Mungu ndiye aliyewaua1
Baada ya kwisha kumalizwa kutiwa kisimani. Mtume (s.a.w.) alisimama kwenye ukingo wa kile kisima akawa anaweta mmoja mmoja kwa majina yao. Alikuwa akisema hivi: “Utba! Shayba! Walid bin Utba!” Na kadhalika “Mmekwisha yakinisha kuwa yale niliyokuwa nikikwambieni kuwa ni kweli? Ama sisi tumekwisha kuona kuwa ni kweli” Sayyidna Umar alimwambia Mtume (s.a.w.): “Unawasemesha maiti?” Mtume (s.a.w.) akamwambia: “Hamkuwa nyinyi mnasikia zaidi kuliko wao, wanasikia kila ninalowaambia lakini hawawezi kusema tu2”
Alipokwisha kusema maneno haya, Mtume (s.a.w.) aliletewa habari kuwa Bwana Abu Hudhayfa bin Utba amekaa kwa unyonge, na kuwa labda kwa ajili ya kusimangwa baba yake pamoja na wale maiti wengine wa Kikureshi waliosimangwa. Mtume (s.a.w.) akamwita Bwana Abu Hudhayfa akamwambia yale maneno aliyoyasikia. Bwana Abu Hudhayfa akamjibu akamwambia: “La! mimi sikukasirika kwa kusikia baba yangu na ndugu yangu na ami yangu wakisimangwa. Lakini nasikitika kumwona baba yangu kafa katika ukafiri. Nalikuwa nikidhani kuwa hapana katika wakubwa wa Kikureshi mwenye akili kuliko yeye, kwa hivyo nikitaraji kuwa mwisho wake lazima atasilimu, akili yake kubwa itamwonyesha ukweli wa dini ya Kiislamu na upotofu wa dini ya masanamu. Lakini leo nimekwisha kukata tamaa. Hasha! Mimi sitawaonea uchungu makafiri waliotufanya yale” Siku hiyo ya vita vya Badr Masahaba walisahau nasaba zao, ujamaa ulikuwa wa dini tu. Hata baadhi ya Masahaba walipigana na baba zao au ndugu zao au watoto wao, na wengine waliwaua khasa.
Baada ya haya Mtume (s.a.w.) na Masahaba zake wakaondoka kwenda Madina pamoja na mateka wao 70. Walipofika Madina Mtume (s.a.w.) aliwataka shauri Masahaba nini wafanye juu ya mateka hao, Sayyidna Abubakr akambwambia Mtume (s.a.w.): “Hawa ni ndugu zako na labda Mungu atawaongoa siku zizi hizi za karibu, basi mimi naona bora kuwatoza kila mmoja kikomboleo makhsusi, khalafu muwaache wende zao.” Sayyidna Umar akamwambia Mtume (s.a.w.): “Shauri iliyobora ni kuwachinja wote” Mwamrishe ami yako Hamza amchinje ndugu yake – Abbas bin Abdul Muttalib – umwambie ndugu yako Ali amchinje kaka yake – Aqil bin Abi Talib – na kila mtu umwamrishe amchinje jamaa yake”. Mtume (s.a.w.) akafuata shauri ya Sayyidna Abubakr, na akamwambia: “Wewe Abubakr unamshabihi Nabii Ibrahim na Nabii Isa katika upole wao, na wewe Umar unamshabihi Nabii Nuh na Nabii Musa katika ukali wao”.
Tena Mtume (s.a.w.) akamtajia kila mmoja katika mateka kiasi cha fedha zinazompasa kutoa ili aachiwe kwenda zake. Ama waliokuwa maskini na hawana cha kujikombolea – wakawa wanajua kuandika – kila mmoja alipewa watu 10 kuwafundisha kuandika, wakisha kujua wende zao, na wale ambao walikuwa maskini na wala hawajui kuandika Mtume (s.a.w.) aliwapa ruhusa vivi hivi wende zao.
Mtume (s.a.w.) alimwambia kila Sahaba anayejiweza amchukuwe mmoja katika hao mateka akakae naye kwake kwa kula na kunywa mpaka waje watu wake wamkomboe. Masahaba hawa waliwatazama vizuri wageni wao hata wenyewe wale mateka yakawajia mapenzi ya kuipenda dini hii ya Kiislamu, na siku zile zile wakaingia, miongoni mwao alikuwa Bwana Abbas bin Abdul Muttalib, Bwana Aqil bin Abi Talib, Bwana Saib bin Yazid, Bwana Shafi bin Saib, hawa wawili wa mwisho ni mababu wa Imam Shafi.
Katika mateka wa siku hiyo alikuweko mkwewe Mtume (s.a.w.) kwa mwanawe mkubwa Bibi Zaynab. Bwana huyu alimzuilia huyu Bibi Zaynab kumfuata baba yake kwenda Madina. Basi alipotekwa Mtume (s.a.w.) alimwambia: “Kikomboleo chako ni kumleta mwanangu. Basi umekubali kuchukua ahadi ya kwenda Makka ya kumleta mwanangu?” Yule bwana akatoa ahadi na Mtume (s.a.w.) akamwachia ende zake Makka. Alipofika huko alimfanyia safari nzuri mkewe na akampa mtu wa kufuatana naye mpaka Madina. Lakini njiani walipingwa na Makureshi. Wakamtaabisha yule bibi sana mpaka akaanguka juu ya ngamia aliyekuwa kampanda.
Makureshi walijizuilia siku nyingi na kuja kuwakomboa watu wao, kwa ajili wakiona udhalilifu kufanya hayo. Lakini khatimaye walikuja kuwakomboa. Waislamu walipata kiasi cha shillingi 10,000 katika vikombolea hivyo, wakazitumia katika kununulia silaha na kwa mambo mengine. Makureshi walivunjika sana kwa vita hivi na wakauchukia zaidi Uislamu, wakatia niya mwaka wa pili kuja na jeshi kubwa zaidi mara 3 kuliko hili, ili walipize kisasi. Kwa hivyo walimlazimisha kila tajiri katika matajiri wao atoe kitu kikubwa katika kutengeneza hivyo vita.
Tangu siku hii ndipo alipopata ukubwa Abu Sufyan – baba yake Bwana Muawiya – na wengineo waliokuwa wadogo zamani, kwani wakubwa wao wote waliuawa siku ya vita vya Badr. Hata Shairi wao mmoja aliwatukana hawa wakubwa wapya akasema hivi:-
Sasa mekuwa wakubwa * Ambao wasingekuwa
Wamepata unasaba * Taadhima na murua
Lau kuwa si misiba * Ya Badr kuingia
Wasingeonja ukubwa * Licha kututawaliya.
Vita vya Badr vilipiganwa mwezi 17 Ramadhan 2 A.H. – January 624 –.
B. VITA VYA UHUD
Uhud ni mlima ulioko meli 3 kaskazini ya Madina, mahali hapa ndipo palipopiganwa vita hivyo vinavyoitwa vita vya Uhud, ambavyo ndivyo vita vya pili vikubwa baada ya vita vya Badr.
Tumeona katika mlango uliopita kuwa Makureshi walishindwa sana katika vita vya Badr, na wakapata aibu kubwa, hata wakaazimia kulipa kisasi mara watakapopata nguvu tu. Basi mara tu walipopata nguvu hizo, Makureshi walitoka Makka kuja kuishambulia Madina, kwa jeshi la watu 3,000. 700 katika hao walikuwa wenye kuvaa nguo za chuma. Pamoja na hawa Makureshi 3,000 waliongezeka watu 70 katika Aus ambao walikuwa wakiuchukia mno Uislamu, hata wakahama katika mji wao wa Madina wakenda kukaa Makka. Kila jamadari mkubwa wa Kikureshi alikuja vitani pamoja na mkewe, ili apate kumtia nguvu kupiganisha vita kwa uzuri. Wakawa wanawake wote waliohudhuria vita hivi ni 15. miongoni mwa majamadari wa Kikureshi siku hiyo walikuwa Bwana Khalid bin Walid, Bwana Amr bin Al As, Bwana Ikrima bin Abu Jahl na Bwana Safwan bin Umayya, – ambao wote mwisho wao walisilimu wakawa Majamadari wa Kiislamu – jeshi hili lilichukuwa farasi 200 wa kupigania na ngamia 3,000 wa kupanda.
Mtume (s.a.w.) hakusikia habari ya hao Makureshi ila walipokuwa wamekwisha kukaribia Madina. Akafanya shauri upesi upesi, akatoka na watu 1,000 kwenda kukutana na hilo jeshi la Kikureshi lenye watu 3,000 na zaidi. Walitoka jioni ya Ijumaa mwezi 11 Mfunguo mosi mwaka wa 3 A.H. na mwezi wa January 625. Walipofika hapo kwenye jabali la Uhud walitua kulingoja jeshi la Makureshi. Usiku jeshi la Kikureshi liliwasili na likakabiliana na la Waislamu. Lakini wakapeana muda wapigane mchana.
Alfajiri ilipoingia Mtume (s.a.w.) alisali jamaa na watu wake wote 1,000. ndani ya sala watu 300 walikimbia pamoja na mkubwa wao aliyekuwa akiitwa Abdalla bin Ubay bin Salul. Huyu Abadalla alikuwa Mwislamu wa uwongo, na nyuma yake alikuwa na chungu ya watu waliokuwa wakijidhihirisha mbele ya Mtume (s.a.w.) kuwa wao ni Waislamu, ijapokuwa Mtume (s.a.w.) na Mashaba zake wakubwa walikuwa wakiwajua, lakini walifanya kama kwamba hawawajui. Wakiwacheza shere na wakiwabeza, na wenyewe hawana habari. Baada ya kurejea hao, Mtume (s.a.w.) alisalia na watu 700 tu kulikabili jeshi la wtu 3,000.
Mtume (s.a.w.) alichagua watu 50 katika hao akawaweka kwenye njia za huo mlima wa Uhud, ili baadhi ya jeshi la Makureshi lisiwajie kwa nyuma wakawa wamo katikati. Akawaekea mkubwa wao aliyekuwa akiitwa Bwana Abdalla bin Jubayr na akawaamrisha kamwe wasiondoke mahali pao hata wakiwaona wenzao wameshinda au wameshindwa. Hawana ruhusa kuondoka ila watapoletewa mjumbe anayetoka kwa Mtume (s.a.w.) kuwaamrisha hivyo. Baada ya kwisha kuamrisha haya, Mtume (s.a.w.) alimchagua Bwana Mus’ab bin Umeyr akamate bendera ya Waislamu, awe jamadari mkubwa apiganishe. Huyu ndiye yule mwalimu wa awali aliyepelekwa Madina kufundisha watu dini. Tena zikajipanga safu za Waislamu, tayari kutiana mikononi na Makureshi.
Waarabu walikuwa hawapigani ila na huku mmoja wao kanyanyua bendera, ikianguka chini – wala asitokee mtu wa kuiokota – pale pale hutawanyika nao wakakimbia. Makureshi walikuwa na dasturi ya kuwaachia Bani Abdid Dar kushika bendera yao wakati wa vita, ila wenyewe Bani Abdid Dar wakiridhia kupewa mtu mwengine, kwa kuwa hapana kwao aliye shujaa na moyo mgumu kuliko huyo. Kwahviyo ndiyo maana Mtume (s.a.w.) akampa bendera mtu aliye katika ukoo wa Bani Abdid Dar, naye ndiye yule Bwana Mus’ab bin Umeyr – Sahaba wa awali aliyepelekwa Madina kufundisha watu dini – .
Baada ya hapa wakatiana mikononi, mtu wa kwanza kuuawa katika Makureshi ni Bwana mkubwa wao wa Kibani Abdi Dar – Talha bin Abi Talha – , aliyekuwa kakamata bendera, alipoanguka chini tu mara ndugu yake – Uthman bin Abi Talha – akainyanyua akawa anapiganisha kama alivyokuwa akifanya kaka yake. Hakuchukua muda ila naye pia akauawa1, mara akaruka ndugu yao wa tatu – Abu Said bin Abi Talha –, akaikamata kupiganisha kama walivyofanya kaka zake, naye yakamfika yale yale yaliyowapata ndugu zake2. Ndugu 3 wote wamekwisha kuuawa. Sasa vita vikawa vinapiganishwa na watoto wa yule Jamadari wa kwanza, na wao wakauawa mmoja mmoja. Walipokwisha mabwana nao ni:-
1. Musafi’i bin Talha1.
2. Harith bin Talha.
3. Kilab bin Talha2.
4. Julaas bin Talha3.
Walipokwisha wakubwa wa nyumba hii walikama bendera mabwana wakubwa wengine wa ukoo huu wa Kibani Abdi Dar, na wao vile vile wakauawa. Hapo tena hakutoka yoyote kuiokota katika Bani Abdi Dar, bali waliiacha inagaragara juu ya mchanga inatafuta wa kuiokota katika Bani Abdi Dar haimwoni! Mwisho wake akainuka mwanamke mmoja - Amra bint Alqama Al Harithiyya – akaikamata akapiganisha, lakini pale pale aliuawa, akaifariki Dunia kama walivyoifariki wenziwe. Baada ya hapa hakuinuka yoyote kuiokota, bali walikimbizana mbio kama kundi la mbuzi lenye kufunguliwa zizini, wakawa Waislamu wanawafuata kwa kuwauwa na kukusanya walivyoviacha na walivyovitupa.
Wale Masahaba 50 ambao Mtume (s.a.w.) aliwaweka kwenye njia za mlima wa Uhud ili baadhi ya jeshi la Kureshi lisiwajie kwa nyuma, walipoona wenzao wanalifukuza mbio jeshi kubwa la Kikureshi, na wao waliteremka mbio ili wawemo katika kukusanya ngawira. Mkubwa wao aliwakataza sana na akawakumbusha maneno ya Mtume (s.a.w.), lakini wapi! Hawakumsikiliza bali walitoa tafsiri zao chungu kuyafasiri maneno hayo ya Mtume (s.a.w.) ili wasiwe wameyapinga. Kila mmoja ametoa tafsiri yake na huyo anakwenda zake kuchanganyika na jeshi kubwa, hawakusalia juu ya njia hizo za majabali ila yule mkubwa wao pamoja na 11 tu hivi.
Majamadari wa Kikureshi katika kukimbia kwao, waliona kuwa wale wapigaji mishare waliokuwako majabalini wameondoka. Pale pale waligeuza baadhi ya majeshi yao ili yaje nyuma ya majeshi ya Waislamu ili wapate kuwatia katikati. Jamadari Kahalid bin Walid na Ikrima bin Abu Jahl waliwajia Waislamu kwa nyuma na wale Majamadari wengine waliyageuza majeshi yao wakayakabili majeshi ya Kiislamu. Hapo ukaingia mtaharuki kwenye majeshi ya Kiislamu! Yasijue yanafanya nini, yakawa yanapigwa mbele na nyuma, na yakawa yanauana wenyewe kwa wenyewe bila kujuana kwa hivyo wakafa wengi.
Katika mtaharuki huo alizuka shujaa mmoja wa Kikureshi akampiga upanga Bwana Mus’ab bin Umeyr – na huku anamdhani kuwa ni Mtume (s.a.w.) – akamwua papo hapo. Bwana huyu alikuwa amemshabihi sana Mtume (s.a.w.), kwa hivyo yule shujaa aliyemwua aliyakinisha kuwa kamwua Mtume (s.a.w.). Pale pale akapiga ukulele mkubwa kuwa amekwisha kumwua Nabii Muhammad (s.a.w.) – shina la fitna limekatika! – habari hii ilitapakaa upesi kama moto kichakani. Makureshi walifurahi furaha isiyo na mfano. Na Waislamu wakafa nyoyo wakababaika wakarukwa na akili, wasijue la kufanya ni lipi. Baadhi yao walikwenda mbio mpaka Madina! Na baadhi yao kubwa ilisimama kupigana bila ya nidhamu, kila mmoja akipigania nafsi yake, na huku anatafuta njia apenye ende zake, akakutane na wenziwe, ajue nini la kufanya baada ya kuwa Mtume (s.a.w.) amekwisha kufa, kwani waliyakinisha kuwa Mtume (s.a.w.) amekwisha kufa.
Watu wawili watatu tu ndio waliopata bahati ya kuwa na Mtume (s.a.w.) wakati ulipopigwa ukelele ule wa kuonyesha kuwa Mtume (s.a.w.) ameuawa. Watu hawa walijitahidi wawezavyo kumpigania Mtume (s.a.w.) asidhuiriwe, lakini wapi! Aliumia sana na mwisho wake akaanguka shimoni, asiweze kupanda kwa machofu aliyokuwa nayo. Pale pale Bwana Talha akashuka ndani ya shimo, akamweka Mtume (s.a.w.) mabegani mwake akainuka naye. Ukingoni mwa hilo shimo alisimama Sayyidna Ali bin Abi Talib akanyoosha mikono yake ili kumvuta nje Mtume (s.a.w.). Bwana Talha alipoinuka naye tu mara Sayyidna Ali alimvuta nje akamtoa salama. Mtume (s.a.w.) alipotoka nje aliona idadi ya wale Masahaba aliokuwa nao imezidi kuliko ilivyokuwa. Sababu ya kuzidi kwake ni hii: wale Masahaba waliokuwa wakipigania nafsi zao – kwa bahati nzuri – walikutana na wenziwao waliokuwa pamoja na Mtume (s.a.w.), wakawapa habari kuwa Mtume (s.a.w.) hajafa, lakini yupo ndani ya shimo anatolewa na Bwana Talha. Masahaba hawa walifurahi furaha wasiopata kufurahi maisha yao. Masahaba wote hawa waliokusanyika hapa sasa pamoja na Mtume (s.a.w.) ni wanaume 14 na mwanamke 1. 8 katika hawa ni Muhajir na 7 katika Ansar. Watu hawa walijitahidi wawezavyo kumpigania Mtume (s.a.w.), lakini baadhi ya Makureshi walimwona kuwa Mtume (s.a.w.) hajafa walifanya kila jitihadi wamwue.
Mmoja katika Makureshi hao ni Ubay bin Khalaf – ndugu wa Umayya bin Khalaf aliyekuwa akimdhili Bwana Bilal – . Kureshi huyu alikuja juu ya farsi wake – upanga wazi na mwili wake wote umefunikwa na nguo za chuma – huku anasema: “Niachieni nimwue Muhammad” Masahaba wale 15 walifadhaika (walifazaika) walijipaniapania kila upande kumzuia asimfike Mtume (s.a.w.). Mtume (s.a.w.) aliazima kijambia kimoja kidogo kwa mmoja katika Mashaba zake, khalafu akawaambia “Jitengeni niachieni mimi mwenyewe peke yangu!” Masahaba wakajitenga na Mtume (s.a.w.) akajiwinda barabara anamngoja afike sawa yake kufika tu, Mtume (s.a.w.) alimsukumia kile kijambia akamchoma nacho kwenye shingo – nafasi ya peke yake iliyokuwa haikufunikwa kwa nguo za chuma katika mwili wa yule Kureshi – . kuchomwa tu kwa kijambia hicho mara yule Kureshi aligeuza farasi wake akarejea kwa wenzake na huku anapepesuka juu ya yule farasi, na anakaribia kusunukia kwa maumivu anayoyaona. Akawafikia wenzake anahema – pumzi juu juu – na huku anasema: “Muhammad kaniua! Muhammad kaniua!” Huku anaonyesha mahali alipochomwa kwa kile kijambia.
Wenzake wakamcheka sana, wakamwambia: “Hatujapata kukuona kuwa mwoga siku yoyote isiokuwa leo. Mara ngapi tumepata kukuona ukichomwa mishare mwilini mwako na huku unaendelea kupigana! Leo huna chochote ila mkwaruzo wa kijambia, nawe unapapatika kama kuku aliyekatwa kichwa!” yule shujaa akajibu: “Hamjui uchungu wake huu mkwaruzo wa jambia la Muhammad! Wallahi! Lau ungegawiwa uchungu huu ninaouona, akapewa kidogo kidogo kila mtu ulimwenguni wote hao wangelihisi uchungu wake na wakafa. Muhammad alinambia kuwa ataniua, basi hapana shaka kuwa nitakufa. Muhammad hasemi kitu ila huwa tu”. Kabla hakufika kwao Makka huyu shujaa wa Kikureshi alikata roho njiani katika mtaa unaoitwa Sarif – baada ya kusononeka kwa saaa nyingi njiani, na kupiga makelele na mapindi – .
Mtume (s.a.w.) hakupata kumwua mtu yoyote kwa mkono wake ila huyu. Asili ya kumwua yeye mwenyewe kwa mkono wake ni hii:-
Mtume (s.a.w.) alikuwa akitembea siku moja katika mji wa Makka. Njiani alimkuta huyu Ubay bin Khalaf amesimama anamlisha farasi wake ngano! Ubay akamwambia Mtume (s.a.w.): “Unamwona farasi huyu ninayemlisha ngano! Sitakuona nje ya Makka ila nitakuua, nami niko juu yake!” Mtume (s.a.w.) akamwambia: “Inshaallah mimi ndiye nitakayekuua nawe uko juu yake” basi ikawa kama alivyosema Mtume (s.a.w.).
Baada ya Mtume (s.a.w.) kumpiga yule Kureshi, Makureshi wengine – waliopata kuweza kumwona Mtume (s.a.w.) na zile chembe mbili za Masahaba waliokuwa pamoja naye, walifanya kama walivyoweza wampate Mtume (s.a.w.) wamwue, lakini wale Masahaba zake walimzunguka kila upande, husemi nyuki wanvyozunguka sega lao la asali. Masahaba hawa walipigana kwa ushujaa mkubwa usiopata kuonekana, hata wengine walipatwa na vilema vibaya vibaya ambavyo viliwaganda maisha yao. Katika ghasia hizi za kumwania Mtume (s.a.w.) lilikuja jiwe la Kureshi mmoja aliyekuwa akiitwa Utba bin Abi Waqqas – ndugu yake jamadari mkuu wa Kiislamu, Bwana Saad bin Abi Waqqas – likampiga Mtume (s.a.w.) kwenye mdomo wake wa chini kwa upande wa kulia likampasua mdomo na likamvunja baadhi ya meno. Muda si muda Kureshi mwengine aliyekuwa akiitwa Abdalla bin Shihab Az Zuhry – jamaa yake Mtume (s.a.w.) kwa upande wa mama yake – alimvurumishia Mtume (s.a.w.) pandikizi la jiwe likampiga usoni, lakampasua huo uso mpasuo mkubwa, – ukawa unamiminika damu kama mfereji –. Mtume (s.a.w.) hakupona maisha yake na kovu ya jaraha hili la usoni, bali alikufa na kovu yake usoni, ili iwe ushahidi wa mambo yaliyomkuta kwa makafiri wa Kikureshi. Masahaba wachache walipomwona Mtume (s.a.w.) katika hali hii walisikitika sana, wakamtaka awaapize waliomfanya haya. Mtume (s.a.w.) akawajibu akasema: “Mimi sikuletwa ulimwenguni kuja kuapiza, nimeletwa kuwaombea viumbe Maghufira na Rahema”. Khalafu akaomba akasema: “Ewe Mwenyezi Mungu! Nakuomba utoe katika migongo yao vijana watukufu, wasimame kwa jitihada zao zote kuinusuru hii dini, kama wanavyoisimamia wazee wao kuipinga” Mwenyezi Mungu aliikubali dua hii ya Mtume (s.a.w.) akajaalia wengi katika hao kuzaa watoto waliousimamia Uislamu katika kuutangaza kwa Ilimu na mapigano. Imam Zuhry ambaye ndiye ‘Shekhe’ wa Maimamu wote 12 wa Kisunni ni mjukuu khasa wa yule Kureshi aliyempasua uso Mtume (s.a.w.) siku hii ya vita vya Uhud.
Makureshi walipoona panga zao haziwezi kumfikilia Mtume (s.a.w.) hata chembe, kwa kuwa kazungukwa na watu wake kila upande, walichafuka kumpopoa kwa mawe, baada ya kupasuliwa uso kinywa na kuvunjwa jino yaliendelea mawe yao kumjia kama mvua, hata mwisho wake likamjia jiwe kubwa likampondeapondea kofia yake ya chuma aliyokuwa kaivaa, na vyuma viwili vya hiyo kofia vikamzama mashavuni! Damu ikamzidi Mtume (s.a.w.) hata akafanya kizunguzungu, akaanguka chini taabani. Masahaba wale wakajikaza wakawafukuza kabisa Makureshi wachache waliokuwa wakiwataabisha. Baada ya hapo wakamtaka Mtume (s.a.w.) aondoke ende pamoja nao kwenye pango la jabali wapumzike, Mtume (s.a.w.) akataka kujiinua lakini asiweze. Bwana Talha akambeba akampandisha kwenye hilo pango, akapumzika hapo kidogo yeye na zile chembe mbili za Masahaba, baada kupumzika kidogo aliinuka Bwana Abu Ubeyda – Bwana mkubwa wa Kisahaba – akamchomoa Mtume (s.a.w.) hiyo misumari miwili iliyokuwa imezama mashavuni. Bwana huyu aling’okwa baadhi ya meno yake kwa kasi za kuivuta misumari hiyo, walipoingia ndani ya pango hili, mara alitokea Bibi Fatma, Bibi Aysha na Mabibi wengine wa Kisahaba ambao walisikia kuwa Mtume (s.a.w.) kauawa, walikuja mabibi hawa ili wapate habari ya hakika, lakini walipofika walimkuta Mtume (s.a.w.) yuhai, wakafurahi sana, Bibi Fatma akaunguza vipande vya majamvi, akapata jivu akambandika nalo Mtume (s.a.w.) katika majaraha yake ya usoni.
Wakati huo wote walikuwa wamekwisha kupumzika, na Makureshi wote wamejikusanya pamoja tayari kuondoka. Mara Masahaba wakasikia sauti ya Abu Sufyan – mkubwa wa Makureshi – inanadi inasema: “Muhammad yuhai au amekufa? Muhammad yuhai au amekufa?” Mtume (s.a.w.) akawaambia Masahaba zake wasimjibu, mara ikanadi tena ikasema: “Abubakr yuhai au amekufa? Abubakr yuhai au amekufa?” pakawa jii1 vile vile, pasipatikane jawabu. Ikanadi mara ya tatu sauti ikasema: “Umar yuhai au amekufa? Umar yuhai au amekufa?” Ilivyokuwa jii vile vile yule Abu Sufyan alisema: “Wallahi! Hawa wote wamekwisha kufa” Sayyidna Umar hakustahamili kusikia haya, alinyanyua sauti akajibu: “Wote hao unaowataja wahai, watayari kukutana nawe na majeshi yako kila wakati” Abu Sufyan akasema: “Katukuka leo mungu mkubwa wetu Hubal! Katukuka leo Mungu mkubwa wetu Hubal! Vita ni mpokezano – siku ya hawa na siku ya wale – na siku hii yetu ya leo ni kwa ile siku yenu ya Badr. Enyi Waislamu! Mtaona katika maiti wenu watu waliokatwakatwa vipande vipande. Mimi sikuamrisha watu wangu kufanya hayo wala sikuwakataza, wala hayakunifurahisha hayo wala hayakunichukiza. Sasa tunakupeni habari yakuwa tunakutakeni tena mwaka wa pili, mwezi wa Shaaban katika mtaa wa Badr.” Mtume (s.a.w.) akamwamrisha Sayyidna Umar amjibu: “Tayari tutakutana hapo” tena akainuka Hind – mke wa Abu Sufyan – akaimba nyimbo zake juu ya jabali lili hili. Baada ya haya Abu Sufyan akaamrisha watu wake washike njia wende zao Makka baada ya kuwazika maiti wao 23.
Baada ya Makureshi kwenda zao Mtume (s.a.w.) na Masahaba zake walishuka kwenda kutazama maiti wao mashahidi, wakaona kuwa watu 74 wamekufa mashahidi – 4 ni Muhajir –. Idadi ya Muhajir ilikuwa ndogo sana siku hiyo kuliko ya Ansar, ndio Mashahidi wao wakawa kidogo. Mashahidi hawa walikuwa wamekatwa vipande vipande, mikono mbali miguu mbali, vichwa mbali na viungo vyengine! Katika waliokuwa wamekatwa vibaya sana ni Bwana Hamza bin Abdul Muttalib – baba yake mdogo Mtume (s.a.w.) na shujaa mkubwa anayepigiwa mfano na Waislmu wote –.
Mtume (s.a.w.) alihuzunika sana kwa kumwona baba yake mdogo huyu katika hali hiyo. Akaapa akasema: “Inshallah na miye nikiwashinda Makureshi mara ya pili nitawakata watu 70 kwa baba yangu mdogo mmoja huyu”. Pale pale ikashuka Aya ya 126 na 127 katika Sura ya 16 (Suratun Nahl) Mungu alimwambia:
Mkitesa teseni kama mlivyoteswa (msiongeze) na mkisubiri (msitese) ndiyo bora zaidi kwa hao wenye
kusubiri (kuliko kutesa)
(Aya ya 126).1
Na subiri wala kusiwe kusubiri kwako ila kwa ajili ya wenyezi Mungu, wala usihuzunike juu yao (wale waliouawa) wala usiwe katika majonzi kwa hayo wanayoyafanya (makafiri) 2
(Aya ya 127).
Ziliposhuka Aya hizi Mtume (s.a.w.) alivunja kiapo chake, akaazimia kuwa hatalipa kisasi tena. Siku ile ile zikashuka Aya za kuwasamehe waliokimbia waliposikia kuwa Mtume (s.a.w.) kauawa, na zikashuka Aya za kuonyesha kuwa wameshindwa safari hii kwa ajili ya kuacha amri ya Mtume (s.a.w.), na wakatakiwa wasiache tena amri yake. Baada ya hapo wakashika njia wakarejea Madina.
C. VITA VYA KHANDAK
Mtume (s.a.w.) alipigana na kabila nyingi za Kiarabu na za Kiyahudi na akazishinda zote kabla ya vita hivi vya Khandak ambavyo vilipiganwa mwezi wa Mfunguo mosi mwka wa 5 A. H. – February 627 –. Asili ya kutokea vita hivi ni hii:-
Wakubwa kabisa watano wa Kiyahudi walitoka wakenda Makka wakawataka wafanye jeshi kubwa la wao Makureshi na wao Mayahudi na sehemu kubwa ya Waarabu waliokuwa wakiitwa Bani Ghatafan, ili wapate kumsaga Mtume (s.a.w.) na watu wake mara moja, Makureshi walifurahikiwa sana na shauri hii ya kwenda kuwasagasaga watu wa Nabii Muhammad, kwani walikuwa hawana adui mkubwa zadi kuliko hawa. Mayahudi hawa 5 wakapatana na Makureshi kuwa vita hivyo viwe katika mwezi wa Mfunguo mosi – mwezi fulani – wawe wamekwishafika Madina.
Baada ya haya wale Mayahudi 5 walitoka wakawendea wakubwa wa matumbo ya kabila ya Bani Ghatafan kuwataka wao wawe pamoja nao na Makureshi, waje kuishambulia Madina kwa umoja wao. Wakubwa hao kwanza walikataa lakini wale Mayahudi waliwapa ahadi kuwa mavuno ya mwaka huo ya nchi yao ya Khaybar yatakuwa yao. Walipowapa habari hii, wakubwa 5 tu wa Kibani Ghatfan ndio waliowatii, wakawapa ahadi ya kuwa watakuwa pamoja nao kuishambulia Madina, na hawatarejea makwao ila baada ya kumsagasaga Mtume (s.a.w.) na watu wake. Basi wale Mayahudi wakawaambia hao Waarabu wawe tayari mfunguo mosi, na mwezi fulani wawe wamekwisha kufika Madina, na wale Waarabu wakaitikia kwa nguvu kuwa watakuwa wamekwisha kufika siku hiyo.
Mtume (s.a.w.) alipopata habari hii ya kuja kushambuliwa kila upande, aliwakusanya Masahaba zake wakubwa akawapa habari hii na akawataka shauri ya kufanya, Masahaba hawa wakashangaa wasijue la kusema. Mara pale pale akaondoka Sahaba mtu mzima wa Kiajemi aliyekuwa akiitwa Bwana Salman Al Farsy akamwambia Mtume (s.a.w.) “Shauri iliyo nzuri ni kuzungusha handaki mji wote wa Madina” Mtume (s.a.w.) akamwambia: “Handaki ndio nini?” Waarabu hawakuwa wakilijua tamko hili wala maana yake, kwani ni tamko la Kiajemi, wala wao Waarabu hawakuwa wakiitumia hila hii katika vita vyao. Aliposikia tafsiri yake Mtume (s.a.w.) alifurahi na akaamrisha lichimbwe hilo handaki lizunguke mji wa Madina katika zote pande zake tatu zilizokuwa ziwazi, ama upande wake wane ulikuwa umezungukwa kwa majumba yalikyokuwa yameshikamana barabara.
Mtume (s.a.w.) aliigawa kazi hii ifanywe kwa ujima wa watu kumi kumi. Kila Masahaba walipewa kuchimba urefu wa dhiraa 40 na upana wa dhiraa 10. Mtume (s.a.w.) alikuwa pamoja nao katika kufanya kazi hii, mchana kutwa wakifanya kazi na usiku wakirejea majumbani mwao. Baada ya siku 6 handaki lote lilikuwa limekwisha kuchimbwa, na Masahaba wako tayari wanawangojea maadui waje, watafute pakupita wasipaone – maadui sasa wako njiani wanakuja –. Mtume (s.a.w.) akaamrisha wanawake na watoto wakakae kwenye ngome mbili tatu zilizokuwa Madina, na yeye na jeshi la watu 3,000 wakatoka wakaja kulizunguka handaki hilo kwa ndani darmadar.
Mara likawatokea jeshi la Abu Sufyan – la Makurehi na waitifaki wao – kwa upande wa kusini. Abu Sufyan alikuja na jeshi la watu 4,000 – la Makureshi na baadhi ya kabila nyengine za Hijaz –. Na pale pale likajimimina jeshi la Bani Ghatafan na baadhi ya kabila zilizo karibu nao, jeshi hili lilikuwa la watu 6,000 likatanda tangu kaskazini mpaka mashariki hata likakamatana na jeshi la Waarabu wa Hijaz. Majeshi haya – kuona lile handaki lililozunguka Madina – yalistaajabu sana yakachukiwa na yakawatukana watu wa Mtume (s.a.w.) kuwa ni woga wanajificha ndani. Lakini kwa hakika woga ni wao! –Watu 10,000 kuja kukabiliana na watu 3,000 tu –. Walijitahidi kila namna wale Waarabu khasa Makureshi kulipindukia lile handaki, lakini hawakuweza, lilikuwa pana sana, lakini baadhi ya watu wachache katika wao waliweza kupindukia wakaja upande waliokuwa Masahaba. Mmoja katika hao – Abdalla bin Naufal Al Makhzumy – alianguka ndani ya hilo handaki akavunjika shingo yake na shingo ya farasi wake, wa pili wao – Amr bin Abd Wud – alifika salama na akakabiliana na Sayyidna Ali, na baada ya muda mchache aliuawa. Huyu Amr alikuwa miongoni mwa mashujaa wakubwa kabisa wa Kikureshi, watatu wao alipigwa mshare akafa. Walipoona hivi wale wenziwao hawakutamani kuliruka tena – kwani walikuona kumoto –. Basi waliridhia kukaa vivyo hivyo nje ya handaki wakirushiana mishare na kupopoana kwa mawe tu.
Katika siku hizi za kuhusuriwa Madina, Mtume (s.a.w.) alionyesha miujiza mingi. Mmoja katika hiyo ni kuwa lilipatikana jiwe moja kubwa sana katika sehemu aliyokuwa akichimba Bwana Salman Al Farsy na wenziwe, jiwe hilo lilipowashinda kulivunja walipanda juu kumpa habari Mtume (s.a.w.). Mtume (s.a.w.) akashuka kwenye hilo jiwe pamoja nao. Alipokwisha kuliona aliagiza aletewe maji kidogo gilasini, alipoletewa maji haya aliyasomea kisha akayamichia kwenye lile jiwe. Baada ya kufanya hivyo akachukuwa mtarimbo akalipiga kwa nguvu, likapasuka pande kubwa na likatoka nuru kama umeme ambayo ilikwenda upande wa kusini, Mtume (s.a.w.) akasema: “Allahu Akbar karibu tutaiteka Yaman iwe yetu”. Akapiga mtarimbo wa pili, ikatoka nuru vile vile kama umeme, ambayo mara hii ilikwenda upande wa kaskazini. Mtume (s.a.w.) akasema: “Allah Akbar! Karibu tutaiteka Sham na miji yote ya Kirumi iliyoko kaskazini”. Sasa akapiga mtarimbo wa tatu, na ukatoka umeme ulioelemea upande wa mashariki. Mtume (s.a.w.) akasema: “Allahu Akbar! Tutauteka Ufalme wote w Kiajemi”. Baada ya mtarimbo huu wa tatu jiwe lilikuwa limekwisha kugeuka mchanga. Bishara hii ya Mtume (s.a.w.) ilipatikana kwa utaratibu wa mpango aliousema. Kwanza ilitekwa Yaman yote katika zama zake mwenyewe Mtume (s.a.w.), kisha zikatekwa nchi za Warumi za kaskazini ya Bara Arabu katika zama za Sayyidna Abubakr na Sayyidna Umar, baadae ukavunjwa ufalme wa Kiajemi katika zama za Sayyidna Umar na Sayyidna Uthman.
Makureshi na wenziwao wao walisalia muda wa zaidi ya wiki tatu wanauhusuru1 mji wa Madina, bila ya kuweza kuingia kwa hilo handaki lililokuwa limeuzunguka mji huo kwa pande zake zote tatu. Ilikuwa hapana njia ya kuweza kuiingia Madina wala kutoka ila katika vichochoro vya ule upande uliokuwa umesaki majumba.
Mtume (s.a.w.) alimtuma mtu ende kwa kificho akamwitie baadhi ya wakubwa wa Bani Ghatafan waliokuwa wanauhusuru mji wa Madina. Wakubwa hao walikuja na Mtume (s.a.w.) akafanya shauri nao kawataka waache kuhusuru na warejee makwao, na Mtume (s.a.w.) atawapa 1/3 ya mavuno ya tende ya Madina ya mwaka huo. Baada ya kusemezana sana, wale wakubwa wa Bani Ghatafan walikubali ile rai ya kwenda zao na jeshi lao la watu 6,000 na kuwacha Makureshi na Mayahudi peke yao wapigane na Mtume (s.a.w.) na watu wake. Kabla hawajaondoka mabwana hawa na shauri hii kuwapelekea wenziwao, Mtume (s.a.w.) aliweta wakubwa wa Kiansar kusikiliza nini rai yao katika sulhu hiyo, kwani Mtume (s.a.w.) alifanya sulhu hiyo kwa ajili ya kuwaonea wao huruma. Ansar wakamwambia Mtume (s.a.w.): “Ikiwa hii si amri ya Mungu wala si amri yako utayotuamrisha wewe kwa rai yako tu, bali ni jambo unalolifanya kwa ajili yetu sisi Ansar tu, basi sisi hatupendi hata kidogo. – Hawa jirani zetu Bani Ghatafan – hawajapata kutushinda wakala tende zetu ngawira siku za Ujahili, watatushinda wale tende zetu ngawira leo, nawe pamoja nasi? Wape habari, Ya Rasula Llah! Kuwa hapana baina yetu na wao ila upanga tu – huo ndio utakaobainisha haki ”. Mtume (s.a.w.) akawambia wakubwa wa Bani Ghatafan: “Mmekwisha kuyasikia maneno ya Ansar, basi jawabu ndiyo hiyo hiyo waliyosema hao”. Wale Maraisi wa Bani Ghatafan wakaondoka wakarejea nje ya handaki – wanangojea wapate fusra nzuri wapate kuushambulia mji huo kufa kupona –.
Baada ya siku tatu hivi tangu kuja yale majeshi alijipenyeza usiku Mwarabu mmoja mtukufu kabisa katika Bani Ghatafan, akaja mpaka kwa Mtume (s.a.w.). Mwarabu huyo alikuwa akiitwa Bwana Nuaym bin Mas’ud, alipofika kwa Mtume (s.a.w.) alitoa salamu, na akamwambia Mtume (s.a.w.) kwa siri maneno haya: “Mungu amenifahamisha ukweli wa dini yako. Basi nakupa habari kuwa mimi ni mmoja katika wafuasi wako, wala hapana yoyote anayejua habri hii isipokuwa mimi na wewe. Basi niamrishe nifanye jambo lolote la kuwaondolea wenzangu taabu hii waliyonayo”. Mtume (s.a.w.) akamwambia: “Wewe ni mtu mmoja tu peke yako utafanya nini? Kama unaweza kufanya kitu basi jaribu kuwagombanisha hawa adui zetu wenyewe kwa wenyewe”. Huyu Bwana Nuaym akaiwafiki rai hii, akamwaga Mtume (s.a.w.) akaondoka akenda zake. Usiku huo ulikuwa wa kiza kikubwa – hapana aliyemwona Bwana huyu wakati alipokuja wala alipoondoka –.
Pale pale aliondoka akawendea wakubwa wa Mayahudi. Akawabishia mlango wa ngome waliyokuwamo, hawa wakubwa wa Kiyahudi na watu wao walikuwa ndani ya mji wa Madina, wakiwangojea Makureshi na Bani Ghatafan walikiuke lile handaki wachanganyike pamoja nao katika kupigana na Waislamu. Bwana Nuaym alipopiga hodi – na wakubwa wa Kiyahudi walipoitambua sauti yake – mara walimfungulia, kwani yeye alikuwa rafiki yao mkubwa kabla hakusilimu. Alipofika ndani wakubwa wote walimzunguka, wakawa wanamwuliza habari. Bwana Nuaym akawaambia: “Nasikitika sana kutoa siri za jamaa zangu. Lakini imenibidi niseme, kwani katika kuitaja siri hiyo pana faida kwenu nyinyi rafiki zangu, na kwa wao pia jamaa zangu. Nimesikia mnong’ono kuwa Makureshi na Bani Ghatafan wanafanya shauri kwenda zao, wakuachieni hapa peke yenu na Muhammad na watu wake watoe kisasi chao chote juu yenu, tusipate tuliyokuwa tukiyataka, naye Muhammad na watu wake wapate waliyokuwa wakiyataka na zaidi. Basi shauri nzuri ninayoiona mimi ni kuwa mwatake Makureshi na jamaa zangu Bani Ghatafan, kiasi cha vijana 30 wawe rahani mikononi mwenu, na muwaambie kwamba hamtawatoa vijana hao mpaka watakapomshinda Muhammad na watu wake. Wakikupeni vijana wao hawataondoka kabisa, ila baada ya kuwashinda na kuwasagasaga hawa adui zetu, na haya ndiyo tunayoyataka sisi Waarabu, na ndiyo mnayoyataka nyinyi Mayahudi. Mayahudi walifurahikiwa sana na rai hii, wakaahidi kuwa watafanya kama walivyoambiwa. Bwana Nuaym akataka wampe ahadi kuwa hawatataja kabisa kuwa yeye ndiye aliyewatajia mnong’ono huu.
Baada ya hapa Bwana Nuaym akenda mbio mpaka kwa Abu Sufyan – mkubwa wa Makureshi – akamwita kipembeni akamwambia yeye pamoja na wakuu wenziwe: “Ipo habari muhimu niliyoiyakinisha sasa hivi, nikakujieni nyinyi upesi hapa, kwani mko karibu, kishga niwaendee jamaa zangu nikawape habari hiyo nao. Habari iliyoko ni kuwa Mayahudi wamejuta kwenda kinyume na Muhammad na kuwa pamoja na nyinyi, kwani wameona mpaka sasa hamkufanya lolote. Kwa hivyo wamekwenda kwa Muhammad kuangukia na kumtaka wawe pamoja naye. Muhammad amekubali, lakini kawataka wamletee vijana 30 watukufu miongoni mwenu na katika Bani Ghatafan, makusudio ya Muhammad ni kuwachinja vijana hawa. Basi Mayahudi wakikutakeni kuwapa watu wowote msikubali kabisa, kwasababu watafanya kama nilivyokuhadithieni, kwani urafiki wao na Muhammad hautapatikana ila kwa kutekeleza haya, na wao kabisa hawawezi kuukosa tena urafiki wa Muhammad.” Wakubwa wa Kikureshi waliyasikiliza vizuri maneno haya, lakini hawakusadiki khasa, bali waliweka majasusi wao kupeleleza zaidi.
Pale pale huyu Bwana Nuaym akawaendea jamaa zake – Bani Ghatafan – akawaeleza kama alivyowaeleza wakubwa wa Kikureshi. Waarabu hao walifurahikiwa na ujasusi wa huyo jamaa yao, lakini walimwambia kuwa hawawezi kuharikisha lolote ila baada ya kuyakinisha zaidi. Baadae wakafanya mkutano wao na wakubwa wa Kikureshi kupeleleza habari hiyo. Yule Bwana Nuaym akasalia huko huko kwa jamaa zake – Bani Ghatafan – kama kwamba hakusilimu wala hakukutana na Nabii Muhammad.
Majasusi wa Kikureshi na wa Bani Ghatafan walijitahidi kupeleleza wasisikie lolote. Hata laasiri ya Ijumaa mwezi 21 Mfunguo pili Waarabu waliona hawawezi kungojea tena, kwani vyakula vyao vilivyobakia ni haba sana, kwa hivyo waliwapelekea habari Mayahudi ya kuwa kesho – Jumaamosi – wawe tayari kutoka kupigana na Mtume (s.a.w.) pamoja nao. Mayahudi waliwajibu Makureshi kuwa jumaamosi ni siku yao ya ibada, hawakuruhusiwa kufanya lolote katika siku hiyo ila ibada tu. Vile vile waliwaambia ya kuwa wao Mayahudi hawatakuwa pamoja nao Waarabu katika mapigano hayo mpaka Makureshi na Bani Ghatafan wawape vijana 30 wawe rahani mikononi mwao, kwani wanaogopa wasije kukimbia hao Waarabu vita vitakaposhika moto, wakawaacha wao peke yao. Makureshi na Bani Ghatafan waliposikia maneno hayo nao walisema: “Ni kweli yale maneno ya Nuaym bin Mas’ud. Hawa Mayahudi ni shauri moja na Muhammad sasa, na wanataka kutula kivuli1. Tutawapelekea habari kuwa hatutawapa rahani ya chochote, licha ya vijana 30 watukufu.” Mayahudi waliposikia maneno haya walinena nao: “Amesema kweli Nuaym. Hawa Waarabu wamekwisha nong’onezana kutuacha sisi peke yetu, tusagwesagwe na Muhammad, tumekwishawagundua.”
Usiku wa jumaamosi ulipoingia uliingia na kiza kikubwa, kwani ulikuwa usiku wa kuamkia mwezi 22, na ukaingia na mingurumo ya radi na pepo kali za dharuba zilizokuwa zikirusha michanga iliyokuwa ikimwingia kila mtu, na ziking’oa mahema na kila kisichonasa barabara juu ya ardhi. Hema za adui zilikuwa zikipeperushwa kila upande, na kilichokuwamo ndani kilipeperushwa na kutawanyika ovyo ovyo, wala wenyewe hawawezi kufumbua macho yao vyema kwa mikondo na mikondo ya huo mchanga uliokuwa ukirushwa. Abu Sufyan alipiga ukulele akasema: “Mimi narejea Makka juu ya ngamia wangu, na kila aliye katika taa yangu2 na arejee, kwani hapana faida ya kusalia hapa.” Kumaliza maneno yake haya kila mtu katika Makureshi na Bani Ghatafan alipanda ngamia wake akashika njia akenda zake, akaacha kila alichokuja nacho. Asubuhi Mtume (s.a.w.) na watu wake walipoamka, waliukuta uwanja mweupe! – hapana ndudu ya mtu – ila vitakataka vyao tu walivyoviacha katika mitaharuki ya kukimbia. Mtume (s.a.w.) akaamrisha lile handaki lifukiwe, na vile vitakataka vilivyoachwa vifanywe ngawira vigaiwe hao waliohudhuria vitani. Baada ya hapa Mtume (s.a.w.) alisema: “Jibashirieni Enyi Masahaba, hamtahusuriwa katika mji wenu huu na adui yoyote tena.”
Vita hivi vya “Khandak” Mwenyezi Mungu amevitaja ndani ya Quran katika Sura ya 33 (Suratul Ahzab). Amesema katika Aya ya 9 na ya 10 na 11.
Enyi mlioamini kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu, wakati walipokujieni maadui (wengi), na sisi tukawapelekea upepo (mkubwa) na askari (wenye nguvu – Malaika – ) ambao hamkuwaona, na Mwenyezi Mungu ni mwenye kuona (kila kitu).
(Aya ya 9)
Wakati walipokujieni kwa juu yenu na chini yenu, na yakakodoka macho, na zikafika nyoyo kooni, na mkawa mnadhani kwa Mwenyezi Mungu kila namna ya dhana.
(Aya ya 10)
Wakati huu ndipo walipotiwa mtihani Waislamu, wakaharikishwa mharikisho mkubwa1.
(Aya ya 11)
Dostları ilə paylaş: |