zote za ulimwengu, na katika nafsi zao, hata iwabainikie kuwa haya ni kweli1
SURA YA SABA
KUWAFUNDISHA DINI WAARABU
WASIOKUWA MAKURESHI.
KUWAFUNDISHA DINI WAARABU
WASIOKUWA MAKURESHI
Mwanzo wa kupewa Utume wake, Mtume (s.a.w.) hakuwashughulikia Waarabu wengine, bali aliwashughulikia Makureshi kwanza, kwani ndio waliokuwa kwenye mji wake na ndio waliokuwa jamaa zake. Aliona kwamba ni wajibu kwanza kuwatengeneza hawa alionao ndipo atoke nje akawatengeneze wengine. Wema uanzie nyumbani, lakini baada ya miaka kidogo kupita wala asione dalili yoyote kwa Makureshi ya kuipenda dini hii, aliona ni shauri nzuri kuingia sasa kuwafundisha dini hii Waarabu wengine, hwenda wao wakaiona nzuri wakaipokea kwa upesi.
A. KUSAFIRI KWAKE KWENDA TAIF NA KUSILIMU KWA MAJINI
Baada ya kwisha kuzikwa Bwana Abu Talib na Bibi Khadija tu, mara Makureshi walizuka kumpinga Mtume (s.a.w.) na kimwudhi kwa mateso yaliyopindukia mipaka baada ya kuwa walijizuia na hayo kwa ajili ya cheo cha Bwana Abu Talib. Utadhani moto wa vifuu vilivyokuwa vikiwaka chini kwa chini, kisha vikawaka mara moja. Si moto wake huo! Basi ndivyo ulivyokuwa mwinuko wa Makureshi kumtaabisha Mtume (s.a.w.), walimwinukia kwa umoja wao, hata asijue pa kuitia nafsi yake. Hapo ndipo alipofikiri kwenda Taif1, kuwalingania dini watu wa mji huo – Bani Thaqif – ambao ni jamaa na ile kabila ya mama yake Mtume (s.a.w.) wa kumnyonyesha – Bibi Halima – .
Baada ya siku ya 10 ya kufa Bibi Khadija Mtume (s.a.w.) aliondoka kwa siri yeye na huru wake, Bwana Zayd bin Haritha, wakenda huko Taif, akafika kwa wakubwa wa mji ule akawafahamisha alilolijia. Wakampa jawabu ambazo zilimvunja moyo wake zaidi kuliko alivyokuwa. Lakini hakukata tamaa kabisa, kwa hivyo aliwendea watu wadogo wa mji ule, nao kadhalika wakampa jawabu za kumvunja vile vile, kama zile za “Mashekhe” wao. Lakini hakuondoka, walipomwona haondoki wale “Mashekhe” waliamrisha watu wa mji wampige mawe kila wamwonapo, mpaka ende zake, basi haikuwahi kutangaa habari hii ila kila mtu alitoka na akiba ya mawe mkononi mwake ili ampige Mtume (s.a.w.) atakapomwona. Alipotokeza nje tu mara walimpopoa kwa mawe, husemi watoto wanapopoa embe zilizowiva! Hakujamsaidia chochote hata kusema anakwenda zake, lakini waliendelea kumfata njiani na kumpiga mawe, na huku wakimpiga sokole muda wa meli 2. aliroa (aliloa) damu tangu kichwani mpaka miguuni! Hawajamwacha kupumzika hata chembe muda wa meli 2 zote hizo! Kila akitaka kupumzika huja wakamwinua wakamlazimisha kwenda, ijapokuwa hawezi! Yule huru wake alijitahidi kumkinga lakini hakujasaidia kitu. Wote wawili waliroa damu chepechepe tangu kichwani mpaka miguuni.
Hata baada ya kurejea wale makatili ndipo walipopata wasaa wa kupumzika. Wakapumzika chini ya mti wa shamba la Utba bin Rabia na ndugu yake1 wale wakubwa wa Kikureshi. Mabwana hawa walipomwona Mtume (s.a.w.) walimtambua na wakamwonea huruma sana wakampa mtumwa wao mmoja vishada vikubwa vya zabibu mbichi ampelekee pamoja na baadhi ya vyakula vingine. Kwa bahati nzuri yule mtumwa alimsaili Mtume (s.a.w.) habari zake zote, na Mtume (s.a.w.) akamjibu suala zake, hayakumalizika mazungumzo ila mtumwa yule alisilimu pale pale2. Bwana zake walijuta kumpeleka, wakailani saa waliompeleka mtumwa wao.
Baada ya kwisha kuondoka kwenye shamba la kina Utba, Jibril akashuka na akamshauri ikiwa atapenda awaangamize3 watu waliomwudhi kama alivyopenda Mtume Nuh. Nabii Muhammad (s.a.w.) alikataa, akasema: “Natumai Mungu atawaongoa wao na watoto wao, wainusuru dini hii kwa jitihada kubwa kama wanavyoipinga sasa, hakika wao hawajui nini dini ya Uislamu, lau kuwa wanaijua wasingeipinga hivi”. Jibril akastaajabu sana kusikia jawabu hii, akamwambia: “Hakika wewe ni Mtume wa rehema, kama alivyokusifu Mola wako katika Quran”1 Jibril akarejea alikotoka, na Mtume (s.a.w.) akashika njia ya kwenda Makka.
Hata alipofika karibu na Makka alipewa habari kuwa hana ruhusa ya kuingia mji wa Makka, kwani aliyemtuma nani kutoka kwenda mji mwengine, alipojua haya alimpelekea habari Akhnas bin Sharyq – mkubwa wa kabila ya mama yake Bani Zuhra – aingie Makka kwa amani yake Akhnas akakataa, Mtume (s.a.w.) akampelekea habari Suhayl bin Amr – mkubwa wa Bani Amr – naye pia akakataa. Kisha ndipo alipompelekea habari Mut’im bin Adiy – mkubwa wa Bani Naufal bin Abd Manaf – na ni yule aliyeuchana mkataba, Mut’im akakubali, akampelekea amri aingie. Tena wakavalia yeye na wototo wake wakenda kwenye Al Kaaba wakatufu ( kuizunguka Al Kaaba mara 7 kwa ajili ya ibada), baada ya kutufu alisimama huyu Mut’im mbele ya wakubwa wa Kikureshi akasema: “Nimempa rurhusa Muhammad arejee katika mji wake Makka, na nimempa amani yangu, kama alivyopewa zamani na baba yake mdogo Abu Talib, na huyo ataingia sasa hivi”. Pale pale akaingia Nabii Muhammad (s.a.w.) na Makureshi wote wanamwona, hawana la kumfanya tena ila kumwudhi kwa maneno, au kwa mikonyezo, akakaa salama kwa muda wa miaka 2, atangaza dini yake bila ya kuwepo mtu yoyote wa kumzuilia. Baada ya miaka 2 kupita, ulipatikana ugomvi baina ya Mtume (s.a.w.) na huyu Mut’im hapo ndipo alipoteswa, hata ikampasa kuhama kwenda Madina. Ugomvi wenyewe ni ile habari ya Miiraji tuliyokwisha kuitaja.
Ajabu iliyokuwa kubwa ni kuwa huyu Mut’im hakusilimu mpaka kufa kwake, kinyume cha wenzake wawili waliokataa kumpa amani Mtume (s.a.w.) . Hao mwisho wao walisilimu na akawa Mwislamu mzuri kabisa yule Bwana Suhay. Lakini Mtume (s.a.w.) hakusahau maisha yake fadhila za Bwana Mut’im, hata alipokufa bwana huyu, Mtume (s.a.w.) alimwamrisha shairi wake mkubwa kabisa aitwaye Bwana Hassan bin Thabit, amsifu kwa nyimbo iliyo nzuri na ndefu. Akamsifu. Katika beti zilizomo katika nyimbo hizi ni hii1:-
Lau kuwa utu wema * unamuweka yoyote
Katika watenda wema * kwa jema lake lolote
Angesalia daima * Mut’im kwetu sote
Mtume (s.a.w.) alifurahi na nyimbo hii na akawaachia watu waiimbe, kukumbuka zaidi ihsani aliyotendewa na Mut’im kulidhihirika siku alipowateka Makureshi 70 na akawa anachukua kikomboleo cha mali mengi kwa kila mmoja. Alisema: “Lau kuwa Mut’im yu hai na akaniomba kuwachia hawa bure ningaliwaachia” wengi katika mateka 70 hawa walikuwa matajiri wa Kikureshi, kikomboleo cha kila mmoja katika hao kilikuwa cha fedha nyingi.
Katika safari yake ya kurejea Taif ndipo walipomjia Majini wakasilimu, kama inavyoonyesha haya Sura ya 72 ya ambayo inaitwa “Suratil Jinn”2 Majini ni viumbe vyepesi vinavyokaa angani, havina viwiliwili, kwa hivyo haviwezi kuonekana na wanaadamu ila vinapojibadili kwa umbo lenye kiwiliwili. Na vina uwezo huo wa kujibadili kwa sura ya kuweza kuonekana, wao na Mashetani wana asili moja. Wale wema wanaofuata amri za Mungu huitwa Majini, na wale wabaya wanaodhuru huitwa Mashetani, hawa Majini ingawa wengine ni Wailsamu kama sisi, lakini hukumu zao ni mbali na hukumu zetu. Mtume (s.a.w.) alirejea huko Taif mwisho wa kumi la mwanzo la Mfunguo pili mwaka wa 3 kabla ya Al Hijra – February, 620 – .
B. KUTANGAZWA UISLAMU SIKU ZA KUHIJI
Tumeona zamani kuwa Mtume (s.a.w.) kwa muda wa miaka mitatu alikuwa akilingania watu dini yake kwa siri. Baada ya hapo ndipo alipodhihirisha ujumbe wake kwa watu wa Makka, wakamfuata wale chembe waliomfuata, na wakampiga vita waliosalia, vita vya kiwiliwili na moyo na roho. Ukawa hapana msiba mkubwa kwa Makureshi kuliko kuona mtu katoka katika safu ya dini yao na ameingia katika safu ya dini ya Nabii Muhammad (s.a.w.), kwa hivyo walikuwa wakifanya kila namna kuzuilia kuingia yoyote katika dini hiyo, akiwa Kureshi au si Kureshi, na wakajilazimisha kumtesa barabara kila anayetoka katika safu yao.
Makka – tangu kabla ya kuja Uislamu – ilikuwa ni mahali patakatifu kwa Waarabu wote, kila mwaka walikuwa wakija kuhiji miezi hii hii wanayoitumia sasa Waislamu katika kuhiji kwao. Basi Makureshi walipoona siku za hija zimesonga waliogopa sana asije Nabii Muhammad (s.a.w.) akatangaza dini yake kwa wageni na akapata watu kumfuata nao wakenda kutangaza dini hiyo vile vile katika miji yao, kwa hivyo waliitana kuja kufanya mkutano katika nyumba yao ya shauri (Parliament) iliyokuwa ikiitwa Dar Nadwa. Nyumba hii ilikuwa pembezoni mwa Al Kaaba ambapo sasa ipo nyumba inayoitwa “Mussalla Hanafi” (mahali wanapokusanyika kusali wenye madhehebu ya Hanafi wakati wanapokuja kuhiji), alikuwa hana ruhusa kuhudhuria katika nyumba hiyo asiyekuwa kijana aliyetimia miaka 40 na akawa mwenye sifa tukufu mbele yao.
Walipokusanyika aliinuka mmoja katika wao akanena: “Huyu Muhammad tukimwachia kusema maneno yake atawateka wengi katika hawa mahaji, na wao watakwenda kutangaza haya kwa wengine wasiokuwapo, kwani lenye kusemwa au kufanywa halikosi wafuasi. Basi mimi naona tutoe watu wa kuwahadhirisha wageni na mtu huyu, wapite kutangaza kuwa Muhammad ni kuhani janja linalopoteza watu” Akainuka Walid akasema: “Hatutakubaliwa maneno yetu kwani hana mmunyomunyo wa kikuhani wakati anaposema”. Akainuka mwengine aksema: “Tutangaze kwa watu wote kuwa yeye ni mwendaazimu, hafuatwi maneno yake”. Akavunja tena Walida akasema: “Nani atakeyesadiki? Yeye haonyeshi alama za wazimu. Nani anayeweza kutaja alama moja ya wazimu wake? Yeye haonyeshi alama za wazimu. Wallahi! Hana hata moja, bali vitendo vyake vyote ni vya mtu mwenye akili timamu”.
Akainuka mwengine akasema: “Mimi naona tutangaze kuwa yeye ni mchawi”. Akavunja tena Walid akasema: “Lakini hafanyi mazingaombwe (mazingaombo) ya wachawi, vipi tutaweza kumtegemeza uchawi?” Wakasema: “Tufundishe wewe la kusema tusadikiwe” Akasema: “Mimi naona tuseme kuwa yeye ni mtamu wa maneno anaweza mara moja kumvuta kila mwenye kumsikiliza maneno yake akayaona ni ya kweli ijapokuwa si kweli” Wote wakakubali shauri hii ya Walid1.
Hata siku za kuhiji zilipokuja waliwatoa watu wakawaweka katika kila njia wanazotokea mahaji, wakiwakhofisha kwa kuwaambia hivi: “Mabwana wa Kikureshi wametutuma tukwambieni kuwa huko Makka kuna mtu jina lake Muhammad amezua dini yake mpya ambayo wao hawaikiri kuwa ni dini, na mtu huyu Mungu kampa uhodari wa kusema usiokuwa na mfano, humvuta mtu mara moja katika dini kiasi cha kumsikiliza tu. Basi Makureshi wanakutahadharisheni na kumsogelea seuze kusikiliza maneno yake, akitaka kukusemezeni mfukuzeni, na huku mzibe masikio yenu. Lau kuwa hayo anayosema Muhammad ni kweli, wao wangalikuwa wa kwanza kumfata, kwani wao wanamjua zaidi kuliko nyinyi”.
Hata mahaji walipokuja katika nchi ya Hijaz aliondoka Mtume (s.a.w.) akiipitia kila kabila katika kabila zao, akiwaeleza habari ya dini yake, lakini hakupata kabila hata moja kumfuata katika aliyokuwa akiyasema. Wote walikuwa wakijipuuzia naye, bila ya kusikiliza aliyokuwa akiyasema, kila akisema wao humhanikiza kwa makelele na kujifunika nguo usoni na kutia vidole masikioni, ili wasimwone wala wasimsikie anayoyasema, ili wasipate kutekeka kwa maneno yake ya uchawi! Na mwisho wake humwambia: “Jamaa zako wanakujua zaidi nao hawajakufuata. Basi hii ni alama kubwa ya kuwa wewe ni mwongo. Wala sisi hatutaacha dini ya wazee wetu kwa ajili ya uwongo wako! Unajidhani wewe una akili zaidi kuliko babu yako, Abdul Muttalib? Mbona hakupata kuwambia watu kuwa dini hii uwongo? Ingekuwa kweli Mungu anataka kuleta Utume angepewa Walid – Bwana wa Makureshi wote – au Urwa – Bwana wa Bani Thaqyf wote –. Unafikiri angekuletea wewe yatima wa Abdul Muttalib?”
Basi ndiyo jawabu aliyokuwa akipata kila mwaka kwa mahaji, na siku nyengine alikuwa akiyapata mabaya zaidi kuliko haya, katika kabila iliyokuwa ikimjibu mabaya zaidi kuliko kabila zote ni kabila ya Bani Hanifa, kabila ya Mtume mzushi aliyezuka baada ya kiasi cha miaka 10 baada ya hapo nao wakamfuata. Na waliokuwa wakimpa jawabui nzuri kidogo ni Bani Shayban, kabila ambayo aliweza kupata watu watatu waliokiri kusilimu. Ama kabila ambayo mwisho wake alipata watu kumfuata ni ya Bani Khazraj – moja katika kabila kubwa mbili za Madina – kama tutavyoona mbele.
Baadhi ya wakati alipokuwa anawapitia Waarabu kuwahadithia habari ya hiyo dini yake mpya, baba yake mdogo – Abu Lahb – alikuwa akimfuata nyuma akiwambia watu: “Msimsikilize mwongo huyu, Wallahi! Wazee wetu hawakuwa wajinga kwa kuwaabudu Lata na Uzza na Manata (majina ya miungu yao mikubwa). Yeye anajifanya kuwa ana akili kuliko wazee wote, si uwongo huo?” Khalafu huwatajia majina ya Waarabu watukufu wa kila kabila, waliokufa zamani, kisha akiwalinganisha na Nabii Muhammad (s.a.w.) na huku akiwauliza: “Mnafikiri huyu ana akili zaidi kuliko wao? Au inamkini kuwa hao ni wapotofu, na huyu na hao chembe mbili alio nao ndio waongofu? Wallahi! Uwongo” Kila Abu Lahb akisema hivi, wale Waarabu wanazidi kuhakikisha maneno walaioambiwa njiani.
Kwa hivi inaonyesha kuwa huyu Abu Lahb alikuwa ni mpingaji mkubwa wa maendeleo ya dini ya Kiislamu, na muudhi mkubwa wa Mtume (s.a.w.) yeye na mkewe na majirani zake. Mtume (s.a.w.) alikuwa mara nyingi akisema: “Mungu alinipa majirani waovu Abu Lahb na Uqba bin Abi Muayt” (baba wa kambo wa Sayyidna Uthman bin Affan). Kila wanapomwona anatoka kwenda kufundisha dini humfuata nyuma, husemi kupe na mkia wa ng’ombe.
C. KUSILIMU KWA WATU WA MADINA
Madina ni mji ulioko kiasi cha meli 300 kaskazini ya Makka, wasafiri wa ngamia wa siku hizo walikuwa wakichukua siku 11 kutoka Makka mpaka huko, wenyeji wa mji huo walikuwa Waarabu na Mayahudi. Na Mayahudi hawa ni wale waliokuja nchi za Kiarabu tangu mwaka 135 A.D. walipofukuzwa Jerusalem Falastin, wakachanganyika na Waarabu kwa lugha kidogo na maskani, ama dini na ada walizishika zile zile zao. Hawa Waarabu wa Madini asili yao ni katika kabila moja iliyotoka Yaman ikaja ikafanya maskan yake hapo Madina, kwanza wote wakijulikana kwa jina la Bani Qayla, kisha wakagawanyika sehemu mbili – Khazraj na Aus – ambazo kila siku zilikuwa katika ugomvi na kuuana, kwa hivyo hata inapotokea kwenda kuhiji, wale Aus walikuwa wakipiga hema zao mbali na Khazraj.
Katika mwezi wa Rajab mwaka wa 11 tangu kuja Utume – Octobre 620– walikuja Makka watu sita katka Khazraj ili kufanya Umra (Hija ndogo), kwa bahati nzuri Mtume (s.a.w.) akapita Jamratul Aqaba (Minaa), akaona hema ya wageni hawa akawendea akawatolea mawidha, akawasomea Quran na akajibizana nao kwa baadhi ya masuala waliyomwuliza, pale pale wote wale 6 waliamini, wakampa mkono Mtume (s.a.w.) wa kuonyesha kuwa wao wamekwishakuwa wafuasi wa dini yake, tena wakampa ahadi kuwa watajaribu wawezavyo wawasilimishe wenziwao walioko Madina. Watu wenyewe waliosilimu mwanzo ni hawa:-
1. Bwana As’ad bin Zurara. 4. Bwana Qutba bin Amr
2. Bwana Auf bin Harith. 5. Bwana Uqba bin Amr
3. Bwana Rafiy bin Malik. 6. Bwana Jabir bin Abdillah
Mara waliporejea kwao kila mmoja alianza kuieneza dini ile kwa rafiki zake, hata siku za hija zilipotimia – yani baada ya miezi 4 au 5 tangu kusilimu kwao – wengi kidogo walikuwa wamekwisha kusilimu, na wakafanya shauri kupeleka watu 12 katika wao waje kwa Mtume (s.a.w.) watake matlaba yao waliokuwa wakiyataka. Hata Mfunguo tatu ulipoandama walimfikilia Mtume (s.a.w.) wageni 12 wa Kiislamu wa Madina, 2 katika Aus na 10 waliosalia ni katika Khazraji, 5 ni katika wale 6 waliokuja katika mwezi wa Rajab, na 7 ni wageni, ndio kwanza kuja kuonana na Mtume (s.a.w.), walimwomba Mtume (s.a.w.) awapelekee mtu akawafundishe Quran na dini, na awe akipita pamoja nao katika kila tumbo la kabila ya Kimadina ili kulilingania dini hii.
Mtume (s.a.w.) aliwapa Bwana Mus’ab bin Umeyr – katika Bani Abdid Dar – na Bwana Abdalla bin Umm Maktum – katika kabila ya Bani Makhzum – naye ni mtoto wa mama yake mdogo Bibi Khadija, aliwapa wawili hawa wakawafundishe Quran na wakatangaze mafundisho ya dini ya Kiislamu. Hata ilipotimia siku ya kurejea baada ya hija kwisha, Mtume (s.a.w.) aliwataka wale wageni 12 wachukue ahadi hii. Akawaambia: “Nataka mnipe ahadi kuwa:
-
Hamtaabudu chochote kingine ila Mwenyezi Mungu.
-
Hamtakwimba wala hamtapokonya misafara ya njiani bila ya haki.
-
Na hamtazini.
-
Na hamtawaua watoto wenu tena1
-
Na hamtasema uwongo.
-
Na hamtaniasi katika kila jema nitakalo kuamrisheni.
Wote wakayaridhia hayo na wakayafuata kama walivyoahidi, mara walipofika Madina, Bwana Mus’ab na Bwana Abdalla waliingia kuitangaza dini katika mji wote wa Madina, haukuwahi kuja Mfunguo tatu mwengine ila matumbo yote ya kabila za Waarabu wa Madina yamesilimu – bila ya upanga wala kitisho –. Matumbo 4 tu katika matumbo ya Kiaus ndiyo yaliyotaakhari kusilimu. Hayakusilimu ila Mtume (s.a.w.) alipokwenda mwenyewe Madina. Ama Khazraj wote walisilimu, hawakusalia isipokuwa wawili watatu tu. Hawa Khazraj ndio waliokuwa jamaa na Mtume (s.a.w.) kwa upande wa bibi mzaa babu yake.
Hata mwezi wa March 622 ulipofika, na siku za hija zikaadia, walimwasilia Mtume (s.a.w.) wageni 75, safari hii kuja kutoa habari kuwa Madina yote imekwisha kusilimu, na Uislamu umeshika mizizi yake barabara, hapana cha kuweza kuusukua na kuung’oa. 2 katika hawa 75 walikuwa wanawake, nao ni Bibi Nusayba bint Amr na Bibi Ummi Many – Asmaa bint Amr – na 62 katika hao wanaume 73 walikuwa Khazraj, 11 tu ndio Aus, ama hawa wanawake wawili wote walikuwa katika kabila ya Khazraj.
Lakini walipofika Makka hawakumjilia Mtume (s.a.w.) wote nyumbani mwake, walikuwa wamekuja na yule mwalimu wao mkubwa, Bwana Mus’ab bin Umeyr, na yeye ndiye aliyempa habari hii Mtume (s.a.w.), na Mtume (s.a.w.) akamwambia wakutane naye wote mahali pamoja usiku wa siku watakapoazimia kurejea kwao.
Hata siku hiyo ilipotimia, wote walikwenda nyuma ya jabali moja usiku sana wakakaa kumngojea Mtume (s.a.w.) – bila ya mtu yoyote kuwaona –. Ulikuwa usiku wa mwezi mkali sana, kwa hivyo hawakuhitaji taa. Mara Mtume (s.a.w.) alifika yeye na Masayyidna Abubakr, Ali na Abbas – Baba yake mdogo Mtume (s.a.w.) – na yeye bado alikuwa hakusilimu. Mtume (s.a.w.) akamwambia Sayyidna Abubakr ende akasimame upande mmoja wa njia ya majabalini ili asije mtu kuwasikiliza maneno yao, na Sayyidna Ali ende upande mwengine. Baada ya Mtume (s.a.w.) kuamkiana na kujuvywa wageni wake, aliwatolea khutba ndefu, akawasomea Aya za Quran na akawalinganishia Uislamu na Ukafiri, tena akawambia kuwa anataka wamwahidi kuwa akenda kwao watamhifadhi yeye na watu wake, kama wanavyohifadhi wake zao na watoto wao wakati wa vita. Akaondoka Bwana Barai bin Maarur akampa mkono akamwambia: “Tumekubali, tutakuekeni juu ya macho yetu” wakasimama wote tena wakampa mkono mmoja mmoja, wakimwambia kama alivyosema Bwana Barai.
Khalafu akaondoka Bwana Abbas akawaambia: “Msimchukue mtoto wetu, khalafu mtakapoona vishindo vya Makureshi na Waarabu wengine mkashindwa njiani, bora tuachieni hapa hapa” wakainuka wale wageni wakazidi kutia nguvu kuwa watamhifadhi na wala hapana chochote kitakachomsibu, maadam kizazi chao kihai. Tena Mtume (s.a.w.) akawachagulia wakubwa 12 – kama Nabii Musa alivyowchagulia wafuasi wake wakubwa 12 – akachagua 9 katika Khazraj na 3 katika Aus, kila mkubwa akapewa matumbo makhsusi yawe yakifuata amri zake. Hapo tena wakamwaga Mtume (s.a.w.), na wakamwambia kuwa watayari, wanamngojea kwa udi na uvumba wampokee kwa mikono miwili, kwa kichwa na miguu, yeye na wafuasi wake wote.
D. KUHAMA MASAHABA KWENDA MADINA
Tumekwisha kuona ya kuwa Waislamu 75 walimjia Mtume (s.a.w.) kutoka Madina katika mwezi wa March 622, na walipokuwa wakenda zao walimpa ahadi kuwa wao wako tayari kwa kumpokea na kumhifadhi yeye na watu wake wakiwasili huko Madina. Basi mara Mtume (s.a.w.) alipopata habari kuwa wale 75 wamekwishafika kwao salama, aliweta Masahaba zake akawaambia: “Mwenyezi Mungu keshakupatieni mahala pazuri na pa amani pa kuweza kwenda kukaa na kuendesha dini yenu bila ya kuteswa na yoyote. Mahala huko ni Madina nimekwishapata habari kuwa ndugu zenu wako tayari kukupokeeni kwa hali na mali, basi kila aliyetayari na aondoke leo kabla ya kesho, kwani ndugu zenu huko wamesimama mikono wazi wanangoja kukupokeeni”. Hazikupita siku mbili tatu baada ya Mtume (s.a.w.) kusema hivi ila baadhi ya Masahaba walikuwa wamekwisha kuwa njiani wanakwenda zao Madina. Mtume (s.a.w.) aliwaambia maneno haya mwanzo wa Mfunguo nne, mwaka wa 13 tangu kuja Utume na katika mwezi wa April, 622. (Waarabu wanaanza mwaka wao mpya kila Mfunguo nne)1.
E. MASAHABA WA MWANZO WALIOHAMIA MADINA
Masahaba wa mwanzo kwenda kuhamia Madina ni hawa nitakaowataja sasa hivi. Nawataja kwa mpango wa kufuatana kutoka kwao Makka, ingawa wengine walikamatwa na jamaa zao njiani wakarejeshwa kwao Makka, wakafungwa huko mpaka Makka ilipotekwa na Waislamu, ndipo walipopata uhuru wao tena. Masahaba wenyewe ni hawa:-
1-2. Bwana Abu Salama na mkewe Bibi Hind bint Umayya. Wote wawili ni katika Bani Makhzum, na ni watoto wa mashangazi zake Mtume (s.a.w.) (au Bibi Hind ni mtoto wa kambo tu). Vilevile huyu Bwana Abu Salama alikuwa ndugu yake Mtume (s.a.w.) kwa kunyonya.
3-4. Bwana Amr bin Rabia pamoja na mkewe – Bibi Leyla –.
5. Bwana Ammar bin Yasir.
6. Bwana Bilal bin Rabah. – Mhabushia –. Ambaye mwisho wake alikuwa muadhini wa Mtume (s.a.w.) katika mji wa Madina, naye ndiye mtumwa wa mwanzo kusilimu.
7. Bwana Saad bin Abi Waqqas bin Waheyb bin Abd Manaf. – Bani Zuhra –. Na ni jamaa sana na mama yake Mtume (s.a.w.). Bibi Amina bint Wahb bin Abd Manaf, alikuwa ni mjukuu khasa wa baba yake mdogo mama yake Mtume (s.a.w.).
8-28. Sayyidna Umar bin Al Khattab. Yeye aliwachukuwa watu 20 wanyonge katika dhamana yake. Yeye tu pake yake ndiye aliyeondoka Makka mchana – na watu wanamwona1 –. Ama wote waliosalia walikuwa wakitoka usiku tu, na mchana wakijificha.
29. Bwana Ayyash bin Rabia – Bani Makhzum –. Ni mtoto wa baba yake mdogo Abu Jahl na ni ndugu yake khasa mama mmoja naye.
30-32. Sayyidna Uthman bin Affan na mkewe – Bibi Ruqayya bint Nabii Muhammad (s.a.w.) – na mtoto wao Bwana Abdalla aliyemzaa walipokuwa nchi ya Mahabushia. Na wengi wengineo wasiokuwa hawa, ambao idadi yao mwisho wake ilifikilia baina ya 150 mpaka 200.
Watu hawa waliondoka wao na roho zao tu na mali yalio mepesi kuchukulika. Ama vitu vyao vyengine vyote waliviacha Makka, vikatawaliwa na jamaa zao wa kikafiri. Hapana Sahaba yoyote – ila Sayyidna Uthman – aliyeweza kuchukuwa mali yake yote, mali ya Sayyidna Uthman yasioweza kuchukulika yalinunuliwa na jamaa zake, wakampa pesa akachukua akenda zake.
Hapakusalia mtaa wowote katika mji wa Makka ila ulikuwa na watu waliouhama kwenda Madina, na ile iliyokuwa ikikaliwa na Bani Madh’un, Bani Bukeyr, Bani Jahsh na Bani Ghannam, ilikuwa mitupu haina ndudu ya mtu, kwani wote waliokuwa wakikaa mitaa hii walikuwa Waislamu. Mitaa yao si kama mitaa tunayoijua sasa, ilikuwa midogo sana.
F. MKUTANO WA MAKURESHI KWENYE NYUMBA YA MASHAURI
Haikupindukia miezi miwili tangu Masahaba walipoanza kuhama Makka ila wote walikuwa wamekwisha kuhama – alisalia Mtume (s.a.w.) na watu wachahe tu katika Masahaba zake –. Miongoni mwao ni Sayyidna Abubakr na Sayyidna Ali. Makureshi walipoona haya waliogopa sana. Wakachelea asije na yeye Mtume (s.a.w.) akenda huko ikawa Madina yote nzima chini ya amri yake, wakaona wafanye shauri upesi, wasije mwisho wakajuta.
Akaondoka Abu Jahal akatafuta vijana watukufu wa Kikureshi ambao hawana damu ya Kibanii Hashim hata chembe ili akafanye nao mashauri katika “Dar Nadwa”. Aliwaalika vijana 14:-
-
Katika Bani Umayya. 1. Katika Bani Makhzum.
-
Katika Bani Naufal. 2. Katika Bani Sahm.
-
Katika Bani Abdid Dar. 1. Katika Bani Jumah
3. Katika Bani Asad1.
Walitoa shauri nyingi katika mkutano wao huo, na zote hazikukubaliwa na watu wote, ila moja ya mwisho tu. Shauri zenyewe ni:-
1. Kuwataka Makureshi wamfunge Mtume (s.a.w.) peke yake katika chumba2. Au
2. Wamzibe macho wamfunge mikono kwa kamba barabara, kisha wampandishe juu ya ngamia aliyetiwa vitunga vya macho asione njia, aachiwe ahangaike naye majangwani mpaka afe kwa njaa na kiu na jua3. Au.
Dostları ilə paylaş: |