SURA YA KWANZA
NASABA YA NABII MUHAMMAD
MAISHA YA NABII MUHAMMAD (S.A.W)
NASABA YA NABII MUHAMMAD
Mtume wetu Muhammad (s.a.w.) ni Mwarabu, katika kabila ya Kikuraishi –kabila bora kuliko kabila zote za kiarabu – na katika ukoo wa Bani Hashim1; ukoo wa kwanza katika koo nne zilio tukufu sana kwa Makureshi; wa pili ni Bani Umayya. Waarabu wote walikuwa wakiwaheshimu Makureshi; kwa sababu Al Kaaba yao ilikuwa katika mji wao na katika mikono yao. Haramia wote wa kiarabu hawakuwa wakijasiri kupokonya kitu katika misafara ya Kikuraeshi, wala mji wao wa Makka haukupata kushambuliwa, ila safari moja mbili tu; na Waarabu wote walichukizwa na kabila hiyo iliyovunja utukufu wa nchi ya Makka. Makureshi walikuwa wanagawika matumbo mengi yanayotafautika katika utukufu wao .
A. WAZEE WAKE WANAUME
Mtume wetu (s.a.w.) (Rehma za Mungu ziwe juu yake ) ni Muhammad bin Abdillah bin Abdil Muttalib bin Hashim bin Abd Manaf bin Qusay. Kila mmoja katika mababu zake alikuwa ni bwana katika wakati wake. Matukufu yote ya Kikureshi aliyakusanya Qusay katika wakati wake na yeye aliwarithisha wanawe .
Makuresih walikuwa na matukufu yao 12 ambayo walikuwa wakiitakidi kwamba kila wenye mawili ni bora zaidi kuliko wenye moja, na ukoo wenye mengi zaidi ndio bora kabisa. Matufu yenyewe ni haya na mengineo, na yote aliyazuiya Bwana Qusay na akawarithisha wanawe .
-
SIQAYA. Kuwatengenezea maji ya kuwatosha watu wanaokuja kuhiji. Makka ilikuwa ina tabu kubwa ya maji. Hapana mto wala maziwa. Maji yakipatikana visimani tu. Na visima vyenyewe vilikuwa mbali mbali, wala havina maji mengi basi walikuwa wanapata tabu kubwa mahujaji wakati walipokuwa wanakuja Makka. Bwana Qusay akaona ni shauri nzuri kutengeneza mahodhi ya ngozi ya kutia maji kuwaekea tayari hao Mahujaji wanapokuja kuhiji. Ukoo mahususi baadaye ulichukua kufanya kazi hii ukadhamini kutoa gharama zote za kuleta maji hayo na kuyatia zabibu na lozi kufanya kama sharubati.
-
RIFADA. Kuwatengenezea chakula cha bure Mahujaji waliokua hawajiwezi kujilisha kwa gharama zao. Ulichukua ukoo mahususi gharama za vyakula hivi ingawa kila mtu aliyetaka alikuwa anayo ruhusa kuusaidia ukoo huo, katika baadhi ya gharama.
-
HIJABA. Kushika funguo za Al Kaaba na kuwa na amri ya kuwafungulia wanaowataka na kuzuilia kuingia wasiowapenda, kazi hii ilikuwa katika mikono ya ukoo makhsusi .
-
LIWAA. Kuwa na ukubwa wa majeshi ya vita wakati vinapokuwa vita, na kuwa mkubwa wa misafara ya biashara .
-
NAD–WA. Kuwa na uraisi wakati wanapokusanyika Makureshi kwenye nyumba yao ya mkutano iliyokua ikiitwa Dar Nadwa. Na mengi yasiokuwa haya ambayo si lazima tuyataje hapa .
Ama Abd Manaf, yeye ndiye baba wa koo tatu katika hizo koo nne tukufu za Kikureshi :
1.Bani Hashim bin Abd Manaf .
2.Bani Umayya bin Abd Shams bin Abd Manaf .
3.Bani Naufal bin Abd Manaf .
Na Bwana Hashim ameitwa hivyo (baada ya kua akiitwa Amir ). kwa ajili ya ukarimu wake mkubwa aliokua akifanya wakati ilipoingia njaa katika nchi ya Hijazi, alikua akiamrisha kupikwa michuzi na kufanywa mikate ya ngano kupewa kila anaekuja, na kupelekewa kila Kureshi katika mji wa Makka. Na Bwana Abdul Muttalib ndiye aliechimba kisima cha zamzam ambacho mpaka leo kinatumika. Kisima hiki kilikua kikitumika zama za Nabii Ismail, baadaye kikazibwa na kabila nyingine zilizotawala Makka, mpaka akakichimba tena Bwana Abdul Muttalib. Na katika miaka yake ya mwisho aliingia katika chama cha watu kidogo waliokua wakikataa kulewa, kuzika watoto wao wanawake wangali wahai na kuabudu masanamu, na zama za ujumbe wake alikataza watu kutufu (kuzunguka Al Kaaba ) bila ya nguo baada ya kua wakitufu bila ya nguo, wake kwa waume, wakiitakidi kuwa nguo ni kitu kinachopata uchafu, kwa hivyo hakistahiki kuvaliwa wakati wa ibada.
B. WAZEE WAKE WANAWAKE
Tumekwisha kuona namna gani wazee wake Mtume (s.a.w.) wanaume walivyokua watukufu mbele ya Makureshi kwa ajili ya utukufu wa baba zao na kwa vitendo vyao vitukufu, walivyokua wakivifanya. Basi vile vile wazee wake wanawake walikua ni wanawake wa nyumba kubwa na wakafanya mambo makubwa. Kwa hivyo yeye Mtume (s.a.w.) ni mtukufu kuumeni na kuukeni, tangu mwanzo wa asili yake.
Mama yake ni Bibi Amina bint Wahab bin Abd Manaf bin Zuhra bin Kilab; katika ukoo wa Bani Zuhra mmoja katika koo zinazohusiana sana na kukutana upesi na zile koo nne tukufu za Kikureshi. Babu watatu wa Mwana Amina – Kilab – ndie babu wa nne wa Bwana Abdalla baba yake Mtume (s.a.w.) . Mwanamke huyu amezaliwa mwaka 546 A.D.na akafa 576.
Ama mama yake mwana Amina ni Mwana Barra bint Abdil Uzza, katika ukoo wa Bani Abdi Dar – ukoo wa nne katika zile koo nne tukufu – . Na bibi yake Mtume (s.a.w.) mzaa baba yake ni Bibi Fatma bint Amr bin Aidh bin Imran bin Makhzum, katika ukoo wa Bani Makhzum – miongoni mwa koo zilizokua mashuhuri mbele ya Makureshi kwa mali na heshima na wingi wa fahari –. Wao walikua washirika wa Bani Umayya – ule ukoo wa pili mtukufu – kwa hivyo walikua wakifanya watakavyo katika mji wa Makka.
Abu Jahl – adui mkubwa wa Mtume (s.a.w.) baada ya Uislam – alikua katika kabila hii, na ni mwenye kuhusiana mno na mwanamke huyu. Lakini juu ya hivyo hatuwezi kusema yeye ni mjomba wake Mtume (s.a.w.). Bibi yake Mtume (s.a.w.) huyu anakua kama shangazi wa Abu Jahl kwa kuzaliwa kwao, si shangazi hasa aliezaliwa na baba yake. Abu Jahl ni mjomba hasa wa Sayyidna Umar – Khalifa wa pili – . Mama yake Sayyidna Umar ni Fatma bint Hisham, na yeye ni Abu Jahl bin Hisham. Jina lake khasa ni Amr. Hili Abu Jahl kaitwa katika zama za Kiislam kwa balaa zake Ama Mama yake Bwana Abdul Muttalib ni katika kabila ya Bani Najjar – kabila kubwa katika kabila kubwa za Kimadina –. Yeye si katika kabila za Kikureshi, alikua ananasibika na kabila za Kiyaman – kabila za Waarabu wa kusini – .
Hapana mmoja katika bibi zake Mtume (s.a.w.) ila ni mtoto wa watu, na mwenye kufanya jambo la kusifiwa. Mtume (s.a.w.) alikua na fahari sana kwa mabibi zake wote, hasa kwa mabibi tisa waliokua wakiitwa Aatika, na saba waliokua na majina ya Fatma – ingawa wanawake walikuwa hawaonekani kitu wakati huo –. Mara nyingi wakati wa kujinasibisha Mtume (s.a.w.) alikua akisema kwa kiarabu “Ana bnul Awatik wal Fawatim” – yaani mimi ni mtoto wa hao Maatika na Mafatima.
Wawili katika hawa Maatika walikua Makureshi, watatu waliokua katika Bani Suleym – kabila iliokua ikipenda sana kujifaharisha kila inapokutana na kabila nyingine za kiarabu wakati wa Kuhiji – na waliosalia ni katika kabila mbali mbali. Ama wale Fatma, mmoja ni yule bibi yake wa Kibani Makhzum, na wengine ni wa kabila mbali mbali za Kiarabu. Baadhi yao ni wa kaskazini ya Bara Arabu, baadhi nyengine ni wa kusini, wengine wa mashariki na wengine wa magharibi. Hapana kabila yeyote ya kiarabu ila imehusiana na Mtume (s.a.w.).
SURA YA PILI
KUZALIWA KWA NABII MUHAMMAD (S.A.W.)
NA MAISHA YA UTOTO WAKE
KUZALIWA KWA NABII MUHAMMAD (S.A.W.)
NA MAISHA YA UTOTO WAKE
Baba yake Mtume (s.a.w.) amezaliwa mwaka wa 545 A.D. alikua ni mtoto wa kumi 10. katika ndugu 12 wanaume. Ama ndugu zake wote wanaume na wanawake ni 14. Yeye alikua ni baba mmoja mama mmoja na Bwana Abu Talib, baba yake Sayyidna Ali (Khalifa wa nne ), lakini Bwana Abu Talib alikua mkubwa kuliko yeye kwa miaka mitano. Alipotimia miaka 24 na kitu, baba yake Bwana Abdul Muttalib, alimposea Mwana Amina bint Wahab – alikua miaka 24 – . Wakaingia nyumbani awali ya mwezi wa Rajab, Agost 570, A. D. Mwezi ule ule bibi huyu alishika mimba ya Mtume (s.a.w.).
Hata ulipokua msafara mdogo wa Kikureshi unatoka kwenda Sham kufanya biashara, baba yake Bwana Abdul Muttalib, alimuamrisha atoke pamoja nao akafanye baadhi ya biashara, ili wapate pesa za kufanyia karamu wakati atakapozaliwa huyo mtoto, kwani mtoto huyo atakua ndiye mtoto wake wa kwanza, kifungua mlango wake. Akenda mpaka Sham na akafanya biashara yake kama alivyoamrishwa na baba yake. Hata wakati wa kurejea, alipofika Madina, alishikwa na homa ya malaria1. Akakaa kwa wajomba wa baba yake, Bani Najjar. Kwani tumekwisha kuona kuwa mama yake Bwana Abdul Muttalib ni mwanamke wa Kimadina. Akaugua kwa muda wa mwezi mzima, kisha akafa katika Mfunguo nne. Akazikwa huko huko Madina katika nyumba ya jamaa yake aliyekua akiugulia kwake siku zote. Alipokufa alikua ni kijana wa miaka 25 na kitu.
Wakati huo alipokufa baba yake, Mtume (s.a.w.) alikua mtoto wa matumboni wa miezi minane – Kama wenye Tarehe wengine wanavyothibitisha, si mtoto wa matumboni wa miezi miwili kama alivyo sema mwenye Maulidi ya Barzanji na wengine –. Mwana Amina alichukuliwa na Bwana Abu Talib, shemeji yake, akakaa eda nyumbani kwake. Baada ya mwezi na kitu akamzaa Mtume (s.a.w.) nyumbani kwa Bwana Abu Talib, katika mtaa unaoitwa Suqu -al-layl, mtaa wa Bani Hashim.
Alizaliwa alfajiri ya Jumatatu mwezi 12 Mfunguo Sita katika mwaka walioazimia Mahabushia kuuteka mji wa Makka – baada ya kua Yaman yote imo chini ya mikono yao – . Lakini Mwenye-ezi-Mungu aliwaletea ndui, yakaangamia majeshi yao kwa muda mdogo, wakapukutika kama kuku. – Hivi ndivyo alivyosema Askalany katika Al-Bukhary, na ndiyo kauli aliyoitilia nguvu Sheikh Muhammad Abdoo katika tafsiri yake –. Na siku hii ya kuzaliwa kwake inawafiki mwezi 20 April 571. Kama alivyo hakikisha haya mwanachuoni mkubwa wa Misr – Mahmoud Basha Al-Falaky –. Na siku hii ya kuzaliwa kwake palitokea ajabu kubwa, kama tunazozisikia vitabuni, kwani yeye ni Mtume (s.a.w.), na kila Mtume ana miujiza yake.Wala si uhodari kwa mtu kukanusha kila asilolijua na lisiloingia katika akili yake. Bali uhodari ni kujitahidi kufahamu. Ikiwa mtu hakuiona “Television” wala haiwezi kuingia katika akili yake ndio atasema ni “Uongo, hapana kitu cha namna hiyo!” Basi na akatae vingi visivyoweza kuingia katika akili yake fupi.
Pale pale alfajiri alipokwisha kuzaliwa Mtume (s.a.w.), alikwenda kuitwa babu yake kuja kumuona mjukuu wake, Babu huyu alifurahi sana, na akamfunikafunika maguo mjukuu wake, akajikongoja naye mpaka kwenye Al-Kaaba. Akafungua mlango, akaingia naye ndani akasimama anamuombea dua kwa mashairi mazuri ya kiarabu aliyotunga mwenyewe wakati ule ule. kisha akarejea naye, na jua bado halijachomoza.
Hata siku ya saba au ya nane alifanya karamu kubwa, na akampa mjukuu wake jina la Muhammad, yaani mwenye kushukuriwa kwa vitendo vyake vizuri. Jamaa zake walipomuuliza sababu ya kumwita jina hili, aliwajibu ya kuwa anamtarajia afikilie cheo hicho cha kushukuriwa na kila mtu. Jina hili kabisa halikua likitumika katika nchi ya Bara Arabu. Hata ilipokua karibu atadhihiri Mtume (s.a.w.). Mapadiri wa Kinasara na Makohani wa Kiyahudi waliokua wakikaa Bara Arabu walikua wakiwatahayarisha majirani zao wa kiarabu waliokua wakiabudu masanamu, Wakiwaambia: “Karibu ataletwa Mtume katika nchi hii yenu, abatilishe hii ibada yenu mbovu ya masanamu” Walipoambiwa hivi wale waarabu waliwauliza nini litakua jina la Mtume huyo, wakawajibu kuwa jina lake litakua Muhammad. Kwa hivyo kila mwenye kusadiki hayo alimwita mwanawe Muhammad. Lakini hayakusikilizana majina haya ila kwa baadhi ya waarabu waliokua wakikaa Shamu tu na Najran (Yaman) ambako Mapadri wengi wa kinasara wakikaa, na vilevile katika Madina ambayo ilikua nusu ya wakaazi wake ni Mayahudi. Hata lilipoanza kutangaa jina la Mtume wetu (s.a.w.), waliokuwa wamekwisha kuitwa kwa jina hili ni watu kidogo tu Bara Arabu nzima.
A. KUNYONYESHWA KWAKE
Mwanamke kijana na mtukufu wa Kikureshi hakua akinyonyesha mwanawe. Ilikua ni aibu kufanya hivyo.Walikua wakinyonyesha kwa siku mbili tatu tu, halafu hupewa mjakazi amnyonyeshe mpaka waje wanyonyeshaji kutoka miji mingine kuja kuwachukua wakawanyonyeshe kwa ijara1. Wanyonyeshaji hawa walikua na misimu miwili ya kuja Makka kutafuta watoto wa kuwalea. Huja kwa msafara mkubwa, wake na waume zao, katika kila siku za kabla ya baridi na siku za kabla ya joto, hukaa na watoto hao muda wa miaka miwili muda wa kuwanyonyesha. Wakisha kuwacha ziwa huwarejesha.
Kwa hivyo mama yake Mtume (s.a.w.) hakumnyonyesha mwanawe ila siku saba tu, baadaye alimpa mwanamke mmoja – Thuwaiba – amnyonyeshe. Mjakazi huyu alitolewa na Abu – Lahb baba yake mdogo Mtume (s.a.w.) – ambaye mwisho wake aligeuka akawa mshinde mkubwa wa dini ya Kiislam – makusudi amnyonyeshe Mtume (s.a.w.) . Akamnyonyesha mpaka ulipokuja msimu wa wanyonyeshaji akachukuliwa na mwanamke mmoja aliyekuwa akiitwa Halima bint Abi Dhuayb, katika kabila la Bani Hawazin, ambayo ilikua ikikaa karibu na Taif yapata meili sitini kutoka mashariki ya Makka. Taif ni mahali pazuri sana kuliko popote katika Hijaz. Pana miti mingi na maji mengi mazuri. Matajiri wengi wa Makka walikuwa wakipitisha huko siku za joto. Kwa hivyo waliwapendelea sana watoto wao wadogo kupata upepo wa mji huo. Joto la Makka halikuwa likiwafaa watoto wadogo, lilikua likiwaletea ugonjwa wa macho na magonjwa mengine. Mwanamke huyu alikaa nae Mtume (s.a.w.) muda wa miaka miwili, kama ada yao ilivyokua. Kisha akamleta ili kuchukua ijara yake. Bwana Abdul Muttalib alimpa ijara yake kamili, kama walivyoagana. Tena akamuamrisha arejee akae naye huko mpaka awe mwana mzima. – wakati huo ilikua kumeingia ugonjwa Makka –. Akarejea naye akakaa naye miaka miwili zaidi, kisha akamrejesha kwao, ingawa alikuwa na hamu sana ya kukaa naye siku zote.
Kabila hii la Bani Hawazin ilikua katika kabila zenye kusifika kwa usafi na ufasihi wa lugha. Hata Mtume (s.a.w.) wakati wanapotokea wageni na wakashangaa kwa ufasihi wake, alikua akisema “Kwa nini nisiwe fasihi, nami nimezaliwa na Makureshi, nikalelewa na Bani Hawazin, na baadae nikateremshiwa Qur-an?” Aliporejea Makka alikaa kwa mama yake. Akapewa yaya mmoja kumlea. Yaya huyu alikuwa mwanamke wa Kihabushia aliyemrithi kwa baba yake. Alikua akiitwa Bibi Barakah au Ummu Ayman (mama yake Ayman) Babu yake pamoja na msaada wa wanawe, ndiye aliyekua akimtazama Mtume (s.a.w.) kwa kula na nguo na mengineyo.
B. KUFA KWA MAMA YAKE
Alipokaribia miaka sita, Mama yake alimchukua Madina kuzuru kaburi la baba yake, Bwana Abdullah. Katika safari hii alikuwa mama yake, yaya yake – Bibi Barakah – na mwenyewe Mtume (s.a.w.) Walifika katika nyumba ile ile aliyofikia baba yake Mtume (s.a.w.) katika mtaa wa Bani Najjar – jamaa wa baba yake Bwana Abdul Muttalib – . Walikaa huko kwa muda wa mwezi mzima. Hata baadhi ya michezo ya kitoto, kama kuogelea – ambao haukuwako Makka – Mtume (s.a.w.) alijifundisha katika maziwa ya Madina.
Alipokwenda Madina mara ya pili kuja kufanya makaazi yake baada ya Utume, alikua katika baadhi ya matembezi yake, akiweza kukumbuka mahali ambapo alifanya jambo katika udogo wake, na majina ya watoto aliokuwa akicheza nao.
Baada ya mwezi, waliaga kurejea kwao Makka baada ya kufanya walioazimia. Wakaagwa na wakapewa watu wa kuwapeleka Makka. Hata walipofika Al Abwaa – meli thalathini kutoka Madina – mwana Amina alishikwa na ugonjwa akafa. Akazikwa pale pale alipokufa, na baada ya kuzikwa mama yake, Mtume (s.a.w.) kwa unyonge alikuja kwa yule yaya yake (yaya wake) akamwambia: “Wewe ndiye mama yangu sasa” Wakashika njia kurejea Makka. Alikufa Bibi huyu katika mwaka 576 A.D. naye ni kijana wa miaka thalathini.
C. KULELEWA KWAKE NA BABU YAKE BWANA ABDUL MUTTALIB
Walipofika Makka, Bwana Abdul Muttalib alimsikitikia sana mjukuu wake, na akamchukua yeye kumlea. Alikua mtu mzima wa miaka 81 na kitu. Alimuonea huruma kubwa sana na alimpenda na akamtunza zaidi ya watoto wake wadogo. Alikuwa hawezi kulala ila awe ubavuni mwake, wala hendi mahala ila pamoja naye.
Bwana Abdul Muttalib alikuwa ana mahali mahsusi pembezoni mwa Al Kaaba, pakitandikwa kwa ajili yake yeye tu, hakai juu ya zulia hilo mtu yoyote pamoja naye. Mabwana wa Kikureshi walikuwa wakikaa mkabala wake tu wakati wa kuzungumza. Ama sasa amekuwa anakaa na huyu mjukuu wake, ingawa hakupata kumkalisha mwanawe yoyote mahali hapo, maana alimuona na ishara za kua mtu mtukufu kabisa.
D. KUFA KWA HUYU BABU YAKE
Haikupindukia miaka miwili baada ya kufa mama yake ila huyu babu yake naye alishikwa na ugonjwa na akafa, na Mtume (s.a.w.) ni mtoto wa miaka minane – kidonda kipya juu ya kovu mbichi –. Mtoto huyu alilia sana, na alimliza kila anaemuona huko mazikoni. Bwana mkubwa huyu aliishi miaka mingi. Alizaliwa mwaka 497 A. D, na akafa mwaka 578 A. D. kwa hisabu ya mwaka wa kuandama miezi, alikua kapinduka miaka 83.
E. KULELEWA KWAKE NA BABA YAKE MDOGO BWANA ABU TALIB
Bwana Abdul Muttalib alipoona ajali yake imefika, aliwakusanya wanawe waliokuwa wakubwa, akawausia kufanya wema juu ndugu zao wadogo – Bwana Abbas na Bwana Hamza –. Bwana Hamza alikua ni kijana wa miaka 12, na alitokea kuwa shujaa mkubwa wa ajabu na akausaidia sana Uislam kwa cheo chake mbele ya Makuresh na kwa ushujaa wake wakati wa vita. Ama Bwana Abbas alikuwa ni kijana wa miaka 11 tu, na mwisho naye alisilimu na akawa baba wa ukoo wa Banil – Abbas (Abbasides).
Halafu baada ya kuwausia haya alimchagua Bwana Abu Talib na Bwana Zubeyr – mahalisa wa Bwana Abdullah, baba yake Mtume (s.a.w.) – akawataka wao ndio wamchukue Mtume (s.a.w.) wamlee, lakini akae katika nyumba ya Bwana Abu Talib chini ya mikono ya mkewe, Bibi Fatma bint Asad bin Hashim bin Abd Manaf. Watu hawa wawili walifuata vilivyo wasia wa baba yao. Bwana Abu Talib alikua ni mtu wa heshima kubwa mbele ya Makureshi, kwani yeye ndie aliyerithi utukufu wa baba yake, lakini alikuwa masikini sana. Alitokea kumpenda sana Mtume (s.a.w.), hata akitaka kuwagaia tunu watoto wake, kwanza humtanguliza yeye Mtume (s.a.w.), akamchagulia kilicho kizuri, ndipo akawapa wengine. Alikuwa hendi popote ila pamoja naye, kwani Mtume (s.a.w.) hakuwa akipenda sana kucheza na watoto kama yeye. Kutwa alikuwa pamoja na Bwana Abu Talib.
Mwanamke huyu Bibi Fatma alikuwa akitukuzwa sana na Mtume (s.a.w.) Hata siku alipokufa Mtume (s.a.w.) mwenyewe aliteremka kaburini pamoja na mtoto wa marehemu huyu, naye ni Sayyidna Ali.
F. KUJIFUNZA KWAKE
Habari ya kusoma haijakuwa katika Hijaz, kwa hivyo Mtume (s.a.w.) aliondokea kama Makureshi wengine, bila ya kujua kuandika wala kusoma kilichoandikwa. Hajakuwako Kureshi yoyote aliyekuwa akijuwa kuandika wala kusoma wakati huo. Ilimu yao ilikuwa kujifundisha mambo yanayohusu maisha yao ya kibedui, kama vita kutunga mashairi ya kusifu ushujaa wao, na kujifundisha kutoa khutba zinazoweza mara moja kuharakisha watu wapigane bila ya kufikiri.
Mtu wa mwanzo aliejifundisha kusoma na kuandika katika mji wa Makka alikuwa ni Bwana Harb bin Umayya – Babu yake Bwana Muawiya –. Alijifunza kwa watu wa Yaman, na yeye akaja kuwafundisha waliotaka katika mji wa Makka, wakati Mtume (s.a.w.) alipopata Utume walikuwapo watu 6 tu katika Makka waliokuwa wakijuwa kuandika. 4 katika hao waliingia katika Uislamu, wakawa ndio waandikaji “Wahyi” (Aya za Quran). Walikuwa ni Sayyidna Abubakr, Sayyidna Umar, Sayyidna Uthman, na Sayyidna Ali.
SURA YA TATU
MAISHA YA UJANA WA NABII MUHAMMAD (S.A.W.)
MAISHA YA UJANA WA NABII MUHAMMAD (S.A.W.)
Mtume (s.a.w.) aliinukia tangu utotoni kwake juu ya sifa za kijitu kizima, hakupata kufanya vitendo vya utoto umri wake wala hajapata hata kuazimia kuvifanya ila mara mbili tu, mara mbili zote hizo Mwenye-ezi-Mungu alimhifadhi navyo. Kitendo chenyewe alichokiazimia kukifanya katika mara mbili zote hizo na – Mwenye -ezi-Mungu akamuhifadhi nacho – ni kutaka kwenda kukesha katika ngoma za arusi mbili za marafiki zake walioowa katika mji wa Makka. Lakini Mungu aliimpa usingizi mkubwa katika masiku yote hayo mawili hata hakuweza kufumbua jicho, wala kunyanyua miguu kwenda mahali1. Hajapata kuhudhuria hata mara moja katika ibada za kuabudu masanamu wala hakupata kula chakula kilichochinjwa kwa ajili yao. Moyo wake ulichukizwa na hayo na ulichukizwa na kila mambo mengine yaliyo mabaya.
A. SIFA ZAKE
Tangu udogo wake Mtume (s.a.w.) aliondokea na sifa nzuri ambazo hapana hata mmoja katika hirimu zake aliyekuwa nazo zote. Kila sifa zinazohisabiwa kuwa ni njema na Waislamu ndizo alizokuwa nazo Mtume (s.a.w.) tangu utoto wake. Bibi Aysha alipoombwa kutaja sifa za Mtume (s.a.w.) kidogo, alisema hivi: “Sifa zake ni zile sifa nzuri zinazosifiwa na Qurani” na katika Qurani zimetajwa chungu ya sifa zilizo nzuri. Mtume (s.a.w.) mara nyingi alikuwa akisema: “Sikupata kufanya hata siku moja yale mambo waliyokuwa wakiyafanya makafiri”. Kwa hivyo yeye hakupata kuabudu masanamu, kulewa, kuzini, kucheza kamari wala hakumdhulumu mtu kitu chake na kama haya. Lakini alikuwa msema kweli, mwaminifu mpole na mwenye haya na sifa nyingi nyinginezo bora kama hizi. Watu wa Makka walikuwa wakimsifu kwa tabia zake, hata wakampa jina la Muhammad Al-Amin (mwaminifu). Alikuwa hatajikani ila kwa jina la Al-Amin. Wakubwa na wadogo walikuwa wakimhishimu na wakimpa amana zao kuwawekea, hata baada ya Utume pia.
B. SAFARI ZAKE ZA BIASHARA
Makureshi kama tulivyoona, walikuwa watu wa biashara, kila Kureshi mtukufu alipata kufanya kazi hii, safari moja walipokuwa baadhi ya Makureshi wakenda Yaman katika biashara zao, baba yake mdogo wa pili Bwana Zubeyr alimshauri ikiwa atapenda kusafiri. Mtume (s.a.w.) aliridhia akenda naye mpaka Yaman, wakakaa huko muda wa siku tatu tu kisha wakarejea, wakati huu Mtume (s.a.w.) alikuwa mtoto wa miaka tisa.
Hata alipotimia miaka 12 mwaka wa 582, alisafiri tena pamoja na baba yake mdogo mwengine, Bwana Abu Talib, safari hii waliazimia kwenda Sham, lakini walipofiaka Busra – mji wa kusini kabisa katika nchi ya Sham – walikutana na Padri mkubwa wa Kinasara jina lake Bahyra1 ambae alimkataza Bwana huyu kusogea na mwanawe zaidi kuliko hapo, akamwambia: “Mtoto huyu namwona ana alama zote za Mtume aliyeambiwa kuwa atakuja, basi naona ni hatari kubwa akenda Sham asije akauawa na Mayahudi huko. Nakunasihi sana urejee naye au umpe mtu mwaminifu arejee naye nawe wende katika biashara zako”. Bwana Abu Talib alimpa mtu arejee naye Makka naye akaendelea na safari yake.
Huyu Padria Bahyra alikuwa mwanachuoni mkubwa wa Kinasara, na alimbashiri Mtume (s.a.w.) lakini yeye hakuwahi kumwamini alipopata Utume, lakini mwanafunzi wake mkubwa Bwana Salman Al-Farsy Mwajemi mara alipopata habari ya kupata Utume wake alisilimu, na aliusaidia Uislamu katika mambo mengi kama tutavyoona mbele.
Baada ya kutimia miaka 15 Mtume (s.a.w.) aliingia katika kufanya biashara ndogo ndogo yeye na mwenziwe aliyekuwa akiitwa Bwana Saib bin Yazid, lakini biashara yao walikuwa wakiifanyia katika miji iliyokuwa karibu na Makka tu. Alipata sifa kubwa ya uaminifu na ukweli katika biashara zake hizi. Mshirika wake huyu alisilimu siku ilipotekwa Makka, na Mtume (s.a.w.) alifurahi sana kwa kusilimu rafiki yake huyu.
Palikuwa na mwanamke mmoja tajiri sana katika mji wa Makka aliyekuwa akiwakodi watu kuchukuwa bidhaa zake kupeleka Yaman na Sham, mwanamke huyu alikuwa akiitwa Khadija. Uaminifu wa Mtume (s.a.w.) ulipomfikia alitaka naye amchukulie bidhaa yake ndogo ili akamuuzie Yaman. Waliagana kuwa atampa Ngamia wawili. Hata alipomwona karejea na faida kubwa sana kuliko alivyotaraji, alitaka akubali kumkodi tena lakini safari hii alimtaka ende Sham, na ujira wake uwe Ngamia wane. Hii ndiyo mara ya pili yeye Mtume (s.a.w.) kwenda Sham. Vile vile katika safari yake hii alikutana na Mapadri wa Kinasara ambao walimuuliza sana sifa za Mtume (s.a.w.) mtumwa wa Bibi Khadija aliyekuwa amefuatana nae kwa ajili ya kumtumikia. Mtumwa huyo aliwaeleza kila sifa zake, na walipozisikia waliyakinisha na wakamyakinishia kuwa atakuwa Mtume. Mtumwa huyu alimpa habari zake bibi yake wakati aliporejea Makka, ndipo bibi huyu alipomtaka Mtume (s.a.w.) amwoe, safari yake hii ilikuwa katika mwaka 595, naye ni kijana wa miaka 25.
Hizi ndizo safari zake nazo hazikuwa zikichukuwa muda mkubwa, laikini kuna vitabu vyengine vinavyodai kuwa Mtume (s.a.w.) alijifundisha dini hii kwa hao Mapadri aliokutana nao katika safari zake. Lakini tukisoma kidogo sharia ya Uislamu tutaona kuwa nyingi katika amri na hukumu zake hazikushabihiana hata kidogo na hukumu na amri za dini ya hao Mapadri. Kwahakika nyingi katika hukumu za Kiislamu hazikuwa zimefikiriwa wala kuandikwa popote kabla ya vitabu vya Kiislamu. Kuna baadhi ya mashtaka ambayo hata leo bado hazikuandikwa hukumu za kukata mashtaka hayo katika mabuku ya sharia nyengine, zimekwisha tajwa hukumu zake katika sharia ya Kiislamu.
Dostları ilə paylaş: |