Mpaka wakati huo waliamini ni Reginald aliyemteka Caroline na kumpeleka porini baada ya kumbaka! Ni habari hiyo ndiyo iliyotolewa na jeshi la polisi na kutangazwa na vyombo mbalimbali vya habari . Pamoja na habari hiyo watu wengi waliomfahamu Reginald walishindwa kuziamini yaliyosemwa na kitendo cha gari la Reginald kukutwa eneo la tukio kilizidisha hali ya wasiwasi kamakweli Reginald alifanya unyama huo lakini hapakuwa na njia ya kumsaidia kwani siku zote mbambwa na ngozi ndiye mwizi! Wengi walisubiri Reginald na Caroline wazinduke wao ndio wangeeleza ukweli.
Mamia ya watu walifurika nje ya lango la kuingilia katika hospitali ya jeshi wakitaka kuhakikisha habari za Caroline kama zilikuwa kweli, watu mbalimbali waliomfahamu Reginald na walimwona kabla ya habari ya tukio hilo walilia na kulalamika wakida Reginald alionewa lakini hilo halikuubadilisha ukweli, Reginald alibaki amelala kitandani akiwa amefungwa pingu pembeni mwa kitanda chake alihesabika jambazi na muuaji.
“Tumekuita dada!” Profesa John Kadiri aliyaanzisha maongezi baada ya muuguzi waliyekuwa wakimsubiri kuwasili.
“Ndiyo nawasikilizeni!”
“Umefanya kazi ya uuguzi kwa miaka mingapi mama?”
“Mimi?”
“Ndiyo!”
“Huu ni mwaka wa kumi na moja!”
“Una nyumba?”
“Hapana!”
“Umeolewa?”
“Hapana!”
“Mshahara wako ni shilingi ngapi?”
“Elfu arobaini na tano!”
“Aisee! Hebu nieleze vizuri kuhusu maisha yako!”
Nesi alishtuka kidogo lakini baada ya profesa John Kadiri na shangazi kujitambulisha ni ndugu wa mgonjwa Reginald aliwaamini na kuwaeleza kila kitu katika maisha yake kuwa alizaliwa familia masikini na ni kwa mshahara mdogo alioupata katika hospitali ya jeshi aliwatunza wazazi wake.
“Sasa sisi tunazo pesa nyingi tunazotaka kukupa lakini utusaidie kukamilisha kazi moja tu wodini kwako!”
“Kazi gani?”
“Utusadiie kumchoma mgonwja wetu dawa hii katika mshipa ili apate nafuu upesi sawa?” alisema profesa John Kadiri akimwonyesha muuguzi kichupa kidogo cha dawa alichokuwa nacho mkononi.
“Ni dawa gani hiyo?”
“Inaitwa Kristapeni!”
“Hebu niione!” Aliomba kichupa kidogo alichokuwa nacho Profesa John Kadiri mkononi, alipopewa alikiangalia kwa kama dakika moja nzima bila kujibu kitu! Taa zilizokuwepo zilimsaidia kuyaona maandishi ya Benzathin cyrstalline penicilline yaliyoandikwa kwenye kichupa hicho yakimaanisha ilikuwa dawa aina ya Kristapeni!
“Mh! Crystapen gani hii nyekundu?”
“Huo ndio muundo wake nilinunua Japan!”
“Sawa nitawasaidia kumchoma lakini kesho sababu naanza zamu ya usiku lakini mtanipa shilingi ngapi?”
“ Tutakupa shilingi milioni mbili!”
“Milioni mbili kwa kazi hii ya kumchoma mgonjwa sindano tu? Aliuliza muuguzi huyo mama wa watoto watatu kwa mshangao mkubwa alichotegemea yeye ilikuwa ni shilingi elfu tano.
Mpaka wakati huo alikuwa bado hajawalipia watoto wake watatu ada za shule na alikuwa katika hatihati ya kufukuzwa katika chumba alichoishi sababu kodi yake kufikia mwisho! Hivyo jambo lililokuwa likielezwa hapo lilikuwa neema kubwa sana kwake wala hakutaka kujiuliza mara mbili ndiyo akubali kufanya alichoambiwa!
“Kama ni hii dawa ya Crystapen tu nitamchoma sasa hayo malipo itakuwaje?”
“Tutakupa hapahapa milioni moja halafu ukiikamilisha hiyo kazi tutakupatia akiba yako, sawa?”
“Sawa nipeni basi mie niondoke!”
Shangazi alifungua mkoba wake na kuchukua burungutu la shilingi milioni moja na kumkabidhi nesi huyo na alizipokea huku akitetemeka mwili wake macho yake hayakuamini kilichotokea, ilikuwa ni mara ya kwanza katika maisha yake kukutana na kiasi kikubwa namna hiyo cha pesa!
Baada ya kuzipokea pesa hizo nesi alikinusa kichupa na kukuta kikinukia manukato mazuri na aligeuza macho yake kumwangalia shangazi usoni.
“Usishangae ni manukato katika mikono yangu hayo!”
“Sawa nilikuwa najiuliza ni Kristapeni gani inayonukia hivi?”
Waliagana na wote kuondoka kurejea makwao walipofika nyumbani Profesa John Kadiri na shangazi hawakumweleza Dk. Cynthia juu ya kilichotokea hotelini walimkuta ndani akiendelea kuwaza juu ya mtoto wake ambaye hata siku hiyo pia hakurejewa na fahamu zake kiasi cha kuanza kuhisi aliumia ubongo wake.
“Jamani mlikuwa wapi?” Dk. Cynthia aliuliza.
“Tulikwenda kuonana na mkuu wa polisi ili jambazi apelekwe mahakamani baada tu ya kurejewa na fahamu zake!”
“Sawa mimi nimefikiri sana juu ya Caroline kutopatwa na fahamu zake leo, hii si kawaida kabisa na nimepanga kumtafuta Dk. Lukonge ili nimshauri ampige picha ya CT Scan kuona kama ubongo wake haukuumia au nyie mnaonaje?”
‘Ni sawa utakachosema wewe ni sawa kwani ni mtaalam unaelewa!”
Walikubaliana juu ya jambo hilo hawakudiriki kumweleza juu ya mpango wa mauaji waliokuwa wamepanga kwani walikuwa na uhakika angeupinga!
****************
Dawa waliyompa muuguzi haikuwa Crystapen kama walivyomweleza!! Bali dawa ya thiodan iliyojazwa ndani ya kichupa cha Kristapen! Profesa Kadiri alikuwa amedhamiria kumuua Reginald akiamini ni yeye ndiye alimteka, kumbaka na hatimaye kujaribu kumuua mtoto wake mpendwa Caroline!
Asubuhi kulipokucha alichofanya muuguzi ni kwenda shuleni kwa watoto wake na kulipia ada zote kisha akaondoka kwenda nyumbani kwa mama mwenye nyumba na kulipa kodi ya mwaka mzima hata mama mwenye nyumba siku hiyo alishangaa.
“Mama Edina leo umepata wapi pesa?”
“Mambo ya bingo hayo mama!”Alisema kwa utani.
Saa mbili kamili ya usiku alikuwa tayari kazini kwake na wauguzi waliokuwa wakimaliza zamu ya jioni walimpitishwa wadini kumkabidhi ripoti ya wodi nzima, walipofika katika kitanda cha Reginald walisimama kidogo
“Huyu mgonjwa anaendelea vizuri fahamu zake tayari zimerejea, huyu hapa ni askari anamlinda si unajua matatizo yake?”
“Ndiyo!”
“Ila ana sindano nyingine ya Pethedine saa tatu alilalamika maumivu na daktari akamwandikia sindano mbili moja tumeshamchoma bado hiyo ya saa tatu!”
“Sawa!” Aliitikia mama Edina huku moyo wake ukifurahia, aliuona muda wa kuichoma sindano hiyo ndiyo wa kuikamilisha kazi yake.
“Ha! Mwenzetu mbona leo meno yote thelathini na mbili nje?” Aliuliza mmoja wa waugui baada ya kushangazwa na furaha ya mama Edina usoni!
********************
Gari lilikuwa likikimbia kwa kasi ya ajabu kuelekea katika mpaka wa Namanga, ilikuwa gari aina ya Peugeot yenye abiria saba ndani yake na miongoni mwa abiria hao alikuwemo Dickson, moyo wake ulikuwa ukipiga kwa kasi ya ajabu, alihofia kukamatwa wakati wowote, alikuwa akisafiri kuelekea Kenya ambako alitegemea kuunganisha kwa ndege kwenda Uingereza kuikimbia kesi iliyokuwa nyuma yake, alikuwa na uhakika lazima Caroline angekufa kwa jinsi alivyomgonga kwa nguvu na gari lake.
“Atakuwa amekufa na hii itakuwa kesi ya mauaji!” Aliwaza Dickson na hakuwa na jambo jingine la kufanya zaidi ya kutoroka! Hakuwa na uhakika wa kuvuka mpaka kwani alijua taarifa na hata picha zake tayari zilikuwa mpakani! Kabla ya kufika mpakani alishuka na kupita njia za vichochorini hadi upande wa Kenya ambako alipanda magari mengi ya kwenda Nairobi. Moyo wake ukatulia.
*******************
Saa mbili na dakika hamsini na tano hivi zikiwa zimesalia kama dakika tano tu kufikia saa tatu kamili muuguzi alinyanyuka kitini na kuchukua dawa tayari kwa kwenda kumchoma Reginald sindano, badala ya kuchukua chupa ya Pethedine dawa ya maumivu aliyokuwa ameandikiwa, alichukua kichupa cha dawa aliyopewa na kuanza kutembea nacho kwenda kitandani ambako alimkuta askari amelala fofofo! Reginald alikuwa macho lakini katika maumivu makali sana!
“Pole sana!”
“Ahsante naomba basi unichome ile sindano ya saa zile! Iliondoa kabisa maumivu yangu!” Alisema Reginald akiomba achomwe sindano ya Pethedine!
“Ndiyo nimekuja kukuchoma hebu geukia ukutani!” Aliamuru nesi hakutaka Reginald aione chupa ya dawa aliyokuwa nayo!
“ Kwani unanichoma matakoni mbona wenzako walinichoma kwenye mshipa?” Aliuliza Reginald.
“We geuka tu!”Nesi alisema huku akitetemeka.
Je nini kitatokea? Reginald atakufa? Nini kitampata Caroline? Fuatilia wiki ijayo.
M
uuguzi aliendelea
kusimama na bomba
lake la sindano mkononi, Reginald naye aliendelea kumwangalia kwa mshangao, aliushangaa utaratibu uliotaka kutumika kumchoma sindano, alijua kama angechomwa kwenye msuli ingechelewa kufanya kazi! Alitaka achomwe kwenye mshipa kama walivyofanya wauguzi wengine ili maumivu yake yapungue upesi. Fahamu zake zilirejea kwa kasi ya ajabu kuliko ilivyotegemewa, maumivu aliyoyapata baada ya kukatwa mguu wake uliomiminiwa risasi ndiyo yaliyomsumbua zaidi.
“Sista mbona wenzako walinichoma kwenye mshipa lakini?”
“Usinifundishe kazi, dawa hii inaweza hata kuchomwa matakoni tafadhali geuka upesi mimi nifanye kazi yangu!”
Reginald alipomwangalia muuguzi mkononi alishangaa kumwona akitetemeka kama mtu mwenye wasiwasi mwingine, alishindwa kuelewa ni kwanini muuguzi alikuwa na hali hiyo na alihisi pengine hakuwa muuguzi mzoefu ambaye angeweza kumsababishia ulemavu!
“Tafadhali geuka nikuchome sindano!”
“No! No! No! Huwezi kunichoma matakoni ni vyema unichome kama walivyonichoma wenzako!”
“Wewe unanifundisha kazi siyo?”
“Siyo hivyo sista lakini sitaki kuchomwa sindano matakoni nasema sitaki!” Reginald alisema kwa sauti ya juu.
Askari alisikia kelele hizo na kuzinduka usingizini kwa hofu kubwa ambayo muuguzi alikuwa moyoni kuamka kwa askari kulimshtua muuguzi sana kwa haraka aliichukua sindano yake na kuondoka nayo kurudi ofisini kwake, mzozo na Reginald alijua ungeweza kumletea matatizo makubwa na hata kusababisha siri yake igundulike.
Alipofika wodini alilitupa bomba la sindano katika ndoo ya uchafu na kuchukua dawa halisi ya Pethedine aliyotakiwa kumchoma nayo Reginald na kwenda hadi kitandani ambako aliichoma katika mshipa kama ilivyokuwa imeagizwa, Reginald alifurahi na hakuchukua muda mrefu akalala usingizi.
*********************
Huku akitetemekea mwili mzima aliketi kitini akijaribu kufikiria angemjibu nini Profesa Kadiri amba ye tayari alishapokea pesa yake ili akamlishie kazi ya kumdunga sindano Reginald.
“Kwani watajuaje kama sikumchoma?”Aliwaza muuguzi
Baadaye wazo jingine lilimwijia kichwani na kujikuta akitaka kujua, kama kweli dawa aliyopewa na profesa Kadiri ilikuwa Kristapeni! Kichupa cha dawa hiyo kilikuwa bado kipo mezani kwake, alikichukua na kukifungua kisha akaminina dawa iliyokuwa imebaki ndani yake kwenye kiganja mkononi mwake.
“Naifahamu ladha ya Kristapeni hebu ngoja niionje!”Alisema na baadaye kulamba dawa hiyo kwa ulimi wake! Alishangazwa na harufu hiyo na baadaye kugundua ilikuwa ni harufu aliyoifahamu kabisa.
“Mh! Hii ni harufu ya nini mbona kama naifahamu?” Aliwaza muuguzi huyo lakini dakika kumi baadaye wakati bado anawaza juu ya jambo hilo alishtuka macho yake yalipoanza kupatwa na kizunguzungu, ni hapo ndipo alipogundua alikuwa amelamba sumu na kufahamu ilikuwa ni sumu ya thiodani!
Alinyanyuka na kutembea hadi kwenye karo la maji na kuanza kunywa maji kutoka kwenye bomba kisha akakiingiza kidole chake hadi kooni, haikuchukua muda akaanza kutapika, pamoja na hayo yote bado kizunguzungu kilizidi kuongezeka.
Ghafla alianguka chini na kuzirai, askari aliyekuwa akimlinda Reginald alimwona muuguzi akianguka na kunyanyuka kukimbia ofisini, alimkuta chini akitoa povu bila kuchelewa alipiga kelele kuomba msaada kutoka kwa wagonjwa, badala ya wagonjwa peke yao kuja hata wauguzi wa wodi nyingine walifika na kumkuta tayari muuguzi huyo ameshafariki dunia!
Kifo cha muuguzi huyo kilizua kitendawili lakini uchunguzi ulipofanyika iligundulika alikunywa sumu aina ya thiodani na kichupa chenye dawa hiyo kilikutwa wodini. Watu wote waliamini muuguzi huyo alijiua lakini sababu ya kufanya hivyo haikujulikana.
Profesa Kadiri aliposikia jambo hilo alishangaa ni kwanini alikufa muuguzi badala ya Reginald! Alikwenda kitandani kwa Reginald kumsalimia na kujifanya hafahamu kitu chochote, mdomoni alicheka lakini ndani ya moyo wake alijawa na hasira, bado alitaka Reginald afe kwa unyama alioamini alimfanyia mtoto wake.
******************
Kila siku Reginald alilia akiomba Mungu awafunulie watu ni kiasi gani hakuwa na hatia, mtu pekee wa kumuokoa katika kesi iliyokuwa ikimkabili ambayo ingepelekea hata anyongwe alikuwa ni Caroline! Ni yeye peke yake aliyeelewa kilichotokea na ni yeye peke yake aliyekuwa na uwezo wa kumtoa Reginald hatiani!
Taarifa alizozipata kutoka wodini kwa Caroline zilieleza kuwa hali yake iliendelea kuwa mbaya siku hadi siku na matumaini ya kupona yalikuwa kidogo, hiyo ilimfanya apoteze kabisa matumaini ya kutoka gerezani alijua mwisho wake ulikuwa kunyongwa.
Kwa mbili mfululizo tangu aingie hospitali hali ya Caroline ilikuwa mbaya hakuwa na fahamu kabisa! Lakini Reginald alipata nafuu na kupelekwa moja kwa moja mahakamani ambako alisomewa mashtaka la kubaka na kujaribu kuua! Alikana mashtaka yote na kupelekwa moja kwa moja mahabusu katika gereza la Segerea, kila siku alilia na alijiona mwenye bahati mbaya aliyeponzwa na usamaria wake!
“Ningejua hata nisingejaribu kumwokoa huyo msichana! Maisha yangu yameharibika sababu yake!”Aliwaza Reginald kila siku lakini alishindwa kumlaumu Caroline moja kwa moja.
Hali yake ilipozidi kuwa mbaya Iligundulika baadaye kumbe gari lilimgonga kichwani na kukipasua kwa ndani na kuharibu sehemu upande mmoja wa ubongo wake, majibu hayo yalipopatikana ililazimu arudishwe tena chumba cha upasuaji ambako alifanyiwa operesheni kuondoa damu iliyoganda na kuungandamiza ubongo wake! Profesa Kadiri na mkewe walizidi kupoteza matumaini yao juu ya mtoto wao kila siku kwao ilikuwa ni kilio tupu.
“There was a brain damage on one of the her brain hemespheres involving the medulla oblongata, even the hearing and speech centres are damaged!(Upande mmoja wa ubongo umeharibiwa vibaya pamoja na medulla oblongata hata vituo vinavyohusika na kuongea na kusikia pia vimeharibika) alisema Dk. Slyvester Lukonge baada ya operesheni alipoongea na Dk. Cynthia na profesa Kadiri juu ya hali ya mtoto wao!
“So Caroline wont hear or speak for life?(Kwa hiyo Caroline hataweza kusikia wala kuongea milele?) Profesa Kadiri aliuliza.
“I’m afraid that is what is going to happen!(Nina wasiwasi hicho ndicho kitakachotokea)
“Oh my God!”(Oh mungu wangu) alipiga kelele Dk Cynthia huku akilia, roho ilimuuma sana alipomfikiria mtoto wake pekee akiwa kiziwi na kipofu! Alishindwa kuelewa ni kitu gani kingefanyika kumsaidia Caroline, alikuwa daktari lakini alikosa kitu cha kufanya.
“Kweli atapona mtoto wangu?” Profesa Kadiri alimuuliza daktari.
“Kupona atapona ila wasiwasi wangu mimi ni kuongea na kusikia na ninafikiri itachukua muda mrefu kidogo kurejewa na fahamu!”
“Sure?(Kweli?)
“She is gonna be in a comatous state for a longtime!”(Atakuwa bila fahamu kwa kipindi kirefu)
****************
Maneno ya Dk. yalikuwa kweli tupu kwani Caroline alikaa hospitali kwa muda wa miaka miwili bila fahamu, kitu pekee alichofanya akiwa kitandani ni kila kati ya tarehe 26-28 kupatwa na kifafa na hiyo ndiyo iliyofanya hali yake izidi kuwa mbaya zaidi.
Katika miaka yote hiyo miwili Reginald aliendelea kusota mahabusu, maisha yake yote yalishaharibika mipango yake yote maishani ilishavurugika,kila kitu chake kilishahamia gerezani Segerea! Taarifa kuwa Caroline kuwa katika hali kutojitambua ilimsikisha sana na ilimkatisha tamaa kwani yeye ndiye mtu aliyemtegemea kueleza ukweli bila Caroline alijua angehukumiwa kunyongwa kwa mauaji ambayo hakuyafanya,jambo hilo lilimuumiza sana moyo wake ukizingatia.
Kila baada ya mwezi mmoja Reginald alifikishwa mahakamani kwa kesi ya kubaka na kujaribu kufanya mauaji, pamoja na kukanusha bado kesi ilionekana kumuelemea na wengi walihisi angehukumiwa, kwa kesi ya kubaka na hukumu yake ilikuwa ni kufungwa maisha!
Ndugu zake wote walishakata tamaa kabisa ingawa walikuwa na uhakika mtoto wao hakutenda kosa hilo hawakuwa na njia ya kumsaidia, walishafanya mpango yote ili wamtoe gerezani lakini ilishindikikana, nyundo aliyoshindilia profesa Kadiri ilikuwa nzima! Yeye alitaka Reginald anyongwe au kufungwa maisha ndio roho yake ingefurahi.
**************
“Mama ni heri uniruhusu nijiue kuliko kuhukumiwa kifungo cha maisha au kunyongwa kwa kosa ambalo kwa hakika sikulifanya! Sikumfanyia kitendo chochote kibaya Caroline mama, nilikuwa nikimuokoa kutoka kwa kijana aliyetaka kumuua kwa kumgonga na gari!” Reginald alimwambia mama yake siku moja alipomtembelea gerezani.
“Hapana mwanangu usiseme maneno hayo!”
“Siyo hivyo mama siwezi kunyongwa bila kosa naomba mkiniletea chakula kesho niwekeeni kichupa cha dawa ya kunguni katikati ya ugali ili nife!Nataka kufa mama nimeteseka kwa muda mrefu sana!”
“Siwezi kufanya hivyo mwanangu kama Mungu anachukua maisha yako acha ayachukue lakini hata siku moja siwezi kukuua ni mimi niliyekuzaa!”
Reginald alikuwa mtoto pekee wa bibi Magreth Lyimo, mwalimu wa shule ya msingi mstaafu! Alikuwa ndiye mtoto wake wa kwanza na ndiye alikuwa tegemeo lake! Mume wake alifariki miaka mingi kabla na kumwachia watoto watatu, Reginald aliyekuwa mtoto wa kwanza wakati huo akiwa darasa la saba, Judith na mdogo wao wa mwisho Neria.
Mama yake alimsomesha Reginald kwa pesa za mshahara wa ualimu na biashara ndogondogo hadi akamaliza chuo kikuu! Watoto wake wengine, Judith na Neria walipata mimba kabla ya kuolewa na kuzaa nyumbani, waliishi na watoto wao nyumbani na hawakuwa na kazi.
Hivyo tegemeo pekee la mama huyo lilikuwa ni Reginald! Kutiwa kwake mahabusu kulimfanya mama huyo akonde kwa mawazo, maisha yake yalibadilika na kuwa mabaya kupita kiasi, alianza hata kulala na njaa jambo alilolisahau kwa muda mrefu.
Alilazimika kuuza nyumba zote za Reginald ili kuigharimia kesi, lakini bado hazikutosha, akatumia pesa zote zilizokuwa katika benki nazo zikamalizika bila kesi kwisha ikabidi auze na nyumba ambayo Reginald alimnunulia na kwenda kupanga katika chumba kimoja eneo la Buguruni na binti zake. Alimpenda mno Reginald alikuwa tayari kufanya lolote kumsaidia na siku zote aliamini mtoto wake hakufanya ukatili huo!
“Reginald! Hawezi kuua, hii ni njama!” Hayo ndiyo yalikuwa maneno yake kila siku.
****************
Kilikuwa ni kikao kingine kati ya madaktari, profesa John Kadiri na mkewe Dk. Cynthia. Madaktari wakijaribu kuwaelewesha wazazi ni kwanini mtoto wao alikuwa amepoteza fahamu kwa muda wote huo!
“Your daughter brain is damaged severely on top of that there is a wave of electric impulses being discharged from the traumatized brain and make muscles contract between 26th up to 28th of every month, up this moment we dont know why is this happening! It makes her condition worse, we have used a lot of anticonvulsives but still no improvement!”(Ubongo wa binti yenu umeharibiwa vibaya sana na zaidi ya hayo kuna wimbi la umeme mwingine unatolewa katika ubongo ulioharibiwa kila tarehe 26-28 ya kila mwezi na kufanya misuli kukakamaa, tumeshindwa kuelewa hii ni kwanini? Tumempatia dawa za kuzuia degedege lakini hazisaidia!) daktari alisema huku akimwangalia Dk. Cynthia usoni.
“Is your daughter Epileptic?”(Mtoto wako ana kifafa?)
“Yes she is!”(Ndiyo!)
“Oh my God! Why didn’t you give us that history from the beginning?”(Oh Mungu wangu kwanini haukutupa historia hiyo kutoka mwanzo?)
“We are sorry!”(Tusameheni sana!)
“Kwa hiyo ni lazima tubadilishe dawa?”
“Itakuwa vizuri sana!”
“Tutamweka kwenye Amylobarbitone,pamoja na Niazepam nafikiri zitamsaidia!
“Fanya lolote daktari maisha ya mtoto wetu yapo mikononi mwako!”
Caroline alianzishiwa dawa hizo na alipozitumia kwa siku mbili tu hali yake ilianza kubadilika na kuwa nzuri, wiki mbili baadye alizinduka kutoka katika hali ya kupoteza fahamu, kila mtu alifurahi lakini hakuwa na uwezo wa kusema chochote, alikuwa ni kama bubu na hakuwa na kumbukumbu yoyote juu ya maisha yake ya nyuma wala hakuelewa kuwa alilala kitandani hapo kwa miaka miwili na miezi mitatu!
“Hii hali niliitegemea kabisa!” Daktari alisema.
“ Kwa hiyo hataongea tena?”
“Hapana inawezekana akaongea baadaye lakini mpaka afundishwe kuongea, hivi sasa huyu ni kama mtoto itabidi afundishwe kufanya kila kitu, ubongo wake umefuta kumbukumbu zake zote!”Alisema daktari lakini kwa profesa Kadiri na Cynthia ilikuwa furaha kubwa kuona mtoto wao akiwa hai tena, hawakujali alikuwa bubu, kipofu wala kiziwi walichotaka ni Caroline tu.
Taarifa za kuzinduka kwa Caroline usingizini zilimfikia Reginald mahabusu, alifurahi kupita kiasi kwani alijua ni yeye pekee ndiye angeweza kumtoa gerezani sheria ya Tanzania haikuwa na uwezo wa kumtendea haki kwani haikuwa na uwezo wa kupeleleza kesi hiyo na kuugundua ukweli.
Furaha yake ilipotea alipoambiwa kuwa pamoja na kuwa kuzinduka Caroline hakuwa na uwezo wa kuongea neno lolote na hakuwa na kumbukumbu yoyote juu ya maisha ya nyuma! Ubongo wake uliumia sana na kupoteza kumbukumbu zake zote.
Ilikuwa imebaki miezi miwili tu hukumu yake ya kesi ya kubaka itolewe na ilionekana wazi angefungwa maisha sababu ushahidi wa cheti cha daktari uliokuwepo ulionyesha kweli Caroline alibakwa, ingawa cheti hakikuonyesha mbegu zilikuwa za nani.
“Watanzania wengi sana wamefungwa kwa makosa ya kubaka bila hatia! Ee Mungu wangu mpe Caroline kumbukumbu zake ili aniokoe katika janga hili!” Alisema Reginald katika maombi yake kwa Mungu aliyoyafanya usiku kucha!
Miezi miwili baadaye:
“Kesi ya kubaka namba 204 ya mwaka huu mshtakiwa ni Reginald Lyimo tafadhali simama!”
Ilikuwa ni sauti ya hakimu iliyosikiwa na mamia ya watu waliofurika ndani na nje ya mahakama kusikiliza hukumu ya Reginald kila mtu alijua Reginald angehukumiwa kifungo cha maisha kwa kesi hiyo, Reginald alisimama kizimbani akiwa na pingu mikononi.
Baada ya Hakimu kusema maneno hayo aliendelea kusoma maelezo ya kesi hiyo tangu ianze, Reginald alisimama kizimbani akilia machozi, alipowaangalia mama na dada zake nao pia walikuwa wakilia machozi ya uchungu, Reginald aliomba Mungu mambo yawe ndoto.
“Una la kujitetea kabla sijakuhukumu?”
“Ndiyo Hakimu!”
“Haya jitetee!”
“Unayemwona hapo pembeni akilia ni mama yangu na wale wawili ni dada zangu nihurumie Hakimu kwani wote wananitegemea mimi isitoshe mimi sikumbaka Caroline, nilikuwa nikimuokoa kutoka kwa mtu aliyetaka kumuua kwa kumgonga kwa gari ila ni vigumu kuthibitisha kama Caroline mwenyewe angekuwepo hapa angesema ukweli!”
Hakimu alikuwa akimwangalia Reginald kwa jicho la hasira, alimwona muuaji na mbakaji na wala hakuyatilia maanani maneno yake.
“Nooooooo! Mheshimiwa Hakimu hapanaaa! Haiwezekani!” Ilikuwa ni sauti ya msichana ikiongea kutoka kwenye lango la kuingilia mahakamani, msichana mmoja alikuwa akiingia mahakamani akiwa ameshikwa na watu wawili! Watu wote mahakamani waligeuka kumwangalia msichana huyo, alikuwa na bendeji nyingi usoni na alitembea kwa magongo.
Je nini kitaendelea? Nani kaingia mahakamani? Je, Reginald alinusuruka na adhabu ya kifungo cha maisha? Fuatilia wiki ijayo !
Sehemu ya 9
No!No!No! Haiwezekani mheshimiwa jaji huo utakuwa uonevu na ni heri fahamu zimenirudia mngeua mtu asiye na hatia!”Alisema msichana huyo akizidi kutembea kwenda katikati ya ukumbi wa Mahakama!
Watu wote waligeuka kuangalia nyuma alikokuwa akitokea, kwa mbali wengi hawakumfahamu na hata Reginald mwenyewe hakumtambua mara moja kuwa msichana huyo alikuwa Caroline.
Alimpomfikia Reginald, Caroline alimwita kwa jina na Reginald alipoangalia kwa makini macho yake yalitua moja kwa moja usoni kwa msichana huyo na ingawa uso wake ulikuwa umefungwa na bendeji nyingi aliweza kumtambua.
“Oh! Caroline ni wewe?”Aliuliza Reginald bila kuyaamini macho yake.
“Ni mimi Reginald nimekuja kukusaidia baada ya kusikia mateso yako nimekuja kusema ukweli sababu najua wanataka kukuua kwa kosa ambalo hukulifanya! Caroline alisema kwa sauti, baba yake aliyekuwepo mahakamani alishangazwa sana na hali hiyo, alishindwa kuelewa, Caroline alitoka vipi hospitali ingawa alikuwa na uhakika fahamu zilishamrejea.
Dostları ilə paylaş: |