F. KUHAMA MASAHABA KWENDA UHABUSHIA
Katika mwaka wa tano – October 615 mwezi wa Rajab – Mtume (s.a.w.) aliwaamrisha watu wake wende katika nchi ya Mahabushia, aliwaambia kuwa Mfalme wa nchi hiyo mwadilifu, anatumai kuwa watapata salama huko, basi akaondoka Makka kila mnyonge asiyekuwa na jamaa wa kumhifadhi. Sayyidna Uthman bin Affan – alipoona kuwa wote hao watakao kwenda huko ni wanyonge tu – aliona kuwa itakuwa bora zaidi kama yeye atakwenda pamoja nao, ili awape nguvu na wasivunjike nyoyo kwa kujiona wao tu ndio walioondoka katika mji wa Makka, Sayyidna Uthaman akamtaka ruhusa Mtume (s.a.w.) ende pamoja na mkewe – Bibi Ruqayya – Mtume (s.a.w.) akampa ruhusa kwa furaha kubwa, wakaondoka kwa siri wakenda mpaka Jidda au bandari nyengine iliyokuwa ikitumika zamani, na huko wakazikuta mashua mbili, wakazikodi mpaka huko wanakotaka kwenda. Watu wenyewe walikuwa 20 tu – 15 wanaume na 5 wanawake1 –.
Walipofika huko mara walikwenda kwa Mfalme wakamtaka ruhusa kukaa katika nchi yake, naye akawapa. Wakakaa huko muda wa miezi mitatu kamili, hata katika mwezi wa Mfunguo mosi, wakapata habari ya owongo kuwa watu wote wa Makka wamesilimu, wakajituta wote kwa umoja wao wakaja Makka, lakini waliyakuta mambo kama zamani na zaidi.
Walipofika Makka walimhadithia Mtume (s.a.w.) na Masahaba wenziwao salama waliyoipata katika nchi ya Mahabushia, kwa hivyo wakafanya hamu nao kwenda2, wakatoka pamoja na wale wa zamani waliokuwa wamerejea, wakarejea tena huko, safari hii walitoka Masahaba 101 – wanawake 18 na wanaume 83 – na mkubwa wa msafara wao safari hii alikuwa Bwana Jaafar bin Abi Talib3 – Kaka yake Sayyidna Ali bin Abi Talib – kwani Sayyidna Uthman hakurejea.
Watu hawa waliondoka kwa siri, hata Makureshi hawakuwaona, hawakupata habari yao ila wamekwishatoka katika mji wa Makka, wakapeleka watu4 kwa Mfalme wa Mahabushia kumwomba awatoe hao Masahaba katika nchi yake na awape wao, lakini yule Mfalme alikataa kabisa ingawa walimwomba sana na wakamhadharisha uovu wa watu hao na kuwa watatia fitna katika nchi yake. wengi katika Masahaba hawa walisalia huko katika Uhabushia mpaka katika mwaka wa 7 A.H. Watu 41 katika hao ndio waliorejea upesi – 33 wanaume na 8 wanawake – .
SURA YA SITA
MAMBO YALIYOTOKEA BAADA YA
MWAKA WA TANO WA UTUME
MAMBO YALIYOTOKEA BAADA YA
MWAKA WA TANO WA UTUME
A. KUSILIMU KWA SAYYIDNA UMAR
Tumeona katika sura zilizopita ya kuwa Sayyidna Umar alikuwa katika watu waliokuwa wakiwatesa sana na kuwadhili Waislamu. Yeye na mjomba wake walikuwa hawana mchezo wa kuwafurahisha zaidi kuliko huo wa kumtesa kila mnyonge aliyesilimu, lakini katika mwisho wa mwaka wa tano1 tangu kuletwa Utume Bwana huyu alisilimu. Alisilimu siku ya Alkhamisi Mfunguo tatu – March 616 – Tangu siku hiyo Waislmau wakaanza kufanya ibada zao nje kwenye Al Kaaba mbele ya Makureshi wote.
B. KUPIGWA PANDE KWA BANI HASHIM NA MAKURESHI
Makureshi walimletea habari Bwana Abu Talib ya kuwa siku fulani watakusanyika katika uwanja wa Al Muhassab ili kutoa amri yao ya mwisho. Kwa hivyo Bwana Abu Talib akawataka Bani Hashim wote waje kusikiliza rai hiyo. Makureshi wakamjia Bwana Abu Talib pamoja na kijana mmoja wa Kikureshi aliyekuwa akiitwa Umara. Kijana huyu alikuwa ni mtoto wa Bwana Walid bin Al Mughyra, alikuwa kijana mwenye sura nzuri mno na shairi hodari mno kuliko Mashairi wote wa kitoto wa Kikureshi. Makureshi wakamwambia Bwana Abu Talib: “Mchukue huyu umfanye mwanao badala ya Muhammad, na sisi tupe Muhammad tumwulie mbali, tupumzike sisi na wewe” Bwana Abu Talib akawaambia: “Muhali hayo. Mnataka nimtwae mtoto wenu nimlishe na nimvike na mumchukue wangu mumchinje? Sikubali kabisa, na lolote liwalo na liwe”. Bani Hashim wote waliokuwako – na vile vile Bani Muttalib – waliyatilia nguvu maneno ya Bwana Abu Talib. Pale pale Makureshi wakaandika mkataba kwamba hapana ruhusa mambo haya matano:-
-
Kusema na Bani Hashim yoyote, wala Bani Muttalib akiwa Mwislamu au si Mwislamu.
-
Kuwauzia chochote wala kununua kitu kwao.
-
Kuoana nao.
-
Kuwasaidia kwa njia yoyote itakayokuwa.
-
Kukaa pamoja nao.
Bwana Abu Talib akainuka akwaambia Bani Hashim na Bani Muttalib kuwa hapana lazima wao kujitia katika taabu hizi zisizowakhusu, lakini wao walikataa ila kuwa pamoja naye, ila Abu Lahb peke yake ndiye aliyeingia upande wa Makureshi. Bwana Abu Talib aliwapa shauri watoke katika mji wa Makka wakakae nje ya mji, wakatoka Bani Hashim wote, wake kwa waume, na Bani Muttalib pia na kila Mwislamu wakenda kukaa mabondeni katika mahala paitwapo “Shiib Abi Talib”. Wakakaa huko muda wa miaka mitatu bila ya kuchanganhyika na Makureshi wengine, mkataba huu uliandikwa katika mwezi wa Mfunguo nne mwaka wa 7 wa kupata Utume – 617 A.D. ukabandikwa juu ya ukuta wa ndani wa Al Kaaba.
Watu hawa walipata taabu kubwa sana ya njaa, hata walikula majani, walikuwa hawauziwi chochote na watu wa Makka, wala hawakuwa wakija mjini ila katika siku za kuhiji tu. Makureshi waliweka majasusi kutazama mtu yoyote asiwapelekee chakula kwa siri, lakini walikuwa wakipelekewa ingawa si cha kuwatosha, pesa zote za kununua vyakula hivi alikuwa akitoa Bibi Khadija, Bwana Abu Talib na baadhi ya matajiri wengine wa Kiislamu. Hata siku moja usiku, Abu Jahl alipokuwa anashika zamu ya kuzuia chakula kuwafikia watu waliokuwa Shiiba Abi Talib, alimwona Hisham bin Amr anaongoza ngamia watatu waliokuwa wamepakia vyakula pomoni, alipotaka kumzuia walipigana. Abu Jahl akakimbia, siku ya pili akawahadithia Makureshi habari ile, na wale wakamhamakia sana Hisham, Bwana huyu akawapa ahadi kuwa hatawapelekea tena, lakini siku ya pili alikutwa tena yeye na mwenziwe Abul Bakhtari, wamechukua vyakula vile vile. Wakapigana na Abu Jahl wakampasua kichwa Abu Jahl akawatisha sana akawaambia: “Leo ni siku yao ya mwisho hawatapata tena chakula. Ama nyinyi mtaona nini Makuredhi watakavyokufanyeni”.
C. KUVUNJWA MKATABA WA MAKURESHI
Yule Hisham lipoona kuwa Makureshi hawatampa nafasi tena kuwapelekea vyakula walioko Shiib, aliona kuwa itakuwa bora kama atapata baadhi ya watoto watukufu wa Kikureshi kama yeye wamsaidie katika jambo hili la kheri, lakini akaona itakuwa bora zaidi akiwaendea wale waliokhusiana kidogo na wale Bani Hashim na Bani Muttalib, akayafikiri majina ya watu wane na yeye awe wa tano. Watu wenyewe ni hawa:-
1. Yeye mwenyewe Hisham bin Amr bin Harith: Baba yake mdogo ni ndugu wa Bwana Abdul Muttalib, ndio maana akawa anawaonea huruma na kuwapelekea vyakula wanavyomtuma. Aliondoka akenda kwa:-
2. Zuhayr bin Abi Umayya: Mtoto wa Shangazi lake Mtume (s.a.w.) – Bibi Aatika bint Abdul Muttalib – akamwambia: “Zuhayr! Unaridhia kula na kunywa na wajomba zako wanalala na wanashinda na njaa? Zuhayr akamwambia: “Tutafanya nini sisi wawili? ukipata wengine mimi tayari” Akaondoka akamwendea.
3. Mut’im bin Adiy bin Naufal: Bwana mkubwa kabisa katika mabwana wa Kikureshi akamwambia: “Mut’im! Unaridhia ziangamie koo mbili za Bani Hashim bin Abd Manaf na Bani Muttalib bin Abd Manaf na wewe Bwana wa Bani Naufal bin Abd Manaf unaona? Huu ndio uungwana? Uko wapi udugu wa Bani Abd Manaf?” akajibu Mut’im: “Nitafanya nini mimi mtu mmoja peke yangu na ukoo wetu peke yetu?” Hisham akamwambia: “Zuhayr bin Abi Umayya yupo pamoja na sisi na hivi nakwenda kutafuta wengine”. Akatoka akenda kwa:
4. Abu Bakhtari bin Harith Al Asady: Mjukuu wa baba yake mdogo Bibi Khadija akamwambia: “Abu Bakhtari! Unaridhia kustarehe na kula na kunywa na Shangazi lako Bibi Khadija anakula majani? Au mnaridhia nyinyi ukoo wa Bani Asad bin Abdil Uzaa bin Kusay kuona matumbo mawili katika matumbo ya Bani Abd Manaf bin Kusay yanaangamia kwa njaa? Huchanganyiki pamoja na mimi na Zuhayr na Mut’im tukaondoa jeuri hii?” akamwambia: “Tafuta mwengine wa tano” Akaondoka akenda kwa:-
5. Zam’a bin Al Aswad Al Asady: Mjukuu mwengine wa baba yake mdogo Bibi Khadija, Babu yake alikuwa katika mabwana wakubwa wa Kikureshi akamwambia kama alivyomwambia Abul Bakhtari. Bwana huyu akaridhia mara moja, akamwambia kuwa atakutana nao usiku huo katika Shiib Al Hajun, baada ya hapo Hisham akawapitia wote wale wa mwanazo, akawaambia wakutane usiku hapo Shiib Al Hajun.
Hata usiku ulipotimia wote 5 walihudhuria bila ya kuchelewa wakayachagua maneno ya kusema, kuonyesha madhara ya mkataba ule, na nani atakayeanza kusema. Hata asubuhi mabwana wa Kikureshi walipokuwa wamebarizi kwenye uwanja wa Al Kaaba, alisimama:
1. Zuhayr: Na jamaa zake wote wapo pale akasema: “Enyi Makureshi tumeridhia kula vyakula vizuri na kuvaa nguo tuzitakazo na Bani Hashim na Bani Muttalib wanaangamia kwa njaa? Wallahi sikai mimi mpaka uchanwe mkataba huu wa dhulma” Abu Jahl akamwambia: “Mwongo utauona vivi hivi uwe ndio kitakataka cha jicho lako, tafuta kazi nyengine ya kufanya”
2. Zam’a akaondoka akamwambia Abu Jahl: “Wewe ndiye mwongo hiki si kitakataka cha jicho la Zuhayr tu, lakini ni cha jicho la kila menye akili”
3. Abul Bakhtar akasema: “Umesema kweli Zam’a”
4. Mut’im akasimama akasema: “Ni kweli maneno yenu na kila atakayesema yasiyokuwa haya ni mwongo”
5. Hisham naye akasimama akawatilia nguvu.
Abu Jahl akasema: “Shauri hii imepikwa tangu jana, lakini Lata (Mungu wao) hatasimama nanyi” mara akainuka Mut’im akaingia ndani ya Al Kaaba akaingoa ile karatasi ya mkataba, akaichanachana.
Mambo haya yalitokea awali ya Mfunguo mosi mwaka wa 10 wa kuja Utume January 6201. watu hawa wote watano hawakuwa Waislamu siku ile, wala hawajasilimu baada yake, ila wawili tu – Bwana Zuhayr na Bwana Hisham – walisaidia kwa njia ya ujamaa tu, mchana ule ule Shiib Abi Talib ilihamwa kila mtu akarejea kwao.
Katika jambo linalokhusu miujiza ya Mtume (s.a.w.) juu ya jambo hili, ni kuwa kabla ya kupatikana habari ya shauri walioiandaa wale watu watano, Bwana Abu Talib alihubiriwa na Mtume (s.a.w.) huko katika Shiib Abi Talib kwamba maandishi yaliyokuwemo katika ule mkataba walioutundika Makureshi Kaabani, yalikuwa yameliwa na mchwa, isipokuwa kila mahala penye jina la Mungu, Bwana Abu Talib – kusikia haya – mara aliwendea Makureshi akawambia maneno aliyosema Mtume (s.a.w.), na akawapa ahadi kwamba kama yatakuwa si kweli hayo maneno aliyoyasema mwanawe, basi yeye ni tayari kuwapa mwanawe wamchinje, kama walivyotaka siku ile ya mkutano.
Ilipofunguliwa Al Kaaba ulionekana ule mkataba umeliwa na mchwa kama alivyosema Mtume (s.a.w.) Lakini wapi! Walizidisha hao Makureshi tashdidi zao.
Mlango wa Al Kaba ulikuwa umenyanyuliwa juu futi 7, wala haukuwa ukifunguliwa ila kwa amri ya mshika funguo za Al Kaaba, naye huwa ni mtu mzima katika ukoo wa Bani Abdid Dar. Hapana mmoja katika wale watu watano waliovunja ule mkataba aliyekuwa katika ukoo huu.
D. KUFA KWA BWANA ABU TALIB NA BIBI KHADIJA
Mara tu baada ya kutoka kule Shiib Abi Talib na kurejea makwao, Bwana Abu Talib alishikwa na ugojwa akafa, alikufa katikati ya Mfunguo mosi mwaka wa 10 wa kuja Utume1. Kwa tarehe ya mwaka wa jua, ulikuwa mwezi wa January 620. Bwana huyu siku alipokufa alikuwa kapindukia miaka 82. kwani alizaliwa mwaka 540. Bwana huyu juu ya kumsaidia Mtume (s.a.w.) kutangaza dini aliyoamrishwa kutangaza, na juu ya kumzuilia kwake na shari za Makureshi, maneno yake wala vitendo vyake havikuonyesha Uislamu. Kwa hivyo wamegawayika Waislamu sehemu mbili katika hukumu ya huyu Bwana Abu Talib.
a. Madhehebu ya Kishia – na baadhi chache katika Suni – yanasema kuwa alisilimu, lakini kwa siri ili asikose hishima yake kwa Makureshi, aweze kupata nguvu za kumhifadhi Mtume (s.a.w.) na shari zao. Ndiyo maana alijidhihirisha kwa maneno na vitendo kuwa hayumo pamoja na Waislamu.
b. Madhehebu yote yaliyosalia yanasema kuwa yeye hakusilimu, kama maneno yake na vitendo vyake vinavyoonesha. Alimsaidia Mtume (s.a.w.) kwa ajili ya ujamaa tu, kama walivyomsaidia Bani Hashim na Bani Muttalib.
Kwa siku ya 3 tangu kufa Bwana Abu Talib, alikufa Bibi Khadija1, bibi huyu alikuwa amefikilia miaka 65 siku hiyo, na Mtume (s.a.w.) alikua mtu wa mika 50 tu, kwani bibi huyu alikuwa mkubwa kuliko Mtume (s.a.w.) kwa miaka 15, siku alipoolewa na Mtume (s.a.w.) alikuwa mwanamke wa miaka 40, na yeye Mtume (s.a.w.) alikuwa kijana wa miaka 25, hivi inaonyesha kuwa alikaa na bibi huyu kwa muda wa miaka 25, bila ya kumwolea mke yoyote wala kumwekea suria hata mmoja, na wakati huo ilikuwa hapana idadi ya wake kuoa.
Vifo vya Bwana Abu Talib na Bibi Khadija vilikuwa msiba mkubwa juu ya Waislamu wote wa siku hizo, maana ni kama tulivyoona, Bwana Abu Talib alimkinga Mtume (s.a.w.) isimfikie shari yoyote waliyokuwa wakimwandalia Makureshi, na Bibi Khadija kwa kuwa aliouna mwendo wa Mtume (s.a.w.) ulio safi kabisa, uaminifu wake na ukweli wake uliokuwa ukipigiwa mfano alimsaidia kwa hali na mali mpaka kufa kwake. Basi hapana la ajabu kwamba kwa Mtume (s.a.w.) na Waislamu wa siku zile vifo vyao vilikuwa zaidi kuliko ukiwa wa yatima aliyeondokewa na baba na mama. Kwa Waislamu mwaka huu unajulikana kwa jina la “Mwaka wa Majonzi”
E. KWENDA MIIRAJI
Moja katika mambo yaliyofanya khitilafu kubwa tangu zama za Masahaba ni “ISRAI” na “MIIRAJI”. “Israi” safari aliyokwenda Mtume (s.a.w.) kwa muda wa saa chache tu katika usiku mmoja tangu Makka mpaka Baitil Maqdis (Jerusalem) na akarejea usiku ule ule. Ama “Miiraji” ni kwenda kwake tangu Baitil Maqdis mpaka kuziona mbingu saba,1 na hazio ni ajabu zote zilizoko huko, khitilafu yao imo katika hiyo safari kuwa imefanyika usiku mmoja au masiku mengi mbali mbali? Tena zilikuwa safari zenyewe zote mbili kwa roho na kiwiliwili chake au moja – Miiraji – ilikuwa kwa roho tupu pasina kiwiliwili cha Mtume (s.a.w.) kwenda? Yaani ilikuwa usingizini kwa kuoneshwa tu. Wengi walisema kuwa zote mbili zilikuwa kwa roho na kiwiliwili, na wengine waliosalia walisema “Israi” tu ndiyo iliyokuwa kwa roho na kiwiliwili ama “Miiraji” ilikuwa kwa roho tupu. Hii ndiyo kauli waliyofata Muutazila2 na baadhi ya wanavyuoni wa sasa. Lakini Suni na Shia na Ibadhi, karibu wote wanasema kuwa hata hiyo “Miiraji” ilikuwa kwa roho na kiwiliwili. Ama “Israi” hapana madhehebu moja yenye kuzingatiwa inayokataa kuwa haikuwa kwa roho na kiwiliwili pamoja, kwani Aya ya kwanza ya Sura ya 17 (Suratul Israi) inaonyesha dhahiri kuwa ilikuwa kwa roho na kiwiliwili3. Mimi kwa kuandika kwangu “kwenda Miiraji” nimekusudia kutaja zote mbili kama wanavyotumia watu wa Unguja. Wao hutumia tamko hili ijapokuwa wanazihadithia zote mbili au “Israi” tupu.
Inahadithiwa kuwa katika usiku wa kuamkia Jumaatatu mwezi 27 Rajab, mwaka wa 12 tangu kuja Utume1 – October 621 – Jibril na Mikail walimletea Mtume (s.a.w.) mnyama mmoja mweupe sana, mrefu kuliko punda na mfupi kuliko farasi, anakwenda kama anaruka, wakamwamrisha ampande ende naye, na wao wakawa wanaruka kwa mbawa zao2 kumfuata – mmoja kuliani na mwengine kushotoni – wakashika njia ya kaskazini kwenda Baitil Maqdis (Falastin – Palastine). Akaonyeshwa mji wa Madina, mlima wa Sinai – ambapo Mungu alimsemesha Nabii Mussa –. Bethlehem – mahala alipozaliwa Nabii Isa – mpaka akafika huko kwenye msikiti wa Baitil Maqdis – ambao ulipata kuwa Qibla cha kuelekea Waislamu – . Huko alikusanyiwa Mitume wote akaonana nao na akawasalisha rakaa mbili jamaa, baadae kila Mtume mtukufu aliinuka akajitaja kwa daraja aliyopewa na Mwenyezi Mungu. Tena wakatawanyika kila mmoja akenda mahala pake.
Hapo ndipo alipoamrishwa kupanda mbinguni (Miiraji) ende akazione zote saba. Samaa (mbingu) kwa kiarabu ni kila unachokiona juu yako, kwa hivyo haijulikani mbingu (Samaa) muradi wake nini. Katika mbingu ya kwanza alimkuta Nabii Adam ya pili Nabii Isa ya tatu Nabii Yusuf, ya nne Nabii Idris, ya tano Nabii Harun, ya sita Nabii Musa na ya saba – ya mwisho – Nabii Ibrahim. Mtume (s.a.w.) alikuwa akimtolea salamu kila mmoja, na wote wakimwitikia kwa furaha na kinyemi.
Kisha akenda kuonyeshwa Moto wa Jahannam na Pepo, alipoombwa na Masahaba wake kusifu alivyoona Peponi, alisema hivi: “Raha na maandalio yaliyoko Peponi ni makubwa sana hata mfano wake halijapata jicho la binaadamu yoyote kuona, wala sikio lake kusikia, wala haujapata kumpitikia katika mawazo yake”.
Khalafu akapelekwa mahala panapoitwa “Sidratil Muntahaa”. Hapo aliletewa Wahyi wa kuamrishwa kusali yeye na umma wake sala 50 za rakaa mbili mbili kila siku, na akaamrishwa kurejea kwenye ardhi tena. Akawa huyo anazishuka mbingu anarejea, alipofika mbingu ya sita Nabii Musa alimwuliza alichoamrishwa kufanya naye akamwambia: “Sala 50 za rakaa mbili mbili kila siku” Nabii Musa akamwambia: “Rejea kwa Mola wako ukatake akupunguzie, kwani hawataweza hayo umma wako” Akawa Nabii Muhammad (s.a.w.) anakwenda na kurejea baina ya Nabii Musa na hapo “Sidratil Muntahaa” akiomba kupunguziwa mpaka zikabaki sala tano1 za rakaa mbili mbili kwanza, kisha walipokuwa Madina zikaongezwa Adhuhuri na Laasiri na Isha, zikawa rakaa nne nne na Magharibi rakaa tatu, na Alfajiri zikawa rakaa zake zile zile mbili.
Mambo yaliyo muhimu aliyoyaona katika safari yake ya usiku ule alipokuwa akenda Baitil Maqdis kutoka Makka ni kuwa Mwenyezi Mungu alimwonyesha adhabu namna kwa namna wanazoteswa watu makaburini mwao kabla ya siku ya Qiyama, kwani kaburi ni kama alivyotwambia Mtume (s.a.w.): “Ima ni bustani katika mabustani ya Peponi au ni shimo katika mashimo ya Motoni” na kama inavyoonyesha haya Aya ya 46 ya Surati Ghafir1. Aya za namna hii za Quran na Hadithi nyingi za Mtume (s.a.w.) zinaonyesha kuwa mtu akitiwa kaburini halali tu na ikawa ndiyo basi, lakini tangu saa anapotiwa kaburini mpaka siku ya kufufuliwa yeye ima yumo katika raha tupu au adhabu tupu au hivi na hivi, kwa kiasi cha wema mtupu wa mtu yule au ubaya wake mtupu au kuchanganyisha kwake wema na ubaya2, na kila dhambi ina teso lake makhsusi na wakati wake makhsusi. Basi katika namana za mateso alizoonyeshwa usiku ule wa MIIRAJI ni:-
1. Mateso ya wasiosali: Vinapondwa vichwa vyao kwa marungu, na kila vikipondwa hurejea vizima mara ya pili, ili vipate kupondwa tena, na vivyo hivyo mchana na usiku.
2. Mateso ya wenye maasi ya tupu zao: Zinawaka moto tupu hizo wala hazishi, kwani kila zikiungua, Mwenyezi Mungu huzibadilishia ngozi nyengine.
3. Mateso ya wasiotoa Zakaa: Wamevalishwa vitema tu, wanapita wakichungwa utupu katika makonde ya miti ya michongoma yenye miba kuliko Mkongoshare na uchungu kuliko mishubiri mani.
4. Mateso ya wenye kutoa mawaidha mema wala wenyewe hawayafuati: Zinakatwa ndimi zao vipande vipande kwa mikasi ya chuma, wala hazishi kila zikikatwa huota tena.
5. Mateso ya wenye kusema watu: Hao huwa na mwasho mkubwa na huumbiwa makucha ya shaba yenye ncha kali, wakawa wanajiparura na kujikwaruza vifua vyao kwa makucha hayo. Na mateso namna namna ya maasi mengine.
Mtume (s.a.w.) akateremka akafika Baitil Maqdis akapanda “Buraqi” wake (jina la yule mnyama aliyekuwa kapanda), akashika njia akarejea Makka –Jibril kuliani na Mikail kushotoni – . Njianai akaanza kukutana na misafara ya mwisho ya Kikureshi iliyokuwa imekawiya kurejea Sham. Tumeona zamani kuwa Makureshi walikuwa na dasturi ya kwenda kufanya biashara Shama siku za joto, na Yaman siku za baridi, na vile vile tunajua kuwa misafara mingi ya kijangwani huwa ikenda usiku, mpaka jua linapokuwa kali mchana ndipo hutua. Basi Mtume (s.a.w.) kwanza alikuta katika Rauhaa (jina la mahala) msafara wa Makureshi mmoja mtupu wenyewe walikuwa hawapo, akashuka akanywa maji yaliyokuwa katika gudulia la hema moja (kusudi ya kuweka alama), kisha akawakuta wenyewe wamekwisha mkamata ngamia aliyekuwa kawakimbia. Akawatolea salamu na huku anakwenda mbio na “Buraqi” wake. Hawakushitukia ila kuhisi vumbi la upepo tu, kisha akaukuta msafara mkubwa mahali pengine, kwa kishindo cha “Buraqi” msafara wote ulitawanyika, na ngamia mmoja akaanguka akavunjika. Tena akaupita msafara mwengine katika mji wa Tan’im (meli 3 kutoka Makka), akaufanyia ishara nao vile vile, ili apate ushahidi mwingi atakapohadithia habari hii.
Karibu ya Alfajiri alifika Makka, akasali rakaa mbili za asubuhi yeye na watu wa nyumbani mwake. Kisha akamwita Bibi Ummu Hani (dada yake Sayyidna Ali) akamwambia: “Ummu Hani! Unajua kuwa baada ya kwisha kusali na nyinyi sala ya usiku nemekwenda Baitil Maqdis?” Akamjibu: “Kisha umepembazuka pamoja na sisi hapa Makka?” Akamwambia: “Naam na hivi nakwenda kuwapa habari Makureshi”. Yule mwanamke akamwambia Mtume (s.a.w.) asende kuwahadithia Makureshi kwani watamsuta na kumzomea, lakini hakukubali alitoka akenda mpaka kwenye Al Kaaba kuwangoja Makureshi waje, mara akaja Abu Jahl –Firauni wa Kikureshi – akamwambia Mtume (s.a.w.) kwa shere: “Je Muhammad liko jipya leo?” Akamjibu: “Lipo jana usiku nalipelekwa Baitil Maqdis kisha nikarejea” Abu Jahl akamwambia: “Nikiweta Makureshi wengine utawahadithia haya? Au unanambia mimi peke yangu?” Akamwambia: “Wete” Abu Jahl akanyanyua sauti kuweta. Hazikutimia dakika kumi na tano ila uwanja wote ulisaki watu Waislamu na makafiri, Mtume (s.a.w.) kusema tu kuwa alikwenda Baitil Maqdis usiku uliopita, mara Makureshi waliinuka wakapiga makofi na kudunda miguu na kuzomea na kupiga vikorombwe, kuonyesha kuwa uwongo wake umezidi, hata baadhi ya Waislamu waliingia upande wa Makureshi wakamkadhibisha Mtume (s.a.w.), mara akaja yule Mut’im bin Adiy aliyempa amani Mtume (s.a.w.) kukaa Makka, akamwambia Mtume (s.a.w.): “Muhammad! mambo yote yako kabla ya leo yalikuwa mepesi. Ama ya leo uwongo wako ni dhahiri! Mimi nashuhudia kuwa wewe ni mwongo. Baitil Maqdis tunakwenda kwa muda wa miezi miwili, unajidai umekwenda huko na kurudi kwa usiku mmoja? Leo mwisho wangu na wewe, huna amani yangu katika mji wa Makka”.
Wakatoka watu kwenda kumhadithia Sayyidna Abubakr maneno aliyosema Mtume (s.a.w.) ili apate kurejea ukafirini naye, kama walivyorejea. Sayyidna Abubakr akawavunja akasema: “Kama kweli anadai hayo, basi mimi nimemsadiki. Mimi namsadiki kwa habari za mbinguni anazoshushiwa na Mungu kila siku, seuze za hapo Baitil Maqdis”. Khalafu akatoka akaja hapo alipo Mtume (s.a.w.). Akamwona kazongwa anaulizwa aeleze sifa za mjengo wa msikiti wa Baitil Maqdis, na yeye hajapata kwenda huko hata mara moja. Lakini Mwenyezi Mungu alimfanidishia1 sura ya msikiti huo mbele ya macho yake, akawa anausifu kama upo mbele yake na Sayyidna Abubakr anasema “Sadakta, sadakta” – unasema kweli unasema kweli – Tena wakamwuliza habari ya misafara yao naye akawajibu habari zake zote, na alama alizowaachia wasafiri hao na mahala alipowakuta. Makureshi wakasema: “Ngojea ikija hiyo misafara yakathibitika haya papo hapo tutakuamini sote” hata siku ilipokuja misafara hiyo na yakathibitika aliyoyanena aliruka Walid bin Mughyra akanena: “Wallahi! Huyu mchawi mkubwa wala hatumwamini mchawi sisi” wote waliokuwa hapo walisema: “kasema kweli Walid, sisi hatutamwamini mchawi, basi wakatawanyika wakenda majumbani mwao.
Siku hii ndipo Mtume (s.a.w.) alipompa Sayyidna Abubakr sifa ya “Siddiq” – yaani mwenye kusadiki mno kuliko watu wote – na tangu siku hiyo akawa anaitwa Abubakr ni Siddiq. Yeye ndiye bora kuliko Masahaba wote wa Mtume (s.a.w.) kwa makubaliano ya madhehebu yote ya Uislamu ila madhehebu ya Shia na Muutazila wa Baghdadi, yasemayo kuwa Sayyidna Ali ndiye aliye bora kuliko wote.
Huku kwenda “Israi” kwa roho na kiwiliwili tangu Makka mpaka Baitil Maqdis na kurejea tena mara ya pili kwa muda mdogo, si muhali hili, kwani Wanavyuoni wakubwa wa Ulaya wanaoshughulika na mambo ya roho (Spiritualists), wamethibitisha kuwa hivyo wanavyoviita roho (Spirits) vinaweza kuwaletea vitu viliyoko miji ya mbali kwa muda mfupi. Kwa mfano walipata kufanyiwa mtihani mara nyingi katika vyumba vitupu visivvyokuwa na ndudu ya kitu – pamoja na milango kufungwa – na wakaweza kuwaletea watu waliokuwa hapo maua yaliyotoka katika nchi ya Machina. Basi wakiwa binadamu wanaweza kufanya haya, Mola hawezi zaidi? Vile vile kuuona ule msikiti wa Baitil Maqdis naye yupo Makka si ajabu, kwani binadamu wamekwisha vumbua “Television” ambayo si inaweza kusikilizisha sauti za viumbe vilivyoko mbali na wewe (kama radio), bali inakuonyesha sura zao khasa. Kwa hivyo yote yanathibitisha ukweli wa Hadithi hii ya Miiraji. Anasema Mungu katika sura ya 41 (Surat Fussilat):
Tutawaonyesha ukweli wa dini yetu katika pande
Dostları ilə paylaş: |