Harry Robertson
Arusha Secondary School,
1979:
“Sababu ya kumpiga tunayo! Nia ya kumpiga tunayo! Na uwezo wa kumpiga Nduli Idi Amin tunayo, ni lazima tumpige!”
Ilikuwa ni sauti ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akiongea na wapiganaji wa Jeshi la Wanachi Watanzania katika ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam.
Hofu ya vita ilikuwa imetanda Tanzania nzima, watu wote hasa wakazi wa mikoa ya kanda ya ziwa kama Mwanza, Kagera na Mara ambayo ipo jirani na nchi ya Uganda walikuwa na hofu kubwa mno!Wengi walishaanza kuikimbia mikoa yao kwenda mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Tanga, iliyokuwa mbali na nchi ya Uganda, walifanya hivyo kuyaogopa makombora ya Nduli.
Miongoni mwa watu waliokimbia alikuwemo mwanamke wa Kihaya aliyeitwa Agripina Rwechungura na mtoto wake mdogo wa kiume Harry Robertson, alikuwa mtoto mzuri sababu ya mchanganyiko wa damu aliokuwa nao, baba wa mtoto huyo alikuwa Mwingereza aliyekuja mkoani Kagera kufanya utafiti wa zao la Kahawa.
Alikutana na Agripina mwaka 1973 na wakawa na uhusiano wa kimapenzi ndipo akazaliwa mtoto huyo ambaye kwa pamoja waliamua kumwita jina la Harry, alikuwa mtoto mzuri kuliko jina lake! Kila mtu alimfurahia mtoto huyo, mchanganyiko wa damu ya kizungu uliifanya ngozi yake iwe na rangi ya senti tano! Rangi adimu ya ngozi.
“Huyu mtoto akikua atakuwa tishio, wenye binti zao ni lazima wawe waangalifu sana, atapiga mimba sana huyu!” Alisema mzee mmoja Harry na mama yake walipoteremka katika mabasi mjini Arusha.
*****************
Mkoani Kagera waliishi mjini Bukoba ambako mzungu Robertson alimnunulia Agripina nyumba kabla ya kuondoka nchini kurejea nyumbani kwao Uingereza mkataba wake ulipokwisha, mjini Arusha Agripina alitegemea kuishi nyumbani kwa dada yake mkubwa Dk. Swai aliyefanya kazi katika hospitali ya mkoa wa Arusha Mount Meru kama daktari wa magonjwa ya wanawake.
Agripina na mwanae walipokelekwa vizuri na Dk. Swai aliyeishi maeneo ya Uzunguni mjini Arusha ambako yeye na mume wake Eric Swai mfanyabiashara maarufu mjini humo waliishi katika nyumba ya kifahari waliyojenga wenyewe, ilikuwa nyumba kubwa mno na waliamua kuwakaribisha Agripina na mtoto wake kuishi nao bila wasiwasi wowote.
Jioni ya siku hiyo waliongea mengi kuhusu nyumbani, Agripina alimweleza Dk. Swai kila kitu kilichotokea Bukoba, pia alimfahamisha kuhusu kuondoka kwa mzungu Robertson nchini na kumwachia mtoto lakini akiwa amemnunulia nyumba kubwa ya kifahari.
“Kama kakununulia nyumba basi inatosha, ukiongeza na hilo toto la nguvu alilokuachia huna wasiwasi huu ni utajiri tosha! Mtoto wako ni mzuri sana Agripina niamini, sijapata kuona mtoto mzuri kama huyu hapa Afrika labda kwenye televisheni, unachotakiwa kufanya sasa ni kuhakikisha unampa Harry elimu bora!”
“Ahsante nitafanya kila kinachowezekana kumtafutia shule nzuri, huko Bukoba alisoma katika shule ya kimataifa ya Rugambwa, alifanya vizuri sana katika masomo yake ya darasa la kwanza!” Alijibu Agripina na waliongea mengi sana Harry akimsikia.
Harry alikaa kimya kwenye kochi pembeni akiwa amekuja nne na mdomo wake ukiwa amechomekewa vizuri kuingia ndani, hiyo ilimfanya apate vishimo katika mashavu yake, ambavyo watu huviita ‘Dimpos’ sifa za kwamba Harry alikuwa mtoto mzuri zilimfanya ajisikie vizuri na aone yeye alikuwa bora kuliko watoto wengine wote duniani.
“Sijui na yeye anajua kuwa ni mzuri ona mapozi yake!” Dr Swai alimtania Harry huku akimchezea shavu lake la kulia, Harry alitabasamu na kuifanya sura yake ionekane ya kuvutia zaidi, Agripina alijisikia vizuri kuwa na mtoto kama Harry! Alifurahi kukutana na mzungu Robertson kwani alimpa alichokitaka.
********************
Mwezi mmoja baada ya kufika mkoani Arusha, vita ilikuwa imepamba moto mpakani mwa Tanzani na Uganda! Harry alikuwa tayari katika shule ya kimataifa ya Arusha darasa la kwanza! Siku alipopelekwa kuandikishwa katika shule hiyo waalimu na wanafunzi walipigwa butwaa kwa uzuri wa sura ya mtoto huyo, walimu walivutana kila mwalimu akitaka asome katika darasa lake! Baada ya mvutano wa muda mrefu hatimaye Harry aliandikishwa katika darasa la kwanza E.
“Mwalimu darasa lako lina wanafunzi wazuri wawili!”Mwalimu mmoja alimuuliza mwalimu wa darasa la kwanza E.
“Yupi mwingine?”
“Si Caroline!”
“Ah!Ndiyo nilitaka kusahau, kwa hiyo ninao Mr na Miss Arusha School au siyo?”
“Mshindi ni wewe bwana!” Walitaniana walimu lakini huo ndio ulikuwa ukweli, Harry na Caroline walilifanya darasa la kwanza E kuwa darasa la aina yake, watoto hao wawili walikuwa na uzuri wa ajabu! Ili mwalimu alipendezeshe zaidi darasa lake aliwapanga Caroline na Harry katika dawati moja!
Harry na Caroline walitokea kuwa marafiki wakubwa na uwezo wao wa darasani pia ulikuwa mkubwa kuliko wanafunzi wengine, ushirikiano wao katika masomo ndio uliowafanya wawe hivyo, wanafunzi wengine waliwaonea wivu!
Ni urafiki wao ndio uliowafanya hata wazazi wao wafahamiane, Cynthia na Agripina walitokea kuwa marafiki wakubwa sababu ya kuzaa watoto wazuri, mara kwa mara walitembeleana nyumbani kwao na kuongea mipango mingi juu ya watoto wao baadaye.
Pamoja na uzuri wote aliokuwa nao Caroline bado tatizo la kifafa lilimsumbua kwa kiasi kikubwa na lilimuumiza sana akili yake, alitamani angekuwa na ugonjwa mwingine wowote lakini si kifafa! Alianguka kila mwezi mara moja kati ya tarehe 26 hadi 28 za kila mwezi.
Wazazi wake walijitahidi kumtafutia tiba lakini hazikusaidia dawa nyingi alitumia bila mafanikio yoyote! Caroline alikuwa mzuri mno kuwa na kifafa na wazazi wake hawakutaka kabisa jambo hilo lijulikane, waliendelea kuufanya ugonjwa wa mtoto wao siri ya familia! Hata mtumishi wao wa ndani hakulifahamu jambo hilo.
Ili kuhakikisha kuwa Caroline haanguki mbele za watu na kuaibika ililazimu kila tarehe 26 hadi 28 ya kila mwezi afungiwe ndani ya chumba chake cha kulala, ni wazazi wake ndio walioruhusiwa kuingia ndani ya chumba hicho! Alisubiriwa mpaka aanguke kifafa ndio aendelee na masomo yake shuleni, chumba hicho hakikuwa na kitu chochote cha chuma au mbao kwa kuogopa kumuumiza wakati wa kuanguka.
********************
Mpaka anamaliza darasa la saba na kuingia kidato cha kwanza Caroline alikuwa bado ni tishio kwa uzuri shuleni kwao kasoro pekee aliyokuwa nayo ni siri yake ya kifafa ambayo hakutaka kabisa igundulike, watu wengi akiwemo Harry walijiuliza ni kwanini kila tarehe 26 hadi 28 ya kila mwezi Caroline hakwenda shule! Hakuna mtu aliyekuwa na uwezo wa kutoa jibu la swali hilo isipokuwa Caroline mwenyewe na hakuruhusu swali hilo liulizwe na mtu yeyote!
Kila aliyediriki kudadisi juu ya kutokuja kwake shuleni alibadilika na kuwa adui mkubwa wa Caroline! Lakini swali hilo hilo liliendelea kumuumiza Harry moyoni mwake hatimaye siku moja alifunga mkanda na kuamua kumwita Caroline na kumuuliza baada ya kumwona akiwa amevimba usoni! hakujua kama jana yake alianguka na kujipiga ukutani.
“Caroline vipi mbona una ngeo?” Aliuliza Harry na swali hilo lilimuumiza sana moyo Caroline.
“Jana nilianguka bafuni wakati naoga!”
“Aisee, pole sana!”
“Ahsante!” Alijibu Caroline.
“Lakini Caroline kuna kitu kimoja nataka kufahamu!”
“Kitu gani Harry!”
“Mbona kila tarehe 26-28 ya kila mwezi huwa hauji shule?”
“Harry ni mambo ya wanawake siwezi kukueleza!” Alijibu Caroline akijaribu kudanganya kuwa tarehe hizo hakwenda shule sababu ya hedhi! Harry aliamini na kujikuta akimwomba msamaha!
“Samahani sana kwa kuingilia mambo yako ya ndani!”
“Hakuna shida!”
Hata walipoingia kidato cha kwanza waliendelea kusoma darasa moja na kukalia dawati moja! Urafiki wao ulizidi kukomaa na utaratibu wa Caroline kutokuja shuleni kila mwisho wa mwezi uliendelea kuwepo, matibabu pia yaliendelea kufanyika lakini bado hakupona kifafa kiliendelea kumsumbua.
Ugonjwa huo ulimnyima Caroline raha ya maisha, hakuwa kama watoto wenzake shuleni, kila siku alihofia kuanguka mbele za watu na alishindwa kuelewa kama ingetokea akaanguka mbele ya wanafunzi wenzake waliomchukulia kama malkia wa uzuri ingekuwa vipi! Alijua ingekuwa aibu na hakutaka aibu hiyo itokee ndio maana alikuwa makini na tarehe.
Urembo wake ulizidi kutisha si kwa wanafunzi peke yao bali hata walimu, watu walizidi kuchanganyikiwa na uzuri wa msichana huyo! Caroline alizidi kupanuka chini na kuwa mwembamba zaidi juu kadri siku zilivyozidi kwenda! Wavulana wengi walimtaka mapenzi lakini Caroline aliendelea kuwakatalia, hakutaka kuwa na uhusiano na mvulana kimapenzi kwani alijua ukaribu wao ungefanya siri yake ijulikane!
“Sitaki nitakaa hivi hivi!”Huo ndio ulikuwa uamuzi wake kila siku, hofu yake kubwa ilikuwa kwa maisha yake ya baadaye, pamoja na umri wake kuwa mdogo bado alifikiria nini kingetoka siku za usoni, alijua yeye kama mwanamke alitakiwa kuolewa na kuwa na watoto!
“Ni mwanaume gani atakubali kuoa mwanamke mwenye kifafa?” Hilo ndilo lilikuwa swali lake la kila siku na lilimuumiza sana moyo, hakuogopa kuolewa tu bali pia aliogopa sana kuzaa watoto kwa sababu alijua kifafa hurithishwa hadi kwa watoto!
“Sitaki pia kuzaa sitaki mtoto wangu aje kuwa na matatizo kama yanayonikuta mimi!”
*******************
“Kwa nini mimi?” siku moja alijikuta akitamka maneno hayo yeye na Harry walipokuwa wakisoma pamoja darasani.
“Unasemaje Caroline?”
“Hapana nilikuwa nawaza mambo fulani tu!”
Siku zote Harry alihisi kulikuwa na kitu kilichomsumbua Caroline lakini hakukifahamu kitu hicho kilikuwa ni kitu gani, mara kwa mara aliyaona macho ya Caroline yakiwa mekundu, ishara alikuwa amelia muda mfupi kabla lakini alipoulizwa Caroline hakuwa tayari kueleza ukweli.
Waliendelea kuwa na urafiki wao hadi kidato cha tatu wote wawili mpaka wakati huo walikuwa bado hawajajua tendo la ndoa lilikuwa kitu gani! Harry alisumbuliwa sana na wasichana lakini siku zote hakukubali.
“Huyu ni wa Caroline bwana!” hivyo ndivyo wasichana walivyosema kwa fikra kuwa kulikuwa na uhusiano kimapenzi kati ya Harry na Caroline! Kitu ambacho hakikuwa kweli hata kidogo.
Wakiwa kidato cha nne ghafla hali ya ajabu ilianza kujitokeza kati yao, Harry alijisikia kumpenda Caroline na Caroline alijisikia vivyo hivyo lakini hakuna shujaa kati yao aliyeweza kuzieleza hisia zake! Mioyo yao iliendelea kuteseka kwa miezi kadhaa bila kutoboleana ukweli, ndipo Harry alipoamua kuusema ukweli wake.
“Caroline nimeishi na wewe kama dada yangu na rafiki kwa muda mrefu lakini siku za hivi karibuni nimeanza kujisikia tofauti kidogo!”
“Tofauti gani?”
“Nakupenda Caroline! Sikudanganyi, ninataka uwe mpenzi wangu na ikiwezekana tufunge ndoa siku moja!”
Caroline hakuyaamini masikio yake alifikiri yamemdanganya, alitaka kukubali lakini alipoufikiria ugonjwa wake alisita kusema ndiyo! Alibaki kimya kwa muda akijaribu kutafuta kitu cha kusema!
“Tafadhali nijibu Caro!”
“Harry, hata mimi ninakupenda lakini nafikiri hutaniweza!”
“Kwa nini?”
“Nina matatizo!”
“Matatizo gani?”
“Siwezi kukueleza ila wazazi wangu hawafurahi kuona mimi na wewe tunakuwa wapenzi!” Caroline alificha lakini alitaka kuuelezea ugonjwa wake!
“Nakupenda Caroline ina maana wazazi wako hawapendi mimi na wewe tuwe na familia siku moja?”
“Basi nipe muda Harry ili nifikirie vizuri!”
Baada ya kuachana Caroline alizidi kufikiria juu ya uamuzi wa Harry! Moyo wake ulimwambia akubali lakini akili yake iliogopa, kila alipoifikiria picha ya kuanguka mbele ya Harry na kukakamaa alizidi kuogopa zaidi! Lakini wiki mbili baadaye alifikia maamuzi ya kukubali.
“Sawa nimekubali Harry lakini katika siku zote za mwezi sitakuwa na wewe tarehe 26-28 kwani siku hizo huwa nipo katika hedhi!”
“Sawa lakini…………!”
“Lakini nini?”
“Au basi tu hilo lisiwe kikwazo!” Harry alitaka kusema kuwa sikukuu yake ya kuzaliwa katika kila mwaka ilikuwa ni tarehe 26 mwezi wa saba!
****************
Penzi lao lilichipuka na kukua kwa kasi ya ajabu na kufikia kiwango ambacho wote wawili hawakukitegemea kabisa!
Harry na Caroline walizidi kuchanganyikiwa katika mapenzi lakini Harry alichanganyikiwa zaidi kumzidi mwenzake, walitembea wakiwa wameshikana mikono kila walikokwenda! Walipigana mabusu mbele za watu bila kujali, Caroline alishindwa kuelewa siku ambayo Harry angegundua alikuwa na kifafa kingetokea nini! Alikuwa na uhakika angemwacha na alishindwa kuelewa angeishi vipi bila Harry!
“Ni heri kufa kuliko kumkosa Harry!”
Mpaka miezi michache tu kabla ya kufanya mitihani yao ya kidato cha nne penzi lao lilikuwa juu mno! Karibu kila mtu shuleni alifahamu juu ya uhusiano wao hata wazazi wa Caroline walilifahamu jambo hilo na lilisababishia ugomvi mkubwa kati yake na mama yake mzazi Dk. Cynthia!
“Umeyasahau matatizo yako siyo? Shauri yako utaaibika mwenyewe na ugonjwa wako!”
“Nafahamu mama lakini nampenda sana Harry na siwezi kumwacha tena ni heri kufa kabisa kuliko kumkosa yeye nitajitahidi kumficha siri hii asifahamu!”
************
Mahafali ya kumaliza kidato cha nne yalipangwa kufanyika tarehe 27 mwezi wa saba ikiwa ni siku moja tu baada ya sikukuu ya Harry ya kuzaliwa! Harry alimpa Caroline taarifa hizo ili ajiandae na alisema ilikuwa ni lazima ahudhurie sikukuu hiyo.
“Tutafanya hiyo ndiyo siku ya mimi na wewe kupongezana kwa kumaliza shule pamoja na siku itakayofuata yatakuwa mahafali yetu itakuwa babu kubwa au sio?”
Caroline alikaa kimya kwa muda na baadaye kuanza kulia machozi, alijua siku hizo zilikuwa ni mbaya sana kwake! Ni katika siku hizo ndiyo alianguka kifafa, alijua angeharibu uhusiano wake kimapenzi na Harry! Alijua wazi kama Harry angefahamu Caroline alikuwa na kifafa asingekubali kuwa naye tena maishani! Aliomba Mungu azibadilishe siku na kuzirudisha nyuma jambo ambalo halikuwa rahisi hata kidogo kufanyika.
“Harry sitahudhuria sikukuu yako na hata mafahali!”
“Kwanini darling?”
“Kwa sababu nilizokwishawahi kukueleza kuwa nitakuwa kwenye hedhi!” Caroline alidanganya.
“Hilo mbona dogo utavaa padi za kutosha nina hakika hutajichafua mpenzi lakini lazima uwepo!”
“Sawa lakini…..!”
“Lakini kitu gani tena Caroline au hunipendi nini?”
“Nakupenda Harry lakini hapana!” Caroline alizidi kuweka msimamo.
“Usipohudhuria pati yangu mimi na wewe basi!” Alisema Harry akinyanyuka kutoka darasani walimokuwa wakisoma pamoja na kuanza kutoka nje.
Caroline alimfuata nyuma huku akilia machozi, hakuwa tayari hata kidogo kumpoteza Harry! Hakuwa tayari kuachwa na mtu aliyempenda kiasi hicho, alimtupia lawama Nyingi Mungu na kuruhusu ugonjwa huu umpate yeye!
“Kwa nini sikuugua ugonjwa mwingine wowote zaidi ya kifafa?” Alijiuliza Caroline huku akitembea kwa kasi.
“Harry! Harry! Harry! Tafadhali simama unisikilize, nakupenda Harry!”
Harry hakusimama alizidi kutembea kwenda mbele zaidi, Caroline alianza kukimbia akimfuata kwa nyuma na alipomfikia Harry alimshika begani.
“Nisikilize mpenzi!”
“Nimekwishasema kama hutakuja kwenye bethidei yangu mimi na wewe basi tena!”
“Basi nitakuja darling lakini nitawahi kuondoka kurudi nyumbani!” Alijibu Caroline, alikuwa tayari kufanya lolote lakini asimpoteze Harry.
“Sawa ili mradi ufike tu!”
“Nitakuja darling usichukie eh!”
“Sijachukia darling nakupenda Caroline!” Walicheka na kukumbatiana.
*********************
Siku ya Julai 26 watu walifurika ndani ya ukumbi wa Sunflower kusherehekea siku ya kuzaliwa kwa Harry Robertson! Caroline alikuwa ndani ya ukumbi huo akiwa mwenye wasiwasi mwingi, alikaa karibu kabisa na Harry, alivaa gauni la kung’aa lililompendeza pengine kuliko wasichana wengine wotte ndani ya ukumbi huo! Aliletewa gauni hilo na baba yake aliporejea kutoka Uingereza, ni siku hiyo ndiyo alilivaa kwa mara ya kwanza.
Aliondoka nyumbani kwa kutoroka, hakumuaga mtu yeyote, wazazi wake waliamini alikuwemo ndani ya chumba amejifungia, baadaye mama yake alipokwenda chumbani alikuta hayupo! Alichanganyikiwa na kumpa taarifa hizo mumewe!
“Yupo wapi?”
“Kwa kweli sifahamu kabisa! Nimekuta chumbani hayupo jamani mtoto huyu anataka kutuaaibisha masikini!” Alisema mama yake. Walihisi alikuwa amekwenda kujiua baada ya kukata tamaa ya maisha ilibidi watoe taarifa polisi na alianza kutafutwa kila mahali.
******************
Mpaka sa nne za usiku tafrija ilikuwa bado ikiendelea, watu walikuwa wakifurahia ndani ya ukumbi wa Sun flower lakini Caroline hakuwa na furaha hata kidogo, alihisi wakati wowote angeweza kuanguka.
“Harry nataka kuondoka! Baba na mama watakuwa na wasiwasi sana!”
“Kuondoka kwenda wapi wewe kula starehe bwana, au hunipendi!”
“Nakupenda!”
“Basi kaa hapa na mimi nitakurudisha baadaye!”
“Hapana!” Caroline alizidi kukataa hakuamini mpaka saa hizo alikuwa hajaanguka.
“Sasa ni wakati wa kufungua muziki na watakaotufungulia muziki wetu ni mr na mrs watarajiwa, Harry na Caroline!” Dj alitangaza na Harry alinyanyuka na kumwomba Caroline amfuate katikati ya ukumbi.
“No! No!No! Sitaki”
“Kwanini?” Harry aliinama na kumuuliza.
“Sitaki kucheza muziki! Nasema sitaki kama ni kuniacha basi uniache Harry!” Alisema Caroline ambaye tayari alishaanza kuona kizunguzungu machoni pake!
Harry alimshika mkono na kumnyanyua kwa nguvu huku watu wakishangilia, ilibidi Caroline ajikaze na kwenda hadi katikati! Muziki ulipigwa kwa ajili yao.
Wakiwa wamekumbatiana ghafla Caroline alianza kupoteza nguvu miguuni na kuanguka chini! Akageuza macho yake kuangalia juu, akaanza kutoa povu mdomoni, mwili wake ulikakamaa na mkojo mwingi ukamtoka!
Watu wote ukumbini walishangaa kuona hali hiyo Harry alijishika mikono yake yote miwili kichwani hakukiamini kilichokuwa kikitokea mbele yake! Hakuamini kama aliyelala sakafuni akitupa mikono na miguu hewani alikuwa ni mpenzi wake aliyempenda Caroline! Harry alihisi ni ndoto.
“Kha! Kumbe kujidai kote huko shoga yetu ana kifafa, lo!” Alisema msichana mmoja nyuma ya Harry!
“Masikini msichana mzuri huyu ana kifafa jamani!” mama mwingine alisema.
Agripina mama yake Harry alisonga mbele ya watu na kumuingizia Caroline kijiko kilichofungwa na kitambaa cheupe mdomoni ili asiume ulimu wake, alikuwa akilia machozi.
Nusu saa baadaye Caroline alizinduka na kuangaza huku na kule kama mtu aliyetoka usingizini, alishangaa kuona watu wote wamemzunguka yeye, nguo zake zililowa mkojo na mdomoni alikuwa na mapovu, alijua tayari amekwishaanguka!
“Harry unaona sasa mambo yako ya kulazimisha?” Alimlaumu Harry.
“Caroline kwanini hukuniambia una kifafaa?”
“Niliogopa Harry, nilijua ungeniacha! Nakupenda sana Harry hata mimi sikupenda kuwa hivi tafadhali usiniache”
Badala ya kujibu Harry alianza kulia machozi, kuona hivyo Caroline alinyanyuka na kuanza kukimbia hadi kwenye jiko la shule ambako alichukua kamba iliyofungia kuni na kuanza kukimbia nayo kwenda msituni!
“Ni heri nife tu!”
Dakika tano baadaye Harry, alitoka mbio kwenda msituni kumfuata, alijua ni lazima Caroline alikuwa amekwenda kujiua! Hakumwona mahali popote msituni, alihisi bado alimpenda Caroline pamoja na kifafa alichokuwa nacho! Alitaka kumuokoa!
“Caroliiiiiiiiiiiiiiiiiiiine! Caroliiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiine!Upo wapi, tafadhali usijue bado ninakupenda hivyo hivyo ulivyo!” Alizidi kuita Harry akitembea katikati ya msitu lakini hakuna mtu aliyemwitikia alijua lazima Caroline amejiua! Sauti yake iliitikiwa na mwangwi.
Je Caroline atakufa? Fuatilia wiki ijayo!
U
likuwa ni usiku wa giza
nene lililotanda kila mahali
lakini Harry hakuogopa aliendelea kulia machozi akipita katikati ya vichaka vyenye miiba chini ya miti mingi ya mikorosho, alikuwa akiliita jina la Caroline lakini hakusikia sauti ya kuitikiwa kutoka sehemu yoyote katika msitu huo! Sauti yake ilijibiwa na mwangwi uliomfanya ahisi ilikuwa ni sauti ya Caroline na kuzidi kuzama msituni akifuatilia! Kwa hakika kwa ukimya uliokuwepo alijua Caroline alikuwa amekufa!
“Ni lazima atakuwa amejinyonga! Masikini Caroline wangu kwanini hakusubiri kidogo? Amechukua uamuzi wa haraka mno ni vyema angenisikiliza kwanza akasikia uamuzi wangu ungekuwa upi!” Alisema peke yake Harry huku akilia.
Wakati akiwaza hayo upande mwingine wa akili yake haukulipitisha hilo kama jibu moja kwa moja uliendelea kuamini Caroline alikuwa hai na alikuwa mahali fulani akitafuta mahali pa kujinyongea, hilo lilimtia nguvu Harry na kumfanya azidi kuita akiamini muda mfupi uliofuata angeitikiwa lakini bado hapakuwa na jibu lolote.
Moyoni mwake Harry aliamini kifafa au ugonjwa wowote ule kisingeweza kuwa kitu cha kumtenganisha yeye na msichana aliyempenda Caroline, roho ilimuuma na alishindwa kuelewa angeishi vipi shuleni katika muda waliobakiza bila kuwepo Caroline na alishindwa pia kuelewa angefanya nini kuzuia kifo kisitokee muda wote alihisi yeye ndiye alikuwa chanzo cha kifo cha Caroline kama kweli angefanikiwa kujinyonga!
“Sikutakiwa kuonyesha mshangao hata kidogo si ajabu hiyo ndiyo ilimfanya Caroline afikiri nitamwacha!” aliwaza Harry.
Ghafla wakati akitembea alishtuka aliposikia kwikwi za kilio cha mtu zikitokea juu ya mti mkubwa wa mkorosho uliokuwa pembeni mwa njia! Haikumchukua muda mrefu kugundua sauti aliyoisikia ilikuwa ya Caroline bila kuchelewa alianza kunyata akitembea kwenda chini ya mti huo.
Alipoufikia alianyanyua uso wake na kuangalia juu kwa sababu ya giza lililokuwepo na majani mengi ya mti huo yaliyotanda kila mahali hakuweza kuona kitu chochote lakini kwikwi za mtu akilia ziliendelea na ndani ya kwikwi hizo alisikia jina lake likitajwa mara kwa mara.
“Ee Mu....ngu kwanini ulini...umba mimi hivi? Kwani..ni ume..ninya...nga...nya Harry?” Sauti hiyo iliendelea kusikika kutoka juu ya mti.
“Caroline, nakupenda tafadhali sana usijaribu kujiua! Nakupenda kwa jinsi ulivyo tafadhali usidiriki kuutoa uhai wako nakupenda Caroline! Kifafa si kitu cha kututenganisha mimi na wewe hata siku moja na hata ungekuwa Ukimwi bado tusingetengana! Tafadhali nipe nafasi nyingine ili uone kama nitakuacha au la! Siwezi kufanya hivyo mpenzi!”Harry alisema huku akipanda mtini kujaribu kumuwahi Caroline aliyekuwa amevaa kamba shingoni tayari kwa kujinyongakabla hajajirusha mtini!
Machozi yalikuwa bado yakiendela kumbubujika Harry kwa wingi, alikuwa akimlilia Caroline hakutaka afe! Ni wazi alimpenda na hakutaka kumpoteza katika maisha yake.
Ingawa hakuwa na uhakika kama angeweza kuwahi kabla hajajirusha, Harry alizidi kutembea juu ya tawi la mti akimwomba Mungu amduwaze Caroline mpaka amfikie! Lakini akiwa hatua kama mbili hivi kabla hajamgusa alishangaa kwa macho yake kumshuhudia Caroline akijirusha na kuning’inia mtini! Kamba ilimkaza shingo na macho yakaanza kumtoka.
“Caroliiiine don’t do it! (Caroline usifanye hivyo!) Alisema Harry lakini alikuwa amechelewa kwani tayari Caroline alikuwa akining’inia mtini ulimi wake ulianza kutoka nje!
Harry alilia kwa uchungu na kujaribu kuivuta ile kamba kwa juu akifikiri angeilegeza shingoni kwa Caroline lakini kwa kufanya hivyo ndiyo alizidi kuikaza! Hakuwa na la kufanya tena mwili wake ulikufa ganzi! Alipoangalia saa yake ya mkononi aligundua tayari ilikuwa saa nne na nusu ya usiku.
********************
Msako wa Caroline:
Polisi kwa kushirikiana na wazazi wa Caroline bado waliendelea kumtafuta kila mahali mahali mpaka wakajikuta wamefika katika hoteli ya Sunflower baada ya kuelezwa na watu kuwa uwezekano wa Caroline kuwa katika hoteli hiyo ambako rafiki yake mpendwa Harry alikuwa akifanya sherehe ya kuzaliwa ulikuwa mkubwa.
“Sasa si ni heri angesema tu kuwa anakwenda kwenye tafrija kuliko kutoroka na kutuhangaisha kiasi hiki!” Alisema baba yake Hollo
“Wewe baba Caro hivi umesahau kuwa hizi tarehe kuwa ni mbaya kwake?” Aliuliza Dk. Cynthia mamaye Caroline.
“Ndiyo nakumbuka lakini….” Profesa John Kadiri alishindwa kuimalizia sentensi yake alijua tarehe hizo huwa hazifai kwa Caroline kutoka nje!”
Walipofika mbele ya hoteli ya Sunflower walishangazwa na idadi kubwa ya watu waliokuwepo pamoja na ukimya uliotawala! Watu walionyesha kuwa na masikitiko makubwa! Ghafla Agripina mama yake Harry alitokeza na kuwafuata waliposimama kabla hawajasema lolote.
Dostları ilə paylaş: |