G. KUJA MADINA WATU WA MTUME (S.A.W.) NA WA SAYYIDNA ABUBAKR
Tumekwisha kuona kuwa Mtume (s.a.w.) alimwacha Sayyidna Ali Makka, ili awarejeshee watu amana zao. Sayyidna Ali alisalia Makka muda wa siku 4 tangu kuondoka Mtume (s.a.w.), akawa anampelekea kila mtu amana yake iliyokuwa kwa Mtume (s.a.w.). Hata iliposalia siku 1 kuondoka kwenda Madina alipanda juu ya jabali akasema: “Yoyote mwenye kuweka amana kwa Nabii Muhammad (s.a.w.) naaje achukue, kabla sijaondoka Makka”. Hata usiku wa siku yane ulipoingia amana zote alikuwa keshazirudisha kwa wenyewe haikusalia hata sindao moja. Papo hapo akamkabidhi Bwana Abbas watoto wa Mtume (s.a.w.), akatoka kwa miguu saa hiyo hiyo akenda Madina. Usiku kucha alikuwa akenda, mchana ukiadia akitafuta pango akajitia kupumzika machofu ya mwendo wa usiku kucha. Alichagua kwenda usiku na kupumzika mchana kwa ajili ya kuchelea kukamatwa na Makureshi, au na watu waliowekwa kuwakamata watakaokuwa wanakimbia kwenye mji wa Makka, alikwenda vivyo hivyo mpaka akafika Madina kabla ya Mtume (s.a.w.) hajaondoaka Qubaa. Alifika taabani kapasuka nyayo na kavimba miguu. Mtume (s.a.w.) alipomwona alimwonea huruma sana, akamkumbatia na akampulizia dua. Haukupita muda ila machungu yote yale yakapotea, na miguu ikanywea, akafuatana na Mtume (s.a.w.) pamoja na Masahaba wengine wakenda Madina.
Mtume (s.a.w.) alipofika Madina alimtoa Bwana Zayd bin Haritha na Bwana Abu Rafy wafuatane na Bwana Abdalla bin Arkat – kiongozi cha Mtume (s.a.w.) na Sayyidna Abubakr – wende Makka wakawachukue watu wa Mtume (s.a.w.) na wa Sayyidna Abubakr. Sayyidna Abubakr aliwapa watu hawa dirham 500 (kiasi cha shilingi 250)1 ili wanunue watakavyohitajia katika hiyo safari yao ya kuwaleta watu wake na watu wa Mtume (s.a.w.).
Walipofika Makka waliwachukua watu wa Mtume (s.a.w.) nao ni:-
1. Bibi Sawda bint Zam’a – mkewe Mtume (s.a.w.) – .
2-3. Bibi Baraka – yaya yake Mtume (s.a.w.) – pamoja na mwanawe. Bwana Usama bin Zayd bin Haritha.
4-5. Bibi Ummu Kulthum na ndugu yake Bibi Fatma.
6. Bibi Fatma bint Asad bin Hashim – mama yake Sayyidna Ali – na ndiye aliyemlea Mtume (s.a.w.).
Bwana Usama bin Zayd alikuwa huru wa Mtume (s.a.w.) aliyezaliwa na yaya yake, Bibi Baraka, na mtumwa wake mwengine, Bwana Zayd bin Haritha. Na juu ya kuwa yeye ni mtumwa, Mtume (s.a.w.) alikuwa akimtukuza sana, hata alimfanya ni amirijeshi wa jeshi kubwa alilokuwa analipeleka Sham, na hali ya kuwa ndani ya jeshi hili walikuwamo Sayyidna Abubakr na Sayyidna Umar na mabwana wengi wakubwa. Mtume (s.a.w.) alifanya hivi ili kuonyesha kuwa Uislamu hauchagua baina ya muungwana na mtumwa, wala baina ya mtoto na mtu mzima, bali hutazama uwezo wa yule mtu tu, kwani huyu Bwana Usama alikuwa mzalia, mweusi mwenye pua ya kupondeka sana, na alikuwa kijana wa miaka 18 tu alipopewa uamiri huo, lakini alikuwa hodari wa kutosha.
Ama watu wa Sayyidna Abubakr waliochukuliwa kuja Madina ni:-
1. Bwana Abdalla bin Abubakr – aliyekuwa akiwaletea habari za Makureshi walipokuwa pangoni – .
2. Bibi Asmaa bint Abubakr – aliyekuwa akiwaletea chakula – .
3-4 Bibi Aysha na mama yake – Bibi Ummu Ruman – mke wa pili wa Sayyidna Abubakr. Ama mke wa kwanza mama yake Bibi Asmaa yeye hakuhama, kwani alikataa kusilimu. Ama mama yake Sayyidna Abubakr hakuweza kuhama kwani mumewe alikuwa hakusilimu na mtu mzima sana.
Wakati huu Bibi Asmaa alikuwa na mimba ya awali kwa mumewe Bwana Zubeyr, akaizaa mimba yake hii Qubaa kabla ya kufika Madina. Mtume (s.a.w.) akaja Qubaa kumfungua koo mtoto, akamwombea dua na akampa jina la Abdillahi bin Zubeyr ambaye mwisho wake alikuwa shujaa mkubwa na Mfalme mkubwa wa Kiislamu.
H. KUPANGWA UDUGU BAINA YA MUHAJIR NA ANSAR
Muhajir walipofika Madina walikuwa maskini hohe hahe, hawana mbele wala nyuma, hawana chakula cha kukila wala maskani ya kukaa, hawana pesa za kuolea wala nguo za kuvaa, kwa hivyo Mtume (s.a.w.) akawakusanya Muhajir wote akachagua katika Ansar wanaojiweza kidogo kiasi cha ile idadi ya Muhajir, kisha akapiga kura. Kila mmoja katika wale Ansar likamwangukia jina moja la Muhajir ili awe ndugu yake, udugu huo ulipopatikana kwa kura ulifanywa kama udugu wa kuzalika. Ikawa kuko kurithiana kwa sudus (1/6) baina ya Muhajir na ndugu yake Ansar. Mungu alisema katika sura ya 4 (Suratun Nisaa) Aya ya 33:
Na wale mliopanga nao udugu wapeni fungu lao1
Hukumu hii ya kurithiana baina ya udugu wa Kiansar na udugu wa Kimuhajir, ilidumu mpaka mwaka wa 8 A.H. – 630 – wakati waliposilimu watu wa Makka wote na wa Bara Arabu nzima takriban. Hapo ndipo iliposhuka Aya ya 75 katika Sura ya 8 (Al Anfal) kuvunja hukumu hii iliyotangulia. Aya yenyewe ni hii:
Na jamaa wa kuzalikana ni wenye kustahiki kurithiana wenyewe kwa wenyewe kuliko kurithiana na Waislamu wengine1.
Ansar walifurahi sana kuwapata ndugu hawa wa Kimuhajir. Kila mmoja katika wao akagawa mali yake sehemu mbili – sehemu moja akampa ndugu yake wa Kimuhajir na sehemu ya pili akasalia nayo mwenyewe –. Vile vile Ansari wengine waliokuwa na wake 2 au 3 waliwaacha baadhi ya wake zao ili wawaoze wake hao ndugu zao wa Kimuhajir waliokuwa hawana wake. Walikuwa wakifanya haya yote kwa radhi zao bila ya kuamrishwa na yoyote. Hata Mungu akawasifu katika Quran kwa ukarimu huu, akasema katika Sura ya 59 (Suratul Hashr) Aya ya 8 na ya 9:
Wastaajabieni mafakiri wa Kimuhajir waliotolewa kwenye majumba yao na mali yao, wakitaka rehema za Mwenyezi Mungu na radhi zake, na wakiazimia kunusuru dini ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake hao ndio wenye kusadikisha kweli Uislamu wao2.
(Suratul Hashr: Aya ya 8).
Na vile vile wastaajabieni wale wenye kukaa Madina kabla ya Muhajir na wakatakasa nia katika Uislamu wao, hali ya kuwa wanawapenda wenye kuhama wakaja kwao, wala hawana haja yoyote katika nafsi zao, japo kuwa wao wenyewe wana uhitaji mkubwa. Na wenye kuhifadhiwa na ubakhili wa nafsi zao hao ndio wenye kufuzu1.
(Suratul Hashr: Aya ya 9).
Haya ni baadhi ya mambo ambayo Ansar wakiwafanyia Muhajir. Lau kuwa si wema wao huo, Muhajir wa kwanza wasingeweza kukaa huko, wala wasingetamani watu wengine nao kusilimu na kuja kukaa Madina. Ndiyo maana Mtume (s.a.w.) akasema: “Miongoni mwa alama za Uislamu wa mtu ni kupenda Ansar”.
Muhajir wote Mtume (s.a.w.) aliwapangia ndugu na Ansar, ila Sayyidna Ali bin Abi Talib, Mtume (s.a.w.) alimwambia: “Wewe ni ndugu yangu mimi, duniani na akhera”2. Sayyidna Abubakr ndugu yake alikuwa Bwana Kharija bin Zuheyr – katika ukoo wa Khazraj na tumbo la Bani Harith –. Sayyidna Umar ndugu yake alikuwa Bwana Itban bin Malik – katika ukoo wa Khazraj na katika tumbo la Bani Salim bin Auf –. Sayyidna Uthman ndugu yake alikuwa Bwana Aus bin Thabit – katika ukoo wa Khazraj na tumbo la Bani Najjar –. Huyu Bwana Aus alikuwa ndugu yake khasa Bwana Hassan binThabit – Shairi mkubwa wa Mtume (s.a.w.) –.
I. KUAMRISHA MTUME (S.A.W.) BAADHI YA MASAHABA ZAKE KUJIFUNDISHA LUGHA YA KIYAHUDI
Tumekwisha kuona katika sura zilizopita kuwa takriban nusu ya wakazi wa Madina walikuwa Mayahudi. Walikuwa na dini ya peke yao na lugha ya peke yao, ingawa walikuwa wakisema Kiarabu, wala Waarabu wa kabla ya Uislamu hawakushughulika kujifundisha lugha ya Kiyahudi, laikini Mtume (s.a.w.) alipokuja Madina aliona kuwa ni lazima kujifundisha lugha ya watu hawa, alikuwa mara nyingi akisema: “Mwenye kujua lugha ya watu wengine ataaminika3 na vitimbi vyao” kwa hivyo alichagua Masahaba wawili wajifundishe lugha yao, wawe na masikio makali ya kusikiliza minongono ya shari watakayokuwa wanainongona Mayahudi. Kwani Mayahudi waliichukia sana dini hii mara tu ilipodhihiri. Masahaba wenyewe waliochaguliwa kujifunza lugha hii ni:-
1. Bwana Zayd bin Thabit – katika Ansar – .
2. Bwana Usama bin Zayd bin Haritha – katika Muhajir – .
J. KUSILIMU KWA BAADHI YA WANAVYUONI WA KIYAHUDI
Mtume (s.a.w.) alikpokuja Madina akaona kuwa karibu Waarabu wote wa Madina wamekwisha kusilimu, alianza kuingiana na Mayahudi, akiwasemesha kuingia katika hiyo dini aliyokuja nayo, akawa kila siku anashindana nao katika masuala ya dini, hata mwisho wake akaweza kuwapata watu kidogo kuingia katika dini ya Kiislamu bila ya nguvu zozote. Walisilimu walipoona hoja za Mtume (s.a.w.) zina nguvu nyingi, na wengi katika wao walikuwa ima katika wanavyuoni wao tu au na matajiri wao pia. Miongoni mwa watu hao ni:-
1. Bwana Abdalla bin Salam pamoja na watu wote wa nyumbani kwake, alikuwa mwanachuoni mkubwa wa Kiyahudi, na bwana mkubwa wa ukoo wake, Bani Qaynuqai, jina lake la asili lilikuwa ni Husweyn, aliposilimu Mtume (s.a.w.) alimgeuza jina akamwita Abdalla.
2. Bwana Mukhayriq: Alikuwa mmoja katika wanavyuoni wa Kiyahudi na tajiri mkubwa wa Kibani Nadhir – ukoo mmoja katika koo tatu tukufu za Mayahudi waliokuwa Madina – aliposilimu mali yake yote aliwaandikia Waislamu waliokuwa siku hizo, kwani hakuwa na jamaa wa kumrithi.
3-4 Bwana Thaalaba bin Saya na ndugu yake, Bwana Usayd bin Saya
5. Bwana Asad bin Ubeyd
6. Bwana Yami bin Umar
7. Bwana Maymun bin Yamin
8. Bwana Abu Said bin Wahb
SURA YA TISA
VITA VYA JIHADI NA MAKUSUDIO YAKE
VITA VYA JIHADI NA MAKUSUDIO YAKE
Makusudio ya Vita vya jihadi ni kupigana Waislamu hata wafikilie katika hali ya kutofitinishwa tena na kuteswa kwa ajili ya dini, iwe dini ya Kiislamu kama dini nyenginezo inafanya ibada zake kwa huria. Wakisha kufikilia hali hii basi hawana ruhusa ya kupigana na yoyote asiyewapiga. Shahada ya maneno yangu niliyoyasema ni Aya 193 katika Sura ya pili (Suratil Baqarah), na tafsiri yake ni:
Piganeni nao hata kusiwepo kuteswa kwa ajili ya dini, na dini iwe huru, wakijizuilia na kukuteseni, basi hapana kufanya jeuri tena1.
Wala haukuweza Uislamu kufikilia hali hii katika nchi ya Bara Arabu ila baada ya kupiganwa vita 65, 27 katika hivyo yeye mwenyewe Mtume (s.a.w.) alihuduria.
Tumekwisha kuona katika sura zilizopita namna nyingi za mateso waliyokuwa makafiri wakimtesa Mtume (s.a.w.) na Masahaba zake, hata ikawa ndiyo sababu ya kuhama baadhi ya Masahaba kwenda katika nchi ya Mahabushia, na baadhi nyengine pamoja na Mtume (s.a.w.) kwenda Madina, lakini yote haya hayajawaombea, walifuatiwa huko huko kwenye nchi ya Mahabushia na mji wa Madina. Mara mbili Makureshi walipeleka watu wao (delegates) kwa Mfalme wa Mahabushia ili kumtia maneno na kumkoroga moyo juu ya Waislamu, lakini hazikufaa kitu fitna zao. Ama huko Madina ndiko walikokufanya mahali pa kupitisha kila namna ya vitimbi vyao juu ya Waislamu. Katika mlango unaofuata huu nitaandika badhi ya vitimbi walivyokuwa makafiri wakimfanyia Mtume (s.a.w.) na Masahaba zake ingawa wao walikuwa hawajaanza kwa chochote kile.
A. VITIMBI AMBAVYO MAKAFIRI WA KIARABU WAMEMFANYIA MTUME (S.A.W.) NA MASAHABA ZAKE WALIPOKUWA MADINA
1. Kurz bin Jabir: Bwana mkubwa wa Kikureshi. Alikuja kwa siri yeye na baadhi ya wenzake mpaka kwenye viunga vya Madina wakawakamata ngamia, mbuzi na kondoo wote waliowakuta, wakakimbia nao mpaka Makka.
2. Abu Sufyan: Bwana mkubwa kabisa wa Kikureshi. Alikuja na watu 200 wa Kikureshi wakashuka kwenye viwanja vya Madina, wakatia moto mkubwa, wakawaua Masahaba wawili, na wakachukua kila wanyama waliowapata, nao ni ngamia 200.
3. Huyu huyu Abu Sufyan alimpeleka shujaa mkubwa Madina kwa siri ili amuuwe Mtume (s.a.w.), lakini hakupata nafasi hata chembe. Akakata tamaa akarejea.
4. Wakubwa wa Bani Lihyan, na wa Bani Adhl na wa Bani Qara, walikuja kwa Mtume (s.a.w.) wakataka awape baadhi ya Masahaba wende wakawafundishe dini, kwani wanatumai kuwa watu wao watasilimu. Mtume (s.a.w.) akawapa watu 6. Walipofika nao waliwageukia wakawatatiza makamba ili kwenda kuwauza Makka kwa Makureshi wapate kuwachinja wakate hamu yao. Wane katika hao walifanya ukaidi kwenda wakawaua papo hapo, na wawili walisalimu amri wakenda nao Makka wakawauza, na huko wakawaua na wakasulubiwa kwa shangwe kubwa.
5. Amr bin Malik: Bwana mkubwa kabisa wa Kibani Amr. Alisilimu akataka kwa Mtume (s.a.w.) ampe watu 70 kwenda kuyafundisha matumbo yote ya kabila yake kubwa dini hiyo ya Kiislamu. Mtume (s.a.w.) alifurahi, akachagua watu 70 mahodari kwa dini kwenda huko, mmoja katika 70 hao alikuwa Bwana Amr bin Fuhyra – yule mtumwa wa Sayyidna Abubakr amaye alikuwa akiwaletea maziwa pangoni – Huyu Bwana Amr bin Malik alisalia kwa Mtume (s.a.w.) na akawapa Masahaba hawa 70 barua wamfikishie mtoto wa ndugu yake Amr bin Tufayl bin Malik. Bwana huyu alipoipata barua hii hakuifuata hata chembe, bali aliamrisha matumbo matatu ya Kibani Sulaym yawaue watu hao wote, matumbo hayo yakawazunguka mara moja, yakawachinja kama kuku.
6. Uyayna bin Hisn: Mkubwa wa Bani Fazara wote. Alikuja na watu 40, juu ya farasi mpaka kwenye viunga vya Madina, wakachukua ngamia 40, wakamwua mlindaji na wakamchukua mkewe – Bibi Leyla – Walimchukua mwanamke huyu mpaka kwao Najd, wakamfanya mchungaji wanyama. Mwisho bibi huyu alipata nafasi akakimbia akaja zake kwa Mtume (s.a.w.) .
7. Watu wanane katika Bani Uql na Bani Urayna walikuja kwa Mtume (s.a.w.) wakajidai kusilimu, wakamwomba Mtume (s.a.w.) wakae huko huko Madina, Mtume (s.a.w.) akawapa ruhusa. Mwisho wakashikwa na ugonjwa wakadhoofika sana, Mtume (s.a.w.) akawaambia wende kwenye viunga vya Madina kwa mchungaji mmoja wa ngamia wa Zakaa. Alikuwa akiitwa Bwana Yasr, naye atakuwa akiwapa maziwa kunywa asubuhi na jioni mpaka wapate uzima warejee Madina. Wakenda huko na yule mchungaji akawapokea kwa uzuri, akawa anawafanyia kama alivyosema Mtume (s.a.w.). Lakini walipopata uzima kidogo tu walimkamata huyu mchungaji miguu na mikono, wakamtoboa macho yote mawili, wakamtoboatoboa ulimi wake kwa miba, na wakamkata viungo vyake vyengine visivyopendezwa kutajwa vitabuni. Baada ya haya wakawachukua ngamia wote hao wakenda nao kwao kwa jamaa zao. Kiunga hiki kilikuwa meli 6 toka mji wa Madina.
8. Habbar bin Aswad na Nafii bin Qays: Mabwana wakubwa wa Kikureshi. Walimchochachocha mikuki Bibi Zaynab bint Nabii Muhammad (s.a.w.) alipokuwa anahama kwenda Madina kwa baba yake, na wakamchochachocha ngamia aliyempanda pia, mpaka akafanya machachari akamwangusha huyu bibi, naye alikuwa na mimba, akaumia sana, akawa mgonjwa siku zote hata ndiyo ikawa sababu ya kufa kwake.
9. Shurahbil bin Amr: Jamaa yake Harith bin Abi Shamir Al Ghassany, Mfalme wa nchi ya Sham. Shurahbil huyu alimwua bure mjumbe wa Mtume (s.a.w.) aliyepewa barua kumletea huyo Mfalme wa Sham. Na mengi mengineyo ambayo yatachukua nafasi kubwa ukitaka kuyaandika. Lakini haya yaliyotajwa yanatosha kuyakinisha uhaki wa Waislamu katika kupigana na hao waliokuwa wakiwatesa kila walipokuwa wanakimbilia.
B. KUONYESHA KUWA UISLAMU HAUKUSIMAMA KWA UPANGA
Watu wengi wanaudhulumu Uislamu kwa kuusingizia kuwa ulitia watu katika dini yake kwa upanga na kuwa watu wote wanaofuata dini hii leo wazee wao walilazimishwa kwa nguvu awali. Lakini huu ni uwongo kabisa, na tarikh ya Quran yashuhudia ya kuwa ni uwongo. Na kamba ya uwongo kama tujuavyo ni fupi, tarikh inatwambia kuwa Dola ya Kiislamu ilitangaa sana zamani, tangu Afrika ya Kaskazini mpaka visiwa vya East Indies kwa urefu, na nchi nyingi katika hizi mpaka leo bado zimo katika Ufalme wa Kiislamu. Basi watu wote wa nchi hizi ni Waislamu mpaka leo? Au walipata kugeuka mara moja zamani wakawa Waislamu, na kisha sasa wamerejea katika dini zao? La kwanza kila mtu anajua kuwa halipo, na la pili halijapata kuwa. Basi vipi wanasema kuwa Waislamu wa mwanzo walilazimisha raia zao kuwa Waislamu? Waislamu wana kanuni ya kuwatoza “Jizya” (Tribute) kwa raia zao wasiokuwa Waislamu. Basi lau kuwa Uislamu unaamrisha kumwua kila asiyekuwa Mwislamu, kanuni hii ya nini kufanywa? Sasa tutazame nchi zilizokuwa katika Dola ya Kiislamu, tuzione ziliamrishwa kutoka katika dini zao?
1. Bani Ghassan na wengi wa Lebanon – Sham – tangu kabla ya zama za Sayyidna Umar wamo katika dini ya Kimasihi1, mpaka leo haijapata kusikilikana kuwa walipata kuachishwa dini yao hiyo tangu wakati ilipotekwa nchi yao zama za Sayyidna Umar mpaka leo.
2. Mayahudi wa Kiyaman tangu ilipotekwa Yaman zama za Mtume (s.a.w.) mpaka leo wamo katika dini yao ya Kiyahudi, hakuna aliyewatesa hata ikawapelekea kuacha dini yao ya Kiyahudi, wametua nyoyo zao zaidi kuliko Mayahudi wanaokaa nchi za Uropa ya Katikati leo.
3. Maqipti (Copts) wa Misr tangu zama za Sayyidna Umar walipoingia chini ya utawala wa Waislamu mpaka leo wanafata dini yao ya Kimasihi. Na idadi yao ni ndogo sana Misr (sita kwa mia ya Waislamu). Na haijapata kusikilikana kuwa walipata kuteswa hata mara moja kwa ajili ya dini yao. Wanaishi kama wanavyoishi Waislamu na wanavaa kama wao.
4. Ma-Asyrian na Masabiina wa Iraq mpaka leo wanafuata dini yao.
5. Ma-Persian walichukua miaka mingi katika kukaa chini ya Dola ya Kiislamu mpaka kusilimu kwao. Wengi walikuwa katika kazi kubwa kubwa za Dola kabla ya kusilimu kwao.
6. Wahispania vile vile ingawa walitawaliwa na Waislamu tangu karne ya 8 mpaka ya 15, lakini hawakulazimishwa kuacha dini yao. Na ipo mifano mingi mingine.
C. TAFSIRI YA BAADHI YA AYA ZA QURAN ZINAZOTAJA JIHADI
Ama Aya za Quran nimechagua kufasiri Aya 9 katika Aya za Sura 5 zilizoshuka Madina wakati Uislamu ulipokuwa na nguvu. Nitazitaja kwa mpango wake ulio Misahafuni. Mungu ameitaja habari hii ya Jihadi mahali 4 katika Sura ya 2 (Suratul Baqara):-
1. Aya ya 190 inasema:
Piganeni kwa ajili ya Dini ya Mungu na wale wanaopigana na nyinyi, wala msifanye jeuri (kwa kuwapiga wasiokupigeni), kwani Mungu hawapendi watu majeuri1.
2. Aya ya 191 inasema:
Wala msipigane nao kwenye ardhi ya Makka mpaka wakupigeni huko, wakikupigeni huko wapigeni2
3. Aya ya 193 inasema:
Piganeni nao mpaka kusiweko kuzuiliwa kufanya dini yenu3
4. Aya ya 256 inasema:
Hapana kulazimishwa kuingia katika dini4.
5. Sura ya 4 (Suratin Nisaa) Aya ya 90 inasema:
Wakijitenga na nyinyi wasikupigeni na wakakufanyieni sulhu , basi hapana njia yoyote aliyokufanyizieni Mwenyezi Mungu kwenda kupigana nao5.
6. Sura ya 8 (Suratul Anfal) Aya ya 61 inasema:
Wakionyesha mapenzi ya kutaka salama, nawe onyesha , na utawakali kwa Mwenyezi Mungu6.
7-8. Sura ya 22 (Suratul Haj) Aya ya 39 na 40 zinasema:
Wamepewa ruhusa nao vile vile wapigane na wale wanaowapiga bure, kwa kuwa wao wamedhulumiwa pasina sababu. Na hakika Mwenyezi Mungu ni mweza wa kuwanusuru2.
(Aya ya 39).
Hao waliotolewa kwao pasina haki yoyote ila kwa ajili ya kunena kuwa Mola wetu ni Mungu tu3.
(Aya ya 40)
9. Sura ya 60 (Suratul Mumtahana au Mumtahina) Aya ya 8 inasema:
Hakuwakatazeni Mungu kuwafanyia wema na uadilifu wale ambao hawajakupigeni kwa ajili ya dini wala hawajakutoeni kwenu4.
Na zipo Aya nyingi sana namna hizi. Kweli haiwezi kukatalika kuwa Uislamu haufuati kawaida, “Akikupiga shavu la kushoto mgeuzie na la kulia” lakini inakatalika kabisa kuwa unaamrisha watu wake kuonea wengine na kuwa hautii watu katika dini yake kwa hoja na dalili, bali kwa nguvu na upanga. Mungu anasema katika Sura ya 16 (Suratul Nahl) Aya ya 125:
Walinganie watu kuendea dini ya Mola wako kwa hikma na nasaha nzuri, na shindana nao kwa mashindano yaliyo mazuri1.
Uislamu haukubali dhila, hauwapendelei watu wake udhalilifu, unawapendelea kila siku wawe watukufu kuliko kila mtu asiyekuwa katika wao. Inawalazimisha wawe tayari kila wakati kumkabili kila adui, Mungu anasema katika sura ya 8 (Suratul Anfal) Aya ya 60:
Wawekeeni tayari (maadui zenu) kila mnachokiweza, nayo ni kila namna ya silaha na mafarasi2.
SURA YA KUMI
VITA VIKUBWA ALIVYOPIGANA NABII MUHAMMAD
VITA VIKUBWA ALIVYOPIGANA
NABII MUHAMMAD (S.A.W)
A. VITA VYA BADR
Tumekwisha kuona kuwa Mtume (s.a.w.) na Masahaba zake walitaabishwa sana katika mji wa Makka, hata ikawapasa katika mwaka wa 5 wa kuja Utume, kwenda nchi ya Mahabushia, na mwaka wa13 kwenda Madina, na mara hii Mtume (s.a.w.) alikuwa pamoja nao. Walitaabishwa kwa kudharauliwa, kwa kuudhiwa, kwa kudhulumiwa mali yao, kwa kupigwa na kwa adhabu nyingi nyinginezo, ambazo nyengine hazifai hata kutajwa hapa, walipokimbia kwenda Madina walikimbia wao tu na baadhi ya nguo zao na vitu vilivyokuwa vyepesi kuchukulika. Ama mali yao yote mengine waliyaacha kuko huko Makka, yakahoziwa na jamaa zao wasiokuwa Waislamu. Hata nyumba alizokuwa akikaa Mtume (s.a.w.) na watu wake pia ziliuzwa.
Walipokimbilia Madina walidhani kuwa watasalimika na mateso na jeuri za Makureshi, waishi maisha ya raha na utulivu, na waabudu Mungu kama wanavyotaka. Lakini wapi! Masahaba hawajakaa siku nyingi Madina ila asubuhi moja waliletewa habari kuwa jana usiku walikuja Makureshi kwenye viunga vya Madina na wamechukuwa kila wanyama waliokuwa huko. Hazikupita siku nyingi sana tena ila waliletewa habari asubuhi nyengine kuwa jeshi la Makureshi jengine lilikuja usiku kwenye viunga vya Madina na likakata mitende yote iliyokuwako huko, likachukuwa kila wanyama waliowapata baada ya kumchinja mchungaji wao na mwenziwe, na baadae wakakiwasha moto kiunga kizima.
Baada ya haya na mengineyo Waislamu walipewa ruhusa nao, kupigana kwa ajili ya kujikinga nafsi zao. Siku moja katika mwezi wa Ramadhan baada ya miezi 19 tangu Mtume (s.a.w.) kuhamia Madina, Mtume (s.a.w.) alipata habari kuwa kuna msafara wa mali mkubwa wa Kikureshi unakuja kutoka Sham, na hauna wa kuulinda ila watu 40 tu, na mkubwa wao ni Abu Sufyan, ambae ndiye aliyekuwa mkubwa siku waliyokuja kwenye viunga vya Madina na wakachukua wanyama na wakamwua mchungaji wao na mwenziwe. Mtume (s.a.w.) aliwahadithia habari hii Masahaba akawaambia: “Kama walivyotuzuilia kwenda Makka na wakatutesa kwa kila namna ya mateso basi na sisi tuwazuilie misafara yao na kupita kwenye mji wetu – Madina –” . Wakamfuata watu 313 – 83 katika Muhajir na waliosalia katika Ansar, wakaondoka Jumaatano mwezi 8 Ramadhan kuufuatia msafara huo. Hawakuwa na wanyama wa kupanda katika msafara wao ila ngamia 76 na farasi 2 tu, wakawa wanapokezana kupanda. Kila ngamia 1 alikuwa na watu wake makhsusi wa kupanda kwa zamu akishuka huyu apande huyu. Ngamia aliyepewa Mtume (s.a.w.) alikuwa apande kwa zamu baina yake na Sayyidna Ali na Bwana Marthad. Ngamia wa Sayyidna Abubakr alikuwa akimpanda kwa zamu baina yake, Sayyidna Umar na Bwana Abdur Rahman bin Auf.
Abu Sufyan kwa ile jeuri yake aliyowafanyia watu wa Madina – aliogopa sana alipokuwa anaikurubia Madina – akaweka majasusi kumsikilizia habari za watu wa Madina, majasusi wake wakamjia wakampa habari kuwa Mtume (s.a.w.) na Masahaba zake wameondoaka Madina ili kuwafuatia wao. Abu Sufyan aliogopa sana, akamkodi Bedui mmoja pale pale aliyehodari kwa kupanda ngamia, ili ende Makka akawete Makureshi waje wahami mali yao ambayo yalikuwa yanapata kiasi cha Paundi 20,000. Alimkodi huyu Bedui kwa Paund 14. Bedui huyu akatoka mbio mpaka Makka hasiti ila kwa dharura kubwa. Kufika tu Makka alipiga kelele juu ya jabali moja kubwa kuwapa habari hiyo Makureshi, Makuresi walifurahi kwani waliona ndio njia ya kwenda kumsaga Mtume (s.a.w.) na watu wake, wasimsaze1 hata mmoja ili waondoshe kabisa dini aliyokuja nayo.
Kila Kureshi mtukufu alivaa nguo zake za chuma papo hapo, akatoka akasimama kwenye uwanja wa Al Kaaba anangoja wenzake. Hazijapita saa nyingi ila walikuwa wamekwisha kusimamisha jeshi la watu 1,000 na ngamia 700 na farasi 100! Watu 600 katika 1,000 hao walikuwa wamevaa nguo za chuma za vita. Hakusalia mtukufu yoyote katika Makureshi ila alivalia kwenda huko, ili apate hishma ya kumwua Nabii Muhammad (s.a.w.) na Masahaba zake.
Watu 12 katika hao Mabwana wakubwa wa Kikureshi walidhamini kulilisha bure jeshi hilo toka kutoka kwake mpaka kurejea. Waliona kuwa inahitajia kuchinja ngamia 10 kila siku. Miongoni mwa hao walaiodhamini kulilisha jeshi hili ni Bwana Abbas bin Abdul Muttalib – Baba yake mdogo Mtume (s.a.w.) – Utba bin Rabia – babu yake Bwana Muawiya kwa upande wa mama yake – Abu Jahl – Farauni wa Umma huu – na Hakym bin Hizam – mtoto wa ndugu yake Bibi Khadija - .
Hili jeshi la Kikureshi lilipokuwa likiondoka lilichukuwa wanawake wengi waimbaji na wachezaji ili waimbe na wacheze muda wa siku tatu baada ya kuwaua watu wa Nabii Muhammad (s.a.w.) wote na yeye mwenyewe pamoja, na kwa ajili ya kuwazidisha mori hao Makureshi watapokuwa wanapigana, ili wasipate kukimbia vita vitaposhika moto. Makureshi walikuwa na yakini kuwa watashinda, ndio maana wakatoka na shangwe hilo la wanawake.
Makureshi baada ya kuona jeshi lao limekamilika, waliondoka hao wanakwenda upande wa Madina – na bendera yao ya vita kaichukua Bwana Saib bin Yazid – babu wa nne wa Imam Shafi –, kwani alikuwa hakusilimu bado siku hiyo. Mambo yote hayo yaliyotokea Makka. Mtume (s.a.w.) na Masahaba zake hawakuwa na habari nayo wao wakijidhani kuwa wanakwenda kuwazuilia hao watu 40 waliokuwemo katika msafara, basi hawakuwa na habari kuwa Abu Sufyan amekwisha wasikia na amegeuza njia na amepeleka mjumbe kuweta watu wa Makka, na kuwa hao watu wa Makka wako njiani wanakuja kuwapiga kwa jeshi lililokubwa zaidi ya mara tatu kuliko lao. Hawakupata habari hii ila wako karibu na mtaa wa Badr. Pale pale Mtume (s.a.w.) aliwakusanya Masahaba zake akawataka shauri ya kufanya katika 2 haya:-
-
Waufate huo msafara wote hao kwa njia yake hiyo mpya uliopita sasa, na baada ya kuwapokonya mali yao wakimbie wende zao Madina?
-
Au waendelee na njia yao hii hii wakutane na Makureshi wapigane nao?
Wengi waliipenda shauri ya kuufata huo msafara, khalafu wakimbilie Madina wakastarehe, kwani walipoondoka Madina hawajaondoka kwa nia ya vita, kwa hivyo wao hawajavalia kivita. Lakini Mtume (s.a.w.) hakuwafiki rai hii. Aliona kuwa wakifuata msafara halafu jeshi la Makureshi litawafata huko huko, lichanganyike na watu wa msafara lizidi wingi wake. Na aliona vile vile Makureshi watakapokuwa wanapigana na mali yao yako mbele yao watazidi kupata ushujaa, wasikubali kukimbia upesi. Lakini juu ya hayo Masahaba wegine walishika rai yao ile ile. Pale pale aliondoa Sayyidna Abubakr akaitilia nguvu rai ya Mtume (s.a.w.). Kisha akainuka Sayyidna Umar akaitilia nguvu vile vile rai aliyoitoa Mtume (s.a.w.) na Sayyidna Abubakr. Baadae akaondoka Sahaba mmoja aliyekuwa akiitwa Bwana Miqdad akasema: “Ee Mtume wa Mwenyezi Mungu! Fanya shauri unayoiona sisi sote tuko pamoja nawe. Wallahi hatutasema kama walivyosema Mayahudi kumwambia Nabii Musa, ‘Nenda wewe na Mungu wako mkapigane, na sisi tutakaa hapa kukungojeni’ Lakini sisi Waislamu tutasema: ‘Nenda wewe na Malaika wa Mola wako mpigane na makafiri, na sisi tutakuwa mkono mmoja na nyinyi katika kupigana nao!’”. Mtume (s.a.w.) alifurahi sana na maneno yake na akamwombea dua. Lakini Mtume (s.a.w.) hakutoa amri yake vile vile, kwani alikuwa hataki kufanya jambo ila kwa radhi ya Masahaba zake wote, walio Muhajir na Ansar. Wote hawa watatu waliosema hapa ni Muhajir. Pale pale aliinuka Bwana mkubwa wa Kiansar – Bwana Saad bin Muadh – akamwambia Mtume (s.a.w.): “Ee Mjumbe wa Mwenyezi Mungu! Sisi sote tumekuamini, na tunakusadiki kuwa kila unalotwambia ni haki, basi fanya kama unavyoona wewe. Sisi tuko tayari kukufuata, hata lau ungelijitumbukiza ndani ya bahari ukawa uanaivuka kwa miguu tungevuka pamoja nawe, asingesalia yoyote”. Hapo Mtume (s.a.w.) ndipo alipowaamrisha waifuate njia wanayotokea Makureshi.
Waislamu wakenda mpaka kwenye mtaa wa Badr. Wakatua hapo penye visima vya maji. Ikawa maji yote ya mtaa ule wanayo wao. Tena Masahaba wakamjengea Mtume (s.a.w.) kiriri ambacho ataweza kuwamo humo aone vipi vita vinapiganwa, na aweze kuashiria kwa amri zake wakati wa vita. Hata wakati wa usiku Mtume (s.a.w.) akapanda kwenye kiriri yeye na Sayyidna Abubakr. Usiku kucha Mtume (s.a.w.) alisimama kusali na kuomba dua wapate kushinda. Akisujudu sijda ndefu ndefu huku anaomba dua.
Masahaba wengine walilala chini karibu na kiriri hiki. Hata asubuhi baada ya kusali wakaliona hilo jeshi la Makureshi linakuja, lakini limepungua baadhi ya watu wake. Mtume (s.a.w.) alisimama akaelekea kibla akamwomba Mungu akasema: “Hawa Makureshi wanakuja na mafarasi wao na jeuri yao, wanakuja ili waniangamize mimi na hawa watu wachache wanaokuabudu! Naomba unipe leo ile nusura uliyonambia kuwa utanipa”. Aidha aliomba dua nyenginezo, na Sayyidna Abubakr akiitikia “Amin”
Jeshi la Makureshi lilikuwa limepungua kidogo wakati huu, na sababu ya kupungua kwake ni: Abu Syfyan – alipojua njia anayopita Mtume (s.a.w.) na Masahaba zake – aligeuza njia nyengine na akasalimika na mali yote kamili. Alipoona hivi aliwapelekea mjumbe wakuu wa jeshi la Makureshi, kuwataka warejee na jeshi lao, kwani wo wametoka kuyahami mali yao ambayo yamekwisha kusalimika. Basi nini faida ya kupigana? Wakubwa wote wa kabila za Kikureshi hawajakubali shauri hii ya Abu Sufyan, wakakataa kurejea wakawa hao wanakwenda zao Badr. Mkubwa wa Bani Zuhra tu ndiye aliyekubali, akarejea yeye na watu wake wote, ndiyo maana ikawa wakati huu lile jeshi la Kikureshi limepungua kidogo. Ukoo wa Bani Zuhra ndio ukoo wa mama yake Mtume (s.a.w.), na vile vile ukoo wa Bani Adiy ulirejea – ukoo wa Sayyidna Umar – .
Makureshi walipokaribiana na Waislamu wakaona maji yao, walikuja mbio ili kuyateka wanywe, Masahaba wakataka kuwazuilia lakini Mtume (s.a.w.) aliwakataza. Baada ya kukabiliana hivi, mtoto wa ndugu yake Bibi Khadija anayeitwa Bwana Hakim bin Hizam, ambaye ni mmoja katika wale Makureshi waliodhamini kulisha jeshi lao, aliondoka akamwendea Utba bin Rabia, aliyekuwa mtukufu kuliko Makureshi wote waliokuwa Makka siku hizo. Akamwomba awatie maneno Makureshi warejee kwao wasipigane na Nabii Muhammad, kwani wote ni wenyewe kwa wenyewe. Utba akainuka akasema: “Enyi Makureshi! Na turejee tusipigane na Muhammad, kwani tukiwashinda tukawaua, hapana mmoja katika sisi atakayeweza kumnyanyulia jicho mwenzake kumtazama, kwani kila mmoja katika sisi atakuwa kamwua mtoto wa mwenziwe au baba yake au mjomba wake au bin ami yake, basi shauri yangu mie ni kurejea na kuwaachia Waarabu wengine wawaue. Na lawama yote ya kurejea leo nirejeshewe mimi. Semeni kuwa mimi ni mwoga, nimekurejesheni baada ya kuwa mko tayari kuwasagasaga” Pale pale akainuka Abu Jahal akawakataza Makureshi kufuata shauri ya Utba. Alisema: “Mwongo huyo anaogopa mwanawe tu aliyopo upande wa Muhammad asiuliwe. Haogopi watu wengine, haturejei popote baada ya kufika hapa. Tutawapiga sasa hivi tuwachinjechinje tufanye karamu tuimbe na tucheze hapa kwenye mtaa wa Badr muda wa siku tatu mpaka Waarabu wote wapate habari ya ushujaa wetu”.
Baada ya kuinuka huyu Abu Jahl na kuvunja ile rai ya Utba, watu wote walimfuata Abu Jahl, ikawa hapana chochote ila vita tu. Dasturi ya Waarabu walipokuwa wakipigana, kwanza hupigana mmoja mmoja. Hutoka mkubwa wa upande huu na wa upande huu wakapigana kwa panga, hata mmoja akimwua mwenziwe ndipo vita vinapoumana ikawa mpata mpatae. Ilivyokuwa hii ndio dasturi yao, basi alitoka kwenye jeshi la Makureshi Utba bin Rabia bin Abdi Shams bin Abd Manaf, na ndugu yake Shayba bin Rabia – na mwanawe – Walid bin Utba, wakasimama juu ya mafarasi wao mbele ya jeshi la Waislamu, kungoja mashujaa wa Kiislamu nao watoke kupigana nao, wakatoka vijana watatu wa Kiansar kukabiliana nao, lakini wale mabwana wakubwa wa Kikureshi walikataa kupigana nao wakasema: “Hutuwataki ila Makureshi wenzetu” wakampigia kelele Mtume (s.a.w.) ili awape Makureshi watatu wenye utukufu kama wao, Mtume (s.a.w.) akamtoa Bwana Ubeyda bin Harith bin Muttalib bin Abd Manaf, apigane na Utba, akamtoa Bwana Hamza bin Abdul Muttalib bin Hashim bin Abd Manaf, apigane na Shayba na akamtoa Sayyidna Ali bin Abi Talib bin Abdul Muttalib bin Hashim bin Abd Manaf, apigane na Walid bin Utba – mtoto mwenziwe –. Wote hawa watatu waliotoka upande wa Waislamu walikuwa jamaa zake Mtume (s.a.w.) khasa.
Bwana Hamza hakuchukua muda ila alimwua Shayba, vile vile Sayyidna Ali hakuchukua muda ila alimwua Walid. Ama Bwana Ubeyda na Utba panga zao zilikwenda sawa sawa, kila mmoja alimpiga mwenziwe dharba ya kumwua, Utba alimalizwa pale pale, na Bwana Ubeyda akafa njiani walipokuwa wakirejea kwao Madina. Makureshi – kuona wakubwa wao wamekufa mara moja – walivunjika moyo sana wakaona kuwa hiyo ni dalili mbaya kwa upande wao. Lakini waliinuka hivyo hivyo kupigana ijapokuwa wana khofu, wala hawakuwa wakipigana mmoja mmoja sasa, bali ilikuwa ovyo ovyo aliyekukabili ndiye wako.
Mtume (s.a.w.) baada ya kuwaambia maneno mazuri Masahaba, na baada ya kuwatia moyo alipanda juu ya kiriri chake, akakaa huko yeye na Sayyidna Abubakr, huku anaomba Mungu na Sayyuidna Abubakr anaitikia, kwenye mlango wa kile kiriri alisimama Bwana Saad bin Muadh pamoja na vijana wa Kiansar ili kuwazuilia maadui wasimfikilie Mtume (s.a.w.). Masahaba walipigana kwa ushujaa mkubwa sana na wakaua idadi kubwa ya Makureshi, ingawa wao Masahaba walikuwa kidogo mara tatu kuliko hao Makureshi. Hata wakati wa adhuhuri Mtume (s.a.w.) aliletewa Wahyi kuwa sasa hivi Masahaba watashinda, wawaendeshe mbio Makureshi, na akaamrishwa achukue gao la mchanga, alimwaiye lile jeshi la Makureshi, na huku anaomba dua. Mtume (s.a.w.) pale pale alichukua gao hilo akalisukumiza kwenye jeshi la makureshi, na huku akisema: “Nazidhalilike nyuso hizi Inshaallah”. Halikusalia jicho la yoyote katika wale ila liliingiwa na mchanga huo, likawa linawasha kama pilipili, kila mmoja asijijue ikawa anaania jicho lake tu, basi wakawaua kama vikuku, na wakawa wanakimbizana mbio kama vibuzi, na huku wanakamatwa na Waislamu na kufungwa kamba. Waliosalimika hawakusimama, walikwenda mbio mpaka kwao. Mwenyezi Mungu anasema katika Sura ya 8 (Suratul Anfal) Aya ya 17:
Siye wewe uliyewamwaia (mchanga), wakati ulipowamwaia, lakini Menyezi Munghu ndiye aliyewamwaia
Baada ya Makureshi kwenda zao Mtume (s.a.w.) aliwaamrisha Masahaba zake wahisabu mateka na wafu wa maadui zao, wakaona kuwa mateka walikuwa 70, na wafu 70. Ama katika Waislamu walikufa 14 tu – 6 katika Muhajir na 8 katika Ansar –. Walivyokuwa hawa maiti wa Makureshi ni wengi, na Masahaba wamechoka sana na itakuwa taabu juu yao kuchimba makaburi 70, Mtume (s.a.w.) aliamrisha wachukuliwe wote hao maiti 70 watiwe kwenye kisima kimoja, kisha kifukiwe. Mtume (s.a.w.) akasimama kutazama, na Masahaba wakawa wanawatia mmoja mmoja. Kila mmoja akitiwa Mtume (s.a.w.) akiwaambia Ansar: “Huyu ndiye fulani”. Kwani baadhi ya vijana wa Kiansar hawakuwa wakiwajua baadhi ya mabwana wa Kikureshi.
Huu ni muujiza kuwa watu 300 waliwashinda barabara watu wanaokaribia elfu, na wakawaulia watu 70 wao na wakawapokonya watu 70. Lakini ukisha kuisoma Aya ya 17 ya Sura ya 8 (Suratul Anfal), na ukajua maana yake, itakuondoke ajabu hiyo yote, Mungu anasema:
Siyo nyinyi mliowaua, lakini Mwenyezi
Dostları ilə paylaş: |