***********
Gari lilikuwa likizidi kwenda kwa kasi, Kennedy akiwa kwenye usukani na bastola za O’brien na Nicky zilikuwa bado zimemlenga Caroline shingoni huku akiamriwa kutulia, kila kitu kilichotokea ndani ya gari kwake kilionekana ni kama ndoto ambayo baada ya muda mfupi angetoka ndani yake. Hakuwa tayari kuamini kuwa alikuwa ametekwa, kwa mara nyingine tena aliulaumu moyo wake kwa kumuamini Kennedy.
“Kennedy nimekosa nini na mnanipeleka wapi?”
“Kwa mumeo!”
“Mama yangu weeee!Kweli mnanipeleka kwa Dk. Ian? Hivi mnajua atakachonifanya? Ataniua tena kwa kifo kibaya sana!”
“Sisi hiyo hatujali hata kidogo, kitu tunachoangalia ni maslahi! Maisha yako hivi sasa ni mali kubwa, kitendo cha sisi kukufikisha kwa mumeo ni kwaheri umasikini!” Alisema Kennedy lakini maongezi yote yalifanyika katika lugha ya Kiingereza.
“Jamani msinipeleke, nihurumieni! Ni heri mniue nyinyi lakini si kunifikisha kwa Dk. Ian!”
“Si ni mumeo lakini?”
“Alikuwa mume wangu na kwa niliyomfanyia nina uhakika ataniua vibaya mno!” Caroline alizidi kujieleza lakini hakuna aliyeonekana kumjali, bastola zilizidi kumlenga na mbele kama kilometa ishirini gari lilipunguza mwendo na kuegesha pembeni.
“Nicky hebu maliza hiyo kazi, muda wa ndege umekaribia!” Kennedy alimgeukia Nicky na kumwambia baada ya gari kusimama huku akimkabidhi kiboksi kidogo alichokuwa nacho mkononi.
“Sawa bosi!”
Kitendo bila kuchelewa Nicky alikifungua hicho na kutoa bomba la sindano pamoja na kichupa kingine kidogo, Caroline alishuhudia kila kitu kilichoendelea huku akitetemeka na alipoangalia vizuri juu ya kichupa ambacho Nicky alikuwa akinyonya majimaji yaliyokuwa ndani yake kwa sindano, aliyaona maandishi yaliyoandikwa Pethedine! Aliijua dawa hiyo, miaka ya nyuma aliwahi kuumia mguu na daktari aliitumia kumchoma ili alale usingizi.
Alielewa walichotaka kufanya, walitaka kumchoma dawa ya usingizi ili alale na wamsafirishe kwa urahisi, alianza kupiga kelele akiomba wasimchome dawa hiyo lakini baadaye alipofikiria vizuri aliamua kutulia na kuruhusu wamchome, hata akina Kennedy walishangazwa na utulivu huo na kuangaliana machoni.
“Ok! Get the stuff into my vein immediately!”(Nichomeni hiyo dawa kwenye mshipa haraka!) Alisema Caroline, alitaka achomwe dawa na alale ili kama atafikishwa kwa Dk. Ian na kuuawa basi afe akiwa usingizini, hakuwa tayari kukutana na Dk. Ian macho kwa macho.
Dawa hiyo ilichomwa kwenye mshipa na mchomaji akiwa Nicky, muda mfupi kabla hajalala alipata nafasi ya kuyafikiria mambo yaliyotokea maisha mwake, alijiona ni mwenye mkosi lakini mara nyingi alijitupia lawama mwenyewe kwa kutochukua maamuzi yaliyo sahihi! Alipowafikiria baba na mama yake roho ilimuuma zaidi, alitamani kuwa nao tena wao walikuwa wazazi wake wasingemtupa hata kama angekuwa na matatizo makubwa kiasi gani.
“Nakufa bila kuwaona baba na mama yang.....!” Kabla hajaikamilisha sentensi hiyo usingizi mzito ulimpitia, hakujua kitu chochote kilichoendelea baada ya hapo.
Kennedy na wenzake walisubiri kwa muda wa dakika ishirini ili alale vizuri ndipo wakaligeuza gari lao na kuanza kuliendesha kwa kasi kurudi mjini Penh ambako walichukua barabara ya Hilbag iliyoelekea uwanja wa ndege wa jiji hilo uliokuwa umbali wa kama kilometa ishirini kutoka mjini. Walitumia kama dakika tano tu kufika uwanjani ambako waliliegesha gari lao katika sehemu maalumu ya maegesho.
Kabla hawajashuka kwenye gari Kennedy alifungua droo iliyokuwa kushoto kwake na kutoa tiketi zao zote pamoja na cheti kilichoonyesha kuwa Caroline alikuwa mwanafunzi mgonjwa aliyekuwa akisafirishwa kutoka Vietnam kwenda Ottawa nchini Canada ambako familia yake iliishi, ulikuwa ni uongo waliopanga ili kufanikisha mpango wao wa kumfikisha Caroline mikononi mwa Dk. Ian.
“Psiiiiiiiiiii!” Kennedy alimwita mfanyakazi mmoja wa uwanja wa ndege aliyekwenda mbio mpaka mahali alipokuwa amesimama.
“ Nikusaidie nini mzee?”
“Tunahitaji machela, tuna mgonjwa ambaye tunasafiri naye kwenda Canada!”
“Sawa subiri kidogo nije!” Alisema mfanyakazi huyo na kuondoka, aliporejea dakika moja baadaye alikuwa na machela waliyokuwa wakiisukuma yeye na wenzake wawili.
“Yuko wapi mgonjwa?”
“Yupo ndani ya gari!”
Vijana hao walisaidiana na O’brien pamoja na Nicky kumshusha Caroline kwenye gari na kumweka juu ya machela! Alikuwa hoi hajitambui bila kuelewa chochote kilichoendelea, alilala usingizi mzito mno ambao haukumpa hata nafasi ya kuota ndoto moja. Baada ya kuteremshwa alipakiwa kwenye machela na walipoangalia saa zao waligundua zilikuwa zimesalia dakika thelathini tu ndege iruke, kifupi walikuwa wamechelewa hivyo zilihitajika juhudi za ziada ili kuwahi ndege.
“Mgonjwa wenu ana matatizo gani?”
“Alianguka ghafla juzi kama kinavyoonyesha hicho cheti madaktari wanasema amepatwa na Kiharusi!” Kennedy alidanganya lakini haikuwa rahisi kugundua sababu cheti kilionyesha hivyo.
“Poleni sana!”
“Ahsante!”
Hawakupata usumbufu wowote ndani ya uwanja na hivyo kufanikiwa kuiwahi ndege, kila mahali walikopita watu waliwapa pole kwa mgonjwa waliyekuwa naye, waligongesha mikono mara kwa mara kujipongeza kwa jinsi kazi hiyo ilivyokuwa rahisi! Hawakuwa na kitu kingine walichokiwaza kichwani mwao zaidi ya pesa, kwa hakika waliamini tayari umasikini walikuwa wamepishana nao njia.
Ndani ya ndege Caroline aliwekwa kwenye kiti cha katikati ambacho kililazwa kabisa na kuwa kama kitanda, pembeni yake mkono wa kushoto alikaa O’brien kulia alikaa Kennedy na Nicky alikaa kiti cha mbele ya Caroline.
Muda mfupi baadaye ndege iliiacha ardhi ya Vietnam lakini dakika mbili tu ikiwa angani rubani na Injinia waligundua kasoro fulani katika injini, kulikuwa na mlio usio wa kawaida! Wote waliangaliana machoni wakifikiria juu ya nini cha kufanya, ghafla ndege ilianza kupunguza nguvu na taratibu ikaanza kushuka ardhini, rubani alifanikiwa kuipeleka hadi chini bila matatizo yoyote na kuigesha vizuri.
Hapakuwa na jambo jingine la kufanya zaidi ya matengenezo yaliyochukua muda wa kama masaa matatu na nusu ndipo ndege iliporuhusiwa kuruka tena, safari hiyo ilikuwa haiendi moja kwa moja Canada, ndege ilikuwa na ratiba ya kupita katika miji ya Stockholm nchini Sweden, Copenhagen nchini Denmark ndipo itue nchini Canada katika jiji la Ottawa, hiyo ilikuwa ni safari ya masaa sita kwa sababu mzunguko mrefu na mwendo wa ndege hiyo haukuwa wa kasi.
Dawa ya Pethedine aliyochomwa Caroline humpa mtu usingizi kwa masaa sita jambo ambalo Kennedy na wanzake hawakulielewa vizuri, waliamini baada ya kumchoma angelala mpaka wanatua nchini Canada, lakini kitendo cha ndege kuharibika na kutua kwa mara ya pili uwanjani kufanyiwa matengenezo kilikula sehemu ya masaa hayo. Wakiwa katika uwanja wa ndege wa Sweden, Caroline alifumbua macho yake! Alipoangaza huku na kule aligundua alikuwa ndani ya ndege, alipotupa macho yake kushoto na kulia aliwaona O’brien na Kennedy wakiwa taabani usingizini. Hakumwona Nicky tu kati yao na hakujua mahali alikokuwa.
Alipotupa macho yake dirishani aligundua ndege ilikuwa nchi kavu sababu aliona ndege nyingine pamoja na majengo, kwake huo ulikuwa wakati muafaka wa kutoroka! Mambo mawili yalimfanya ashindwe kuchukua uamuzi huo haraka. Kwanza, hakujua mahali Nicky alikokuwa si ajabu kama angenyanyuka lazima angeonekana.
Pili, hakujua walikuwa katika uwanja gani! Pengine walikuwa nchini Canada na kushuka kwake labda kungemtia mikononi mwa Dk. Ian jambo ambalo hakutaka kabisa litokee.Aliamua kutulia na muda mfupi baadaye alisikia sauti ya kike ikitangaza kuwa ndege ingeruka katika muda wa dakika tano kutoka katika uwanja wa Copenhagen kuelekea Ottawa nchini Canada.
“Ha! Kumbe tulikuwa Dernmark?” Aliwaza Caroline.
Alijua wazi uwanja wa ndege uliofuata ndiko alikokuwa akisubiriwa kwa hamu na kifo chake, alizidi kuogopa kwa hakika hakuwa tayari kuingia tena mikononi mwa Dk. Ian lakini alishindwa ni kwa njia gani angeweza kumwepuka. Kabla ndege haijaanza kusogea mbele Caroline alitupa macho yake kwenye kiti cha mbele na kumwona Nicky naye akiwa amelala fofofo, tena yeye hadi udelele ulimdondoka mdomoni!
“Mungu wangu hii ndiyo nafasi pekee ya kuokoa maisha yangu!” Aliwaza Caroline na bila kusita aliufungua mkanda uliomfunga kwenye kiti, alipousikiliza vizuri mwili wake aligundua nguvu za kutosha zilikuwepo kumwezesha kurotoka, alinyanyuka taratibu na kusimama wima! Si Nicky, Kennedy wala O’brien aliyeshtukia hatua hiyo. Lakini ghafla Kennedy alijitingisha na kujigeuza, kuona hivyo Caroline alirudi kwa kasi akajitupa kwenye kiti na kuendelea kujifanya hana fahamu! Kwa jicho lake la pembeni alimshuhudia Kennedy akimwangalia kwa mshangao, alikuwa ameusikia mlio wa kiti wakati Caroline akijitupa.
Ili kuhakikisha kuwa kweli Caroline alikuwa bado yu usingizini Kennedy aliingiza mkono kwenye mfuko wa shati lake na kutoa pini yenye ncha kali, aliizamisha moja kwa moja kwenye paja lake la kulia ili kuona kama angeshtuka, macho yote mawili yakiwa yamemwangalia Caroline usoni ili kuona kama angekunja uso wake jambo ambalo lingemaanisha ni yeye aliyejitupa kitini.
*****************
Harry alimshuhudia mzee mmoja akiwaamuru jambo wanaume wenye nguvu walioingia ndani ya chumba hicho, mwanzoni alifikiri wanaamrishwa kumuua lakini alishangaa baadaye mmoja wa wazee hao alipomkabidhi kwa wanaume hao wenye nguvu ili wampeleke kwenye jengo la benki ya watu wa Sudan kuchukua pesa yake! Waliamriwa kumpa ulinzi uliotakiwa.
“Au ulitaka tukulipe kwa utaratibu gani?”
“Kwani hamuwezi kuniingizia hizo pesa kwenye akaunti yangu iliyoko katika benki ya Standard Bank ya Uingereza ambayo ina tawi katika kila nchi? Mkiniwekea katika akaunti yangu ninaweza kuzichukua pesa hizo hata nikiwa katika Jamhuri ya Sokomoni ambako nina kazi ya kufanya!” Alisema Harry.
“Hiyo ni rahisi sana, maana kutembea na pesa nyingi katika nchi isiyokuwa na amani kama hii ni hatari!”Alisema mzee mwingine na Harry akaandikiwa hundi ya jumla ya dola za Kimarekani Milioni.................
Ilikuwa furaha mno kwake na hata wakati akitembea kwenda benki alikuwa akiimba wimbo wa mafanikio moyoni mwake, hata mara moja hakumfikiria Caroline ingawa alijua kwa wakati huo alikuwa katika matatizo makubwa sana na pengine tayari alikuwa mfu.
“Tayari nimeshakuwa Rais wa Sokomoni!”
Sokomoni ilikuwa ni nchi ndogo jirani kabisa na Tanzania, ilikadiriwa kuwa na idadi ya watu wasiozidi milioni tano! Ilikuwa ni Jamhuri ya kwanza katika Afrika kuamua kuanzisha mfumo wa vyama vingi, Raia wa nchi hizo mbili walikuwa na mahusiano makubwa sana kulikuwa na watu wengi waliokuwa na ndugu pande zote mbili za nchi hizo, lilikuwa si jambo la ajabu kukuta shangazi anaishi Sokomoni na baba anaishi Tanzania.
Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Harry, alikuwa na uraia pande zote mbili kwani bibi yake mzaa mama na mama zake wengine wadogo waliishi katika Jamhuri hiyo na mara nyingi hata yeye mwenyewe alikwenda huko na kutambulika kama raia. Kwa pesa nyingi aliyopata alitaka kuutumia upenyo huo kuukwaa Urais wa Sokomoni kupitia chama chochote cha siasa kilichokuwa katika Upinzani akiwa katika umri mdogo.
Baada tu ya kukabidhiwa hundi yake alisindikizwa hadi mjini ambako aliiweka hundi hiyo katika akaunti yake na siku hiyo hiyo alipanda ndege iliyompeleka moja kwa moja hadi nchini Sokomoni ambako alikuta vuguvugu la uchaguzi limepamba moto.
Watu wa kwanza aliwafuata akitaka kujiunga na chama chao kwa lengo la kuwa Mfadhili na hatimaye kugombea walikuwa wenye chama cha CKMW au Chama cha Kutetea Maslahi ya wananchi.
Je, nini kitatokea? Harry atafanikiwa kuwa Rais? Na je ndani ya ndege nini kitampata Caroline? Na je wazazi wake atakutana nao? Fuatilia wiki ijayo.
S
indano aliyochomwa
mwilini mwake
ilimsababishia Caroline maumivu makali kupita kiasi, Kennedy alikuwa ametumia nguvu nyingi sana kuizamisha sindano hiyo pajani mwake lakini pamoja na maumivu yote hayo Caroline hakudiriki kujitingisha, aliyafahamu madhara ya kufanya hivyo!
Alibana pumzi kwa nguvu zote, hakukaza macho hata kidogo na wala hakuonyesha mshtuko wowote usoni mwake! Hata yeye mwenyewe alishindwa kuelewa ni vipi aliweza kuyahimili maumivu makali kama hayo, aliamini kweli kwa binadamu wakati wa shida hupata nguvu za ziada.
Kwa kitendo hicho Kennedy aliridhika kabisa kuwa Caroline alikuwa bado yu usingizini, hakutaka kupoteza muda zaidi aliangusha kichwa chake kwenye kiti na dakika chache baadaye alikuwa akikoroma!
“Kalala!” Aliwaza Caroline
Dakika chache tu baadaye ndege ilikuwa angani ikiitafuta nchi ya Dernmark, Caroline alikuwa bado amefumba macho yake akiendelea kujifanya hana fahamu! Hakutaka kufumbua macho mapema kwa kuogopa kugundulika, mawazo yake yote yalikuwa ni kwa jinsi gani angeweza kujiokoa kutoka mikononi mwa kifo kilichokuwa mbele yake.
Katika masaa machache yaliyokuwa mbele yake alitakiwa kuwa maiti hilo hata yeye alilifahamu na hakuwa tayari kufa kirahisi, watu pekee waliokuwa na uwezo wa kuzuia asiokoke ni waliokuwa pembeni yake na aliyekuwa amekaa kiti cha mbele yaani Kennedy, O’brien na Nicky! Hao ndio waliokuwa wakimpeleka kwa Dk. Ian ambako yeye alikufananisha na machinjioni.
“Lakini pengine Dk. Ian anaweza kunionea huruma hasa nikimwambia kuwa Harry aliniteka na kwenda kunitelekeza Vietnam!” Aliwaza Caroline lakini alishindwa kuelewa ni kwa jinsi gani angeweza kumshawishi Dk. Ian mpaka ayaamini maneno yake.
“Hiyo ni sawa na kucheza kamari! Siwezi kufanya hivyo akikataa si nitakufa? Siwezi kujipeleka mwenyewe kufuata kifo changu, ni lazima nijaribu kujiokoa kwanza ikishindikana basi!” Aliendelea kuwaza Caroline.
Ndege iliendelea kukatiza mawinguni katika anga ya Sweden ikielekea Dernmark ambako abiria walishatangaziwa kuwa ingetua katika muda wa masaa mawili yaliyokuwa mbele yao, abiria walishachoshwa na safari na walitamani kufika Canada haraka.
“Tukifika Copenhagen kama watakuwa bado wamelala nitashuka hapohapo na kuondoka zangu!” Aliwaza Caroline na alitamani sana hali hiyo itokee, kwa hakika hakutaka kabisa kukutana uso kwa uso na Dk. Ian! Aliufahamu ukatili wake na alikuwa na hakika angeuawa.
******************
Mpaka zikiwa zimesalia dakika ishirini ndege itue katika uwanja wa ndege wa Copenhagen Kennedy, O’brien na Nicky walikuwa bado wako usingizini na Caroline alikuwa akiwaangalia kupitia kwenye kona ya macho yake yote mawili! Hakutaka kufumbua macho kwa kuogopa kugundulika, alizidi kumwomba Mungu watu hao waendelee kulala ili ndege ikitua tu katika uwanja wa Copenhagen achoropoke na kutoroka.
“Ndege inakaribia kutua katika uwanja wa ndege wa Copenhagen, abiria wote tunaombwa kufunga mikanda yenu tayari kwa kutua!” Ilisikika sauti ya kike ikiongea kutoka katika spika zilizokuwa pembeni mwa viti vya abiria. Ni sauti hiyo iliyowafanya Kennedy na wenzake kuzinduka kutoka usingizini na walipoamka tu wote walimtupia macho Caroline mahali alipolala! Aliona kila kilichoendelea na alilaumu ni kwanini waliamka. Caroline alishuhudia wakifunga mikanda yao vizuri tayari kwa kutua, roho ilimuuma sana na matumaini ya kunusurika na kifo yalizidi kupungua, baada ya kufunga mikanda yao alitegemea wangesinzia tena lakini haikuwa hivyo walikuwa macho mpaka wakati ndege inatua katika uwanja wa Copenhagen ambako waliendelea kuongea mengi kuhusu malipo ya pesa nyingi iliyokuwa mbele yao kama wangefanikiwa kumfikisha Caroline mikononi mwa Dk. Ian.
“Ah! tutakuwa matajiri sasa!” Kennedy aliwaambia wenzake
“Si bado yupo usingizini lakini?” Nicky aliuliza.
“Ndiyo hawezi kuamka sasa hivi ile dawa ni kali sana!”
“Kwa kweli tumecheza mchezo mkali sana, hakuna mtu anayeweza kushtukia dili hili!”
“Hata shetani mwenyewe hawezi kuelewa!”
“Masikini msichana wa watu anakwenda kufa!” Kennedy alisema huku akimshika shavu Caroline.
“Sasa sisi tufanye nini wakati tunahitaji pesa?”
Kila kitu ambacho Kennedy na wenzake waliongea Caroline alikisikia na kuzidi kutishika zaidi, alihisi mwili kutetemeka, alikiogopa sana kifo kilichokuwa mbele yake! Alijua asingeweza kusamehewa kwani Dk. Ian aliipenda sana ndege yake. Caroline alijutia ujinga wake wa kutekwa kimapenzi kirahisi, alijilaumu kwa kushindwa kutofautisha mapenzi ya kweli na ya uongo.
“Dalili za kwamba Harry hakunipenda niliziona tangu mwanzo tukiwa Arusha, aliponikataa kwa sababu tu nilikuwa na kifafa! Sasa sijui ni kitu gani kilichonifanya nimwamini kwa mara ya pili na kumwacha mtu aliyeniponyesha ugonjwa uliofanya Harry aniache na kuyabadilisha kabisa maisha yangu! Kwa kweli sitamsamehe Harry maishani mwangu na ni lazima nimtafute kokote aliko duniani ili nimwonyeshe kuwa alichokifanya si kitu kizuri, labda nife lakini kama nikiwa hai na nikafanikiwa kufika huko Tanzania au hata Sokomoni ni lazima nimuue tena kwa mkono wangu mwenyewe na si yeye tu na wenzake wote waliochangia kuniumiza katika maisha yangu ni lazima waende kaburini” Aliendelea kuwaza Caroline.
Mpaka ndege inaondoka Copenhagen kuelekea mwisho wa safari yao nchini Canada, nchi ambayo Caroline hakutaka kabisa kufika, Kennedy na wenzake walikuwa bado hawajalala usingizi maongezi yao yalikuwa juu ya pesa tu, hakuna kitu walichotamani kama kufika Canada na kumkabidhi Caroline mikononi mwa Dk. Ian.
Dakika thelathini na tano baadaye ndege ikiwa angani Caroline kupitia katika pembe ya jicho lake la kushoto aliweza kukiona kichwa cha Kennedy kikiyumba upande mmoja hadi mwingine na muda mfupi baadaye alitulia, jambo lililoonyesha tayari alikuwa usingizini kwa mara nyingine! Kwa kutumia jicho lake la upande wa kulia alimwona O’brien naye akicheza mchezo wa aina hiyo hiyo na dakika chache baadaye naye alitulia.
Caroline alishindwa kuelewa watu hawa walikuwa ni wa aina gani waliopenda usingizi kuliko kitu kingine chochote, alitamani kuwa na uwanja mwingine wa ndege kutua kabla ya kuingia Ottawa lakini haikuwa hivyo, nchi iliyokuwa mbele yao ilikuwa ni Canada peke yake na huo ndio ungekuwa mwisho wa safari ni katika mji huo ndiko kifo chake kilikokuwa, alitamani kufanya lolote asifike kabisa katika mji huo! Ilikuwa ni afadhali aruke kupitia dirishani na aanguke ardhini na kupasuka kuliko kuingia mikononi mwa Dk. Ian.
“Nitafanya nini mimi? Nitafanya nini kujiokoa? Yaani kweli niingie mikononi mwa Dk. Ian? Haiwezekani! Ni lazima nifanye jambo” Caroline aliwaza na kujiuliza maswali mengi sana bila kupata majibu.
“Ndege ya shirika la ndege la British Airways ndiyo unayosafiri nayo kutoka Vietnam kwenda Canada! Ni shirika la uhakika na salama, kila mara unapofikiria kusafiri tumia shirika hili ni raha na salama.Ndege yetu inategemewa kutua katika uwanja wa ndege wa Ottawa katika muda wa saa moja ijayo na huo ndio utakuwa mwisho wa safari yetu, pelekeni sifa ya shirika letu popote muendako na mabaya yetu tuelezeni sisi!” Iliendelea kusema sauti ya msichana aliyekuwa akiongea na kipaza sauti, alitumia Kiingereza, Kiswidishi na Kifaransa. Safari hii Kennedy na wenzake hawakuzinduliwa na sauti hiyo, waliendelea kulala fofofo.
“Ha! Bado saa moja tu! Ee Mungu nisaidie!” Caroline alijikuta akitamka.
*************
“Chukua hii!”
“Ni nini?”
“Chukua tu itakusaidia, mimi ilishanisaidia mara nyingi sana nilipoingia katika matatizo!”
“Ni nini lakini?”
“Ni sumu ambayo ukimgusa nayo mtu kwenye ngozi yake hutumia dakika kumi kupenya katika ngozi na kwenda kwenye damu! Ambacho hufuata baada ya hapo ni mtu kukauka na kufa katika muda wa dakika ishirini! unachotakiwa kufanya ni kunawa mikono katika muda wa sekunde thelathini baada ya kuigusa kama hukufanya hivyo hata wewe mwenyewe unaweza kufa!”
Caroline aliipokea dawa hiyo iliyokuwa katika muundo wa unga mweusi na kuifunga katika kipande cha karatasi ya nailoni, alishauriwa na mzee huyo aishonee katika pindo lake la gauni hivyo ndivyo alivyofanya, alifurahi kuipata na alipanga kuitumia kukamilisha lengo lake la kuwaua watu wote waliomfanyia unyama maishani.
“Wa kwanza kumuua na sumu hii atakuwa Harry!” Aliwaza baada ya kumaliza kuishonea katika pindo la gauni lake.
Hayo yalikuwa maongezi yaliyofanyika kati ya mzee Nelson na Caroline porini, usiku kabla hawajaondoka kwa farasi kuelekea mjini Penh! Kwa sababu hakuuona umuhimu wa sumu hiyo kabla ya kufika Tanzania au Sokomoni, Caroline alijikuta amesahau kama alikuwa nayo. Lakini akiwa katika mawazo mengi ya namna gani angeweza kujiokoa ikiwa ni dakika kama arobaini na tano kabla ya ndege kutua katika uwanja wa Ottawa, aliikumbuka sumu hiyo.
Akiwa Penh kwenye mgahawa wa bibi Suzanne alinunua gauni jingine akawa na magauni mawili aliyobadilisha mara kwa mara lakini bahati nzuri siku aliyotekwa alivaa gauni alilotoka nalo porini hivyo sumu ilikuwa katika pindo la gauni lake.
“Yes!Yes!Yes!Yes! Nakushukuru sana mzee Nelson, kweli umeokoa maisha yangu! Ni lazima niitumie sumu hii kutoroka, ni lazima hawa wajinga wafe kabla ndege haijatua!”
Alipowaangalia Kennedy na O’brien aligundua walikuwa usingizini na aliposikiliza vizuri katika viti vya mbele alimsikia Nicky akikoroma akajua naye alikuwa akiota ndoto zao za utajiri! Huo kwake ulikuwa ndio wakati muafaka wa kutekeleza alichotaka kukifanya. Kwa utaalam wa hali ya juu alijikunja nakushika gauni lake kwa chini na kuanza kulipapasa katika pindo lake.
Haikumchukua muda mrefu akawa tayari ameshaligusa fundo la mahali sumu yake ilipofichwa, alizichana nyuzi zote na kukitoa kifuko cha nailoni kilichokuwemo, akiwa amelala hivyo hivyo alikifungua na kuchukua kiasi kidogo cha sumu na kukimwaga katika kiganja chake, sumu iliyobaki aliifunga vizuri na kuiweka pembeni mwake.
Kwa mkono wake wa kulia alichukua sumu iliyokuwa katika kiganja chake, akaunyosha mkono wake na kumpaka Kennedy shingoni, hakushtuka wala kujitingisha, aliamini kwa huyo kazi ilishakamilika! Bila kusita wala kuchelewa alichukua sumu nyingine na kumpaka O’brien usoni! Kwa huyo naye alijua kazi imekamilika akawa amebaki Nicky aliyekuwa kiti cha mbele kwa huyo ilimlazimu asimame taratibu bila kutingisha kitu chochote na kumpaka begani, alifanya mambo yote hayo bila kushtukiwa na abiria waliokuwemo ndani ya ndege.
Kwa maelekezo aliyopewa alitakiwa kunawa mikono yake katika muda wa sekunde thelathini tofauti na hapo hata yeye sumu hiyo ingemuua! Baada ya kukamilisha kazi ya kuwagusa kilichofuata mbele yake kilikuwa ni kunawa, hakuwa na maji lakini kwa alivyofahamu ndani ya ndege kulikuwa na bafu na maji ya kutosha. Alichofanya ni kunyata taratibu na kumruka Kennedy akaingia kwenye korido na kuanza kutembea kwenda bafuni ambako alisukuma mlango na kukuta umefungwa, ilivyoonekana kulikuwa na mtu mwingine ndani ya choo hicho akijisaidia.
“Ngo!Ngo!Ngo!” Caroline alianza kugonga mlangoni ili afunguliwe.
“Pra...ttaata....pra....ttaatta,pra...ttaata!” Hiyo ndiyo sauti aliyoisikia kutoka ndani ya choo hicho, hakuhitaji muda mrefu kuelewa kuwa kulikuwa na mtu akiharisha vibaya sana ndani ya choo hicho.
“Please open the door for me!”(Tafadhali nifungulie mlango!) Caroline alisema kwa sauti lakini mtu aliyekuwa ndani hakusikia, aliendelea na shughuli yake kama ilivyopangwa.
Alishindwa kuelewa ni kipi afanye, zilibaki sekunde chache sana kabla sumu haijamdhuru yeye mwenyewe! Tayari alishaanza kusikika kizunguzungu, hakuwa na la kufanya zaidi ya kuuparamia mlango wa choo cha wanaume, hakuona aibu kwani alitaka kuokoa maisha yake! Lakini alikuta nao pia umefungwa jambo lililoashiria ndani ya choo hicho kulikuwa na mtu. Caroline alichanganyikiwa na kushindwa kuelewa ni wapi angepata maji ya kunawa kwani bila hivyo hata yeye angekufa.
Je nini kitatokea? Fuatilia wiki ijayo.
H
arry alifika nchini
Sokomoni akitokea Tan
zania na katika muda mfupi alioishi nchini humo alijipatia umaarufu mkubwa na kufahamika na karibu kila mtu wakubwa kwa wadogo, kilichomfanya ajulikane sana ni kitendo chake cha kutumia pesa nyingi kukifadhili chama kikuu cha upinzani nchini Sokomoni, Chama cha kutetea maslahi ya wananchi (CKMW)
Alitumia pesa nyingi sana kukiimarisha chama hicho na kuisaidia jamii ya watu wa Sokomoni iliyokuwa masikini, aliwapatia vijana wengi ajira na mikopo ya mitaji ili wajiajiri wenyewe. Ni hilo ndilo lilimpa umaarufu mkubwa katika nchi hiyo iliyokuwa chini ya Utawala wa chama kimoja tangu kupata uhuru wake mwaka 1972 kutoka kwa wakoloni katika mapinduzi yaliyoongozwa na Rais wa Kwanza wa nchi hiyo,Gabriel ambaye baadaye alifuatiwa na Rais wa pili wa nchi hiyo Derrick aliyeingia madarakani kwa kuipindua Serikali ya Rais Gabriel ambaye awali ndiye alimnyang’anya Derrick mke wake Kabula.
Dostları ilə paylaş: |