda mrefu Makka kisha ndipo akirejea kwao, kwani mama yake alikuwa mwanamke wa Kikureshi.
Mtume (s.a.w.) baada ya kurejea kwa Sayyidna Abubakr, alimwita Sayyidna Ali bin Abi Talib akampa naye habari ile ya safari yake, lakini alimwambia kuwa asiondoke kwanza, asalie nyuma aje kwa kituo. Watu wa Makka japokuwa walikuwa wakigombana na Mtume (s.a.w.), lakini hawakusahau uaminifu wake! Kwa hivyo wengi katika wao walikuwa wakimpa fedha zao awawekee amana. Basi fedha hizi ndizo zilizomweka Sayyidna Ali hata asende naye Madina. Makureshi walikuwa wakijua kwa yakini kuwa Nabii Muhammad (s.a.w.) hasemi uwongo, yote anayoyasema ni kama anavyodai kwani yeye ni “Al Amin As Sadiq” mwaminifu msema kweli. Lakini walikuwa hawayapendi yale mambo aliyokuja nayo tu ambayo yanakwenda kinyume kabisa na yale mambo waliyoyarithi kwa wazee wao, na ambayo wakiyafuata yatavunja hishma na jeuri zao, yawafanye wao ni sawa sawa na wale wanyonge na mafakiri – nguvu na mali isiwe ndiyo sharia tena, bali haki na insafu ndiyo sharia – watu wote wawe sawa mbele ya haki.
Makureshi wengi wakubwa walimkabili Mtume (s.a.w.) wakampa habari hii, kuwa wao wanamjua kuwa anasema kweli lakini hawayataki yale mambo aliyokuja nayo. Aya ya 33 ya Sura ya 6 (Suratul An’am) ni shahidi kwa haya niliyosema1.

B. SAFARI YA MTUME (S.A.W.) NA SAYYIDNA ABUBAKR KWENDA MADINA

Tumekwisha kuona kuwa Makureshi walifanya mkutano kwenye nyumba yao ya shauri siku ya Jumaamosi mwezi 25 Mfunguo tano, na wakapatana wakamwue Mtume (s.a.w.) usiku wa Ijumaa, mwezi mosi au mwezi pili Mfunguo sita. Na tumekwisha kuona vile vile kuwa Mtume (s.a.w.) alipewa habari hii, naye akamjuvya Sayyidna Abubakr na akaagana naye kuwa atampitia kadiri ya usiku wa saa nane ili wafuatane wende Madina.


Usiku ulipoingia barabara – na watu wakawa hawaonekani tena kupita njiani – wale vijana wa Kikureshi waliochaguliwa kumwua Mtume (s.a.w.) walikuja kwa umoja wao nyumbani kwa Mtume (s.a.w.) na wakaizunguka nyumba hiyo “darmadar”. Baada ya muda mdogo kupita tangu kuja kwao, baadhi yao waliparamia nyumba ile ili wapindukie kwa upande wa uani. Kiasi cha kutokeza nyuso zao tu mara walionekana na wanawake waliokuwemo nyumbani kwa Mtume (s.a.w.), na wakaanza kupiga kelele za khofu, walipoona kuwa wenye nyumba hawajalala bado, walishuka upesi wakajificha, wakingojea wayakinishe kuwa wote wamelala. Katika kungoja kwao kule mara Mungu aliwaletea usingizi mkubwa ukawachukua moja kwa moja.
Muda wote huu Mtume (s.a.w.) alikuwa yu macho, akingojea saa zake zitimie atoke. Hata zilipotimia alimwamsha Sayyidna Ali akamjuvya kuwa anaondoka, alipofika nje aliwakuta wale vijana wa Kikureshi wakukuu katika usingizi, wanaukoromea tu, Mtume (s.a.w.) akachukua ukofi mzima wa mchanga akawa anawanyunyizia nao na huku anasoma sura ya “Yasin” na huku anakwenda zake, alifika nyumbani kwa Sayyidna Abubakr akamkuta tayari anamgojea, wakashika njia wakenda zao.
Waliacha njia ya kaskazini ambayo walijua kuwa watafuatwa kwa njia hiyo, wakashika njia ya kusini mpaka kwenye Ghar Thaur, pango liliyopo kwenye jabali liliyoko kiasi ya meli 2 kusini ya Makka, walipofika pango hili Sayyidna Abubakr ndiye aliyeingia mbele ili kutazama kama hapana cha kudhuru, akaziba kila matundu yaliyokuwa wazi, tena ndipo alipomwambia Mtume (s.a.w.) aingie1.

Huko Makka wale Makureshi wakaamka, wakajiona kuwa wana mchanga kichwani na mlango wa Mtume (s.a.w.) ulipofunguliwa wakamwona Sayyidna Ali tu ndani, hayupo Mtume (s.a.w.), pale pale Makureshi wakatawanyika njia zote kumtafuta. Lakini kwanza walikwenda nyumbani kwa Sayyidna Abubakr, wakamkuta Bibi Asmaa, Abu Jahl akamwuliza: “Kenda wapi baba yako?” Alipomwambia kuwa hajui kenda wapi alimzaba kofi la uso, hata vipuli vyake (ear rings) vikadondoka, na uso ukamwiva mwekunduu! Walivyokuwa hawakupata bado jawabu ya kuweza kuwaonyesha alipo Mtume (s.a.w.), walimkodi Bedui mmoja aliyekuwa hodari wa kufata nyayo za mwenye kutafutwa aliyekuwa akiitwa Abu Kurz Al Khuzai, wakatoka wote nyuma yake, wakikagua Makka yote, mwisho wake aliweza kutambua njia yake, wakaingia kuitafuta kwa hadhari kubwa hata wakapanda juu ya lile jabali ambalo ndani yake ndimo lilipokuwamo lile pango alilojificha Mtume (s.a.w.). Walipofika hapo juu yule mfuata njia akawambia: “Sasa alama ya njia yake imekatika lazima yumo ndani ya pango lile” akawaashiria kwenye pango lililokuwa kiasi cha futi 40 na walipo wao. Vijana vya1 Kikureshi walipotaka kuliparamia. Umayya bin Khalaf mmoja katika mabwana wakubwa wa Kikureshi, aliwapigia kelele za ukali, akawaambia: “Hamna akili nyinyi kama huyu tuliyepoteza pesa zote kwa kumkodi? Vipi mtu ataweza kupita katika pango lile pasi na kuharibu utando wa mabuibui wale waliotanda pango lote? Au vipi njiwa wataweza kukaa pale na kulalia mayai yao ikiwa pana mtu ndani ya pango lile? Wallahi! Mabuibui wamelitumia pango hili kwa kutandia kabla ya kuzaliwa yeye Muhammad. Hajui chochote mfuataji huyu” wakashika njia wakenda zao.


Mabuibui hawa na njiwa wale hawajakuwapo zamani, kama alivyodai Umayya, bali wote walikuja alfajiri ya siku ile, ili wapate kuwaziba macho Makureshi, wasimwone Mtume (s.a.w.) na Sayyidna Abubakr.
Walipokata tamaa kuwa hawataweza kumwona katika viunga vya Makka, Makureshi walizialikia kabila nyengine kuwa yoyote atakayemleta Nabii Muhammad (s.a.w.) ijapokuwa kesha kumwua atapata zawadi ya ngamia 100. Nabii Muhammad na Sayyidna Abubakr walisalia katika pango muda wa siku 3 – Ijumaa, Jumaamosi na Jumaapili – na kila usiku akiwajia Bibi Asmaa na chakula, Bwana Abdalla na habari zote za Makureshi, na Bwana Amir bin Fuhayra na mbuzi wake usiku na alfajiri, ili awakamie maziwa wanywe.
Usiku wa Jumaatatu ulipoingia barabara alikuja Bibi Asmaa na vyakula vya kuchukua njiani mpaka Madina, akaja Bwana Amir bin Fuhayra na ngamia wawili aliowanunua Sayyidna Abubakr kwa ajili ya kupanda yeye na Mtume (s.a.w.) – mmoja wake na mmoja wa Mtume (s.a.w.) – na akaja yule Bedui waliomkodi kuwapeleka Madina kwa njia za ndani ndani. Jina la bwana wa Kibedui huyo lilikuwa Bwana Abdalla bin Arkat, na vile vile alikuwa akiitwa Bwana Abdalla bin Uraykit.
Baada ya hapo walipanda ngamia wao wakashika njia wakenda zao Madina, na Bibi Asmaa akarejea Makka, katika wale ngamia wawili mmoja alipandwa na Sayyidna Abubakr, na nyuma yake yule Bwana Amir bin Fuhayra. Yule Bedui alimpanda ngamia wake mwenyewe, waliacha njia inayopitwa na misafara, wakashika njia ya pwani, hata siku ya Jumaatano mchana, wakafika mahala panapoitwa Qudayd, kwa muda wa siku mbili walikuwa hawakuonja maziwa ya mbuzi, kwa hivyo walikuwa wakiyatamani sana. Hapo Qudayd walimkuta Bibi mmoja amekaa kwenye hema yake. Bibi huyu alikuwa mashuhuri sana kwa ukarimu wake aliokuwa akiwafanyia kila waliokuwa wakimpitia kwenye hema hiyo na kwa kufanya biashara pia.
Mtume (s.a.w.) na wenziwe walishuka hapo, na wakamtolea salamu bibi huyu na wakamtaka awagawie maziwa kidogo au awauzie ili wakate hamu yao. Yule bibi alisikitika sana akawaambia: “Hapana chembe ya maziwa nyumbani kwetu leo, wala hapana mbuzi wa kukama hapa. Mbuzi wote wamekwenda machungani. Tena siku hizi ni za taabu kubwa, majani yamekuwa haba kwetu kwa ajili ya uchache wa mvua, kwa hivyo hatuwezi kupata maziwa ila machache tu ambayo hayatutoshi hata sisi wenyewe, seuze kusalia na kuwapa wapita njia. Tunasikitika kupita watu watukufu kama nyinyi, nasi tukawa hatuna cha kukupeni” Mtume (s.a.w.) alitupa jicho upenuni mwa hema ya yule bibi, akaona kibuzi kidogo king’onda kimesimama kinasinzia kwa ugonjwa. Akamwambia yule bibi: “Si yule mbuzi yupo upenuni pale? Kwanini hatukamii maziwa yake? sisi tutakupa pesa utakazo” Akamjibu: “Wanangu! Mimi sitaki kukukhinisheni maziwa, bure ningekupeni licha kuwa mtanipa pesa, lakini mbuzi yule mnayemwona ni king’onda na mwenye ukurutu tangu kichwani mpaka miguuni, na viwele vyake ni vikavu kuliko kiriba kikavu. Hatoi tone moja la maziwa, hawezi hata kuwafuata wenziwe machungani kwa ajili ya ung’onda wake. Mwendo wake ni wa ‘tata miguu mipya’ tu”. Mtume (s.a.w.) akamwambia: “Utanipa ruhusa nimkame nitazame bahati yangu?” Akamjibu: “Kama utaweza kupata kitu mkame”
Mtume (s.a.w.) akamvuta yule mbuzi akamtoa uwanjani, akavipapasa viwele vyake, na huku anapiga Bismillahi. Muda si muda viwele vilionekana vimejaa maziwa na vimevimba, huneni viwele vya mbuzi mwenye kuzaa karibuni, Mtume (s.a.w.) akachukua chombo akakama akakijaza maziwa tele, akampa bibi yule, bibi akanywa shiba yake. Akakama tena mara tatu, akawapa wale wenziwe aliokuwa nao, na bakuli la tano akanywa yeye mwenyewe. Baada ya hapo akakama bakuli la sita akamwachia yule bibi ili amwekee mumewe atakapokuja. Hapo tena wakashika njia wakenda zao, huku nyuma alikuja mume wa yule bibi, alipoona maziwa alistaajabu sana, akamwuliza mkewe: “Umepata wapi maziwa haya, wala hapana mbuzi anayetoa tone la maziwa?” Mkewe akamhadithia mambo yote yaliyopita siku ile tangu kuja kwa wale mpaka kuondoka kwao, na akamtajia sifa moja moja ya yule bwana aliyemkama mbuzi hata akapata maziwa hayo. Mumewe akamwambia: “Huyo ni mgomvi wa Makureshi tuliyesikia kuwa ametoka Makka. Ningekuwepo hapa nikayaona haya machoni mwangu, ningemwamini papo hapo na nikenda naye endako”. Pamenenwa kuwa bwana huyu na mkewe mwisho wao walikuja kwa Mtume (s.a.w.) Madina wakasilimu. Jina la bibi huyu lilikuwa Bibi Aatika na la mumewe ni Bwana Aktham1.
Tumeona katika milango iliyopitwa kuwa Makureshi walitoa ilani kuwa watampa ngamia 100 yoyote atakayemkamata Nabii Muhammad (s.a.w.) akamleta kwao Makka, kwa hivyo kila shujaa alivaa barabara, akatoka kumfuata, kila mtu na mkuki na upinde na mshare, juu ya farasi wake, kila mmoja katika hawa anataka yeye awe na hishma hiyo ya kumkamata Mtume (s.a.w.), hata siku ya Jumaatano siku ya tatu toka kutoka pangoni, shujaa mmoja aliyekuwa akiitwa Suraqa2 alipata habari ya mahali alipo Nabii Muhammad. Akavalia pale pale akawafuata kwa kunyemelea mpaka akawaona hakuwahi kupiga shoti3 mbili tatu ila yule farasi wake aliteleza akaanguka. Baada ya kumwinua alitwaa vijiti vyake vya kupiga bao4 akapiga, vikamwonyesha kumkataza kuwatafuta, lakini alivikhalifu akamtoa shoti tena farasi wake. Pele pele akajikwaa tena, lakini akajizoazoa juu ya yule farsi akainuka. Bwana huyu akapiga bao lake mara ya pili, nalo likamkataza tena, lakini akalikhalifu akamtoa mbio farasi wake, hata alipokuwa karibu na kuwafikilia, miguu ya farasi wake ilitumbukia ndani ya ardhi akazuilika hawezi kuchopoka. Hapo akapiga makelele ya kutaka amani, na Mtume (s.a.w.) akampa, pale pale akachopoka akasimama pembezoni mwa Mtume (s.a.w.). Suraqa akamwambia Mtume (s.a.w.): “Mimi nina yakini kuwa jambo lako hili litatangaa, na litaenea Bara Arabu yote, basi nataka unipe barua yako ya amani ambayo nikimwonyesha mtu wako yoyote atanipa amani na atanisaidia, mimi nachukua ahadi kuwa sitamjulisha mtu yoyote habari yenu mpaka mfike mnakokwenda na nitampoteza kusudi anayetaka kukufatieni kwa njia hii” Mtume (s.a.w.) akaamrisha aandikiwe barua hiyo ya amani. Tena wao wakashika njia yao ya kwenda Madina na Suraqa akashika njia yake ya kurejea kwao.
Baada ya siku mbili tatu Suraqa alikutana na Abu Jahl. Alipomwuliza habari ya Mtume (s.a.w.), alimjibu kuwa yeye hajui. Lakini Abu Jahl alimshika sana na akamyakinishia kuwa yeye ana yakini kwamba Suraqa amemfuata Mtume (s.a.w.). Mwishowe Suraqa alimkiria haya na akamhadithia yote yaliyomfika farasi wake, na akamtaka yeye Abu Jahl asilimu pia kama alivyosilimu yeye, kwani Nabii Muhammad (s.a.w.) ni Mtume wa haki. Abu Jah alimjibu akamwambia: “Masikini roho yako! Ndiyo kwanza sasa unajua kwamba Muhammad ni Mtume wa haki? Mimi tangu zamani najua kuwa ni Mtume wa haki lakini sitaki kumfuata tu. Kwanini kila utukufu wawe nao Bani Hashim peke yao? Bani Hashim wametoa watukufu na sisi Bani Makhzum tukatoa. Wakatoa mashujaa na sisi tukatoa, na wakalisha tukalisha. Hata leo walipokuwa farasi wao na wetu wanagusana magoti kwa kukaribiana anatokea kwao Mtume (s.a.w.) aliyeletwa na Mungu! Wallahi sitamfata. Tutapata wapi sisi Mtume (s.a.w.) wa kumlinganisha na wao? Basi kwa hivyo sitamwamini tukapata kuwapa cheo hiki Bani Hashim peke yao”.
C. KUWASILI MTUME (S.A.W.) MADINA

Watu wa Madina walipata habari kuwa Mtume (s.a.w.) ametoka Makka na anakuja Madina. Wakawa kila siku wanatoka nje ya Madina ili kumlaki huko huko kwenye viunga vya Madina kabla ya kuingia mjini. Ikawa kila siku kazi yao ni kwenda viungani kumngoja Mtume (s.a.w.) mpaka jua likiwa kali sana hurejea makwao.


Baada ya kuachana na Suraqa Mtume (s.a.w.) alikutana na msafara mdogo wa biashara wa Kikureshi ambao ndani yake walikuwemo Bwana Talha na Bwana Zubeyr. Mabwana hawa wakawatafutia nguo nzuri mno katika nguo walizotoka nazo Sham, wakampa Mtume (s.a.w.) na Sayyidna Abubakr. Nguo zenyewe zilikuwa nyeupe tupu. Nguo nyeupe tupu ndizo alizokuwa Mtume (s.a.w.) akizipenda kuzivaa na wakiwakafinia maiti wao.
Walipokaribia Madina, Mtume (s.a.w.) na Sayyidna Abubakr walikoga wakajinadhifisha na wakabadilisha nguo zao za safari kwa zile nguo mpya walizopewa na Bwana Talha na Bwana Zubeyr. Hata Jumaatatu mwezi 121 Mfunguo sita – 20 Sept. 622 – wakati wa mchana yaliwadhihirikia majumba ya Qubaa – kiunga kiliyopo kiasi cha meli 2 kusini ya Madina – . Siku hii vile vile Waislamu wa Madina walitoka nje ya mji – kiungani – kumngojea, walimngoja muda mrefu hata jua lilipokuwa kali walirejea, kama walivyokuwa wakifanya kila siku. Hata kadiri ya saa tano hivi Yahudi mmoja alipokuwa akienda kwenye konde yake aliona ngamia watatu wanakuja na wamepandwa na watu wane, akakata kuwa hao ndio Nabii Muhammad (s.a.w.) na wenzake, alikwenda upesi juu ya jabali lililokaribu yake akapiga ukulele kwa mwisho wa sauti yake akisema: “Ee Bani Qayla! Huyo mtu wenu anakuja! Huyo mtu wenu anakuja!” Hili jina la Bani Qayla ndilo jina ambalo zikiitwa kabila mbili za Aus na Khazraj zinapochanganyishwa pamoja, na kila moja katika kabila hizi ilikuwa imegawika kwa matumbo mengi, kama tutakavyoona.
Hakuwahi Yahudi huyu kumaliza wito wake ila kila mwenye kumsikia aliiacha kazi yake, akawa anakimbilia upande uliokuwa ukija wito huo, na huku yeye naye anawalingania wenziwe. Watu wa Madina wote walikimbilia huko Qubaa, lakini hawakuwahi kufika wote ila Mtume (s.a.w.) alikuwa kesha kuwasili Qubaa, – mkukuu huko mbele ya wenyeji wake Bani Amr – tumbo katika kabila ya Aus. Alifikia nyumbani kwa Bwana Kulthum bin Hadm1 – bwana mkubwa wa tumbo la Bani Amr na tajiri wao wote – Bwana huyu siku hiyo hakuwa Mwislmu bado, alikuwa katika dini yao ya zamani. Lakini siku zile zile alisilimu. Mtume (s.a.w.) alipumzika hapo Qubaa muda wa siku 4 – Jumaatatu, Jumaane, Jumaatano na Alkhamis –. Siku ya Ijumaa akenda zake Madina, muda wa siku hizi 4 alizokaa Qubaa baraza yake ilikuwa nyumbani kwa Bwana Saad bin Khaythama – mjane na tajiri wa Bani Amr wote – Siku ya pili ya kufika kwake Qubaa alitoa amri ujengwe msikiti hapo, lakini msikiti haukuwahi kwisha ila Mtume (s.a.w.) aliaga kwenda zake Madina. Huu ni msikiti wa mwanzo uliojengwa na Waislamu.
Asubuhi ya Ijumaa mwezi 16 Mfunguo sita – 24 Sept. 622. – Mtume (s.a.w.) aliondoka Qubaa na shangwe kubwa kwenda mjini Madina2, sala ya Ijumaa ilimkuta njiani, kwenye mtaa wa Bani Salim bin Auf – tumbo katika Bani Khazraj – Akashuka hapo akasali Ijumaa na jeshi lake lote, hii ndiyo sala ya mwanzo ya Ijumaa Mtume (s.a.w.) kuisali, hawakuwa wakisali sala hii walipokuwa Makka. Wakisali rakaa za Adhuhuri tu. Hata walipokwishasali. Mtume (s.a.w.) alipanda ngamia wake kwenda Madina. Bani Salim walimwomba sana asalie kwao lakini Mtume (s.a.w.) aliwashukuru na akawaambia: “Ngamia huyu ameamriwa na Mungu atue mahali anapopenda (Mungu). Basi popote atakapotua ndipo nitakapofanya makazi yangu”. Mtume (s.a.w.) akashika njia kwenda zake huku watoto na wanawake wa Kimadina wanapiga vidafu (duf) na wanatumbuiza. Kila tumbo alilokuwa akilipitia lilikuwa likimwomba kukaa kwao, Mtume (s.a.w.) akilijibu jawabu yake ile ile, na wakati wote huo tangu alipotoka kwa kina Bani Salim bin Auf, alikuwa ameziwachia khatamu za ngamia wake ili atue atakapo huyo ngamia. Matumbo aliyokutana nayo na yakamwomba kukaa kwao ni:-
1. Bani Salim. 2. Bani Bayadha. 3. Bani Saida. 4. Bani Adiy bin Najjar. – kabila ya mama wa babu yake, Bwana Abdul Muttlib, Bibi Salma bint Amr –. Hata alipofika mtaa wa (5) Bani Malik bin Najjar, yule ngamia alipiga magoti kwenye nyumba ya Sahaba mmoja – Bwana Abu Ayyub –Pale pale aliruka yule Bwana Abu Ayyub akachukua mizigo yote iliyokuwa juu ya mgongo wa ngamia akaingia nayo ndani kwake. Papo hapo yule ngamia akaondoka akapiga magoti kwenye kiwanja kikubwa mbele ya nyumba ya bwana huyu Abu Ayyub, Mtume (s.a.w.) akaamrisha kinunuliwe kiwanja hicho ili ajenge nyumba zake na msikiti mkubwa kwa ajili ya watu wote. Naye akashukia nyumbani kwa Bwana Abu Ayyub.
D. MJI WA MADINA
Madina ni mji ulioko kiasi cha meli 300 kaskazini ya Makka, nao ulikuwa na neema zaidi kuliko Makka, kwani ulikuwa una baadhi ya viziwa na vijito vidogovidogo. Kwa hivyo ulikuwa ukiogopwa na Waarabu wengine kwa homa zake za “Malaria”, wakazi wake walikuwa baina ya watu 2,500 mpaka 3,000, kabla ya Mtume (s.a.w.) na watu wake waliokuwa Makka hawajenda huko. Idadi ya hao waliotoka Makka pamoja na Mtume (s.a.w.) haikuzidi kuliko watu 300 na kitu. Hao wenyeji wa asili wa Madina Mtume (s.a.w.) aliwapa jina la “Ansar” – wenye kunusuru dini ya Mwenyezi Mumgu na Mtume wake (s.a.w.) – na waliokuja kukaa Madina aliwapa jina la “Muhajirin” – wenye kuhama kwao. Yaliachwa majina ya kabila zao, Quran ilipokuwa ikiwataja, ilikuwa kabisa haiwataji ila kwa majina haya, hapajakuwa tena Bani Aus au Bani Khazraj, wala Bani Makhzum au Bani Asad. Kwani majina haya yakitajwa mara kwa mara yatawakumbusha khasama zao zilizokuwa hazishi maisha. Katika Quran walikuwa wakitangulizwa “Muhajirin” kisha wakitajwa “Ansar” kwahivi inaonyesha ya kuwa hiyo daraja ya “Muhajir” ilikuwa bora zidi kuliko daraja ya “Ansar”.
E. KUKAA MTUME (S.A.W.) NYUMBANI KWA BWANA ABU AYYUB
Nyumba ya Bwana Abu Ayyub ilikuwa na tabaka mbili, juu akika yeye mwenyewe na chini akikaa Mtume (s.a.w.) na mkewe – Bibi Sawda – mkewe wa peke yake siku hizo. Bwana Abu Ayyub alimwomba sana Mtume (s.a.w.) akae tabaka ya juu, na yeye na mkewe wakae chini, lakini Mtume (s.a.w.) alikataa kabisa, akamwambia: “Mwenye nyumba yake ni mwenye kustahiki zaidi kukaa juu kuliko mkaribishwa, na vile vile hapa chini patakuwa pepesi kwa wanaokuja kuzungumza na mimi” Bwana Abu Ayyub aliridhia kwa hayo. Mtume (s.a.w.) na mkewe wakakaa nyumbani kwa Bwana Abu Ayyub miezi 7 – muda wa kumalizika kujengwa msikiti na nyumba zake – . Muda wote huu aliokuwa akikaa nyumbani kwa Bwana Abu Ayyub, chakula chake kikitoka kwa Bwana Saad bin Ubada, na Bwana As’ad bin Zurara – mabwana wakubwa wa Kiansar – Yule Bwana Saad bin Ubada mkubwa wa Bani Khazraj na huyu Bwana As’ad bin Zurara mkubwa wa Bani Aus.
Bwana Abu Ayyub aliishi muda mrefu baada ya kufa Mtume (s.a.w.), hata aliwahi kuwamo katika jeshi alilolipeleka Bwana Muawiya kuipiga “Byzantium Empire” akafa karibu na mji wa Constantinopie mwaka 52 A.H. – 673 – na mpaka leo kaburi lake lipo hapo linazuriwa. Jina lake khasa Bwana huyu ni Bwana Khalid bin Yazid Al Khazrajy – katika tumbo la Bani Malik bin Najjar – .
F. KUJENGWA MSIKITI WA MADINA NA NYUMBA ZAKE

Kile kiwanja alichokitaka Mtume (s.a.w.) kukinunua kilikuwa kiwanja cha mayatima 2 – Sahl na Suheyl – wamekitrithi kwa mzee wao. Mtume (s.a.w.) akataka kutiliwa thamani yake, Ansar wakakataa kabisa, wakasema kuwa wao watawalipa hao vijana thamani yake, lakini Mtume (s.a.w.) hakukubali bali alimwamrisha Sayyidna Abubakr akinunue kwa pesa zake, tena ampe Mtume (s.a.w.) ajenge msikiti na nyumba zake. Sayyidna Abubakr akakinunua kwa dinar 10 (kadiri ya paund 5 na kitu). Uwanja wenyewe ulikuwa mkubwa sana, na Mtume (s.a.w.) alichagua kipande cha yadi 50 kila upande kiwe ndicho cha msikiti wake.


Masahaba wote wakaingia katika kazi hii ya kujenga msikiti – hapana mmoja aliyesalia – si katika Muhajir wala Ansar, hata yeye mwenyewe Mtume (s.a.w.) alikuwa akichukua mchanga na matufali pamoja nao, na huku akiitikia pamoja nao beti 2 walizokuwa wakiziimba kwa pamoja, baada ya kumaliza beti zao Mashairi wakubwa waliokuwa wakiimba nyimbo za kuwatia watu hima. Beti mbili zenyewe ni hizi:-

Hapana maisha mema * ila hayo ya Qiyama

Rabi wape Ansari * na Muhajiri rehema
Ilichukua miezi 7 tangu kuanza kujengwa msikiti huo mpaka kwisha kwake, mjengo wake ulikuwa namna hii: Ulitomewa kwa matufali na ukasakafiwa kwa mapongoo na makuti ya mtende, na ardhi yake ilikuwa mchanga mtupu bila ya kutandikwa matufali wala majamvi. Walitobolewa milango 4, mlango mmoja kila upande, lakini haujakuwa na alama ya kibla, kama inavyokuwa nayo misikiti ya sasa, kwani huku kutia alama za kibla (mihirabu) kwenye misikiti kumeanza wakati wa Dola ya Bani Umayya. Urefu wake kwenda juu ulikuwa kadiri ya yadi 4, na ndani ulikuwa na vipia (columns) ya vigingi vya magogo ya mitende ambayo watu wakivielekea wanaposali sala za Suna. Mtume (s.a.w.) kasema kuwa thawabu za sala moja katika msikiti wake huu ni kiasi cha thawabu za sala 1,000 katika misikiti mingine, ila ule wa Makka, kwani huo ni bora zaidi kuliko wa Madina1. Kiwanja kilichokuwa kimeachwa wazi upande wa mashariki, kilitumia kwa kujengewa vijumba vya wakeze Mtume (s.a.w.) na vya wanawe.
Aliamrisha vijengwe vijumba 3 kwanza, kimoja cha mkewe Bibi Sawda, cha pili cha Bibi Aysha – ambaye ilifungwa ndoa yake tu Makka ikafanywa arusi yake baada ya kuhama nyumbani kwa Bwana Abu Ayyub, na cha tatu kilikuwa ni cha watoto wake waliokuwa wajane bado, nao ni Bibi Ummu Kulthum na Bibi Fatma na wanaowatazama. Nafasi iliyosalia aliitumia kwa kujenga vijumba vipya kila akioa mke mwengine. Vijumba hivi vilikuwa na urefu na upana wa yadi 4 tu kila upande. Nyumba zote nyengine za Mtume (s.a.w.) alizowajengea wake wengine zilikuwa za namna hii hii, za yadi 4 mraba. Na ima zilikuwa na chumba kimoja na ukumbi, jiko na choo, au zilikuwa na chumba kimoja tu na choo na upenu wa kupikia.


Yüklə 0,69 Mb.

Dostları ilə paylaş:
1   2   3   4   5   6   7   8   9   10   ...   15




Verilənlər bazası müəlliflik hüququ ilə müdafiə olunur ©muhaz.org 2024
rəhbərliyinə müraciət

gir | qeydiyyatdan keç
    Ana səhifə


yükləyin