“Jamani karibuni sana!”
“Ahsante!”
“Nani kawapa habari za matatizo yaliyotokea hapa?”
“Matatizo? Matatizo gani?” Dk. Cynthia aliuliza kwa mshangao.
Agripina alikaa kimya baada ya kugundua walikuwa hawajui lolote, lakini baadae aliamua kujipa moyo na kusema ukweli hakuona sababu ya kuendelea kuficha.
“Tulikuwa hapa katika sherehe ya kuzaliwa mwanangu Harry, kila mtu alikuwa na furaha! Lakini ghafla wakati wa kufungua muziki Caroline alipatwa na tatizo!”
“Tatizo gani?”
“Alianguka kitu kama kifafa lakini sidhani kama ni kifafa!” Agripina alijaribu kupunguza uzito wa tatizo ili asimuumize sana Cynthia akiamini alikuwa hafahamu.
“MUNGU WANGUUUUUU! UNAONA SASA MTOTO HUYU ALIVYOTUAIBISHA!” Alisema Dk. Cynthia kwa sauti kubwa, kila mtu alishangazwa na kauli hiyo.
“Sasa hivi yuko wapi?” Baba yake Caroline aliuliza!
“Alipozinduka dakika kama kumi zilizopita alichomoka na kukimbia kuelekea msituni na muda mfupi baadae Harry nae aliondoka kumfuata hapa tulipo tunajiandaa kwenda kuwatafuta huko huko msituni!”
Bila kusita wala kusema lolote wazazi wa Caroline, polisi na watu waliowakuta kwenye hoteli ya Sunflower waliungana kwenda msituni kuwasaka Harry na Caroline ilianza, kila mtu aliamini Caroline alikwenda msituni kujiua baada ya kuaibika! Mama na baba yake walilia machozi kwani Caroline alikuwa mtoto wao pekee.
Dakika chache baada ya kuingia msituni walianza kusikia mwangwi wa sauti ya Harry akiliita jina la Caroline na wote walikimbia kuelekea mahali mwangwi huo ulikotokea, mbele kidogo sauti ilipotea lakini walizidi kusonga mbele kila mtu aliamini wangewapata wote wakiwa hai.
Ghafla hatua kama mia tano hivi katikati ya pori wote wakitembea katika njia ndogo huku miili yao ikiwa imelowa umande kutokana na ukungu uliokuwepo usiku huo walisikia minong’ono chini ya mti mkubwa wa mkorosho uliokuwa pembeni ya njia, ilikuwa ni sauti ya mtu akimbembeleza mtu mwingine asijinyonge tayari ilikuwa saa 4:28.
“Jamani wapo humu!” alinong’ona mmoja wa maaskari na watu wote walianza kunyata kuingia chini ya mti huo huku tochi zao zikiwa zimezimwa ili kuepusha kuwashtua, walipofika chini ya mti waliziwasha tochi zao ghafla na kushangaa kumuona msichana akijirusha kutoka mtini na kuning’inia huku akitupa miguu yake huku na kule.
Harry alipoangalia chini aliona kundi kubwa la watu akajua walikuwa wamekuja kumsaidia, hakumtambua hata mtu mmoja kati yao!
“Jamani nisaidieni kuokoa maisha ya mpenzi wangu!” Alisema Harry baada ya kuwaona watu hao chini!
Mmoja wa askari waliokuwepo aliinyosha bunduki yake na kwa kutumia singe kali ya bunduki hiyo alianza kuikata kamba na Caroline alianguka na kufikia mikononi mwa mmoja wa Maaskari, alikuwa kimya kabisa na hakuonekana kuhema hakuna mtu aliyekuwa na uhakika Caroline alikuwa hai au amekufa.
Walikimbia mbio hadi Sunflower hoteli ambako walichukua gari na kuondoka kwa kasi kuelekea hospitali ya Mount Meru! Ndani ya gari la polisi walipanda baba na mama yake Caroline na gari lao lingine liliendeshwa na askari mwingine na ni katika gari hilo ndilo walipanda Harry na watu wengine akiwemo mama yake Agripina!
Mpaka wanafika hospitali Caroline alikuwa bado kimya na hakuonyesha dalili yoyote ya kuhema wala moyo wake kudunda. Baada ya kupokelewa alikimbizwa hadi chumba cha wagonjwa mahututi ambako aliwekewa mashinde ya hewa safi ya oksijeni na akafungiwa mashine nyingine ya kuushitua moyo wake daktari alidai kulikuwa nafasi kubwa ya kuokoa maisha yake. Dripu za kupandisha mapigo zilichomekwa kwenye mishipa yake nazo zikawa zinakwenda kwa kasi kuingia ndani ya mishipa yake.
Wazazi wake waliendelea kulia wakiwa wamekata tamaa kabisa ya maisha ya mtoto wao kurejeshwa! Waliumia zaidi kwa sababu Caroline alikuwa mtoto wao pekee na ndiye alikuwa tegemeo lao kwa kila kitu ikiwemo kurithi mali zote waliokuwa nazo! Hawakuwa na uwezo wa kuzaa mtoto mwingine tena.
******************
Kwa polisi ilikuwa si rahisi kuamini Caroline alijinyonga mwenyewe! Kitendo cha kumkuta Harry juu ya mti kiliwafanya wafikiri alikuwa akimnyonga! Waliamua kuanzia upelelezi wao kwa Harry, walimkamata na kwenda nae moja kwa moja hadi kituo cha polisi cha kati Mjini Arusha ambako walichukua maelezo yake na kumweka rumande!
Aliingia rumande akilia kwa uchungu kwa sababu alijua wazi hakuwa na hatia, alijaribu kadri alivyoweza kuwaelewesha askari ni kiasi gani alimpenda Caroline na asingeweza kumuua lakini hakuna mtu aliyeonekana kumwamini!
Baadhi ya watu walianza kufikiri labda kweli Harry alifanya kitendo hicho baada ya kubaini Caroline alikuwa na kifafa, lakini kwa umri wake na jinsi alivyoonekana wengi waliamini isingekuwa rahisi kwake kufanya hivyo.Alilala mahabusu kwa siku mbili mfululizo akiwa amefunguliwa jarada la mauaji na upelelezi ulikuwa bado ukiendelea.
Baba yake Caroline alijua wazi Harry asingeweza kufanya hivyo lakini aliamua kunyamaza kwa kuamini Harry alichangia matatizo ya mtoto wake, hivyo hata kuwekwa ndani ilikuwa ni adhabu tosha kwake. Agripina alijaribu kufanya kila aliloweza kumwekea mwanae dhamana lakini ilishindikana kwa sababu kesi hiyo iliitwa ya mauaji! Roho ilimuumakwa sababu alijua mwanae hakufanya kosa lolote lile!
****************
Masaa 48 baada ya kuingizwa wodini ndiyo Caroline alizinduka! Neno la kwanza alilotamka baada ya kurejewa na fahamu lilikuwa Harry! Aliliita jina hilo kama mara mbili hivi kisha akafumbua macho yake na kuangaza huku na kule na kuwaona wazazi wake, mama yake alikuwa bado akilia machozi.
“Mama mbona unalia?”
“Kwanini ulitaka kujiua Caroline mwanangu wakati unajua wewe ndiye mtoto pekee tunayekutegemea na hatuna uwezo wa kupata mtoto mwingine!”
“Mama nimeaibika mno sina mahali pa kuificha sura yangu ni heri nife?”
“Yaani ndiyo ujiue? Ni wangapi walio na matatizo kama yako na wengine makubwa ziadi lakini wanaishi?”
“Ndiyo mama, lakini najua kabisa Harry ataniacha na mimi siwezi kuishi bila yeye ni heri nife tu mama! Kwanza Harry yupo wapi”
“Polisi walimchukua!”
“Polisi walimchukua!Kwanini?”
“Walidhani eti ndiye aliyetaka kukunyonga!”
“Baba!”
“Naam mwanangu!”
“ No! Haiwezekani, Harry hawezi kufanya hivyo, Harry hawezi kuniua, ni mimi mwenyewe niliyetaka kuitoa roho yangu! Tafadhali nendeni mkawaambie polisi wamwachie haraka iwezekanavyo vinginevyo nitautoa uhai wangu!” aliongea Caroline akilia.
Baba yake hakuyachukulia maneno hayo mzaha pale pale bila kuchelewa alitoka hadi nje na kuingia ndani ya gari lake na kwenda moja kwa moja kwenye ofisi ya mkuu wa polisi wa mkoa aliyekuwa rafiki yake mkubwa.
“Vipi mbona unahema?” Kamanda wa polisi wa mkoa aliuliza.
“Bwana mtoto wangu amezinduka na anadai kuwa huyu kijana mnayemshikilia hakuhusika kabisa na kitendo hicho, yeye alikuwa akijaribu kumuokoa na amesema kama hatutamwachia basi atajiua tena!”
“Lakini huyu binti yako vipi? Hivi anajua kweli kuwa kitendo cha kujiua ni kosa katika nchi hii, shauri yake atafungwa!” alisema kamanda na baadae alimwita askari mmoja wa kike na kumwagiza amletee faili la kesi ya Harry na amwite pia askari aliyekabidhiwa kupeleleza kesi hiyo!
Muda kama dakika kumi baadae askari aliingia ofisini akiwa na faili na kumkabidhi kamanda na alianza kuyapitisha macho yake akilisoma faili hilo, alipofika mwisho alimwamuru askari wa upelelezi kumtoa Harry ndani ya mahabusu na wakaondoka nae kwenda hospitali ya Mount Meru, hata kamanda wa polisi pia aliongozana nao.
Harry alipoingia wodini, Caroline alinyanyuka kitandani na kwenda kumkumbatia kwa furaha, watu wote walishangaa na baada ya kukumbatiana wote walianza kulia machozi.
“Harry tafadhali usiniache!”
“Nakupenda Caroline siwezi kufanya hivyo tafadhali niamini ingawa nimeteseka sana mahabusu! Walifikiri eti nilitaka kukunyonga, kweli naweza kukuua wewe kwa ninavyokupenda Caroline? “
“Huwezi kufanya hivyo!”
Watu wote waliokuwemo ndani ya chumba hicho waliendelea kushangazwa na waliamini kweli vijana hao walipendana na hapakuwa na jinsi ya kuwazuia wasiendelee na mapenzi yao! muda mfupi baadaye Caroline na Harry walianza kutembea kwenda nje ambako Harry alitaka kufahamu ukweli.
“Nilizaliwa kwa matatizo kwani wakati wa kuzaliwa nilikuwa mkubwa kuliko njia ya mama yangu ya uzazi ikabidi madaktari wanivute kwa kutumia vyuma! Ni madaktari hao ndio walionisababishia kifafa! Tangu utotoni nimeugua ugonjwa huu! kila mwezi tarehe kati ya 26-28 ni lazima nianguke kifafa, uliponiuliza juu ya jambo hilo nilikudanyanga kuwa huwa nipo katika siku zangu za hedhi hiyo si kweli bali huwa nafungiwa ndani ya chumba mpaka nianguke ndio niendelee na masomo!” Alisema Caroline akilia machozi kichwa chake kikiwa kimeegemezwa begani kwa Harry na kulowanisha shati lake.
“Kwanini hukuniambia ukweli tangu mwanzo Caroline?”
“Niliogopa!”
“Uliogopa nini?”
“Nilijua ungeniacha!”
“Lakini ulifanya vibaya sana kunificha ningejua nisingekulazimisha uje kwenye tafrija ingeendelea kubaki siri yetu wawili lakini sasa wanafahamu watu wengi!”
“Nisamehe Harry lakini naomba usiniache!”
“Kwanini unaongelea sana swala la kuachwa?”
“Harry ni mwanaume gani anayeweza kukubali kuwa na mpenzi mwenye kifafa?”
“Mimi naweza!”
“kweli?”
“Ndiyo Caroline!”
“ Kumbuka Harry hata mimi sikupenda kuwa hivi basi angalau univumilie mpaka tumalize shule huko mbeleni unaweza kuoa mwanamke mwingine na sitakuzuia lakini kwa sasa maisha yangu ni bure bila wewe!” alimaliza Caroline huku akilia.
Baadaye maaskari waliondoka kurejea makazini kwao, hapakuwa na kesi tena faili lilifutwa.
*******************
Jioni ya siku hiyo Harry alirejea nyumbani kwao ambako ugomvi mkubwa uliendelea kati yake na mama yake akizuia uhusiano wake na Caroline.
“Sitaki kukuona tena na yule msichana usije kutuletea watoto wenye kifafa kwenye ukoo wetu!”
“Mama kwani kifafa kinaweza kwenda kwa watoto?”
“Wewe hujui kuwa kifafa kinarithiwa?”
Moyo wa Harry uliuma na ghafla akili yake ilibadilika, alianza kujisikia tofauti juu ya Caroline
Siku ya tatu hali ya Caroline ilikuwa nzuri na wazazi wake waliamua kumpeleka shule ili aendelee na masomo yake! Alikwenda shuleni akiwa na hamu kubwa ya kuonana na Harry kwa sababu tangu waachane alikuwa hajampigia simu jambo ambalo halikuwa kawaida katika maisha yao ya urafiki alitaka kufahamu ni kitu gani kilitokea ingawa tayari alishaanza kuhisi kulikuwa na tatizo.
Wakati anaingia shuleni alimwona Harry akiongea katikati ya kundi la wasichana walioonekana kumuuliza juu ya kilichotokea. Bila kufahamu ambacho kingempata Caroline aliamua kumfuata kwenye kundi hilo. Habari zake za kuanguka kifafa zilishaenea shule nzima! Kila alikopita vidole vilimfuata nyuma, Caroline alijisikia vibaya na alitakani ardhi ipasuke aingie ndani yake kukimbia aibu.
“He! Michana mzuri hivi ana kifafa!”
“Alikuwa anaringa sana huyu tutamwona sasa kila tarehe 26-28! Tutakuwa tunamfuatilia!” walisema wasichana wawili aliopishana nao njiani, maneno hayo aliyasikia na yakamtia simanzi kubwa sana moyoni mwake lakini alijitahidi asilie.
Alipolifikia kundi hilo la wasichana Harry alikuwa bado yupo katikati akijaribu kusimulia yaliyotokea tena kwa sauti alijifanya hajamwona Croline ingawa alikuwa nyuma yake! Wasichana wote waliokuwa wakicheka walinyamaza ghafla, Caroline aliwasalimia lakini hakuna aliyeitikia.
“Harry!” Caroline aliita lakini Harry hakuitika. Akaita tena lakini bado alikuwa kimya akiendelea kuongea na wasichana kwa sauti ya chini! Ikabidi Caroline asogee na kumgusa mgongoni ndipo Harry akageuka na kumwangalia, sura aliyoivaa usoni siku hiyo haikuwa sura ya kawaida hata kidogo! Caroline hakuwahi hata mara moja kumwona Harry katika sura hiyo.
“Darling vipi?” Caroline aliuliza.
“Caroline it is history now! (Caroline yaliyotokea kati yetu hivi sasa ni historia tu!)
“He! Unasemaje Harry!”
“Naomba uchukue hii barua ukaisome kwa wakati wako!” Harry alimkabidhi Caroline barua hiyo na kuondoka zake kurudi katikati ya kundi la wasichana na kuendelea na maongezi yake.
Wasichana wote walimcheka Caroline kwa sauti, huku akilia Caroline alitembea kwa unyonge na kwenda hadi nyuma ya darasa lao na kuanza kuisoma barua hiyo, kabla hata hajafikia mwisho wake aliangua kilio, barua hiyo iliandikwa:-
Je barua hiyo imeandikwa nini? Na nini kitampata Caroline? Fuatilia wiki ijayo.
Mpendwa Caroline,
Nakubali kwa asilimia mia moja kuwa wewe ni msichana mzuri pengine kuliko msichana mwingine yeyote niliyewahi kumwona maishani mwangu!
Na ninakiri kukupenda Caroline na sikutegemea hata kidogo kuwa maneno ninayotaka kuyasema hapa ningeyasema maishani mwangu lakini nimelazimika kufanya hivyo ingawa sipendi.
Caroline ulifanya vibaya sana kunificha tangu mwanzo kuwa wewe ni mgonjwa wa kifafa kwani ungeniambia mara tulipofahamiana labda ningekuwa na maamuzi tofauti na niliyoyachukua! Kuanguka kwako mbele ya watu siku ya sherehe yangu ya kuzaliwa kuliniaibisha na kunifedhehesha sana! Kwa hivi sasa kila ninakopita nazomewa na kuambiwa natoka na msichana mwenye kifafa, mama yangu hataki hata kukuona na ametishia kujinyonga kama mimi na wewe tutaendelea kuwa wapenzi!
Caroline nashindwa nitafanya kitu gani ili niendelee kuwa na wewe! Kwa sababu hiyo napenda kutamka wazi kwamba tangu dakika unapoisoma barua hii sitaki tena uhusiano wa kimapenzi! Unaweza kutafuta mvulana mwingine yeyote anayeweza kuvumilia fedheha ya kuwa na mwanamke mwenye kifafa!
Sina mengi nakutakia kila la kheri katika maisha yako!
Ahsante,
Ni mimi,
Wako wa zamani,
Harry Robertson.
Ilikuwa asiimalize barua hiyo hadi mwisho lakini alijikaza akiamini labda mistari ya mwisho ingeweza kusema “Hata hivyo nitakuwa na wewe wakati tukitafuta matibabu” Lakini haikuwa hivyo mpaka anamaliza kuisoma barua hiyo shati lake la shule lilikuwa limelowa kwa machozi! Alihisi mwili wake kuishiwa nguvu na alifikiri angezirai wakati wowote! Moyo wake uliuma sana na alishindwa kuelewa ni kwanini mwanaume aliyempenda kiasi hicho, mwanaume aliyemwonyesha jinsi dunia ilivyo alikuwa ameamua kuumiza moyo wake!
Maneno ya mwisho aliyoyasema Harry msituni kuwa asingemwacha hata kama angekuwa mgonjwa wa Ukimwi yalimtia moyo na kumfanya ajisikie bado alipendwa na Harry! Alishindwa kuelewa maneno hayo yalipotelea wapi! Harry hakuwa mtu wa kubadilibadili maneno hivyo ndivyo alivyomfahamu.
Alipoangalia kwenye kundi la wasichana alimwona Harry akiwa katikati bado akiendelea kuongea tena bila kujali! kama vile kilikuwa hakijatokea kitu chochote! Moyo wa Caroline ulizidi kuumia, alitamani ardhi ipasuke na aingie ndani yake kukwepa aibu na maumivu yaliyokuwa mbele yake.
“Now I know boys tell sweet words superficially but hurt badly inside!(Sasa nimeelewa kweli wavulana husema maneno matamu juu juu lakini huumiza vibaya sana kwa ndani!) Alisema Caroline wakati akinyanyuka kutoka kwenye msingi aliokuwa amekaa.
Hakutaka kuendelea kubaki shuleni tena kwani asingeweza kuelewa kitu chochote darasani, machozi yalizidi kumbubujika bado hakuamini kama maneno katika barua hiyo yaliandikwa na Harry mvulana aliyezoea kumtamkia mara zisizopungua kumi kwa siku kuwa alimpenda kupindukia na alitaka kuwa mume wake baadaye! Caroline alimtupia lawama nyingi Mungu kwa kumpa sura nzuri lakini akaruhusu apate ugonjwa mbaya wa kumdhalilisha!
Huku akilia aliendelea pia kuwalaumu wazazi wake kuwa kuruhusu madaktari wamvute kwa vyuma wakati wa kuzaliwa na kuuharibu kabisa ubongo wake kitu kilichomsababishia kifafa!
“Kwanini hata sikuzaliwa kwa operesheni badala ya kuvutwa?” Alijiuliza Caroline.
Pamoja na lawama zote hizo bado ukweli ulibaki palepale kuwa Caroline alikuwa mgonjwa wa kifafa na tayari suala hilo halikuwa siri tena kila mtu shuleni na hata mitaani alielewa pamoja na uzuri wake Caroline alikuwa mgonjwa.
Akiwa mwenye mawazo mengi kupita kiasi alinyanyuka na kuanza kutembea taratibu kuelekea kwenye lango la kuingilia shuleni kwao, hakuwa na haja ya kwenda ofisini kwa walimu kuomba ruhusa ya kuondoka shuleni tena! Alishafikia uamuzi wa kuacha shule, hakutaka kusoma tena kwa sababu ya kuogopa kuzomewa na wanafunzi wenzake kila siku na si kusoma tu bali hakutaka kuishi tena Caroline alitamani kufa kuikwepa aibu na maumivu.
“Kama Harry asingenikataa ningefikiria kuishi lakini hivi sasa sitaki tena, ni bora nife!” Aliwaza Caroline wakati akitembea kwa miguu kutoka shuleni.
Kidogo agongwe na daladala lililokuwa likija kwa kasi wakati akijaribu kukatisha barabara kutoka shuleni kwao kwenda upande wa pili,kama si dereva wa gari hilo kufunga breki mambo yangekuwa mengine.
“Wee msichana unaleta uzuri wako siyo? Utakwenda ahera au umechoka kula pilau?” alifoka dereva wa daladala lililotaka kumgonga Caroline bila kujua kuwa huko ahera ndiko hasa Caroline alikotaka kwenda siku hiyo!
“Ee bwana Suka umekiona lakini kifaa chenyewe?” konda wa daladala hilo alimwambia dereva wake na abiria wengine ndani ya gari walitoa vichwa vyao kuchungulia nje! Kila mmoja wao alitingisha kichwa akikiri kuwa Caroline alikuwa mzuri kupita kiasi.
“Hivi kumbe wasichana wanaochorwa kwenye magazeti wapo? Mimi nilifikiri ni michoro tu! Huyu msichana anafanana kabisa na picha ambazo huchorwa kwenye gazeti la Bongo!” Alisema abiria mwingine na gari lilizidi kwenda kwa kasi.
“Konda hebu nilegezee hapo kwenye tuta!” Sauti ya mvulana mmoja ilisikika kutoka kiti cha nyuma na dereva alipunguza mwendo wa gari badala ya kupitia mlangoni kijana huyo aliruka na kutokea dirishani na kuanza kumkimbilia Caroline aliyekuwa upande wa pili wa barabara!
Caroline alitembea kuelekea kwenye duka lililoandikwa Manyilizu Chemist! Lilikuwa ni duka la madawa, mita kama mbili hivi kutoka alipokuwa Caroline kijana huyo aligundua Caroline alikuwa akilia machozi.
“Anti mambo?” Kijana huyo alianza kumsemesha lakini Caroline hakujibu kitu alizidi kububujikwa na machozi huku akitembea kwa kasi kuelekea kwenye duka dawa lililokuwa mbele yake.
Kijana huyo hakukata tamaa alizidi kumfuata kwa nyuma na alipofika dukani Caroline aliingia na kijana alibaki nje akisubiri.
“Vipi dada mbona unalia?” Muuza duka aliuliza.
“Naumwa sana na kichwa kaka!”
“Pole sana dada yangu nikusaidie nini?”
“Nisaidie vidonge kumi vya klorokwini najua hii ni malaria!”
“Sawa kidonge kimoja ni shilingi 20 kwa hiyo ni shilingi 200!”
“Sawa nipe!” Alisema Caroline wakati akimkabidhi muuza duka noti ya shilingi 5000 aliyokuwa nayo mfukoni, alipokabidhiwa dawa hakutaka hata kusubiri chenji yake alitoka nje na kuanza kukimbia! Ilibidi mwenye duka amkimbilie hadi akampata.
“Dada chenji yako hii hapa!” Alisema muuza duka na Caroline alipokea chenji na bila hata kutoa shukrani alianza kuondoka mbio.
Kijana aliendelea kumfuata kwa nyuma bila kuchoka, alikuwa amevutiwa kiasi cha kutosha na sura ya Caroline naye katika maisha yake hakuwahi kuona msichana mwenye sura nzuri kama ile!
“Lazima nimwambie shida yangu, sijui anaishi wapi Arusha hii? Mtoto wa nguvu kiasi hiki bado sijamwona na mimi ndiye bingwa wa ……….!” Aliwaza kijana huyo akimfuatilia Caroline kwa nyuma mbele alimshuhudia akiingia katika duka jingine la madawa alisimama nje akimsubiri.
“Dada una klorokwini hapa dukani kwako?”
“Cheti cha daktari kiko wapi?”
“Sina ila huwa natumia dozi ya 4/4/2/2!”
Maneno hayo ya Caroline yalimridhisha dada muuza duka na kujikuta akimuuzia Caroline vidonge vingine kumi vya klorokwini! Maongezi yao yote aliyasikia na kushtuka, aligundua lengo la msichana huyo halikuwa jema hata kidogo na kwa hali aliyomwona nayo alielewa wazi msichana huyo alitaka kujiua kwa vidonge.
“Lakini kwanini msichana mzuri kama huyu ajiue?” Alijiuliza kijana huyo bila kujua suluhu!”
Alipotoka dukani Caroline alishangaa kukuta kijana huyo aliyevaa nguo za kupendeza, kichwani kwake akiwa amenyoa panki na chini amevaa viatu aina ya mokasini nyeupe akimsubiri. Alimwangalia kwa jicho la chuki na kuonyesha kabisa hasira yake waziwazi! Caroline aliwachukia wanaume wote duniani kwa sababu ya kitendo alichofanyiwa na Harry, aliwaona wanaume wote duniani ni wanyama na hakutaka tena uhusiano wowote na mvulana yeyote!
“Hivi wewe unanitafuta kitu gani au wewe ni kibaka nini?”
“Hapana dada mimi naitwa Richard Nelson nimemaliza kidato cha sita katika shule ya sekondari ya Umbwe sijui mwenzangu unaitwa nani?”
“Jina langu siyo shughuli yako, tafadhali naomba uniache ufuate mambo yako sitaki unifuatefuate na ukizidi kunisonga nitakupigia kelele za mwizi!” Alisema Caroline huku akilia.
“Sawa dada lakini naomba usifanye unavyotaka kufanya kwani mimi nitaumia sana sababu nimekuona kwa macho yangu!”
“Ninavyotaka kufanya? Yaani kitu gani?”
“Najua unataka kujiua! Tafadhali usifanye hivyo hebu nieleze tatizo lako labda ninaweza kukusaidia!”
“Kunisaidia? Utanisaidia nini wewe sitaki kukuona mbele ya uso wangu ondoka sasa hivi!” Alisema Caroline kwa ukali na kuanza kuondoka akitembea kwa kasi, Richard alizidi kumfuata kwa nyuma hakuwa tayari kuona roho ya msichana mzuri kama Caroline ikipotea alitaka kufanya kila kilichowezekana kuokoa maisha yake.
Mbele kidogo Caroline aliingia tena katika duka jingine na kutoka na chupa ya maji akiendelea na safari yake Richard akiwa nyuma yake akizidi kumbembeleza asifanye alichotaka kufanya!
Katika hali ambayo Richard hakuitegemea na katika kasi ya ajabu walipofika pembeni mwa uwanja wa Sheikh Amri Abeid, alishuhudia Caroline akitupia vidonge mdomoni mwake, wala hakujua ni muda gani alivitoa vidonge hivyo kutoka kwenye vifuko vyake na kwa haraka aliinamisha chupa ya maji mdomoni na kuanza kumeza.
Kama upepo Richard aliruka na kumwangusha Caroline chini na kumkaba shingo ili asimeze vidonge hivyo! Watu waliokuwa jirani na eneo hilo walipoona kitendo hicho walifikiri mwanafunzi anakabwa na kibaka! walitoka mbio na kwenda hadi eneo hilo na mmoja wao bila kuchelewa alirusha jiwe kubwa lililotua moja kwa moja kichwani kwa Richard na kumpasua! Damu nyingi zilivuja ikabidi amwachie Caroline aliyetumia nafasi hiyo kuvimeza vidonge vyote alivyomwaga mdomoni mwake.
“Jamani mimi siyo mwizi najaribu kuokoa maisha ya huyu dada amekunywa vidonge vingi vya klorokwini anataka kujiua!” Alipiga kelele Richard.
“Wewe muongo tu nyie ndio vibaka mnaotusumbua mitaani leo lazim ufe maana kila tunapowapeleka polisi mnaachiwa!”
“Ndiyo!Ndiyo! Ndiyo! Huyu ni kibaka anataka kuniibia mkoba wangu wa pesa!”Alisema Caroline baada ya kumeza vidonge alionekana kuwa na nguvu.
Watu wengi walianza kuwasili na kumpiga Richard kwa mawe, marungu na matofali huku Caroline akishuhudia kitendo kile cha kikatili, alijua Richard alipigwa kwa kuonewa lakini kwa hasira aliyokuwa nayo dhidi ya wanaume wote duniani hakujali wala kumwonea huruma! Richard alizidi kushambuliwa Caroline akiwa amesimama pembeni akishuhudia.
“Nipisheni!Nipisheni!” Alisema mtu mmoja akiwa na tairi la gari pamoja na galoni ya mafuta ya petroli akiwa na ameuma kiberiti mdomoni kwake alikuwa ameamua kumchoma Richard kwa moto kama walivyofanywa vibaka wengine!
Wananchi wote walimpisha akaanza kummwagia Richard mafuta mpaka akalowana kabisa! Kabla hawajamtia kiberiti walishangaa kuona Caroline akiyumba na kuanguka chini kisha kupoteza fahamu zake.
“jamani vipi au kweli kanywa vidonge nini?” Walijiuliza wananchi na walipompekua katika mfuko wake wa shati walikuta vifuko viwili vilivyoandikwa chloroquine 4/4/2/2 kila kimoja na vyote havikuwa na kidonge ndani! Hiyo ilimaanisha kweli binti huyo alikunywa klorokwini kwa lengo la kujiua!
“Jamani mimi siyo mwizi jamani! kitambulisho changu cha shule hiki hapa!” Alisema Richard akiwa amenyanyua kitambulisho chake mkononi, mmoja wa watu alikichukua na alipokisoma kweli kilionyesha alikuwa mwanafunzi aliyemaliza kidato cha sita katika shule ya sekondari ya Umbwe mwezi mmoja kabla.
Dostları ilə paylaş: |