“Caroline atakuwa kafa au kapatwa na matatizo?” Aliwaza Richard kichwani mwake bila kupata majibu wakati mmoja wa maaskari akitoa pingu kiunoni kwake na kuanza kumsogelea Richard tayari kwa kumfunga!
“Upo chini ya ulinzi halali wa jeshi la polisi na tafadhali sana usijaribu kufanya fujo vinginevyo nguvu ya jeshi itatumika!”
“Sawa lakini kosa langu hasa ni lipi napenda kufahamu!”
“Unahusishwa na kupotea kwa msichana Caroline jana, maelezo hayo yanatosha mengine zaidi utaelezwa kituoni!” Alijibu askari.
Pingu ziliizunguka mikono ya Richard kwa nyuma na kwa nguvu akatolewa chumbani na kupelekwa moja kwa moja kwenye gari la polisi liliondoka kwa kasi kwenda kituoni ambako Richard alihojiwa na kutoa maelezo yake juu ya kupotea kwa Caroline waliyekuwa naye siku moja kabla na alieleza kila kitu.
“Nilimwacha ukumbini jana baada ya kuanguka kifafa mbele za watu! Nilikasirika kwa sababu Caroline hakunieleza tangu mwanzo kuwa alikuwa mgonjwa wa kifafa!”
“Alitokaje ukumbini?”
“Kwa kweli sifahamu!”
“Lakini si wewe ndiye ulikwenda naye?”
“Ndiyo lakini....!”
“Lakini nini?”
“Hilo ndilo kosa langu afande kwani Caroline amepatwa nini? Amekufa?” Aliuliza Richard kwa mshangao.
“Hata sisi hatujui!”
“Tafadhali niambieni ukweli, bado nampenda sana Caroline nilifanya makosa makubwa kumwacha ukumbini jana, rafiki yangu alinishinikiza kufanya hivyo! Nampenda Caroline!”
“Mpaka sasa hatufahamu kilichompata ila hajaonekana tangu jana kuna habari zinadai atakuwa amejiua au amebakwa na wahuni, shangazi yake ndiye ametoa taarifa hapa na tayari tumemekwisha mkamata mwenzako mmoja!”
“Nani! Dickson?”
“Hapana ni msichana, anaitwa Mariam Hassan, huyo Dickson bado tunamsaka ila kuna msamaria mwema ametupigia simu kuwa katika pori la Msata huko Kibaha kuna gunia limetupwa na ndani yake kuna msichana analia, askari wetu wameondoka sasa hivi kwenda huko!”
“Unafikiri msichana ndani ya gunia hilo atakuwa ni Caroline au?”
“Kwa kweli sina uhakika sana!” Alijibu askari huyo aliyeonekana kumjali sana Richard.
“We afande hebu muingize huyo rafiki yako mahabusu si umekwishamaliza kuchukua maelezo yake?” Mkuu wa kituo aliuamuru askari aliyekuwa akiongea na Richard.
“Ndiyo afande!”
“Sasa maongezi mengi ya kazi gani?”
“Nilikuwa najibu maswali yake fulani fulani!”
“We hebu fungua mkanda bwana, vua viatu na hiyo saa yako!” Mkuu wa kituo alimwamuru Richard na alipomaliza alianza kumvuta mwenyewe kumpeleka mahabusu.
“Una nini kingine kwenye hiyo kaptura yako?”
“Sina kitu mkuu!”
“Haya ingia humo ndani uongee na rafiki zako upesi!”
“Sawa lakini naomba mnisaidie basi kumpigia simu baba yangu Arusha namba zake ni mbili,tatu....!” Kabla hajamaliza alizabwa kibao usoni na kuingia mwenyewe mahabusu.
“Nani apige simu! Sisi? Hiyo si kazi yetu ingia Sheratoni ukale piza!” Alisema mkuu wa Kituo.
Richard alitembea kinyonge na kuingia ndani ya mahabusu, kabla ya mwili wake wote haujaishia ndani alisikia sauti ikimwita kwa nyuma na alipogeuka alimwona Mariam akichungulia kutoka mahabusu ya wanawake iliyokuwa upande wa pili. Macho yake yalikuwa yamevimba na yalikuwa mekundu kupita kiasi sababu ya kulia, ilionekana alikuwa amelia sana kabla.
Huo nido ukawa mwanzo wa Richard kuingia mahabusu! alilia kwa sababu alijua hana hatia na alimpenda mno Caroline asingeweza kumdhuru! Kosa pekee alilojilaumu kwa kulifanya ni kumwacha Caroline ukumbini peke yake hata hivyo alimlaumu Dickson kwa kosa hilo, ndiye aliyemshawishi kumwacha baada ya kumcheka akidai hapakuwa na sababu ya yeye kuwa na uhusiano na mwanamke mwenye kifafa.
Mpaka wakati huo hakufahamu ni wapi rafiki yake Dickson alikokuwa lakini alielewa ni lazima angekamatwa na kuungana naye mahabusu, hilo kwa Richard halikuwa suala kubwa, kilichomsumbua zaidi akilini mwake ni Caroline! alimwomba Mungu Caroline apatikane.
************
Magazeti ya siku hiyo yaliandika habari juu ya kuvurugika kwa shindano la Miss Bongo baada ya mrembo aliyeshinda kuanguka kifafa ukumbini na hatimaye kupotea, na aliyechanguliwa baada ya mshindi kuonekana ana kifafa, pamoja na mpenzi wa msichana aliyepotea walikuwa wakiisaidia polisi kufuatia kupotea kwa mrembo huyo!
Habari za kupotea kwa Caroline na kukamatwa kwa Mariam zilitangazwa pia katika redio mbalimbali na wazazi wa Caroline walizisikia habari hizo wakiwa nyumbani kwao Arusha walichanganyikiwa kiasi cha kutosha na kulazimika kusafiri kwa haraka kwenda Dar es Salaam ili kujua kwa undani kilichotokea! Shangazi yake Caroline aliogopa kuwajulisha kwa simu kwa hofu ya kulaumiwa kufuatia kitendo chake cha kumruhusu Caroline kuondoka nyumbani kwenda kushiriki mashindano ya urembo, hapakuwa na njia ya kuwaeleza kuwa Caroline alidanganya na akaeleweka.
Mama yake Caroline alilia njia nzima hadi wanaingia Dar es Salaam siku hiyo saa mbili ya usiku.
*****************
Reginald Simon alikuwa kijana wa Kitanzania, mtanashati pengine kuliko wavulana wote katika jijini Dar es Salaam. Hali hii ilitokana na pato la kazi nzuri aliyoifanya kama Afisa Mali Asili mkoa wa Pwani! Kilichomwezesha kuipata nafasi hiyo katika umri mdogo si kingine bali ni Elimu nzuri aliyokuwa nayo katika mambo ya misitu aliyoipata nchini Urusi ambako alisoma kwa miaka kumi!
Katika umri wa miaka thelathini tu Reginald alimiliki nyumba mbili za kifahari jijini Dar es Salaam na moja kubwa mjini Kibaha. Pia alimiliki gari nzuri aina ya Surf New Model! Lililomfanya aonekana mwenye uwezo mkubwa zaidi.
Pamoja na vitu vyote hivyo Reginald alikuwa bachela! Hakutaka kuoa na aliishi peke akidai mwanamke aliyestahili kuwa mke wake alikuwa bado hajazaliwa! Ni tabia yake hii iliyowafanya wasichana wengi kuchanganyikiwa kimapenzi juu yake na kujipitishapitisha ili awaone lakini hawakupata kitu chochote, pesa na uzuri wa sura yake uliwatia kiwewe!
Pamoja na kufanya kazi mkoani Pwani Reginald aliishi Mikocheni jijini Dar es Salaam, alilazimika kusafiri kila siku kwa gari asubuhi kwenda kazini kibaha na kurudi Dar es Salaam ni siku za Jumamosi pekee yake ndizo alibaki kibaha. Sababu ya kubaki ilikuwa ni kujishughulisha na shughuli za uwindaji alizozifanya katika pori la Msata Kibaha! Alipenda sana kuwinda hilo ndilo jambo alilolifanya katika siku za mwisho wa wiki.
**************
Ilikuwa ni siku ya Jumamosi majira ya saa nne, Reginald alikuwa akipita katikati ya pori huku akimvuta swala aliyemuua kumpeleka mahali alikokusanya wanyama aliowaua siku hiyo, hiyo ilitokea baada ya kuishiwa na risasi katika bunduki yake! Mara ghafla aliona kitu kama gunia likiwa limetupwa chini, tairi za gari zilikuwa zikionekena pembeni mwa gunia hilo.
“Labda ni wafanyabiashara wa mkaa wamesahau mkaa wao hapa!” Aliwaza Reginald lakini baadaye alishtuka alipoona gunia hilo likichezacheza na ilifuata sauti ya msichana akilia kutoka ndani ya gunia hilo, moyo wake ulipiga harakaharaka ikabidi atoke mbio kwenda kujificha katika kichaka kilichokuwa jirani na eneo hilo huku moyo wake ukidunda kwa nguvu.
Alishindwa kuelewa ni kitu gani kilikuwa kimetokea mpaka msichana akawekwa ndani ya gunia na kutupwa eneo hilo.
“Ingekuwa ni sauti ya mwanaume ningeweza kufikiri labda ni dereva teksi alitekwa na na majambazi wakaja kumtupa hapa ili afe lakini kwa msichana sielewi kilichotokea lakini hapa ni lazima kuna tatizo tena tatizo kubwa!” Alizidi kuwaza Reginald.
Upande mmoja wa moyo wake uliposikia msichana akizidi kulia na kuomba msaada ulisikia huruma na kujikuta akitamani kutoka ndani ya kichaka kwenda kumfungulia lakini alisita kufanya hivyo kwa sababu hakujua waliomtupa walikuwa umbali gani kutoka eneo hilo na isitoshe alijua wazi kwa kufanya hivyo alama za vidole vyake zingeweza kubaki kwenye gunia na baadaye kumponza, mawazo hayo yalimfanya azidi kuvuta subira!
“Lakini acha kwanza nijulishe polisi juu ya suala hili, nafanya hivyo kama msamaria mwema!” Alisema na kisha akaichomoa simu yake iliyokuwa kiunoni na kuanza kupiga namba 999 ili kuwajulisha polisi juu ya tukio alilolishuhudia.
Simu hiyo ilipokelewa na askari wa doria ndani ya gari la polisi aina ya gofu naye bila kuchelewa alipiga simu ya upepo kituoni kutoa taarifa hiyo. Kipindi taarifa inafika kituoni ndio askari walikuwa wamerejea kutoka hotelini kumkamata Richard!
“Nendeni haraka huko porini na mfuate maelezo hayo hayo aliyowapeni huyo msamaria mwema wahini ili muokoe maisha ya huyo msichana, inawezekana ndiye tunayemtafuta!” Mkuu wa kituo alisema.
“Sawa afande!” Walijibu maaskari na kutoka nje ambako waliingia ndani ya gari aina ya Rangerover la polisi, ni gari pekee ndilo lilitumika katika masuala ya haraka ya polisi.
Kasi ambayo gari liliondoka nayo kituoni ilimshangaza kila mtu aliyekuwepo na baadhi ya walifikiri ni gari la mashindano!
“Watafika kweli hawa?” Mkuu wa kituo alimuuliza askari aliyekuwa akipita karibu yake.
“Watafika tu afande wala usiwe na wasiwasi!” Vumbi lilitimka kituoni na kuwaacha watu hawaonani.
**************
Saa nzima baadaye Reginald akiwa amejificha kichakani alishuhudia gari likija taratibu na kuegeshwa pembeni mwa gunia hilo, aliteremka kijana mmoja mrefu na mtanashati na kulisogelea gunia hilo! Reginald alianza kusikia tena sauti ya msichana ndani ya gunia akiomba msaada kwa kijana huyo huku akitaja jina la mtu aliyemtupa pale kuwa ni Dickson.
“Ha! Kumbe wewe ni Dickson?”
“Ndiyo! Lazima nikuue ili kukunyamazisha milele!” Alisema kijana huyo na msichana ndani ya gunia alianza kumbembeleza kijana huyo asimuue kwa ahadi ya kutosema kuwa alimbaka lakini kijana huyo alizidi kusisitiza kuwa angemuua atake asitake. Reginald aliyasikia maongezi yao yote na kujua kilichokuwa kikiendelea.
“Ha! Kumbe huyu kijana anataka kumuua msichana aliyeko ndani ya gunia! Haiwezekani lazima nifanye kitu fulani kumuokoa msichana huyu! Lakini huyu kijana anaweza kuwa na bunduki na akanimaliza! Laiti bunduki yangu ingekuwa bado ina risasi ningemuua kutoka hapa hapa kichakani!” Alisema Reginald kwa masikitiko. Alihofu kijana huyo angeweza kumuua!
“Lazima nikuue kwa kukugonga na gari, nikusagesage kabisa malaya wewe!” Alisema kijana huyo na dakika mbili baadaye aliingia ndani ya gari lake na kuanza kurudi kinyumenyume hatua kama kumi alisimama na kuanza kulijaza gari lake moto ili akienda mbele aligonge gunia alilokuwemo msichana huyo kwa nguvu.
Reginald alizidi kusikia sauti ya msichana akibembeleza asiuliwe lakini kijana huyo hakusikia kitu wala hakuona huruma, Reginald alishindwa kuelewa ni kosa gani msichana huyo alifanya mpaka kustahili kifo cha kutisha kiasi hicho!
Reginald alijishika kichwani kwa woga alipoona gari likiondoka kwa kasi ya ajabu na kuligonga gunia hilo mpaka likaruka mbele! Msichana ndani ya gunia alitoa kilio mara moja tu na kunyama kimya!
Bila huruma kijana ndani ya gari alianza kulirudisha kinyumenyume tena ili aligonge kwa mara ya pili ni hapo ndipo Reginald aliposhindwa kuvumilia, hakuwa tayari kuona binadamu akiuawa kikatili namna hiyo mbele ya macho yake.
Kabla gari halijaenda mbele kuligonga gunia tena Reginald alijikuta akichomoka kichakani mbio akiwa na bunduki yake isiyo na risasi hata moja mkononi mwake, alikuwa amemlenga Dickson ndani ya gari.
“Mikono juu! Nasema mikono juu!” Reginald alitishia kwani suala la bunduki kukosa risasi lilikuwa siri yake.
“Mungu wangu! Wewe nani tena?” Reginald aliuliza kila mara.
“Utanifahamu baadaye lakini kwa sasa nasema nyosha mikono yako juu!” Aliendelea kusema Reginald ingawa alijua wazi bunduki yake haikuwa na risasi.
“Hapa bora nife kabisa kuliko kukamatwa ni heri kifo cha risasi kuliko hicho kifo kilichopo mbele yangu!” Alijisemea moyoni mwake Dickson na ghafla kama risasi alichomoka ndani ya gari lake na kuanza kukimbia kuelekea porini, Reginald hakuwa na muda wa kumfukuza kwa nyuma, alimshukuru Mungu kwa kilichotokea.
Hakutaka kupoteza muda wake, palepale alilisogelea gunia hilo na kuanza kulifungua, hakuamini macho yake alipokutana na sura ya Caroline msichana aliyesifika kwa uzuri katika jiji la Dar es Salaam, hata yeye binafsi alimfahamu.
“Caroline!”
“Na..a..m!” Aliitika Caroline kwa shida, damu nyingi zilikuwa zikimtoka na mkono na mguu mmoja ulikuwa umevunjika kiasi cha mifupa kuchungulia nje.
“Lakini nini kimetokea Caroline?”
“Wana....ta...ka kuni..ua!”
“Akina nani?” Reginald aliuliza tena lakini hakujibiwa swali hilo, caroline alikaa kimya huku damu ikimtoka puani na mdomoni, gari lilimgonga vibaya, Reginald alilia machozi kwa uchungu kuona msichana mzuri kama huyo anakufa mkononi mwake lakini hakuwa na uwezo wa kuokoa maisha ya binti huyo mzuri!
Ghafla alisikia muungurumo wa gari nyuma yake na alipogeuza shingo gari aina ya Rangerover lililoandikwa maneno “POLISI” ubavuni lilikuwa likiendeshwa kuelekea mahali alipokuwa kabla halijaegeshwa vizuri, maaskari zaidi ya kumi walikuwa ndani yake waliruka na kutua ardhini huku bunduki zao zikiwa zimemlenga Reginald.
“Hapohapo ulipo mshenzi mkubwa wewe! Kwanini unaua kikatili kiasi hiki?” Alisema mmoja wa maaskari hao na Reginald alishangaa kuona anaitwa mshenzi, alijikuta akisimama wima bunduki yake likiwa mkononi.
“Jamani mimi sio muuaji aliyefanya mauaji haya kakimbia....!” Kunyanyuka kwa Reginald akiwa na bunduki mkononi kuliwafanya maaskari walifikiri alitaka kuwashambulia kwa bunduki yake! Kitendo bila kuchelewa askari mmoja alimimina risasi tano mwilini mwa Reginald palepale akaanguka chini huku damu zikiruka kutoka mwilini mwake kama bomba.
“”Si..o....ye...ye!”” Caroline alisema kwa shida lengo lake likiwa ni kuwaeleza maaskari kuwa aliyetaka kumuua hakuwa Reginald lakini alikuwa amechelewa, tayari Reginald alikuwa chini akitupatupa miguu hewani.
Miili yote miwili ilibebwa na kuwekwa ndani ya gari la polisi na liliondoka kwa kasi kuelekea hospitali ya Tumbi Kibaha kwa lengo la kujaribu kuokoa maisha ya Caroline, kwa upande wa Reginald maaskari wote walikuwa na uhakika alishafariki dunia!
Je watu hawa wataokolewa? Nini kinaendelea katika simulizi hii ya kusikitisha?
Fuatilia wiki ijayo.
T
ayari wazazi wa Caroline
walikuwa jijini Dar es Sa
laam tena upanga nyumbani kwa shangazi yake na Caroline, walikuwa katika mjadala mzito juu ya kilichotokea.
“Nilishindwa kuwapeni taarifa juu ya jambo hili!”alisema shangazi
“Kwanini sasa?” profesa Kadili aliuliza swali jingine.
“Kwa sababu nilifanya makosa kumruhusu Caroline kutoka nyumbani katika tarehe za hatari!”
“Usijali sana dada kwa hiyo hivi sasa yupo wapi?”
“Bado hajapatikana polisi wanaendelea kumtafuta na haijulikani alipo!”
“Kwani baada ya kuzinduka kutoka katika kifafa alikwenda wapi?”
“Taarifa nilizozipata na ambazo hata polisi wanazo,alikimbia kwenda nje kuwafuata wavulana wawili na msichana mmoja waliokwenda nae ukumbini!”
“Kwanini hao wavulana na huyo msichana wasikamatwe na kuhojiwa?”
“Tayari wawili kati yao wamekwisha kamatwa na wapo rumande!”
“Wanasema nini juu ya Caroline?”
“Wamekana kuondoka naye ukumbini huku wakilia! Mvulana mmoja ndiye bado hajakamatwa lakini polisi bado wanaendelea na msako!”
“Kwa akili ya Caroline ilivyo nina uhakika kabisa atakuwa tayari ameshajiua! Siyo kitu rahisi kwake kuanguka mbele za watu wengi halafu aendelee kuwa hai si mnakumbuka aliyofanya Arusha!”
“Usiseme hivyo baba Caroline! Mtoto atakuwa hai tu!” alisema mama yake Caroline.
Baada ya maongezi hayo Kimya kikubwa kilipita katikati yao ni kwikwi za kilio tu zilizosikika, ilikuwa ni siku ya huzuni kubwa sana katika maisha ya Dk. Cynthia na mumewe Profesa John Kadiri ambao kwao Caroline alikuwa mtoto pekee na hawakuwa na tegemeo la kupata mtoto mwingine.
Caroline alikuwa kila kitu kwake ukimuondoa kaka yake waliyechangia nae mama, Dennis ambaye kwa wakati huo alikuwa mfanyabiashara mkoani Dodoma! Kwa sababu hiyo Cynthia hakuwa tayari kimwili na kiroho kumpoteza Caroline sababu tu ya ugonjwa wa kifafa! Aliendelea kulia akilitaja jina la mtoto wake!
Ukimya uliokuwepo ulikatishwa ghafla na mlio wa simu iliyokuwa mezani, shangazi alinyanyuka haraka na kwenda kuipokea simu hiyo!
“Hallow!.....ndiyo!...... nani anaongea? Ha! Kweli?…..yupo wapi?” Aliendelea kuongea shangazi katika simu.
Maongezi yake pamoja na kuwa profesa Kadiri na mkewe Cynthia hawakuyasikia bado walielewa kilichoongelewa kutokana na majibu aliyoyatoa shangazi! Sura yake ilijaa tabasamu lililopotea muda mfupi kabla simu haijakatika!
“Ha!Kweli? Hali yake ikoje? ….atapona?….tunakuja sasa hivi nipo na wazazi wake hapa nyumbani kwangu!”
Tayari Dk. Cynthia na mumewe walikuwa wima kabisa wakimsubiri shangazi amalize kuongea, mabadiliko ya sura yake na machozi yaliyomtoka yalionyesha kulikuwa na tatizo kubwa lililotokea!
“Vipi dada?” Profesa John Kadiri aliuliza.
“Twende hospitali ya jeshi Caroline amepatikana lakini hali yake ni mbaya sana!”
“Nini kimempata?”
“Sikuelezwa vizuri nyie twendeni tu!”
Walitoka nje na kuingia ndani ya gari na safari ya kwenda hospitali ya jeshi ilianza mara moja! Hospitali ya jeshi ilikuwa umbali wa kama kilometa mbili kutoka upanga alipoishi shangazi lakini sababu barabara kuwa ya lami iliwachukua kiasi cha kama dakika tano tu kufika na kuegesha gari lao na wote watatu walishuka na kuanza kutembea kuelekea mapokezi.
“Jamani tunamuulizia ndugu yetu!”
“Dada hata salamu?”
“Samahani ndugu yangu vichwa vyetu vimeingiliwa na mdudu, utanisamehe kwa kutokuwa mstaarabu!”
“Hakuna tatizo dada hapa kwetu ndio hivyo tunapokea watu wenye matatizo mbalimbali! Sijui mgonjwa wako ni nani?”
“Anaitwa Caroline John Kadiri!”
Shangazi alipotaja tu jina hilo nesi alionyesha mshtuko wa ajabu! Jambo lililowafanya shangazi, Dk. Cynthia na mumewe kushindwa kuelewa ni kitu gani kilikuwa kimetokea kabla hawajafika hospitali!’
“Vipi amefariki?” Dk.Cyanthia alijikuta akiuliza bila kutegemea.
“Hapana lakini hali yake si nzuri, amekimbizwa chumba cha upasuaji!”
“Kwani nini kilimpata?”
“Alitekwa na kijana mmoja aliyempeleka porini akiwa amefungwa ndani ya gunia!”
“Mungu wangu kijana gani huyo?”
‘Kakamatwa na kapigwa risasi kama tano hivi na maaskari kwenye mguu wake wa kulia alipoletwa hapa maaskari wakifikiri amekwisha kufa lakini daktari alipompima aligundua alikuwa bado anahema! Hivyo wote wapo chumba cha upasuaji wakifanyiwa operesheni!”
“Sasa sisi tufanye nini dada yangu?”
“Nyie kaeni pale kwenye benchi msubiri mpaka watoke chumba cha upasuaji!”
“Sawa!” Alijibu Dk. Cynthia huku akijifuta machozi na kwenda kwenye benchi ya kukaa! Walikaa hapo kwa dakika kama kumi tu roho zikiwa haziwapi na wote waliondoka na kuanza kutembea kuelekea chumba cha upasuaji huko walikaa katika benchi lililokuwa nje ya chumba hicho muhimu na kuanza kusubiri Caroline.
*****************
Kazi ya kumshona sehemu alizopasuka na kuiweka sawa mifupa ya Caroline iliyovunjika vibaya, haikuwa ndogo, iliwachukua madaktari muda wa masaa mawili tu kuikamilisha huku chupa za damu na maji zikiendelea kuingia katika mishipa yake, baada ya kazi hizo kukamilika Caroline alifungwa P.O.P mkononi na mguuni, zikiacha sehemu zilizokuwa na vidonda peke yake kuwa wazi! Kwa jinsi kazi hiyo ilivyofanyika kwa uangalifu matumaini ya Caroline kupona yalikuwa makubwa sana.
“Dk. Cynthia vipi mbona upo hapa umetoka lini Arusha?” Lilikuwa swali kutoka kwa Kepteni Slyvester Lukonge daktari bingwa wa upasuaji wa jeshi! Yeye na Dk. Cynthia walisoma pamoja chuo kikuu.
“Mtoto wangu yuko huko ndani anafanyiwa upasuaji!”
“Mtoto wako? Ni yupi maana maana hii operating Theater yetu ina vyumba vitano! Sasa sijui yuko chumba gani”
“Anaitwa Caroline!”
“Ahaaa! Kumbe Caroline ni mtoto wako?”
“Ndiyo mtoto wangu wa kwanza na pekee tuliye naye! Huyu hapa ni mume wangu anaitwa Profesa John Kadiri”
Dk. Lukonge alishikana mkono na profesa Kadiri wakisalimiana, baada ya salamu Dk. Lukonge aliwapa pole
“Ni mimi na Dk. Kepteni Gindu Sweya ndio tumemfanyia operesheni hiyo!”
“Atapona lakini?”
“Atapona ila aliumia sana kwani amepata compound fracture katika mguu na mkono wake wa kushoto pia amevunjika mbavu tatu za ubavu wa kushoto! Inavyoonekana kuna watu walimpiga na vitu vizito baada ya kumbaka.
“Alibakwa?”
“Ndiyo kwa sababu kuna mbegu za kiume zimeoneana katika sehemu zake za siri!”
Jibu hilo la daktari lilimfanya hata profesa Kadiri alie machozi! Profesa John Kadiri alipandwa na hasira kupita kiasi na alimwonea huruma mtoto wake kwani hata kama angepona kulikuwa na uwezekano mkubwa aliambukizwa Ukimwi na wabakaji hao.
Maongezi yao hayakuendelea zaidi kwani muda mfupi baadaye lango la chumba cha upasuaji lilifunguliwa na machela mbili zikatoka zikiwa zimeongozana! Waliagana na daktari na kuanza kuzifuata machela hizo kwa nyuma, mbele mita kama hamsini moja ilisimama kwenye wodi iliyoandikwa maneno Male WD 1, ilikuwa wodi ya wanaume na ukafunguliwa machela ikaingizwa ndani.
Hawakusimama hapo waliamua kuifuata machela nyingine iliyoongoza hadi kwenye wodi iliyaondikwa Female wd 2 maneno ya kiingereza yaliyamaanisha ilikuwa ni wodi ya wanawake namba mbili, machela iliingizwa ndani ya wodi na wao waliifuata.
“Jamani saa za kuona wagonjwa sio hizi, yaani usiku huu mnataka kuona wagonjwa?Hebu tufuate taratibu za hospitali!”
“Sawa binti lakini tulitaka tu kumchungulia mtoto wetu mara moja!”Dk. cynthia alisema.
“Hapana mama haturuhusiwi kufanya hivyo njooni kesho asubuhi!”
Dk. Cynthia hakutaka kubisha alifungua mkoba wake na kutoa kitambulisho akamkabishi muuguzi huyo ili akisome, alitupa macho yake juu ya kitambulisho hicho kisha akanyanyua uso na kumwangalia tena Dk. Cynthia usoni! Hakusema kitu zaidi ya kuwaruhusu wamwangalie mgonjwa mara moja.
“Fanyeni haraka kabla muuguzi mkuu hajafika itaniletea matatizo mimi!”
Walitembea kwa harakaharaka hadi kwenye kitanda alicholazwa Caroline na kumwangalia kila mtu kati yao alisikitika kiasi cha kutosha! Ilikuwa si rahisi hata kidogo kuamini aliyelala kitandani pale alikuwa mtoto wao Caroline, uso wake ulikuwa umevimba na ulijaa bendeji nyingi zenye rangi nyekundu, mkono na mguu wake ulifungwa mhogo wa POP na alionekana kuhema kwa shida hakuwa na fahamu yoyote sababu ya madawa ya usingizi aliyopewa chumba cha upasuaji.
“Kwa hali niliyoiona mtoto wetu atapona lakini najiuliza ni kwanini walitaka kumuua? Je ni sababu ya kuugua kifafa tu? Na kwanini sasa walimbaka mwanangu kabla ya kumfanyia ukatili huu?” Alisema Dk, Cynthia wakitembea kwenda nje ya wodi.
“Haiwezekani ni lazima mtu aliyefanya ukatili huu afe! Hawezi kumfanyia mwanangu kitendo hiki halafu yeye akandelee kuishi!” Aliwaza profesa Kadiri.
Walipotika wodini walichukua gari lao na kuondoka kuelekea nyumbani, usikuw wa siku hiyo hakuna aliyepata usingizi kati yao walikesha wakiongea na kupanga kitu cha kufanya ili haki itendeke.
“Ni lazima sheria ichukue mkondo wake, ni lazima watu hawa wafungwe kabisa!”Alisema Dk. Cynthia kwa hasira.
Wakati Dk. Cynthia akiwaza juu ya sheria kuchukua mkondo wake, ndani ya kichwa cha mumewe iliendelea mipango ya mauaji na katikati ya usiku alimtoa dada yake nje na wakapanga kitu cha kufanya.
“Tutamtafuta mtu na atamuua hapo hapo kitandani alipolala, jambazi mkubwa yule!”
“Tutamuua na nini?” Shangazi aliuliza.
“Nitatumia dawa fulani! Wewe hiyo niachie mimi, cha msingi apatikane nesi wa kufanya hilo jambo!” Profesa Kadiri aliongea akionyesha hasira yake yote.
******************
Jioni ya siku hiyo Shangazi na profesa Kadiri walikuwa ndani ya hoteli ya Starlight wakiwa wamejificha pembeni kabisa mwa ukumbi wa hoteli hiyo, walikuwa hapo kumsubiri mtu mmoja muhimu waliyeamini angesaidia kuikamlisha azima yao! Hawakutaka kumshirikisha Dk. Cynthia katika mpango huo.
Aliyekuwa akisubiriwa alikuwa mmoja wa wauguzi katika wodi aliyolazwa Reginald, waliomba kuonana naye baada ya kazi ili awasaidie katika mpango mzima wa kumuua Reginald kabla hajazinduka usingizini!
Dostları ilə paylaş: |