Wananchi waligundua makosa yao na kwa kuogopa polisi walianza kusambaa taratibu mpaka wote wakaisha na kuwaacha Caroline na Richard wakiwa wamelala chini peke yao! Damu nyingi ziliendelea kuvuja katika mwili wa Richard! Mwili wake ulipasuliwa pasuliwa kwa mawe na matofali, nguo zake zote zililowa lakini pamoja na hali hiyo mbaya alimsogelea Caroline na kuanguka juu yake.
“Nina..kufa saba..bu ya kuo..koa mai..sha ya..ko! Haina shi..da Mun.gu ana..jua!” Alisema kwa tabu Richard.
Hapakuwa na msaada wowote ule watu wote walishakimbia kutoka eneo hilo kuogopa polisi! Hakuna aliyejitokeza kulisogelea eneo hilo,kila mtu aliogopa kuhusishwa na kosa la kujichukuliwa sheria mkononi.
Kadri msaada ulivyozidi kuchelewa ndivyo vidonge vya klorokwini vilivyozidi kuingia katika damu ya Caroline na kumwathiri zaidi! Macho yake yalikuwa mazito sababu ya athari za dawa hizo, kizunguzungu kilimtawala! Alijitahidi kufungua macho yake lakini alishindwa na alipogusa juu yake alishika mwili wa mtu alijua mtu huyo hakuwa mwingine bali Richard!
“Ninaitwa Caroline ni vyema unifahamu kabla sijafa samahani kwa kukusababishia kifo Richard ni hasira iliyonifanya hivyo! Nisamehe Richard kabla hatujafa ninajua hauna makosa aliyestahili kufa ni Harry” Alisema Caroline kwa taabu!
“Usijali lakini tatizo lako ni nini!”
“Siwezi kukuambia ila naomba samahani kwa yote yaliyokupata!”
Hakuna mtu aliyejitokeza kuwapa msaada wowote! Kwa Caroline ilikuwa furaha lakini kwa Richard ilikuwa huzuni kubwa kukutana na kifo mahali ambapo hakutegemea!
Je watapona? Futilia wiki ijayo.
B
inadamu wote duniani
hawawezi kuwa na mioyo
na tabia ya aina moja kwani wakati Richard anamwagiwa mafuta ya petrol, msichana mmoja aliingiwa na huruma sana na kupiga simu polisi.
“Ni eneo gani hilo?”
“Hapa ni karibu kabisa na uwanja wa Sheikh Amri Abeid njia ya kwenda kituo cha mabasi!”
Baada ya simu hiyo maaskari walingia ndani ya gari na safari ya kuelekea eneo waliloelezwa na mpiga simu hiyo ilianza, walipofika eneo waliangalia mahali kuliko kuwa na mkusanyiko watu lakini hawapakuona na kuzidi kusonga mbele.
“Afande nafikiri ni pale!”
“Wapi?”
“Pale walipolala watu wawili ardhini!”
“Inawezekana!” Alijibu dereva wa gari hilo aliyekuwa na V mbili begani na kukata kona haraka kuelekea mahali alipoonyeshwa. Msichana mmoja aliwafuata mbio.
“Afande ni mimi ndiye niliyewapigia simu!”
“Binti wamekuwaje hawa watu lakini?”
“Huyu kijana amepigwa na wananchi wenye hasira baada ya huyu msichana kudai alitaka kumpora mkoba wake! Lakini yeye alidai alikuwa akimuokoa huyu msichana baada ya kunywa vidonge vya klorokwini kwa lengo la kujiua!”
“Ilikuwaje huyu msichana akafikia hatua hii sasa?” Maaskari waliendelea kuuliza maswali wakati wakiwapakia ndani ya gari.
“Alianguka peke yake na alipochunguzwa mfukoni alikutwa na vipakiti viwili vilivyoandikwa juu yake Chloroqwine 4/4/2/2!”
“Vilikuwa na vidonge?”
“Vyote viwili havikuwa na kidonge hata kimoja!”
“Aisee inawezekana kweli huyu binti alikunywa vidonge!”
Wote wawili walipakiwa ndani ya gari na kuondoka kwa kasi kuelekea hospitali ya Mount Meru, hakuna hata raia mmoja aliyejitokeza zaidi ya msichana huyo! Watu wote waliogopa sababu waligundua waliua kimakosa.
Mapokezi walipokelewa vizuri,Richard alikimbizwa chumba cha upasuaji na Caroline alikimbizwa chumba cha wagonjwa mahututi ambako tumbo lake lilisafishwa na kuwekewa dripu za maji katika mishipa yake ili kuyapunguza nguvu madawa yaliyokuwa kwenye mishipa yake ya damu! Hakuna mtu aliyekuwa na uhakika Caroline na Richard wangepona!
“Mama yangu wee! Ni Caroline!” Alipiga kelele mmoja wa wauguzi baada ya kumchunguza vizuri Caroline usoni.
“Caroline gani?”
“Mtoto wa mzee John Kadiri anayesifika kwa uzuri Arusha nzima!”
“Nasikia ni msichana hana boyfriend sasa imekuwaje akaamua kunywa sumu?”
“Ah! Wapi! Si anatoka na mwanafunzi mwenzake aitwaye Harry!”
“Sasa tufanye kitu gani?”
“Tupige simu nyumbani kwao ili tuwajulishe wazazi wake!”
Richard aliporudishwa kutoka chumba cha upasuaji sehemu nyingi za mwili wake zilikuwa zimeshonwa, chupa za damu na maji zilikuwa zikimiminika kuingia katika mishipa yake.Muuguzi mmoja alimwangalia kwa makini na kumtambua.
“Ha! Kumbe huyu naye ni mtoto wa jaji Lushinga!”
Simu zilipigwa kwa familia zote mbili za Caroline na Richard na katika muda wa dakika arobaini na tano tu hospitali ilijaa idadi kubwa ya ndugu na marafiki huku wengi wakilia! Haikuchukua muda mrefu sana taarifa hizo zilifika katika shule ya sekondari ya Arusha! Wanafunzi wengi walimiminika kwenda hospitali ya Mount Meru kumwona Caroline, mtu mmoja muhimu hakujitokeza naye ni Harry! Hakujitokeza kabisa hospitali na wala hakuumizwa na taarifa hizo.
Wanafunzi wengine katika shule ya sekondari ya Arusha walipopewa taarifa kuwa Caroline alikunywa vidonge vya klorokwini kwa lengo la kujiua walisikitika sana, walipoonyeshwa barua ambayo Harry alimwandikia Caroline walisikitika zaidi na walimtupia lawama Harry kwa tatizo lililojitokeza.
Si wanafunzi peke yao waliofikiria hivyo bali polisi pia! Harry alikamatwa jioni ya siku hiyo akiwa shuleni na kupelekea kituoni ambako alifanyiwa mahojiano na baadaye kuwekwa rumande! Akiwa ndani alijilaumu kwa kitendo alichokifanya! Kwa ndani alihisi bado alimpenda Caroline lakini alimwogopa mama yake na wanafunzi wenzake.
Dk. Cynthia na mumewe walisikitishwa na kitendo cha mtoto wao kutoka kujiua na walimchukia Harry wakiamini barua yake ndiyo ingesababisha kifo cha mtoto wao, walikuwa na uhakika ni yeye aliyemshawishi mtoto wao kuingia katika uhusiano wa kimapenzi! Kitendo cha kumkatia mapenzi ghafla waliamini ndicho kilichomsababishia matatizo.
“Labda apone lakini mwanangu akifa sijui kitakachotokea kwa kweli?” Baba yake Caroline alifoka hospitalini.
**************
Masaa arobaini na nane baadaye mapigo ya moyo wa Caroline yaliyokuwa yameshuka kiasi cha kutishia maisha yake yalianza kupanda taratibu na hatimaye kurejea katika hali ya kawaida kabisa! Alipofumbua macho yake na kukuta baba na mama yake wapo pembeni mwa kitanda chake.
“Nani ameniokoa? Nataka kufa mimi? Niacheni nife nimekwishasema sitaki kuishi!” Alisema Caroline huku akijaribu kuketi kitako kitandani, mwili wake ulikuwa na nguvu za ajabu lakini baba na mama yake walimkandamiza kitandani na kubaki amelala chali.
“Mama!”
“Naam mwanangu!”
“Niache nife mama, Harry hawezi kitendo alichonifanyia!”
“Msamehe mwanangu maisha yako ni bora kuliko huyo Harry, tufikirie mimi na baba yako wewe ndiye mtoto wetu pekee ukifa tutafanya nini? Tafadhali usijiue mwanangu!”
Caroline aliendelea kulia kwa uchungu hakuuona kabisa umuhimu wa kuendelea kuishi duniani, alihisi kufedheheka vya kutosha, uzuri wake haukuwa na maana yoyote kwake Harry alikuwa amefanya kitendo cha kumuumiza moyo wake ambacho hakuwahi kutegemea kufanyiwa maishani mwake.
“Harry! Harry! Harry! Kweli unanitenda hivi mimi, sawa tu!”
“Mwachie Mungu mwanangu” Dk Cynthia alimwambia Caroline.
“Sawa mama lakini nimefanya kosa moja baya sana!”
‘Kosa gani?”
“Nimesababisha kifo cha mtu asiye na hatia!”
“Nani?”
Caroline alimsimulia kila kitu kilichotokea mpaka Richard akishambuliwa na mawe na watu akidhaniwa ni mwizi!
“Nilikuwa na hasira mama!”
“Ni mtoto wa jaji Lushinga baba yake alikuja hapa jana kukuona, akasema hali ya mtoto wake ilikuwa ikiendelea vizuri alisikitika sana kwa kilichotokea!”
“Atapona lakini mama?”
“Baba yake alisema matumaini yapo!”
“Ee Mungu wangu, mama nipelekeni nikamwombe msamaha huyo kaka sasa hivi, nimemkosea sana!”
Wazazi wake walikataa na Caroline alikubali kwa shingo upande na kubaki kitandani kwa wiki kama tatu akipatiwa matibabu, siku ya kwanza ya wiki ya nne alishtukia mlango wa chumba alicholazwa ukifunguliwa na kuingia kijana mwembamba mrefu akiwa amefungwa bandeji sehemu kubwa ya uso wake, mikono yake yote miwili ilikuwa imefungwa na piopii!
Kijana huyo alitembea kwa kuchechemea kuelekea kwenye kitanda cha Caroline na alipomwangalia usoni aligundua kijana huyo ni Richard! Alinyanyuka kitandani na kumfuata, alipomfikia alipiga magoti chini na kuanza kumwomba msamaha.
“Nisamehe sana Richard ilikuwa ni hasira dhidi ya wanaume!” Aliongea Caroline huku akilia machozi.
“Nilikusamehe tangu siku hiyo Caroline, kitu kimoja ninachotaka kukueleza ni kwamba pamoja na yaliyojitokeza bado nakupenda Caroline na penzi langu ni la kweli tafadhali nikubalie niwe mpenzi wako, nina hakika Mungu ametunusuru kutoka katika kifo ili tuwe wapenzi!”
“Naogopa Richard!”
“Unaogopa kitu gani?”
“Siwezi kukueleza ila ni hicho ndicho kilinifanya nitake kujitoa roho, hutaniweza Richard!’
“Kwanini nisikuweze?”
“Basi tu!”
“Na kwanini ulitaka kujiua sasa?”
“Siwezi kusema!”
Wiki mbili tu baadaye wote wawili waliruhusiwa kutoka hospitali hali zao zikiwa nzuri, wazazi wa pande zote mbili waliketi pamoja na kuyamaliza mambo hayo wakimshukuru Mungu kwa kuokoa maisha ya watoto wao, polisi walipofuatilia ili Caroline afikishwe mahakamani kwa kosa la kutaka kujiua mambo yalizimwa kimya kimya!
Caroline na Richard waliendelea kuwa marafiki wakubwa! Kwa sababu ya mapenzi aliyokuwa nayo Caroline alimshinikiza baba yake amwachie Harry kutoka mahabusu.
“Mwachie tu baba yote anayajua Mungu hata ukimfunga haitasidia kitu!”
‘Hapana ni lazima nimpe somo maana hii ni dharau sasa, nakumbuka huko nyuma pia ulisema hivyo hivyo tukamwachia!”
“Sawa baba lakini hatutakiwa kuhesabu makosa!” Maneno hayo yalimfanya profesa John Kadiri kukubali kumsamehe Harry.
*************
Hali ya Arusha haikuwa nzuri kwa Caroline tena, alizidi kukonda sababu ya mawazo juu ya Harry, alitembea njiani akiongea peke yake, kila alipomwona Harry akipita alilia machozi, alimpigia simu mara kwa mara kumbembeleza waendelee lakini kila mara Harry alikata simu.
“Inabidi Caroline ahamishwe Arusha vinginevyo atakuwa mwehu!” Ulikuwa ni ushauri wa mtaalam wa magonjwa ya akili wa hospitali ya Mount Meru.
Dr Cynthia na mumewe John Kadiri walikubaliana na ushauri wa daktari ikabidi mwezi mmoja baadaye utaratibu wa haraka kumhamishia Caroline Dar es Salaam kwa shangazi yake ulifanyika huko aliendelea na masomo katika shule ya sekondari ya wasichana ya Jangwani.
****************
“Paaaaaaaa!” Ulikuwa ni mlio mkubwa katika makutano ya barabara ya Morogoro na Swahili eneo la zimamoto, daladala mbili zilikuwa zimegongana uso kwa uso! Abiria walikuwa wakiwashambulia madereva wa magari hayo kwa kusababisha ajali kizembe! Ajali hiyo isingetokea kwenye mataa kama madereva hao wangefanya kazi yao vizuri!
Msichana mrembo alikuwa akipita kandokando ya barabara ya akielekea shule ya sekondari ya Jangwani ni msichana huyo ndiye aliyesababisha ajali hiyo kutokea kwani badala ya madereva wa daladala kuendesha magari walibaki kumshangaa binti huyo alivyotembea na kutingishika kwa nyuma.
*************
Jiji la Dar es Salaam ni kubwa na lenye idadi kubwa sana ya watu ni kitu kigumu sana kujulikana ndani ya jiji hilo! Lakini kuingia kwa Caroline kulilitingisha jiji zima la Dar es Salaam, alikuwa gumzo midomoni mwa watu. Kila aliyemwona hakuamini kama kulikuwa na wasichana wazuri kiasi kile! Kila dereva aliyepita na kumwona Caroline ilikuwa ni lazima akanyage breki na kumwangalia angalau kidogo ndiyo aondoke! Waalimu wa kiume katika shule ya sekondari ya Jangwani walichanganyikiwa kwa uzuri na sura ya mwanafunzi huyo mgeni kutoka Arusha.
Jambo hilo lilimkera sana Caroline ambaye kwa donda alilosababishiwa na Harry ambalo lilikuwa bado halijapona aliuahidi moyo wake kutompenda mwanaume mwingine tena maishani! Aliwachukia wanaume kuliko kitu kingine chochote.
Pamoja na yote aliyotendewa na Harry bado aliendelea kumkumbuka kama mwanaume aliyemwonyesha dunia ilivyokuwa kwa mara ya kwanza, bado alihisi upande mmoja wa moyo wake ulimpenda Harry na aliamini kama ingetokea siku moja akaja kwake na kumuomba waendelee asingesita kukubali, zaidi ya Harry hakutaka mwanaume mwingine zaidi.
******************
Miaka mitatu baadaye:
Ratiba ya maisha ya Caroline jijini Dar es Salaam ilikuwa ni ileile! Kila tarehe 26-28 ya kila mwezi alijifungia ndani akisubiri kuanguka kifafa! Alikuwa mwangalifu sana na tarehe hizo kiasi kwamba hakuna mtu hata mmoja aliyegundua tatizo lake.
Watu wote waliendelea kumpa heshima ya msichana mrembo kuliko wote jijini Dar es Salaam, waandaji wa mashindano ya urembo walimfuata mara nyingi ili ashiriki mashindano hayo lakini hakukubali kwa sababu sheria za shule hazikumruhusu.
Caroline alipomaliza kidato cha sita miaka mitatu baadaye aliwashangaza wazazi wake alipofaulu na kupata divisheni 1!! Kwa furaha Dk. Cynthia na mumewe profesa Kadiri walimwambia achague nchi yoyote aliyetoka kwenda ili wampeleke kupumzika, Caroline alichagua Uingereza.
Kwa miezi miwili alikaa Uingereza kama zawadi kwa ushindi alioupata! Huko Uingereza aliishi na familia moja iliyokuwa na uhusiano na wazazi wake, akiwa huko alimfikiria Richard lakini hakujua mahali pa kumpata kwani alishapoteza anuani zake na hata jina la chuo alichosoma!
***************
Akiwa ndani ya ndege ya British Airways akirudi Tanzania alishtukia kijana amesimama mbele yake na kumwita kwa jina.
“Hee! Richard!” Alijiitikia kwa mshangao.
“Vipi?” Unatoka wapi huku wewe chaurembo?” Richard aliuliza.
“Nilikuwa hapa UK kwa miezi miwili!”
“Bila hata kunitafuta?”
“Sikujua kama uko hapa!”
Waliongea mengi na Richard alimweleza Caroline juu ya mapenzi yake kwake na alimtakia wazi kuwa alitaka kumuoa, kwa mara ya kwanza Caroline alihisi kumpenda Richard lakini kila alipoufikiria ugonjwa wake wa kifafa kisichopona alizidi kuchanganyikiwa! Alijichukia mwenyewe.
“Nitafikiria lakini kuna kitu itabidi nikueleze kwanza!” Alijibu Caroline.
“Sawa tu!”
Uwanja wa ndege wa Dar es Salaam walipokelewa na kijana mmoja aliyeitwa Dickson akiwa na mpenzi wake Mariam! Dickson alipomwona Caroline alipigwa na butwaa kwa uzuri aliokuwa nao na Richard alipomwona Mariam alibaki mdomo wazi kwa uzuri wa msichana huyo.
Shangazi yake Caroline alimpokea na kumpakia ndani ya gari na Dickson, Richard na Mariam waliondoka ndani ya gari walilokuja nalo hadi Mikocheni nyumbani kwao na Dickson. Kwa sababu Mariam alikuwa mwanafunzi wa chuo cha Usimamizi wa fedha (IFM) baada ya kufika nyumbani aliondoka kurudi chuoni na kuwaacha Dick na Rich peke yao.
“Mshikaji kile kifaa vipi?” Dickson alimuuliza Richard.
“Si ndiye yule mtoto wa Arusha aliyenisababishia matatizo kipindi kle umesahau?”
“Aisee ndiye yule?”
“Ndiyo bwana ila sasa hivi kazidi kuwa mzuri!”
“Aisee usimwachie mshikaji kaza kamba angalau ufidie kidogo maumivu uliyoyapata!”
“Safari hii sikubali lazima nimpate na akikubali nitaka nimuoe kabisa ili nikiondoka kurudi Uingereza niondoke naye!”
“Poa tu, lakini kati yake na Mariam nani zaidi?”
“Caroline zaidi!”
“Ah! Wapi ni Mariam zaidi huuoni usafiri wake!”
Yalitokea mabishano makali kati yao na hawakufikia muafaka kila mmoja wao akisema wa kwake ni zaidi.
************
Miezi mitatu baadaye mambo yalishakolea kati ya Caroline na Richard! Caroline alihisi kuchanganyikiwa na penzi la Richard hakuwahi kufikiria kuwa siku moja angechanganywa na mwanaume kiasi hicho baada ya kuapa kuwa asingempenda mwanaume tena. Kilichomsumbua akilini mwake kilikuwa ni tatizo la kifafa, siku zote hakuzisahau tarehe 26-28!
“Siku akijua itakuwaje? Au yakitokea kama yaliyotokea kwa Harry?” Swali hilo lilimsumbua sana kichwani mwake! Lakini bado hakuwa tayari kuisema siri iliyosema moyoni mwake.
*****************
Mashindano yalikuwa yamefikia hatua ya tano bora.
“Mshiriki anayefuata sasa ni mwakilishi wa Ilala, Mariam Hassan!”Ukumbi mzima ulishangilia kwa vigelegele.
Richard na Dickson walikuwa nyuma kabisa ya ukumbini wakiangalia kwa chati! Alipotajwa Mariam, Dick aliruka juu na kushangilia lakini Richard alinyong’onyea na kukosa raha kabisa! Dick alianza kumzomea.
“Nilikuambia mshikaji kuwa Caroline siyo kitu! Ukabisha unao sasa hata kwenye tano bora hayumo!”
“Anayefuata ni Caroli…..!” Kabla hata Jaji hajamaliza sentensi yake Richard aliruka juu na kuanza kushangilia huku akikimbia kwenda jukwaani! Hakuamini kama alikuwa amelisikia jina la mpenzi wake likitajwa.
Ilikuwa siku ya tarehe 27/12/1999 watu walifurika ndani ya ukumbi wa Diamond Jubilee kushuhudia kinyang’anyiro cha Miss Tanzania! Ni mabishano ya “nani zaidi” yaliwafanya Richard na Dickson kuwashinikiza Mariam na Caroline washiriki mashindano hayo.
Awali mashindano hayo yalipangwa kufanyika tarehe 14/10/1999 lakini yaliahirishwa sababu ya kifo cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere! Ni tarehe hizo zilizomfanya Caroline akubali kushiriki mashindano lakini yalisogezwa mbele hadi tarehe 27/12/999! Alikataa lakini Richard alimlazimisha kwa kitisho cha kuacha kumuoa na kwenda naye Uingereza.
“Mbona Mariam anashikiri yeye siyo msomi?”
“Siyo hivyo Richard najua ni kwanini sitaki kushiriki siku hiyo ingekuwa siku nyingine yoyote sawa kwani hawawezi kufanya mwezi wa kwanza? Au tarehe 30/12/1999?” Aliuliza hakuwa tayari kushiriki lakini badala ya kushawishiwa sana na Richard alikubali kwa shingo upande akitegemea labda siku hiyo isingekuwa mbaya kwake, alitamani aanguke tarehe 26 au 28!
************
Kipindi cha kuulizwa maswali kwa washiriki wa tano bora kilimalizika na Jaji maarufu jijini Dar es Salaam Bw. Manjit alisimama wima kutaja majina ya washindi wa Miss bongo
Gari aina ya benzi lililokuwa zawadi ya mshindi wa Miss Tanzania lilikuwepo ukumbini hapo! Minong’ono ya chinichini ilisikika Caroline akitajwa karibu na watu wote ukumbini kuwa ndiye alistahili kuwa mshindi! Wakati huo Caroline alikuwa nyuma ya pazia akitetemeka hali yake aliisikia si nzuri alihisi kizunguzungu.
Jaji alitaja majina ya washindi namba nne na tatu, ukumbi wote ulipiga kelele na kushangilia kwa furaha, nyuma ya pazia walibaki watu wawili tu mariam na Caroline.
“Haya mzee mwenzangu nani anaibuka dume kati yangu mimi au wewe!” Dick aliuliza lakini Richard hakujibu kitu alisubiri sauti ya jaji Mkuu.
“Mshindi wa pili ni Mariam Hassan!” Ukumbi wote ulipiga kelele na kushangilia baada ya kujua Caroline ndiye alikuwa ameibuka mshindi wa Miss Tanzania! Richard alilia kwa furaha.
“Nilikueleza mzee mwenzangu Caroline ni kifaa cha nguvu ukabisha unaona sasa!” Richard alimwambia Dickson.
“Miss Tanzania mwaka huu ni Caroline John Kadiri!”
“Nyanyuka twende wewe ndiye Miss Tanzania!” Wasichana wenzake walimwambia lakini hali ya Caroline haikuwa nzuri.
“Sitaki kwenda jukwaani!” Alikataa Caroline.
“Kwanini?”
“Najua mwenyewe!” Alijua wakati wowote angeanguka kifafa muda mfupi baadaye Richard na Dickson pamoja na mwaandaaji walipokwenda na kumleta hadi jukwaani ambako kizunguzungu kilizidi.
“Richard! Richard! Richard!”
“Naam Darling!”
“Nirudishe nyuma ya pazia upesi!”
“Kwanini?”
“Wewe nirudishe tu!”
“Hapa....!” kabla Richard hajakamilisha sentensi yake Caroline alianguka sakafuni, akageuza macho na povu likamtoka mdomoni! Watu wote ukumbi mzima walishika mkono kichwani na wengine kuzomea.
“Miss Tanzania ana kifafa!”
Richard alimwaga machozi ya huzuni.
Je nini kitatokea? Fuatilia wiki ijayo.
Caroline ni msichana mrembo kupita kiasi mwenye siri kubwa moyoni mwake, siri ya ugonjwa wa kifafa! Siri ambayo hataki mtu mwingine yeyote zaidi ya wazazi wake aifahamu lakini inakuwa vigumu kufanya hivyo kwani tayari amekwishaanguka mara mbili mbele za watu! Mara ya kwanza alianguka mbele ya mpenzi wake Harry na akaachwa! Mara ya pili ameanguka baada ya kutangazwa tu kuwa mshindi wa Miss Bongo zawadi yake ikiwa gari aina ya Benz! Ameanguka mbele ya mpenzi wake mpya, Richard. Je nini kitampata na siri yake hiyo? Endelea............
Watu wote waliokuwa ukumbini walipigwa na butwaa sababu ya hali iliyojitokeza, mikono ya watu wengi ilikuwa kichwani kwa uchungu! Wachache hasa wasichana waliowashangilia washindani wengine waliotupwa na Caroline wakisikika wakizomea kwa sauti ya juu! Lilikuwa ni jambo la kusikitisha kupita kiasi, hakuna mtu aliyekuwa tayari kuamini kuwa msichana mrembo kama Caroline alikuwa ameanguka kifafa tena mbele ya watu baada ya kutangazwa ni mshindi wa Miss Tanzania.
“Karogwa! Karogwa!” Sauti ilisikika kila sehemu ukumbini, watu wasijojua siri ya ugonjwa wa Caroline walipiga kelele.
Caroline alikuwa amelala chali jukwaani akiwa amezungukwa na watu wengi, kila mtu alitaka kumwona mrembo aliyeanguka kifafa! Wapiga picha wa magazeti mbalimbali walikuwa bize wakipiga picha zake kwa ajili ya magazeti yao siku iliyofuata.
Richard alisimama mbele ya Caroline akilia machozi, hakuwa tayari kuamini kilichokuwa kimetokea usiku huo, kwa uzuri aliokuwa nao Caroline hakutakiwa kabisa kuwa na kifafa! Hiyo ilikuwa kasoro mbaya sana, kwa Richard yaliyotokea usiku huo yalikuwa ni kama ndoto!
Dickson na Mariam walimpigapiga Richard mgongoni kumfajiri kwa yaliyojitokeza lakini alizidi kulia, alimpenda mno Caroline lakini alihisi asingeweza kuendelea na msichana mwenye kifafa! Kwake ilikuwa ni bora aishi na msichana kikojozi kuliko mwenye kifafa!
Upande mwingine kichwani mwake alihisi kulikuwa na kitu kilichofanya kwa lengo la kumharibia Caroline ushindi wake. “Kuna mtu amefanya uchawi ili achukue ushindi” Aliwaza Richard.
Dakika kama arobaini na tano baadaye Caroline alishtuka na kuketi kitako jukwaani, alifungua macho na kuangalia kila upande, alishangaa kukuta idadi kubwa ya watu wamemzunguka! Hakuwa na kumbukumbu juu ya kitu chochote kilichotokea na hakukumbuka pia alikuwa mahali pale kufanya jambo gani! Kumbukumbu zote juu ya mashindano ya Miss Bongo aliyokuwa akishiriki zilikuwa zimepotea.
Alipoangalia vizuri kati ya watu waliomzunguka alimwona Richard akilia moyo wa Caroline ulishtuka na kujikuta akisimama wima kutaka kujua kilichotokea!
“Richard kimetokea kitu gani hapa mbona watu wamejaa?”
Richard hakujibu kitu bali aliendelea kutokwa na machozi jambo lililozidi kumtia wasiwasi zaidi Caroline, hakuwa na kumbukumbu hata kidogo juu ya kilichompata! Alipounyanyua mkono wake wa kulia kwa lengo la kujikuna usoni alikumbana na mapovu mdomoni! Aliushusha tena ukatua kwenye gauni lake zuri la kutokea jioni alilovaa kwenye maonyesho hayo lililobuniwa na mbunifu maarufu wa mavazi jijini Dar es Salaam Bw. Merinyo,nalo pia lilikuwa limelowa!
Aliunyanyua mkono wake na kuuweka puani na kugundua nguo yake ililowa na mkojo ni hapo ndipo kumbukumbu zilimwijia kichwani mwake kuwa alianguka kifafa!
Machozi yalianza kumbubujika, aligeuka na kutaka kumshika Richard begani, lakini mikono yake ilitupwa na Richard alianza kuteremka ngazi haraka kutoka jukwaani, ilionyesha wazi alikuwa akiondoka ukumbini kwenda nyumbani! Nyuma yake walifuata Dickson na mpenzi wake Mariam.
Waliamua kuondoka kumwacha Caroline peke yake ukumbini! Hakukubaliana na jambo hilo na kuteremka mbio jukwaani, aliwafuata hadi nje ambako kulikokuwa na kiza kinene, alipita katikati ya magari kuelekea mahali lilipoegeshwa gari la Dickson walilokuja nalo lakini kabla hajalifikia liliondoshwa kwa kasi na kumwacha peke yake.
“Richard! Richard! Richard please don’t leave me here”(Richard!Richard! Richard! Tafadhali usiniache hapa) alipiga kelele Caroline lakini gari halikusimama liliondoka kwa mwendo wa kasi, maumivu aliyoyapata Caroline moyoni mwake hayakuwa na kitu cha kulinganishwa nayo.
Hakuelewa mahali pa kwenda baada ya kutoka hapo lakini pia hakuwa na sababu ya kurudi tena ukumbini ambako watu waliendelea kuzomea wakiwaomba waandaaji wamtangaze mshindi wa pili wa mashindano hayo Mariam kuwa mshindi wa kinyang’anyiro hicho.
Muandaaji hakuwa na namna nyingine yoyote zaidi ya kukubali na Mariam akatangazwa Miss Tanzania usiku huo huo bila hata yeye mwenyewe kuwepo! Kifupi mashindano yalivurugika.
Dostları ilə paylaş: |