“Binti hujanilipa!”
“Subiri kidogo baba narudi muda si mrefu!”Alisema Caroline akiingia ndani ambako aliweka mizigo yake chini sehemu ya mapokezi na kwenda baa ambako alinunua chupa ya maji kisha kuinama na kukitoa kikaratasi chenye sumu katika gauni na kukishika vizuri mkononi, akakifungua na kuimwaga sumu kiasi kiganjani mwake na kujipaka katika vidole vyake vya mkono wa kulia.
Kwa haraka alikwenda hadi mahali ilipokuwa mizigo yake na kufungua pochi yake akatoa noti ya shilingi elfu kumi, iliyohitajika kwa malipo ilikuwa shilingi elfu tano lakini Caroline hakuwa na muda wa kutafuta chenji! Alichotaka kufanya wakati huo ni kumuua dereva wa teksi ili yeye awe salama.
Alitembea haraka hadi nje, akiwa ameishika noti mkono wa kulia pamoja na maji, alimkabidhi dereva noti kisha akampa mkono wake wa kulia ili waagane, mkono huo ndio ulikuwa na sumu! Wakiwa wameshikana alimwangalia mzee huyo kwa macho ya huruma kwani alijua nae alikuwa njiani kuelekea jehamanu!
Dereva aliondoka, mbele kama nusu kilometa hivi akiwa katika msongamano mrefu ya magari kuelekea kituo cha polisi cha kati alikokuwa akielekea ili kutoa taarifa juu ya mwanamke wa ajabu aliyembeba ndani katika gari lake, alianza kusikia kizunguzungu na baadaye mwili mzima ulianza kukakamaa na macho yakageukia juu!
Magari yakawa hayasogei mbele na kusababisha msongamano mrefu zaidi, madereva wa daladala walipoangalia vizuri baada ya kuona magari hayasogei kwa zaidi ya nusu saa, walimgundua mzee huyo akiwa amekufa ndani ya gari lake.
Walilisukuma gari na kuliweka pembeni na magari yakaendelea na safari zake, simu ilipigwa polisi na mwili wa mzee huyo ukaja kuchukuliwa kupelekwa hospitali ya rufaa ya Muhimbili kwa uchunguzi zaidi, taarifa ilipotoka saa moja baadaye ilionyesha mzee huyo alikufa kwa sumu ya Thiodane kali inayopenya katika ngozi.
Sumu hiyo ilitambuliwa kuwa ndiyo iliyoua watu wengi nchini Canada! Wasiwasi kuwa muuaji aliyekuwa akisakwa dunia nzima alikuwa ameingia Tanzania ulitanda! Usalama uliimarishwa na msako mkali zaidi ulianzishwa, Caroline aliyaona yote hayo kupitia kwenye televisheni na kuingiwa na hofu kubwa zaidi, aligundua kuwa ilikuwa ni lazima abadili sura yake kabla hajakamatwa lakini asingeweza kufanya hivyo kabla hajakutana na Dickson.
Hakuwa tena katika hoteli New Africa kama alivyopanga, baada ya dereva wa teksi kuondoka akijua mbele angekufa aliamua kubadili hoteli na kuhamia hoteli ya Livingstone iliyokuwa ilala, huko alichukua chumba ghorofa ya juu kabisa na kujificha.
**********
Saa moja na nusu jioni alipiga simu katika hoteli ya Landmark walikofikia Dickson na mkewe, simu hiyo ilipokelewa na msichana wa mapokezi.
“Nikusaidie?”
“Naomba kuongea na mgeni aitwaye Dickson!”
“Naweza kufahamu nani anaongea?”
“Mwambie naitwa Vicky!”
“Subiri!”
Dakika moja tu baadaye tayari Caroline na Dickson walikuwa katika maongezi yao, swali la kwanza alilouliza Dickson baada ya kupokea simu ni kama Vicky alikuwa tayari, sura ya bandia iliyotengenezwa na mzee wa Kijapan, Sumo ilimchanganya akili Dickson, hakuwahi kukutana na msichana mzuri kiasi kile! Hata sekunde moja hakuwahi kuwaza kuwa mtu aliyekuwa anapanga kuonana naye ndiye alikuwa muuaji wake!
“Nakuja!”
“Nipo Livingstone namba 11 usichelewe!”
“Nipe dakika tano tu!”
“Ok!”
Dakika sita baadaye gari ilisimama moja yahoteli ya Livingstone, ilikuwa ni Landcruiser Vx ambayo Dickson alikodi kwenye hoteli ya Landmark ili aendeshe mwenyewe! Alimkuta Caroline akimsubiri nje.
“Twenzetu!”
“Ahsante!”Alijibu Caroline huku akipanda garini.
“Tunaelekea wapi sasa?”
“Bahari beach panafaa zaidi hakuna watu wengi, lakini mkeo umemuaga vipi?”
“Achana naye wanawake wa kizungu hawana maana!”
Kasi ambayo gari ilikwenda nayo haikuwa ya kawaida kwani katika muda wa dakika ishirini tayari walishafika kwenye hoteli hiyo iliyoko ufukweni mwa bahari ya Hindi na kushuka, walitembea wakiwa wameshikana mkono kwa mkono kuelekea pembeni mwa hoteli hiyo na kuketi ufukweni.
“Utakunywa kitu gani?”
“Nitakunywa maji!”
“Chakula?”
“Sasa hivi hapana!”
Alipopita mhudumu Dickson alimwita na kumwagiza chupa mbili za maji, yalipoletewa wote waliendelea kunywa taratibu, kwa Caroline huo ndio ulikuwa wakati muafaka wa kufanya mauaji ya kulipiza kisasi aliyoyapanga, mambo ambayo Dickson alimfanyia yalikuwa mabaya mno, kila alipofikiria kitendo cha kubakwa na kufungiwa ndani ya gunia, kisha kugonjwa na gari! Moyo wake ulizidi kushikwa na hasira kwa maoni yake Dickson hakustahili kuishi.
Muda mfupi baadaye wakiongea Dickson alijikuta akimkumbatia Caroline na kuanza kupiga mabusu mengi akionyesha upendo wake, Caroline aliuona huo ndio ulikuwa mwanya wa kulifanya alilotaka kulifanya, alipenyeza mkono wake hadi kwenye pindo la gauni na kuitoa karatasi yenye sumu, sumu iliyokuwa imebaki ilikuwa ni kidogo sana na aliamua kuimalizia kwa Dickson! Aliimwaga yote kiganjani kisha kuipaka shingoni mwake Dickson bila yeye kufahamu.
“Niachie ninywe maji kwanza!”Alisema baada ya kukamilisha kazi hiyo, Dickson alimwachia na Caroline akaichukua chupa ya maji na kuanza kunywa baadaye alinawa mikono yake yote na kuwa safi, waliendelea na maongezi Caroline akisubiri matokeo ya sumu.
“Nasikia kizunguzungu! Nasikia kizunguzungu!”Alianza kulalamika Dickson sekunde chache baadaye.
Kuona hivyo Caroline aliivua sura yake ya bandia na kubaki na sura yake halisi, alitaka Dickson aelewe kuwa ni yeye aliyefanya kitendo hicho.
“Hukukosea uliposema sauti yangu ilifanana na ya Caroline, mimi ni Caroline! Ninakuua kulipiza kisasi kwa ulivyonifanyia!”
“Mungu wangu Caroline ni wewe?”
“Ni mimi!”
“Nisame……!” Dickson hakumalizia sentensi yake akaanguka chini na kukauka, Caroline aliichukua sura yake ya bandia na kuitupa pembeni mwa mwili wa Dickson, kisha akachukua ufunguo wa gari na kukimbia moja kwa moja hadi nje ambako alilichukua gari walilokwenda nalo na kukimbia hadi hotelini ambako aliliegesha na kushuka mbio akielekea hotelini.
“Vipi binti wewe ni mpangaji hapa?” Mlinzi alimzuia asiingie hotelini!
“Ndiyo!”
“Upo chumba namba ngapi?”
“Namba 11!”
“Mbona sura ya mwenye chumba siyo hii? Mimi namfahamu vizuri mwenye chumba hicho!”
Ikatokea hali ya kutoelewana, ilikuwa ni lazima Caroline aingie chumbani na kubadilisha sura, alitamani kuwa na sumu yake ili ammalize pia mlinzi huyo lakini hakuwa nayo.
Mambo yamezidi kuchachamaa kwa Caroline, hivi kweli atafanikiwa kuikamilisha kazi yake ya kulipiza kisasi bila kukamatwa? Fuatilia wiki ijayo
D
akika tatu tu baada ya
Caroline kuondoka
ufukwe wa Hoteli ya Bahari Beach na kuingia ndani ya gari aina ya Landcruiser walilokwenda nalo na kuondoka akiwa tayari amekwishampeleka Dickson kuzimu, kijana aliyehudumia vinywaji alifika kwenye meza yao kuona kama kuna vinywaji vilivyohitajika zaidi, alishangazwa na ukimya alioukuta na alipoangalia vizuri alimwona mtu akiwa amelala mchangani! Moyo wa mhudumu huyo ulishtuka ghafla ikabidi asogee karibu zaidi ili kufahamu kilichotokea.
Mwanaume alikuwa amelala chini huku macho na ulimi vikiwa umetoka nje! Alionekana mwenye sura ya kutisha, mhudumu huyo alipiga kelele akiita watu wamsaidie, dakika mbili tu baadaye walinzi wa hoteli hiyo kutoka kampuni ya Omega Security walifika kutaka kujua kilichotokea.
“Nini tena?”
“Mtu kafa!”
“Kafa? Yupo wapi?”
“Hapo chini!”Alisema kijana huyo na walinzi kwa kutumia tochi zao walimulika ardhini katika eneo alilokuwa amelala Dickson! Hakuwa mtu tena, jina lake lilishabadilika na kuwa maiti! Mwili wake ulikuwa mweusi kama mkaa na mgumu kama ubao! Kilikuwa kifo cha kushangaza kila mtu alibaki mdomo wazi.
“Mh! Sijawahi kuona kifo cha kutisha kama hiki!”
“Hata mimi!”
“Imekuwaje lakini?”
“Yaani ni jambo la kushangaza sana, mimi ndiye niliwaletea vinywaji kisha nikaondoka ili kuwapa nafasi waongee vizuri, niliporudi kutaka kujua kama walihitaji huduma zaidi ndio nikakutana na hali hii!”
“Ina maana walikuwa wawili!?”
“Ndiyo walikuwa pamoja na msichana mmoja mrembo hivi!”
“Yuko wapi?”
“Yeye sijamkuta!”
“Basi yeye atakuwa anafahamu chanzo cha kifo cha huyo bwana!”
“Inawezekana kabisa!”
Walishauriana kwa muda na kufikia uamuzi wa kupiga simu polisi kuwataarifu juu ya tukio hilo, hazikupita hata dakika kumi tangu taarifa ipelekwe, gari la doria likawa limekwishafika hotelini hapo likiwa na maaskari wasiopungua sita wote wakiwa na bunduki aina ya SMG mikononi mwao, wawili kati yao walivaa kiraia!
“Vipi kuna matatizo gani hapa?”
“Mtu kafariki dunia!”
“Kwa sababu gani?Alikuwa anaumwa?”
“Hapana! Nafiiri kanyweshwa sumu!”
“Umejuaje?”
”Mwili wake umebadilika na kuwa mweusi kama mkaa na mwanamke aliyekuja naye ametoroka!”
Mwenye hoteli hiyo alieleza kila kitu kwa askari kisha kuwachukua hadi mahali mwili wa Dickson ulipolala! Maaskari walishangazwa na jinsi mwili ulivyokuwa mweusi na walipomulika pembeni mwa mwili huo walikiona kitu ambacho wafanyakazi wa hoteli pamoja na walinzi hawakukigundua mapema.
“Kha! Hii si sura ya bandia?”Alisema mmoja wa maaskari hao baada ya kukiokota kitu alichokiona ardhini.
“Hebu!” Askari mwingine aliomba na alipopewa aliivaa usoni sura hiyo.
“Ehee! Alifanana hivi hivi!”
“Huyu lazima ni yule mwanamke anayetafutwa!”
Maaskari walianza kuulizia kwa wafanyakazi wa hoteli hiyo jinsi mwanamke huyo alivyokuwa, alivaa vipi na mwili wake ulikuwa na ukubwa wa saizi gani, walikuwa na uhakika asilimia sabini kuwa mwanamke aliyefanya mauaji hayo ndiye Serial Killer.
“Huyu ni yule yule! Mimi niliiona ile maiti ya dereva teksi, ilikuwa na hali hiihii, inabidi watu wawe makini sana, huyu muuaji kwa hakika kaingia Tanzania na ni lazima akamatwe!”Alisema askari mmoja na kisha kupiga simu makao makuu ya Polisi kutoa taarifa juu ya tukio hilo aliongea na ASP, Selemani Mvungi Mkuu wa Kitengo cha Upelelezi!
“Chukueni hiyo maiti muipeleke Muhimbili haraka sana! Na kijana aliyewahudumia vinywaji mchukueni ili asaidie polisi, ongeeni na walinzi kuona kama wanaikumbuka namba ya gari walilokuja nalo!”
“Sawa afande!”
Baada ya maongezi hayo simu ilikatwa na hapo hapo kama amri ya jeshi ilivyo askari walimwita mlinzi aliyekuwa nje wakati gari linaingia na kuanza kumhoji!”
“Ulikuwepo?”
“Ndiyo!”
“Unaweza kukumbuka namba za gari?”
“Ya mwishoni ni 9 na huku mwanzo kuna 47, kuna herufi moja hapa kati siikumbuki vizuri!”
“Ina rangi gani?”
“Nyeupe!”
“Ina maandishi mengine yoyote mbavuni?”
“Ndiyo!”
“Imeandikwa hoteli Landmark Ltd!”
“Ahaaa! Basi inawezekana ni gari la hoteli hiyo lililokuwa limekodishwa! Kuna magari ya kukodisha na kuendesha mwenyewe pale”Mmoja wa maaskari aliyekuwa akichukua maelezo alisema na baaadye kumgeukia kijana aliyewahudumia.
“Wewe ukimwona huyo mwanamke unaweza kumfahamu?”
“Kwanini nisimfahamu wakati nimemwona kwa macho yangu?”
“Wewe utaongozana na sisi kituoni, unahitajika ili uisaidie polisi kidogo!”
“Kazi yangu je?” Aliuliza kijana huyo kwa mshangao, aliielewa maana ya kuisaidia polisi.
“Hiyo utafanya baadaye!”
Maiti ilipakiwa ndani ya gari la polisi na gari liliondoka kuelekea hospitali ya Rufaa ya Muhimbili, tayari ilishatimu saa nne na nusu ya usiku! Ilipopokelewa madaktari walishangazwa na hali ambayo maiti ilikuwa nayo!
“Jamani hivi huu ni ugonjwa gani? Kuna maiti nyingine niliipokea mchana nayo ilikuwa hivi hivi! Hivi hii si Gangrene kweli?” Aliuliza daktari akimaanisha ugonjwa wa kuoza na kuharibika sehemu ya mwili sababu ya mishipa ya damu kushindwa kupeleka damu katika eneo husika.
“Hapana! Hii ni sumu Dk! Tena sumu kali sana!”
Daktari wa zamu aliandika katika karatasi na kuthibitisha kifo na kuwaagiza maaskari waipeleke maiti ya Dickson chumba cha maiti haraka iwezekanavyo ili ihifadhiwe kwa ajili ya uchunguzi siku iliyofuata.
Gari la polisi likiwa na kijana huyo liliondoka hospitali na kwenda moja kwa moja hadi hoteli ya Landmark ambako liliegeshwa kwenye maegesho yaliyokuwa mbele ya hoteli hiyo na maaskari walishuka na kutembea hadi mapokezi.
“Binti hujambo?”
“Sija...mbo shikamo...moo!”
“Mimi naitwa Herman, wewe mwenzangu unaitwa nani?” Askari alijaribu kumzoea msichana huyo ili kumwondolea hofu.
“Naitwa...twa....twa.... Bupe!”Aliongea msichana huyo kwa sauti ya kukatikakatika ingawa kwa pozi.
“Sasa dada Bupe, sisi nduguzo tunashida!”
“Shida ga....gani?Niwasaidie? Ka…ka….ka...kaka zangu?” Aliuliza msichana huyo kwa sauti ya kukatikakatika!
“Sisi ni makachero wa polisi, tunauliza kama hapa kwenu mna Landcruiser nyeupe ambayo namba zake zinaanzia na 47 na kumalizia na 9?”
Bupe aliinamisha kichwa kwa muda wa kama sekunde tatu akifikiria, alikuwa akivuta kumbukumbu zake kuona kama kweli kulikuwa na gari la aina hiyo.
“Hebu subirini kidogo nije!”Alisema msichana huyo huku akimshuka kwenye kitu kirefu alichokalia na kuanza kutembea hadi kwenye korido, aliingia ndani ya chumba kilichokuwa nje tu ya ofisi yake mlangoni kiliandikwa Meneja! Wakati akitembea nyuma yake aliacha gumzo kwa jinsi msichana huyo alivyoumbika!Alikuwa mwembamba mrefu na mwenye mguu uliojaa vizuri! Kila alipotembea nyuma yake alitingishika kama vile kitu kitadondoka!
“Mzee Kapinga!”Alimwita mzee aliyekaa nyuma ya meza kubwa yenye kung’aa, alikuwa na upara huyo ndiye alikuwa Meneja wa hoteli.
“Naam binti!”
“Kuna maaskari wanaiulizia ile Landcruiser yetu nyeupe, hivi iko wapi?”
“Maaskari wanaiulizia?”
“Ndiyo!”
“Wapo wapi?”
“Mapokezi!”
“Iliondoka na yule mpangaji mwenye mke mzungu ambaye yupo chumba namba 210!Asije kuwa kapata ajali au kaenda kuitumia gari yetu kwenye shughuli ya ujambazi, maana tangu atoke ile saa moja hajarudi au karudi?”
“Bado! Ha...ta...ta...hata mimi nashangaa”
“Hebu waite hao maaskari waingie hapa ndani niongee nao!”
”Sa….sa….sa….sawa bosi!”
Bupe alisema na kutoka nje ya ofisi ya Meneja alichofanya akiwa nje ni kumwita askari aliyekuwa amesimama mbele ya kaunta kwa mkono, askari wawili walimfuata hadi mlangoni.
“Meneja anawaita!”
“Yupo wapi?”
“Humu ndani!”
Maaskari wawili waliingia ndani ya ofisi ya Meneja na kuanza kuongea naye, hawakuona sababu ya kuficha kitu chochote, walieleza kila kitu kilichotokea bayana!
“Gari yenu imetumika kufanya mauaji! Kuna mwanamume alikwenda nayo Bahari Beach akiwa na mwanamke, huyo mwanaume amekufa na tunafikiri amekufa kwa kunyweshwa sumu! Tunahisi huyo mwanamke aliyemuua ndiye anayetafutwa sana duniani hivi sasa!”
“Mh! Ina maana yule mpangaji wetu kutoka Uingereza amekufa! Haiwezekani, huyo ndiye alikodi hilo gari jioni!”
“Gari alilokodi lina namba 47 mwanzoni na kuishia na 9! Kama ni hivyo basi kafariki kwa kunyweshwa sumu!”
“Hebu subiri kwanza!”Meneja alisema na kunyanyua simu iliyokuwa mezani kwake na kupiga chumba alikopanga Dickson na mke wake, aliitikiwa na sauti ya kike iliyoongea Kiingereza kizuri, alifahamu wazi mwanamke huyo ndiye alikuwa mke wa Dickson.
“Can I speak to your husband?” (naweza kuongea na mumeo?)
“He is not back yet! I don’t know what happened to him, he left at 7:30 promising to be back at around 8:30!”(Hajarudi bado sijui kimempata kitu gani, aliondoka saa 1:30 akiahidi kurudi saa 8:30!) Alisema mama huyo kwa wasiwasi.
“Tafadhali usimwambie kitu chochote!”Maaskari walimtahadharisha.
“Ok! Thanks I just wanted to say hi!”(Haya asante, nilitaka tu kumsalimia!) alisema Meneja na simu ikakatwa.
“Kwa hiyo gari lilikodiwa siyo?”
“Ndiyo, lakini mara ya mwisho kama nusu saa iliyopita kuna mtu kanipigia simu na kuniambia lipo hoteli ya Livingstone limeegeshwa nje! Nyie mnasema mmeliacha bahari Beach?”
“Hapana! Inavyodaiwa huyo mwanamke aliondoka nalo baada ya kufanya mauaji, hebu acha sisi twende kwanza huko Livingstone hoteli! Tukaangalie si ajabu huyo mwanamke amepanga hapo!”
“Ok! Nijulisheni mkimkamata ili nije nichukue gari letu!”
“Lakini gari hata likipatikana huwezi kulichukua leo, itachukua muda kidogo!”
Gari la polisi liliondoka hotelini Landmark kuelekea hoteli ya Livingstone kwa kasi ya ajabu! Bunduki za maaskari zikiwa tayari mikononi kwa lolote, ulikuwa ni msako wa kumsaka mwanamke muuaji aliyekuwa akisakwa na dunia nzima! Ilikuwa ni lazima akamatwe, askari waliamini kama wangemkamta wao ndiyo wangechukua zawadi ya dola 30 zilizokuwa zimetolewa kwa yeyote ambaye angesaidia kukamatwa kwa mwanamke huyo.
“Watatupa kweli?”
“Ndiyo, kwanini wasitupe wakati sisi ndiyo tumemkamata?”
“Wewe unalifahamu vizuri jeshi letu lakini? Watasema sisi ni waajiriwa hatuhitaji zawadi! Angekuwa mtu mwingine wangempa”
Maaskari waliendelea kuongea gari ikielekea hoteli ya Livingstone alikopanga Caroline.
*********************
Bado kulikuwa na mvurugano mkubwa katika lango la kuingilia hotelini Livingstone, mzee wa Kikuria aliyekuwa mlinzi kwenye hoteli hiyo hakuwa tayari hata kidogo kumruhusu Caroline aingie ndani hakuamini kama alikuwa mteja wao, sura yake ilikuwa tofauti na ya msichana aliyechukua chumba! Kitendo cha Caroline kuivua sura ya bandia na kusahau kuivaa tena akiwa ufukweni baada ya kumuua Dickson ndicho kilisababisha yote hayo.
Alichodai mzee huyo ni kwamba, alimfahamu mteja wa chumba namba 11! Hofu ilizidi kumwingia Caroline, alijua wazi sura yake ilikuwa mali mtu yeyote ambaye angewezeshwa kukamatwa angekuwa tajiri tangu siku hiyo! Alishangaa ni kwanini mpaka wakati huo mlinzi huyo wa Kikuria alikuwa bado hajaigundua sura yake, Caroline alijitahidi kuongea huku sura yake ikiwa imeinamishwa ili kuuficha uso wake, hakuwa na uhakika na maisha yake alijua wakati wowote mambo yangemharibikia.
“Haiwezekani binti!Nyie ndio watu hatari unaweza kuingia ndani ya chumba cha mtu halafu vitu vikapotea mimi nikafungwa bure!”
“Siyo hivyo mzee mimi ndiye niliyepanga katika chumba hicho labda hukuniangalia vizuri wakati naingia!”
“Usinifanye mjinga, uzee wangu upo kwenye meno lakini siyo macho, meno yote nimepoteza lakini binti macho ninayo na ninaona kuliko wewe, wewe hapa hujawahi kufika!”
“Basi mzee nisaidie!”
“Haiwezekani!Nimesema haiwezekani!”Mzee huyo aliongea kwa sauti ya juu kiasi kwamba walinzi na baadhi ya wapita njia walianza kusimama ili kusikiliza kilichokuwa kikiendelea, hofu ya caroline ilizidi kuongezeka, kwa hofu ya kugundulika, alijikuta akifikia uamuzi wa kuivua tisheti yake na kuiweka kichwani akiacha matiti yake yamefunikwa na sidiria peke yake. Mlinzi alimwona kama mtu aliyetaka kuchanganyikiwa, hakuelewa maana ya kitendo hicho.
“Mzee nisaidie basi!”
“Bwana ondoka hapa mimi nimekwishasema haiwezekani kukuruhusu uingie ndani ya hoteli!”
Kwa mara ya kwanza Caroline alijisikia kusinyaa mwili, nguvu zilimwishia alijua alikuwa amefikia kifo chake bila kuikamilisha operesheni yake ya kuwaua wabaya wake wote. Aliumia kuwaacha Reginald,Leonard, Richard na Harry!
“Hivi kweli nife bila kumuua Harry? Hapana haiwezekani, ni heri wengine wote wabaki lakini Harry afe!”
***************
Wakati hayo yakiendelea kwenye lango la kuingilia hoteli ya Livingstone, gari la polisi lilizidi kukaribia! Maaskari walikuwa na hamu kubwa ya kumkamata Caroline, kwa sababu kuu mbili! Ya kwanza ni kumwona mwanamke aliyesumbua dunia na ya pili ni kupata kitita cha dola milioni thelathini! Waliamini huo ndio ungekuwa mwisho wa umasikini wao!
Je, nini kitatokea? Fuatilia wiki ijayo. Nimeamua kuanza hadithi nyingine ili kuziba pengo la hii ambayo itabidi ikatishwe ili itoke kwenye kitabu kinachoendelea kuchapwa! Mnaweza kuleta maoni yenu. Hadithi yangu mpya ni hii ifuatayo, ifuatilieni bila kuchoka nina uhakika ni nzuri pengine kuliko zote ambazo nimewahi kuandika:
HAIJAISHA ITACHAPWA.
Dostları ilə paylaş: |