B. WAKUU WA KIARABU WALIOKUWA WAKIJA KWA MTUME (S.A.W.) KUSILIMU
Tumekwisha kuona ya kuwa Mtume (s.a.w.) hakupigana tena vita vikubwa na Waarabu baada ya vita vya Hunayn. Bali alisalia katika mji wa Madina anatengeneza mambo ya miji aliyoiteka na anayoazimia kuiteka kwa salama bila ya vita. Watu wake aliowapeleka kwenye miji hiyo waliyoiteka ili wafundishe dini walikuwa mahodari sana, wakajitahidi kuzitia kwenye dini ya Kiislamu kila kabila zilizokuwa hazikusilimu bado. Kila kabila moja ikisilimu wakichagua baadhi ya wakubwa wake wakiwapeleka Madina ili kuonana na Mtume (s.a.w.) na kujifundisha zaidi mambo ya Uislamu, ili wapate kuja wafundisha wenziwao. Basi muda wa miaka miwili Mtume (s.a.w.) alikuwa katika mji wa Madina tu akiwapokea kila wakubwa wa kabila hizo zilizokuwa zikisilimu. Palitengenezwa mahala makhsusi pa kufikia watu hao wanaokuja, na zikatafutwa njia maalum za kupatikana chakula cha kuwalisha watu hao, muda wa kuwapo huko Madina mpaka kwenda zao makwao.
Baadhi ya mabwana hao waliokuwa wakija walikuwa ni wale wale ambao Mtume (s.a.w.) aliwaambia waingie katika dini hii wakakataa katakata, bali walimtukana na kumpiga pia. Lakini ulimwengu umegeuka, sasa wanakuja wenyewe kusilimu bila ya kulazimishwa wala kushikiliwa.
Baada ya mwaka mmoja kwisha tangu kutekwa Makka, kabila nyingi za kiarabu zilikuwa zimekwisha kusilimu, lakini nyengine zilikuwa bado zinaendelea na dini yao ya kikafiri. Siku za hija zikasonga sasa, Mtume (s.a.w.) akapenda kwenda kuhiji, lakini aliona vibaya kwenda kuchanganyika na makafiri katika kuhiji, kwani alijua kwamba makafiri watakuja kuhiji kama ada yao, kwa hivyo alimwamrisha Sayyidna Abubakr ende akahijishe Waislamu wanaotaka kuhiji. Akatoka Sayyidna Abubakr na watu 300, wakenda zao Makka kuhiji.
SURA YA KUMI NA NNE
KUHIJI KWA SAYYIDNA ABUBAKR NA HIJA YA MTUME (S.A.W) YA KUAGA
KUHIJI
A. KUHIJI KWA SAYYIDNA ABUBAKR
Huku nyuma Madina Mtume (s.a.w.) alipoona kuwa Waarabu waliosalia wasiosilimu bado ni wachache mno – si wakustahili kuwa ndio sababu ya kuwazuilia wenziwao walio wengi na kutekeleza dini yao vilivyo – alimfatishia Sayyidna Abubakr Sayyidna Ali ili ende akawatolee hutba Waarabu wote watakaohudhuria uwanja wa Arafa siku ya mwezi 9 Mfunguo tatu, ya kwamba asije kuhiji tena kafiri baada ya mwezi huo, na hapana ruhusa kuhiji tena utupu – kama wengi walivyokuwa wakifanya zamani – na kwamba Mtume (s.a.w.) mwenyewe atakuja mwakani kuhiji. “Asiye mwana aeleke jiwe” Sayyidna Ali akafanya kama alivyoamrishwa. Basi baada ya kwisha hija yao watu wote walirejea makwao na huku wanasimlia hutba walioisikia ikitolewa na Sayyidna Ali, wale chembe ya Waarabu ambao waliokuwa bado hawakusilimu waliona kuwa “Nyungu imekwisha wiva” wala hapana ila kusilimu tu. Kwa hivyo baada ya kurejea kwao, waliwaamrisha wakubwa wao wende nao kwa Mtume (s.a.w.) kupeleka habari ya Uislamu wao kama walivyokwenda wenziwao. Mabwana hao wakafanya kama walivyoamrishwa. Mtume (s.a.w.) akawapokea kama aliyokuwa akiwapokea wenziwao.
B. KUHIJI MTUME (S.A.W.) HIJA YA KUAGA
Miezi ya hija ya mwaka wa pili haijawahi kuja ila takriban Bara Arabu yote ilikuwa imekwisha kusilimu. Kwa hivyo siku ziliposonga aliwabainishia watu ya kuwa ameazimia safari hii kwenda Makka kuhiji. Kabila za nje ya Madina hazikusikia habari hii ila zilijimimina Madina mashangwe kwa mashangwe. Madina ilikuwa kama mzinga wa nyuki kwa ghasia na mvumo na msongano. Hata mwezi 24 Mfunguo pili mwaka wa 10 A.H (February 632) Mtume (s.a.w.) alitoka na wake zake wote tisa – baada ya kwisha kusali Adhuhuri – kwenda kuhiji, na nyuma yake ana kundi la watu 12,000 ambalo lilikuwa likiongezekaongezeka, mpaka lilipofika Makka lilikutana na kama hilo na zaidi linawangojea.
Wakati wa Laasiri wakafika Dhul Hulayfa, wakatua ili walale hapo waondoke siku ya pili. Siku ya pili – baada ya kusali Adhuhuri – Mtume (s.a.w.) na watu wake walikoga na kujitia manukato na akavaa kila mmoja shuka moja nyeupe chini na akajitanda shuka ya pili juu. Kisha wote wakaelekea Kibla wakahirimia na wakanyanyua sauti kutamka “Talbia” Si weupe huo ulioonekana wakati huu. Weupe wa mwangaza wa jua la Adhuhuri. Weupe wa mchanga wa jangwa hilo, weupe wa nyuso za watu hao, weupe mtupu wa nguo zao, na – mwisho kabisa – weupe wa usafi wa nyoyo zao. Kisha hao wakashika njia wakenda zao, na huku wananyanyua sauti kutamka “Talbia” Talbia ni dua inayosomwa kila wakati na wenye kuhiji1.
Hata Jumaamosi ya mwezi 3 Mfunguo tatu 10 A.H. (March 632) jeshi hilo liliegesha kwenye mtaa wa Dhii Tuwa likalala hapo. Hata siku ya pili mchana, hilo likaingia Makka kwa njia ya Kaskazini iitwayo Kadaa likaingia uwanja wa Al Masjidul Haram kwa mlango uitwao Babus Salam. Likatufu Al Kaaba mara 7, na Mtume (s.a.w.) yupo juu ya ngamia wake naye anatufu, ili kila mtu amwone namna anavyotufu. Baada ya kusali rakaa mbili za “Tawafu” wakaenda kwenye kisima cha Zamzam, kila mmoja akanywa mafunda ya kumtosha kiu yake – hali ya kuwa kisima kimejaa vile vile – husemi ila hakijachotwa hata kata moja.
Kisha wakaondoka wakaenda “Kusai”1 mara 7 baina ya jabali la Safaa na Marwa, masafa baina ya majabali haya mawili yanakurubia robo meli, baadae wakavua nguo zao nyeupe wakavaa nguo zao za dasturi na kikawahalalikia kufanya kila kilichokuwa halali kabla ya kuhirimia kwao huko.
Hata mwezi 8 Mfunguo tatu ulipokuja, walihirimia tena wakati wa asubuhi na wakaondoka wakenda Mina, mtaa uliopo kwenye thuluthi ya awali ya njia baina ya Makka na Arafa, na baina ya Makka na Arafa ni meli 15, wakatua hapo kabla ya Adhuhuri wakashinda na wakalala. Asubuhi siku ya Ijumaa mwezi 9 Mfunguo tatu mwaka wa 10 A.H. (March 632) Mtume (s.a.w.) akatoka na jeshi lake kwenda kusimama Arafa. Walipofika kwenye mtaa wa Namira walitua wakapumzika, hata jua lilipopinduka waliondoka wakaenda kusimama kwenye uwanda wa Arafa. Mtume (s.a.w.) akasimama juu ya ngamia wake, akaamrisha zinyamazwe kila kelele, kwani alitaka kutoa hutuba. Akatoa hutuba kubwa akakataza ndani yake kuuana, kuchukuliana mali , kutukanana na kusemana. Tena akawaamrisha sana watu wawafanyie mema wanawake na watumwa, kisha akawaamrisha Waislamu wote washikamane na Qurani na maneno yake Mtume (s.a.w.). Akasema: “Nakuachieni vitu viwili ambavyo mkishikamana navyo hamtapotea kabisa, Kitabu cha Mungu na Hadithi zangu”2 Mwisho wa hutuba yake akamshuhudisha Mwenyezi Mungu kuwa amefikisha kila aliloamrishwa kufikisha. Watu wote wakashuhudia kuwa kweli kafikisha. Kisha akamwamrisha kila aliyehudhuria hapo amjuvye habari hii asiyehudhuria.
Ilivyokuwa wamehudhuria watu wengi kwenye huo uwanja wa Arafa, ilikuwa muhali watu wote kusikia sauti ya Mtume (s.a.w.). Kwa hivyo waliwekwa watu wengi kila upande wa uwanja huo ili wafikishe kwa sauti zao kali maneno ya hutuba hiyo ya Mtume (s.a.w.) kwa kila waliokuwa mbali. Miongoni mwa hao waliochaguliwa kufanya haya alikuwa Bwana Rabia bin Umayya bin Khalaf, mtoto wa yule kafiri mkubwa aliyekuwa akimwudhi Mtume (s.a.w.) na Masahaba wake!
Hutuba ilipokwisha Bwana Bilal aliadhini, na Mtume (s.a.w.) akasalisha Adhuhuri na Laasiri pamoja. Baada ya kutoa salamu ilishuka Aya hii ya 3 katika Surat Al Maaida.
Leo nimekwisha kukukamilishieni dini yenu , na nimekwisha kukutimizieni neema zangu, na nimekuridhieni Uislamu uwe dini yenu1
Iliposhuka Aya hii Mtume (s.a.w.) aliwasomea watu wote waliokuwa huko, baada ya kwisha kuisoma, Mtume (s.a.w.) alimwona Sayyidna Umar analia sana. Kwa hivyo akamwuliza sababu ya kulia kwake. Naye akajibu: “Nalia kwa kuwa siku zako za kufa zimekaribia. Wewe Mungu amekuleta ulimwenguni kufundisha watu dini, na leo amekwisha kupa habari ya kwamba umekwisha kumaliza kazi yake aliyokupa kuifanya” Tangu kushuka Aya hii mpaka kufa Mtume (s.a.w.) ni miezi 3 na siku 3.
Baadaye wakatawanyika chekwa2 kwenye uwanja wa Arafa, kila mmoja akaelekea Kibla anafanya ibada zake azitakazo. Wakasalia hapo mpaka Magharibi. Hapo tena wakaondoka wakaenda kulala Muzdalifa. Ikiwa unatoka Arafa hiyo Muzdalifa ipo thuluthi ya njia baina ya Arafa na Makka, nusu ya usiku ulipokwisha waliamrishwa wanawake na wanaume, wazee na watoto watangulie Minaa, wakapige mawe kwenye “Jamarat”. Kisha wende zao Makka wakatufu, na baadae wakarejee Minaa wakapumzike. Watu hawa wakafanya kama walivyoamrishwa “Jamarat” ni viguzo vitatu vilivyoko Minaa ambavyo Waislamu huvipiga mawe siku za Hija.
Hata baada ya kwisha kusali Asubuhi, Mtume (s.a.w.) akaondoka pamoja na wanaume waliosalia wakenda zao Minaa. Walipofika kwenye bonde linaloitwa Wadi Muhassir Mtume (s.a.w.) aliwaamrisha waokote mawe ya kwenda kupiga hizo “Jamarat” za Minaa, nao wakaokota, walipofika Minaa wakazipiga hizo “Jamarat” Kisha Mtume (s.a.w.) akawatolea hutuba. Ndani ya hutuba hiyo ya leo aliwaaga, akawaambia: “Sidhani kuwa nitakutana nanyi tena mahala hapa. Hii ndiyo mara yangu ya mwisho nafikiri” Baadaye wakenda kuchinja wanyama wao waliokuja nao kwa ajili ya kuwachinja. Tena wengine wakanyoa nywele zao zote, na wengine wakapunguza tu. Mtume (s.a.w.) aliponyowa nywele zake aliamrisha kila mtu apewe kidogo kidogo. Kinyozi wake aliyemnyoa siku hiyo ni Bwana Maamar bin Abdalla. Badaye wakakoga wakavaa nguo zao za sikukuu wakajitia manukato wakenda zao Makka ‘Kutufu’ na ‘Kusai’. Kisha wakarejea Minaa wakakaa huko muda wa siku 3, mpaka baada ya Adhuhuri ya Jumaatano, mwezi 13 Mfunguo tatu (March 632) Mtume (s.a.w.) na watu wake wakaondoka wakenda Makka kuaga msikiti wa Al Masjid Al Haram. Lakini walipofika mtaa wa Al Muhassab walitua. Wakashinda usiku wakenda Makka wakatufu “Tawafu” ya kuaga, kisha hao wakashika njia ya kusini iitwayo Kudaa. Kabla ya alfajiri ya Alhamisi wakenda zao Madina. Muda waliochukua tangu kuingia kwao Makka kwa ajili ya kuhiji mpaka kutoka kwenda zao ni siku 12, wameingia Jumaapili mwezi 4 wakaondoka Alhamisi mwezi 15.
SURA YA KUMI NA TANO
KUFA KWA NABII MUHAMMAD (S.A.W)
KUFA KWA NABII MUHAMMAD (S.A.W)
Mtume (s.a.w.) alirejea Madina mwezi 20 Mfunguo tatu wa mwaka wa 10 A.H – 632. Lakini tangu kurejea kwake hakua na afya nzuri kama zamani, ila ugonjwa haukumtupa kitandani bado. Hata lilipokuchwa jua la kuamkia Jumaatano mwezi 29 Mfunguo tano, Mtume (s.a.w.) alitoka na mtumwa wake Abu Muwayhiba, wakenda wakazuru makaburi ya kiwanja cha Al Bakii akawatolea salamu waliozikwa huko na akawaombea dua. Khatimaye akarejea nyumbani kwake akamkuta Bibi Aysha anajida1 kuwa kashikwa na kichwa barabara, na huku analia na kusema: “Ee kichwa changu wee!” Mtume (s.a.w.) akamwambia: “Anayestahiki kusema kichwa changu wee ni miye si wewe. Kwani mimi nitakufa kabla yako wewe. Lau ungekufa kabla yangu mimi. Wallahi! Ningekutengeneza mimi mwenyewe vizuri na ningekusalia kwa dua nyingi na nzuri nzuri”.
Mtume (s.a.w.) kuamka tu asubuhi aliamka na kichwa kikali na homa ndogo, kila siku ikipambazuka na homa ilikuwa ikizidi. Lakini vivyo hivyo alikuwa akijikaza kwenda msikitini kusali na kwenda kumtimizia ngono za kila mke katika wakeze tisa. Hata ugonjwa ulipomzidi sana aliwaomba wakeze wampe ruhusa augulie nyumbani kwa Bibi Aysha, nao waje kumwuguza huko huko. Mabibi hao wote walikubali shauri hiyo, wakahamia nyumbani kwa Bibi Aysha kumwuguza mume wao mtukufu. Nyumba hii ya Bibi Aysha ilikuwa karibu na Msikiti kuliko nyumba za wake wenziwe, ndio maana Mtume (s.a.w.) akaichagua, ili aweze kuhudhuria Msikitini na kusalisha mwenyewe kila kipindi. Navyo ndivyo alivyokuwa akifanya.
Lakini sala ya Isha ya kuamkia Ijumaa, mwezi 9 Mfunguo sita ilipoadia, akapelekewa Mtume (s.a.w.) mjumbe kwenda kumwita, alikutikana taabani, kwa hivyo aliamrisha aambiwe Sayyidna Abubakr akasalishe. Akafanya kama alivyoamrishwa, akawa yeye ndiye mwenye kusalisha mpaka kufa kwa Mtume (s.a.w.). Hata siku moja baada ya kusalisha Sayyidna Abubakr, Mtume (s.a.w.) alijikongoja – na huku kashikwa na watu wawili – akaja msikitini akapanda juu ya mimbar, akasema maneno haya: “Enyi watu! Pana mtu mmoja ambaye Mwenyezi Mungu amemkhiyarisha baina ya Dunia na Akhera, naye amechagua “Akhera”. Sayyidna Abubakar akafahamu madhumuni ya maneno haya ya Mtume (s.a.w.), kwa hivyo akalia akasema: “Tunakufidia kwa roho zetu, Yaa Rasula Llah!” Kisha Mtume (s.a.w.) akaendelea kusema: “Hakika mwenye neema kubwa juu yangu miongoni mwenu, kwa mali yake na nafsi yake, ni Abubakr” Kisha akasema: “Enyi Muhajir! Jiusieni kuwafanyia wema Ansar. Wao ndio vipenzi vyangu ambao tumekimbilia kwao, wakatufanyia kila ihsan. Walipeni mema kila watakaokufanyieni mema, na mwasamehe kila watakaokufanyieni mabaya” Baada ya haya Mtume (s.a.w.) akashuka akajikongoja mpaka kwake.
Tangu siku hiyo hakutoka tena kwani ugonjwa ulimzidi sana, ila alfajiri ya Jumaatatu mwezi 12 Mfunguo sita, alikuja msikitini akasali nao rakaa ya mwisho ya sala hiyo. Baada ya kumalizika rakaa yake ya pili, aliwakabili watu akasema: “Enyi watu! Moto unawangojea wabaya, na Pepo imeandaliwa wema. Zimekukabilini fitna za dini kubwa kubwa. Kila zikisha fitna zitafuatwa na nyenginezo. Wallahi! Hapana yoyote katika nyinyi anayenidai haki yake. Wallahi mimi sikuhalalisha ila kilichohalalishwa na Qurani, wala sikuharamisha ila kilichoharamishwa na Qurani” Kisha akakaa akazungumza nao mpaka kadiri ya saa moja au mbili ya mchana. Baadaye akawaaga akenda zake kwake, na kila aliyekuwepo hapo akenda kwenye jambo lake. Sayyidna Abubakr akamwaga Mtume (s.a.w.) ende shamba akamtazame mkewe, na Mtume (s.a.w.) akampa ruhusa, watu wote walifurahi wakaona ya kuwa Mtume (s.a.w.) kesha pona, sasa hivi atakamata kazi zake kama zamani.
Lakini baada ya kurejea kwake tu, alihisi nguvu zake zinamwacha upesi upesi. Akajitupa juu ya kitanda akazungukwa na wake zake na mwanawe Bibi Fatma, mara zikaonekana juu yake alama za ‘Sakratilmaut’ (kukata roho). Bibi Aysha akampakata juu ya mapaja yake, na wenziwe wote wakakizunguka kitanda cha Mtume (s.a.w.) na macho yao yanamiminika machozi njia mbili mbili. Karibu ya kitanda kilikuwapo kibakuli cha maji ambacho Mtume (s.a.w.) alikuwa akichovya ndani yake mkono wake, kisha akifuta kwa maji hayo uso wake, na huku anasema: “Enyi watu! Hakika kutoka roho kuna machungu makubwa” wakati huo aliingia mtu mmoja na msuwaki mkononi mwake. Mtume (s.a.w.) akaashiria apewe msuwaki huo. Bibi Aysha akamtafuniatafunia, kisha akampa, na Mtume (s.a.w.) akautia kinywani akawa anasuwakia kidogo kidogo.
Pale pale ule msuwaki ulimtoka mkononi, akaregea yu taabani! Akakodoka macho kutazama juu – huku anakata roho – na huku anasema: “Nakwenda kwa rafiki yangu Mtukufu, nakwenda kwa rafiki yangu Mtukufu” wanawake waliokuwako ndani jinsi walivyokiangua kilio hicho hata mji wote ulitikisika.
Muda si muda watu wote wakimbizana kuja nyumbani kwa Mtume (s.a.w.) mbio – nguo mikononi – Mtu wa mwanzo kufika alikuwa ni Baba yake mdogo, Bwana Abbas, kufika tu aliufunga mlango kwa ndani, akawaacha watu wote nje, kuingia ndani alimwona mwanawe anamaliza pumzi zake za mwisho, na pale pale akakata roho, Bwana Abbas akamfumba macho, akambana kinywa, akamnyoosha viungo, kisha akamgubika guo moja kwa moja tangu kichwani mpaka nyayoni.
Baadaye akatoka nje akawapa habari waliokuwapo hapo ya kuwa Mtume (s.a.w.) amefariki Dunia. Si msiba uliotokea siku hiyo! Si mtaharuki uliowazukia watu hao! Si huzuni isiyopata kuonekana mfano wake. Si kujigubika huko kulikojigubika mji wa Madina siku hiyo! Bwana Abdalla bin Unays – kusikia tu kwamba Mtume (s.a.w.) kafa – alianguka papo hapo chini – mkavu – amekwisha. Sayyidna Uthman na wengi wengineo iliwapooza miguu, wasiweze kuvuta hata hatua moja, wakapigwa na bumbuwazi kamili! Wengine walitokwa na fahamu, wakawa wanakwenda njiani mapepe! Hawajui watokako wala wendako, Sayyidna Umar akatafuta njia mpaka akaingia ndani kwa maiti. Akamfunua uso wake akaona Mzuri, una bashasha na kutoa nuru kama zamani. Furaha ilimrarulia nguo, akasema: “Wallahi! Hajafa. Uso huu si uso wa mtu aliyekufa. Waongo wakubwa wanaosema kuwa amekufa!” Kisha akatoka nje na upanga mkononi, na huku anasema: “Mtume (s.a.w.) hakufa. Yoyote atakayesema kuwa Mtume (s.a.w.) amekufa nitampiga kwa upanga huu. Wanafiki wakubwa nyi1! Mtume (s.a.w.) atakufa kabla dunia yote haijasilimu? Muhali huo!” watu walioko nje wakababaika, hawajui wafuate maneno ya Bwana Abbas aliyesema kuwa Mtume (s.a.w.) amekufa au maneno ya Sayyidna Umar, anayechaga kuwa hukufa, ila roho yake imekwenda mbinguni kisha itarejea.
Muda si muda alitokea Sayyidna Abubakr – pumzi mbili mbili – macho paani. Watu wakamzonga kwa vilio na masuali. Wanamuuliza yepi yaliyo kweli, maneno ya Bwana Abbas au maneno ya Sayyidna Umar, Sayyidna Abubakr akaingia ndani kwa maiti akamfunua uso akambusu, akasema: “Unanukia vizuri na unapendeza, kama katika uhai wako. Wallahi! Mimi nakiri ya kwamba umekufa. Mungu hatakuonjesha mauti mara mbili. Inakutosha taabu iliyokukuta katika kukata roho sasa hivi. Wallahi! Sisi tunashuhudia ya kwamba umetekeleza ujumbe, umeunasihi umma, na umesimama juu ya haki za Mungu na za wanaadamu, ukazitekeleza vilivyo. Amani ya Mungu na Rehema zake zikushukie asubuhi na jioni” Baada ya hapa alifululiza Msikitini, akapanda juu ya Mimbar akahutubu akasema: “Enyi watu! Kama palikuwa katika nyinyi ambaye akimwabudu Muhammad, basi Muhammad amekwisha kufa. (Naakatafute Munghu mwengine). Ama ambaye alikuwa akimwabudu Mungu, basi Mungu yu hai milele hafi. Mungu amesema katika Quran:
Hakuwa Muhammad ila Mtume tu ambaye wamepita kabla yake yeye Mitume wengi. Basi atakapokufa au atakapouawa mtarejea katika ujinga? Basi yoyote atakayerejea katika ujinga wake hatamdhuru Mungu chochote1
Baada ya kusikia maneno haya watu wote waliyakinisha – hata Sayyidna Umar pia – ya kuwa kweli Mtume (s.a.w.) amekufa. Basi hapo ndipo walipoingia kutafuta khalifa na kutengeneza shauri ya kuzika. Akachaguliwa Sayyidna Abubakr kuwa Khalifa, baada ya upinzani mkubwa uliokuwepo katika mkutano wa kuchagua, alipata sauti nyingi kuliko sauti alizopata Sayyidna Ali na kuliko alizopata Bwana Saad bin Ubada – bwana mkubwa wa Kiansar wote – Baadhi ya Ansar na Muhajir – wasiokuwa Bani Hashim – walimtaka Sayyidna Abubakr, ama Bani Hashim wote2 na baadhi ya Ansar walimtaka Sayyidna Ali, na Ansar waliosalia walimtaka Bwana Saad bin Ubada1.
Muda huu walipokuwa wanamchagua Khalifa, Sayyidna Ali na jamaa zake, walikuwa katika kazi ya kumwosha Mtume (s.a.w.)2. Mtume (s.a.w.) alipakatwa na Bwana Al Fadhil bin Abbas bin Abdul Muttalib, akaoshwa na Sayyidna Ali bin Abi Talib bin Abdul Muttalib, na aliyekuwa akitilia maji ni Bwana Abbas bin Abdul Muttalib. Ama mahuru wake Mtume (s.a.w.) wawili – Bwana Usama bin Zayd na Bwana Shakran – wao walikuwa wakiwasaidia. Baada ya kuoshwa lilichimbwa kaburi kuko huko chumbani alikokufia – chumba cha Bibi Aysha – na aliyesimama kutengeneza hilo kaburi na kulitilia mwanandani ni Bwana Abu Talha wa Kiansar. Baada ya hapa wakamvua nguo za kuoshea, wakamkafini kwa nguo tatu nyeupe za pamba, baada ya kufukizwa kwa udi vyema na kutiwa manukato vizuri. Kisha akalazwa juu ya kitanda kwenye ukingo wa kaburi, akafunikwa guo moja kwa moja. Baadaye wakapewa ruhusa watu kuingia kumwaga Mtume wao (s.a.w.). Yakawa makundi haya yanaingia na haya yanatoka, mchana kutwa wa Jumaatatu na mchana kutwa wa Jumaane na usiku kucha wa kuamkia Jumaatano. Hata karibu na alfajiri ya hii Jumaatano. Mtume (s.a.w.) alishushwa kaburini mwake, akazikwa kama wanavyozikwa Waislamu wote wengine. Walioshuka kaburini siku hiyo ni:-
Bwana Abbas, Sayyidna Ali. Na mabwana hawa wengine wajao:-
Al Fadhil bin Abbas, Qutham bin Abbas na Shakran.
Mtume (s.a.w.) amekufa mchana wa Jumaatatu mwezi 12 Mfunguo sita mwaka 11 A.H – 8 June 632, na akazikwa karibu na alfajiri ya Jumaatano mwezi 14. Alipokufa ulikuwa umri wake ni miaka 63 barabara.
Hii dunia dania *** Haidumu na bashari.
Akhi! Yakutosha haya *** Kutawafu Mukhtari.
Watu walijililia *** Mwishowe wakasubiri.
Ayyuhal Maghruri *** Ina khadaa dunia.
Dostları ilə paylaş: |