Maisha ya nabii



Yüklə 0,69 Mb.
səhifə10/15
tarix10.12.2017
ölçüsü0,69 Mb.
#34382
1   ...   7   8   9   10   11   12   13   14   15

D. VITA VYA HUNAYN
Hunayn ni jangwa liliyoko Kusini ya mashariki ya Makka. Katika mahali hapo yalikusanyika matumbo ya kabila mbili kubwa za Waarabu – Bani Hawazin na Bani Thaqyf – Hawa wa mwanzo walikuwa Mabedui, na hawa wa pili wakikaa kwenye mji. Watu hawa walipoiona Makka imekwisha kuingia mikononi mwa Waislamu, waliona hapana mji mwengine mkubwa wa kuja kupigwa ila mji wa Taif – mji mkubwa wa Bani Thaqyf – Kwa hivyo wakakusanyika wakubwa wa Bani Hawazin na Bani Thaqyf wakafanya shauri ya kwenda kuwapiga wao Waislamu, kabla wao kuwajia. Wakaagana kukusanyika hapo Hunayn. Bani Hawazin wakamchagua Malik bin Auf kuwa mkubwa wao na Bani Thaqyf wakamchagua Kinana bin Abd Yalil – mmoja katika wale wakubwa wa mji wa Taif walioamrisha watu wao kumpiga Mtume (s.a.w.) alipokuja kufundisha Dini katika mji wao – Hazikupita siku nyingi ila majeshi ya Bani Thaqyf yalikuwa yamekwishakufika hapo Hunayn, walikuwa si chini ya watu 30,000! Hawa Bani Hawazin walikuwa wakisifika mno kwa uhodari wa kupigana kwa mishare.
Miongoni mwa watu 30,000 hawa nusu yao walikuwa wanawake na watoto. Kwani hawa Bani Hawazin walikuwa mabedui wanaohangaika kila mahali na wake zao, watoto wao na wanyama wao na kila wanachokimiliki, kwa hivyo walipokuja hapo Hunayn walikuja na watu wao wote, wakawalazimisha wenziwao – Bani Thaqyf – waje na wake zao watoto wao wanyama na mali yao mengine vile vile. Mkubwa wa Kihawazin alikuwa akiitakidi kuwa maadam kila mtu kaja na mkewe na wanawe basi hataweza kukimbia vita vitakaposhitadi, bali atasimama viyo hivyo kupigana wasije watu wao wakatiwa mikononi na adui zao.
Mtume (s.a.w.) alipopata habari hii ya Bani Hawazin na Bani Thaqyf, alipeleka majasusi watatu kutazama kila jambo lao. Majasusi hawa waliporejea walimhadithia Mtume (s.a.w.) kila kubwa na dogo lililokhusu jeshi hili. Mtume (s.a.w.) akalikusanya jeshi lake alilotoka nalo Madina kuja kuipiga Makka, nalo lilikuwa lina watu 10,000 – 700 Muhajir, 4,000 Ansar na 5,300 katika kabila nyengine za Kiarabu zilizokuwa zimesilimu – Makureshi walipomwona Mtume (s.a.w.) anazatiti kupigana na Bani Hawazin nao pia walijikusanya wakatimia watu 2,000 wakampa habari Mtume (s.a.w.) ya kuwa watamfuata watu elfu mbili kumsaidia katika vita hivyo. Miongoni mwao kuna waliozimia kwenda wakapate ngawira tu au wakabaraganye (wakaparaganye) utaratibu wa jeshi la Kiislamu au wakapate nafasi kumpatia wasaa Mtume (s.a.w.) wa kumwua kwa ghafla, kwani wengi katika hawa walikuwa hawakusilimu bado. Ilivyokuwa sasa watu wamezidi – na Mtume (s.a.w.) hana silaha za kutosha – Mtume (s.a.w.) aliazima baadhi ya silaha kwa wakubwa wa makafiri wa Kikureshi, wengine walikuwa bado hawakusilimu. Aliazima nguo za chuma 100 kwa Safwan bin Umayya bin Khalaf, na akaazima mikuki 3,000 kwa Naufal bin Harith bin Abdil Muttalib.
Hata mwezi 10 Mfunguo mosi mwaka wa 8 A.H. (February 630) Mtume (s.a.w.) alitoka na jeshi lake la watu 12,000 kwenda kuwashambulia hao maadui kabla wao hawajashambuliwa nao. Mtume (s.a.w.) hakupanda farasi safari hii, bali alipanda nyumbu wake aliyekuwa akiitwa “Shahbaa” hao wakashika njia wakenda zao upande wa Hunayn.
Huku nyuma Bani Hawazin na Bani Thaqyf wakapata habari kuwa Mtume (s.a.w.) anakuja kuwashambulia. Hata walipojua kuwa wapo karibu na kufika, walikwenda wakawazingia kwenye njia ya majabalini (Pass) ambayo walijua kuwa lazima wataipita. Waliizingia njia hiyo kwenye midomo yake yote miwili na wakawapanga vizuri wapigaji mishare juu ya vilele vyake. Hata wakati wa Alfajiri Mtume (s.a.w.) alifika njia hiyo, akawa anaingia yeye na watu wake, na nje bado kiza.
Hawakuwahi kuchomoza barabara upande huu wala hawakuwahi kumalizika upande ule ila mara walishambuliwa kwa panga na mikuki mbele na nyuma, na kwa mishare juu yao – husemi ila mvua – Muda si muda majeshi ya Makureshi yakaingia mbioni yanakimbilia makwao Makka. Kivangaito kikaingia. Watu 2,000 wote wanakimbia wakati mmoja bila ya nidhamu na huku wanapigwa! Wale Waarabu 5,300 waliokuja na Mtume (s.a.w.) – kuona Makureshi wanakimbia – nao wakawaamrisha watu wao kukimbia vivyo hivyo. Maji yakazidi unga. Muhajir na Ansar wakadahadari wasijue la kufanya, hawaoni kitu ila ghasia tu na kusukumwa huku na huko, wala hawamjui Mtume (s.a.w.) yuko wapi, kakimbia? – nao wapate kukimbia – au yupo hapo wapate kusimama kumpigania? Kila mmoja kadahadari hajijui wala hajitambui wala hajui la kufanya. Wengi wakaingia mbioni nao, na wengine wakajibanza walipo, watazame nini kitajiri.
Muda wa ghasia zote hizi Mtume (s.a.w.) alikuwa kakaa juu ya nyumbu wake na Masahaba 12 wanaume na 1 mwanamke wamemzunguka wanamlinda, hata ukucha usimpate. Katika hao ni baba yake mdogo – Bwana Abbas bin Abdul Muttalib – na mtoto wa baba yake mdogo, Bwana Abu Sufyan bin Harith ambaye alikuwa kashika khatamu ya yule nyumbu, ili asije akafyatuka akenda mbio na Mtume (s.a.w.) juu yake, kumalizika kivangaito hiki tu Mtume (s.a.w.) alimwamrisha Bwana Abbas apige kelele kuweta Muhajirin na Ansar tu. Bwana Abbas akanyanyua sauti akaanza kuweta haukumalizika ukulele wa tatu ila watu si chini kuliko 300 wamekwisha kufika kwa Mtume (s.a.w.). Pale pale Mtume (s.a.w.) aliamrisha kuwashamnbulia maadui zao, na huku Bwana Abbas anazidi kuweta wengine, wakati huu Waislamu walijikaza barabara, wakafumba macho wakakaza meno, ikawa hapasikilizani chochote ila sauti za silaha tu. Mtume (s.a.w.) akafanya kama alivyofanya katika vita vya Badr. Alichukua gao la mchanga akalisomea kisha akalivurumisha upande wa maadui, halikupatikana jicho lolote katika macho yao ila liliingiwa na mchanga huo, likawa linawasha kama pilipili kichaa, muda si muda wale maadui wakaanza kukimbizana mbio na kuacha wake, watoto, wanyama na kila chao! Waislamu wakawa wanawafuatia na kuwaua, kuwateka na kuwapokonya mali yao. Hawakuwahi kurejea baadhi ya Waislamu waliokuwa wamekimbilia mahala pa mbali kidogo ila walivikuta vita vimekwisha, na mateka wametiwa pingu, wamesimama mbele ya Mtume (s.a.w.). Mtume (s.a.w.) akaamrisha mateka na ngawira zipelekwe kwenye mtaa wa Jiirana ambao unapata meli 20 toka Makka.
Baada ya kupumzika kidogo zikateremshwa Aya 3 zilizopo katika Sura ya 9 (Suratut Tawba). Nazo ni:
Hakika tumekunusuruni1 katika mahali pengi na siku ya Hunayn (pia), wakati ulipokupandisheni kichwa wingi wenu, usikusaidieni chochote, bali ilidhiki ardhi juu yenu, kisha mkageuza migongo yenu na huku mnakimbia.

(Aya ya 25).


Kisha akashusha Mwenyezi Mungu rehema yake juu ya Mtume wake na juu ya Waislamu na akashusha askari ambao hamkuwaona, na akawaadhibu makafiri, na haya ndiyo malipo ya makafiri.

(Aya ya 26).


Kisha akakubali Mwenyezi Mungu toba ya anayemtaka katika waja wake, na Mungu ndiye mwenye msamaha mkubwa na mwenye rehema nyingi1.

(Aya ya 27).


Baadaye Mtume (s.a.w.) na watu wake wakaondoka kwenda Jiirana kugawa ngawira, alipofika alikuta ngawira ambayo hajapata kuiona maisha yake, alikuta mateka 600, ngamia 24,000, mbuzi 40,000 na fedha yenye uzito wa ratli 250! Ngawira hii ikagawiwa sehemu 5. Sehemu moja – ikawa ya Mtume (s.a.w.) pamoja na wengine waliotajwa ndani ya Quran – na sehemu 4 zilizosalia zikagawiwa wale waliosimama kupigana, kila aliyekuwa akipigana kwa miguu alipata ngamia 4 na mbuzi 40, na kila aliyekuwa akipigana juu ya farasi alipata ngamia 12 na mbuzi 120. Baadhi ya watu wengine walipata mateka wa kibinaadamu khasa. Ama katika ile sehemu yake, Mtume (s.a.w.) aliwachagua baadhi ya wakubwa wa Kiarabu ambao Uislamu wao haukuwa na nguvu sana bado, akampa kila mtu sehemu kubwa. Miongoni mwa hao aliowapa ni mabwana hawa:-
1. Abu Sufyan: Bwana mkubwa wa Kikureshi. Alimpa ngamia 100 na ratli mbili unusu za fedha.
2-3. Yazid na Muawiya: Watoto wa huyu Abu Sufyan, alimpa kila mmoja ngamia100 na ratli mbili unusu za fedha. Baba yao alimwomba Mtume (s.a.w.) awape kama alivyompa yeye, na Mtume (s.a.w.) akakiri.
4. Hakim bin Hizam: Bwana mkubwa wa pili wa Kikureshi wakati huo. Yeye alipewa ngamia 300 tu.
5. Safwan bin Umayya: Aliyewaazima Waislamu nguo zake za chuma, Mtume (s.a.w.) alimjazia bonde zima – lililokuwapo hapo – ngamia na mbuzi. Bwana huyu akasilimu papo hapo. Akasema: “Wallahi! Hafanyi ukarimu huu ila Mtume (s.a.w.).”
6. Suhayl bin Amr: Aliyeandikiana na Mtume (s.a.w.) mkataba wa Hudaybiya, kama tutakavyouona katika mlango unaokuja. Huyu alipewa ngamia 100.
7. Aqraa bin Habis: Mkubwa wa Bani Tamim waliokuwa pamoja na Mtume (s.a.w.). Alipewa ngamia 100.
8. Uyayna bin Hisn: Mkubwa wa Bani Fazara waliokuwa pamoja na Mtume (s.a.w.). Mtume (s.a.w.) alimpa ngamia 100.
9. Abbas bin Mirdas: Mkubwa wa Bani Sulaym waliokuwa pamoja. Mtume (s.a.w.) alimpa ngamia 100.
Na wakubwa wengine wengi wengineo kila mmoja alipata ngamia 100 au 75 au 50, au 25, kwa mujibu wa cheo na ukubwa wake, na idadi ya watu wake aliokuja nao katika kusaidia.
Wakati alipoanza kuwagawa mateka, mwanamke mmoja katika wale aliwaambia wakubwa wa vita ya kuwa yeye ni ndugu yake Mtume (s.a.w.) wa kunyonya, na akawaomba wamwachie. Wale wasisadiki bali walimchukua wakenda naye kwa Mtume (s.a.w.) wakamhadithia habari yake. Mtume (s.a.w.) akamsaili, hata ilipombainikia kuwa kweli yeye ndiye yule ndugu yake wa kunyonya aliyekuwa akiitwa Shaimaa – Mtume (s.a.w.) aliinuka mahali alipokuwa kakaa akajitandua shali yake akamtandikia akalie – akamfanyia hishma kubwa, akamwuliza habari ya mama yake yule wa kunyonyesha (Bibi Halima) na baba yake, naye akamjibu kuwa wote wawili wapo. Baada ya haya Mtume (s.a.w.) akamkhiyarisha kukaa pamoja naye au kurejea kwao. Akakhiyari kurejea kwao majangwani kuliko kukaa kwenye miji, Mtume (s.a.w.) akampa ruhusa kwenda zake, baada ya kumpa watwana wawili na mjakazi mmoja na chungu ya ngamia na mbuzi. Na yule mama yake Mtume (s.a.w.) Bibi Halima, akaja na Mtume (s.a.w.) akamfanyia kama haya na zaidi.
Baada ya wiki nzima kupita, wakaja wakubwa 14 wa Kibani Hawazin kubainisha kuwa wao na watu wao wote wanasilimu, na wanaomba warejeshewe watu wao, Mtume (s.a.w.) akawajibu kuwa yeye aliwangoja sana kabla ya kuwagawa, lakini alipokuwa hajawaona alikata tamaa ya kuja kwao, ndipo alipowagawa. Pale pale akawakusanya Masahaba akawakhutubia kuwaambia habari walioleta wakubwa wa Kibani Hawazin. Akawaambia: “Hawa ndugu zetu wa Kibani Hawazin wamekuja kwenu wanatubia kwa makosa yao, na wanaomba warejeshewe wake zao na watoto wao. Mimi naona rai nzuri kuwapa watu wao hao kila waliokuwa wamenistahikia mimi na jamaa zangu – Bani Abdul Muttalib – basi nawaamrisha sasa hivi warejeshwe. Na mwenye kupenda miongoni mwenu kufanya haya na afanye, na malipo yake atayapata kwa Mungu. Ama anayetaka sharti tumlipe kitu basi nitampa ngamia 6 kwa kila mateka mmoja aliyenaye na akamtoa kuwarejeshea wenyewe.”
Wakubwa wa Waarabu wote waliokuwako hapo waliinuka wakasema kuwa wao na watu wao wameridhia kuwatoa mateka hao pasina kutaka malipo yoyote. Ila wakubwa wa kabila tatu walikataa kuwatoa bure, wakubwa wenyewe ni hawa:
Aliinuka Aqraa bin Habis – mkubwa wa Bani Tamim – akasema: “Ama mimi na watu wangu haturidhii ila kwa kupewa badali” tena akainuka Uyayna bin Hasn – mkubwa wa Bani Fazara – akasema kama alivyosema mkuwa wa Bani Tamim. Tena akainuka Abbas bin Mirdas – mkubwa wa Bani Sulaym – akasema kama walivyosema wale wenzake wawili. Lakini pale pale walimzukia Bani Sulaym wote wakasema: “Hutuwafiki rai yako”. Tutawatoa mateka wetu bure kama alivyofanya Mtume (s.a.w.) na Muhajir na Ansar na wengineo”. Abbas huyu akasema kwa hamaki sana: “Sijapata kuona watu kama nyinyi! Mnanivunja mkubwa wenu mbele za watu wote hawa? Msingefanya kama walivyofanya Bani Tamim na Bani Fazara? Huu ndio udhalilifu leo”. Yeye kumkhalifu Mtume (s.a.w.) haoni vibaya, anaona vibaya kukhalifiwa yeye.
Baadaye Mtume (s.a.w.) akawalipa wale waliokataa kutoa mateka wao bure, kisha akawapa Bani Hawazin watu wao wakenda zao kwao, na wengi katika wao walikuwa wamekwisha kuupenda Uislamu, wakaazimia kuutangaza kwa kila namna kwa jamaa zao. Mtume (s.a.w.) alipowatoa mateka wa Bani Hawazin alikataa kuwatoa wake na watoto wa Malik bin Auf yule mkubwa wao. Akasema hawatoi mpaka mwenyewe ende kuwaomba au kuwakomboa, naye ampe.
Huyu Malik – alipojiona wameshindwa – hakwenda majangwani kwao, kama wenziwe Bani Hawazin, lakini aliwafuata Bani Thaqyf wakenda kujitia kwenye ngome za Taif zilizokuwa zikisifiwa kwa imara yake na kwa ustadi wa kujengwa kwake na kwa wingi wa vyakula vilivyokuwamo ndani yake. Mtume (s.a.w.) na Masahaba zake walizihusuru ngome hizi muda wa siku tatu wasiweze kuziingia, kisha ndipo walipokwenda Jiirana kugawa ngawira zao za Hunayn, wala wasizirejee ngome hizo, wala Bani Thaqyf hawakutoka ndani huko, kwani wale wenzao Bani Hawazin sasa wamekuwa adui zao, watawakamata wawapeleke kwa Mtume (s.a.w.). Huyu Malik kupata habari hii ya kuwa watu wake hawataachiwa ila ende mwenyewe kuwaomba, alifanya taratibu mpaka akatoka kwenye zile ngome akamwendea Mtume (s.a.w.) katika mtaa wa Jiirana. Mtume (s.a.w.) alifurahi kumwona, akamrejeshea wake zake watoto na mali yake, na akampa ngamia 100, na akamfanya mkubwa wa kabila yake kama alivyokuwa zamani na akawa Mwislamu. Baada ya vita hivi Mtume (s.a.w.) hakupigana tena vita vikubwa na kabila za Waarabu, kwani zote zilianza kumwogopa kweli kweli.
Baada ya siku 13 kupita, Mtume (s.a.w.) aliondoka kwenye mta wa Jiirana, naye kanuia kwenda kufanya Umra (Hija ndogo) Makka. Akafika Makka akafanya Umra yake kisha akarejea Madina pamoja na Masahaba zake, na wale Waarabu wakarejea kwenye nchi zao na chungu ya mali. Makureshi wakasalia Makka kama zamani, kila mtu na ukubwa na hishma yake, ila wengine walikuwa Waislamu na wengine wachache kabisa bado walikuwa makafiri. Lakini haukupita muda mkubwa ila walisilimu.


SURA YA KUMI NA MOJA

KUPATANA MTUME (S.A.W.) NA MAKURESHI
KUPATANA MTUME (S.A.W.) NA MAKURESHI
A. SULHU YA HUDAYBIYA
Hudaybiya ni mahali karibu na Makka. Mahali hapo ndipo walipoandikiana shuruti za sulhu Mtume (s.a.w.) na Makureshi. Sababu ya kutokea sulhu hii ni: Waislamu wote walioko ulimwenguni wanajua ya kua nguzo za Uislamu ni tano. Lakini nguzo hizo hazikuwajibika zote mara moja: zilikuwa zikiwajibishwa moja baada ya moja mpaka zikatimia tano. Nguzo ya awali iliyowajibishwa ni kukiri kuwa Mungu ni mmoja na Bwana Muhammad (s.a.w.) ni Mtume wake. Nguzo hii iliwajibishwa tangu siku ya awali ya Uislam. Khalafu mwaka wa 12 wa Kiislam1 ziliwajibishwa sala 5 tunazozisali. Mpaka katika mwaka wa 2 A.H. 623 December — kulipasishwa kutoa zaka2, na baada ya mwezi mmoja kukapasishwa kufunga Ramadhan. Ama kwenda kuhiji hakukupasishwa ila katika mwaka wa 6 A.H. -628 A.D. na hii faradhi ya Hija inagawanyika sehemu mbili — sehemu moja huitwa Hija na sehemu ya pili huitwa Umra. Umra inaweza kufanywa katika miezi yoyote uitakayo, ama Hija haisihi ila katika Mfunguo mosi na Mfunguo pili na Mfunguo tatu tu3.
Basi baada ya kufaridhiwa Hija, Mtume (s.a.w.) alitoka na watu 1,400 kwenda nao Makka kutekeleza faradhi ya Umra kwanza. Kila mmoja katika watu hawa alihirimia na akachukua mnyama wake kwenda kumchinja Makka. Kuhirimia ni kuvaa nguo za Hija. Walipofika pahali panapoitwa Usfan, Masahaba walipata habari ya kuwa Makureshi wametoka na jeshi kukutana nao njiani wapate kuwazuilia kuingia Makka kwenda kufanya hiyo Umra. Mtume (s.a.w.) aliwaamrisha watu wake wageuze njia ili wasikutane na Makureshi na aliwaamrisha wakutane kwenye mtaa uliokua ukiitwa Hudaybiya. Walipofika hapo Masahaba walitua na wakapiga hema zao wanangojea amri ya Mtume (s.a.w.).
Muda si muda alikuja mjumbe aliyeletwa na Makureshi kuja kumwuliza Mtume (s.a.w.) sababu inayomleta Makka yeye na jeshi hilo kubwa. Mtume (s.a.w.) akambainishia nia yao na sababu iliyomleta yeye na watu wake huko Makka, na akamtuma awaambie Makureshi kuwa anawaomba wampe ruhusa aingie afanye Umra muda wa siku 1 tu, khalafu aondoke aende zake – kama walivyokua wakifanya Waarabu wengine –. Mjumbe huyo akarejea kwao akawahadithia Makureshi maneno aliyosema Mtume (s.a.w.), na yeye akatoa shauri kuwa ni bora kumwachia kuja kutekeleza hiyo Umra. Makureshi wasimsadiki wala wasikubali rai yake. Bali walipeleka wajumbe wengine kwa wengine kuja kumtisha Mtume (s.a.w.) na watu wake kuwa Makureshi watawajia kuwasagasaga. Lakini matisho yao hayakufaa kitu. Kila mjumbe aliporejea kwao aliwapa shauri ya kuwaachia kuingia lakini wazee wa Kikureshi walikataa kabisa, wakaona ni aibu kuwaachia washinde wao kuingia katika mji wao.
Mtume (s.a.w.) alipowaona wajumbe wa Kikureshi wote hawakufaa kitu, alimpeleka mjumbe wake aliyekuwa akiitwa Bwana Khirash. Bwana huyu kufika Makka Makureshi walimkamata wakamfunga na wakamkata miguu ngamia aliyekuwa kampanda. Baada ya kumtaabisha kwa muda mrefu walimwachia ende zake bila ya jawabu yoyote. Huyu Bwana akarejea kwa Mtume (s.a.w.) akampa habari ya mambo yote yaliyompata. Mtume (s.a.w.) akatafuta mtu mwengine wakumpeleka kwa Makureshi akawayakinishie ya kuwa hakujia vita, pasionekane mtu yoyote anayeweza kwenda huko salama na kurejea salama bila ya kufinywa hata ukucha ila Sayyidna Uthman bin Affan, kwani alikuwa mzalendo wa kweli katika mji wa Makka. Alikuwa Bani Umayya kwa baba na mama, na hao wazee wake wote ndio waliokuwa “Mashekhe” wa Kibani Umayya ambao hakivunjwi kijiti katika mji wa Makka ila kwa amri yao. Sayyidna Uthman akaupokea utumwa huu kwa furaha kubwa, akenda mpaka huko Makka, akawafikshia ujumbe wa Mtume (s.a.w.). Wazee wake walikataa kufuata shauri yake na wakamtia maneno barabara arejee katika dini ya wazee wake. Sayyidna Uthman alipokataa naye shauri yao walimtia katika nyumba wakamfunga muda wa siku 3 ili apate kuzidi kufikiri muda wa siku hizo.
Baada ya kungojewa kwa muda mrefu asionekane, huku nyuma ulizuka mshindo wa kuwa Sayyidna Uthman kauawa. Mtume (s.a.w.) alikasirika sana kuona Makureshi wamemwua mjumbe wake – na mjumbe hauawi –Mtume (s.a.w.) aliinuka na kutoa khutba, akasema ya kuwa yeye lazima atakwenda Makka akapigane na Makureshi kwa ajili ya kulipiza kisasi cha Sayyidna Uthman, na anayetaka kumfuata na ainuke ampe mkono wa kumwahidi kuwa atakwenda pamoja naye, Masahaba wote 1,400 wakainuka kumpa mkono kuwa watakuwa pamoja naye katika kwenda huko. Mtume (s.a.w.) akasema: “Na lau Uthman alikuwa hapa pamoja nasi mkawa mnaniahidi kuwa pamoja nami katika kufanya jambo lolote naye angeliniahidi kama mnavyoniahidi. Basi mkono wangu nauambatisha na huu ili iwe kama Uthman ananipa naye wake. Mkono wangu huu badala ya mkono wake, kwani yeye amekwenda kutekeleza utumwa wangu.” Baada ya kwisha kuahidi huku, mara walimuona Sayyidna Uthman huyo anachomoza. Waislam wote walifurahi furaha kubwa kumwona mwenzao hakuuawa, na kujiona kuwa wote wameshamwahidi Mtume (s.a.w.). Mwenyezi Mungu ametaja kutoa ahadi huku katika aya ya 18 ya sura ya 48. (Suratul Fat-h). Amesema:
Mwenyezi Mungu amewapa radhi Waislamu walipokua wakikuahidi chini ya mti…1
Makureshi waliposikia tu kuwa Mtume (s.a.w.) anapeana ahadi na watu wake kuja kupigana nao, mara walimwachia Sayyidna Uthman, na wakapeleka watu wao wakafanye sulhu na Mtume (s.a.w.). Mkubwa wa watu hao alikuwa akiitwa Suhayl bin Amr. Suhayl alipofika kwa Mtume (s.a.w.) na akatoa shauri ya kupatana na Makureshi, Mtume (s.a.w.) alifurahi sana, ili watu wake wapate kupumzika kidogo na taabu za vita. Sulhu aliyoitengeneza Suhayl na Mtume (s.a.w.) akaridhia ni ya mambo haya 7 yajayo, na aliyeziandika shuruti hizi kwa khati yake ni Sayyidna Ali, kwani yeye alikuwa mmoja katika waandikaji barua na mikataba ya Mtume (s.a.w.). Walikuwapo Masahaba wengine nao walikuwa wakimuandikia Mtume (s.a.w.) vile vile, lakini siku ile Makureshi walitaka kwa Mtume (s.a.w.) usiandikwe mkataba huo ila kwa khati ya mmoja katika jamaa zake, na Mtume (s.a.w.) akamkhitari Sayyidna Ali. Ama nakla yake ya pili iliandikwa na mmoja katika mashujaa wakubwa wa Kiansar, Bwana Muhammad bin Maslama Al Ausy. Mashahidi waliotia sahihi zao chini ya mkataba huu ni Mabwana hawa, Abubakr Siddiq, Umar bin Al Khattab, Uthman bin Affan, Abdur Rahman bin Auf, Saad bin Abi Waqqas, Abu Ubeyda na Muhamad bin Maslama, katika upande wa Makureshi ni Mikriz bin Hafs na Huwaytib bin Abdil Uzza na wengineo.
Shuruti zilizokuwa katika mkataba huu ni:

  1. Arejee Mtume (s.a.w.) na watu wake wote safari hii, asiingie yoyote katika wao katika mji wa Makka.

  2. Waje mwakani wakae muda wa siku 3 katika nafsi ya mji wa Makka, hata siku ya 4 washike njia wende zao makwao.

  3. Watapokuja wasiingie Makka na silaha zozote ila panga tu, nazo ziwe hazikufutwa – bali ziwemo ndani ya ala zao – bila ya kutolewa hata mara moja.

  4. Wazuile kupigana muda wa miaka 10 baina ya Waislam na Makureshi, na baina ya Waitifaki (Allies) wa Waislam na Waitifaki wa Makureshi.

  5. Kabila yoyote ya Kiarabu inayo ruhusa kuwa Waitifaki wa Waislam au Waitifaki wa Makureshi bila ya kufanyiwa chuki na yoyote.

  6. Mwanamume yoyote wa Kikureshi, atakayetoroka kwao pasina amri ya jamaa zake akaja Madina kusilimu, lazima Mtume (s.a.w.) amfukuze na amtoe huko Madina. Na Mwislamu yoyote atakayeacha dini ya Kiislam, akaja Makka kufuata dini ya Kikureshi, Makureshi hawatamrejesha, bali watampokea awe wao.

  7. Hapana ruhusa kutengua hata shuruti moja katika hizi kabla miaka 10 kupita.

Mtume (s.a.w.) alizikubali shuruti zote hizi, ili wapate amani kidogo wapumue nyoyo zao, ingawa baadhi ya Masahaba walipinga sana katika kukubaliwa baadhi ya shuruti hizi. Aliyefanya ghasia kubwa zaidi ni Sayyidna Umar – katika Muhajir – na Bwana Saad bin Ubada na Bwana Usayd bin Hudhayr1 – katika Ansar –. Lakini Mtume (s.a.w.) na wengi katika Masahaba zake walizikubali shuruti zote hizi, ingawa dhahiri yake mbaya juu yao, Walizikubali vivyo hivyo kwa ajili ya kupatikana ile shuruti ya 4 na ya 5. Kwa shuruti ya 4 Waislam watatua nyoyo zao wapumzike na vita vya kila siku, muda wa miaka 10. Ama kwa shuruti ya 5 wataweza kwenda katika kabila za watu wengine walio itafiki nao na kuwafahamisha kwa salama uzuri na ukweli wa dini yao, na Waarabu wengine vile vile watakuwa wanaweza kuja Madina kufanya biashara zao, na kila wakija watachanganyika na Waislamu na watakuwa wanasikia maneno ya Mtume (s.a.w.) na aya za Quran na mazungumzo ya dini ya Waislamu, hata mwisho wake watavutika kufuata dini hiyo. Navyo ndivyo ilivyokuwa.


Jeshi kubwa kabisa alilotoka nalo Mtume (s.a.w.) kabla ya sulhu hii ni hili jeshi la Hudaybiya. Nalo lilikua na watu baina ya 1,400 na 1,500. Haikupindukia miaka miwili tangu siku hiyo ila Mtume (s.a.w.) alikwenda kuipiga Makka kwa jeshi la watu 10,000! Mtume (s.a.w.) hakwenda kuwapiga watu wa Makka ila baada ya kuwa wao Makureshi wenyewe wamevunja ile shuruti ya 4 ya mkataba. Mwenyezi Mungu ameisifu sulhu ya Hudaybia kuwa ni kushinda kukubwa kwa Waislamu. Ameitaja habari hii katika Aya ya 1 ya sura ya 48 (Suratul Fat-h)1.
Walipokua wanaandika shuruti hizi za mkataba mara walimuona Bwana Abu Jandal bin Suhayl bin Amr kawasimamia na pingu mikononi na vipande vya minyororo miguuni, amekonda kuliko mwenye ugonjwa wa kifua. Kuonekana tu, Suhayl alimwambia Mtume (s.a.w.), “Huyu ndie wa mwanzo ninayekutaka usimpokee, bali utupe wenyewe.” Mtume (s.a.w.) akamwambia Suhayl; “Lakini bado hatukuandika.” Suhayl akamwambia: “Kama humrejeshi basi hapana sulhu baina yetu na nyinyi.” Mtume (s.a.w.) akamwambia Abu Jandal; “Rejea afadhali, na Mwenyezi Mungu atafanya kheri.” Pale pale akainuka baba yake akampiga bakora za fimbo yenye miba, na Waislam wote wanaona, na Bwana Abu Jandal anasema: “Mnanirejesha kwa makafiri wakanifanye hivi na zaidi? Mnamwona kafiri huyu anavyonifanya?” Kila Muislamu alikuwa anatetemeka na anatoka machozi na anauma kidole, lakini hana la kufanya, kisu kimepata mfupa!

Baada ya kuandika mkataba huu Makureshi walirejea kwao Makka na Abu Jandal wao, na Waislamu wakakaa palepale kidogo, wakanyoa nywele zao, wakabadilisha nguo zao za kuhirimia na wakawachinja wanyama wao waliowaleta ili wachinje Makka lakini sasa waliwachinja hapo Hudaybiya. Baadae wakashika njia kurejea kwao Madina, na nyoyo zao zimetua kwa kuwa hapana vita tena.

Ama huku nyuma Makka, Sahaba mwingine aliyekua akiitwa Bwana Abu Basiir alikata naye minyororo yake kwenye mtikati wake, akatafuta ngamia akampanda mpaka Madina. Mara siku moja alipokuwa amekwishafika Madina, Masahaba kutahamaki wanamwona Bwana Abu Basiir kasimama mbele ya majlis ya Mtume (s.a.w.) anatoa salamu. Masaba wote walifurahi kumwona, lakini Mtume (s.a.w.) alikataa kumwachia kukaa Madina. Alimwambia: “Kumbuka, Abu Basiir, mkataba wetu na Makureshi. Unataka tuwe sisi ndio wenye kuvunja ahadi? Nenda zako na Mungu atakutengenezea la kheri nawe.”

Bwana Abu Basiir hakuwahi kuwaaga ila mara waliwaona wajumbe wawili walioletwa na Makureshi kwa Mtume (s.a.w.) kuja kumtaka huyo Bwana Abu Basiir, na kuwakumbusha Waislam ahadi zao walizoandikina na Makureshi. Mtume (s.a.w.) akawaambia: “Mnamwona huyu! Hatukumpa ruhusa ya kukaa na sisi hata siku moja, akapumzika machofu ya njiani. Mnamwona huyu yuwima, anapania kupanda juu ya ngamia wake. Basi huyo mtu wenu mchukueni!” Wale wajumbe wakamchukua mtu wao wakendazao naye. Kila mmoja katika wajumbe hao wawili alikuwa kapewa na Makureshi upanga mkali amwue huyo Bwana Abu Basiir pindi akiwafanyia ghasia. Bwana Abu Basiir alipotambua haya alinyenyekea vilivyo, hata ukapatikana urafiki mkubwa baina yake na hawa viongozi wake.


Siku moja walipokuwa njiani, Bwana Abu Basiir alimwambia mmoja katika wale watu wake wawili: “Hebu nipe huo upanga wako niuone ukali wake na vipi uzuri wa chuma chake.” Yule aliyeambiwa alihadaika akatwaa huu upanga akampa Bwana Abu Basiir. Naye akafuta pale pale kwenye ala yake na akampiga nao wa shingo akakifyeka kichwa. Mjumbe wa pili wa Kikureshi kuwona mwenziwe anagaragara ndani ya damu yake alipiga mbio juu ya farasi wake mpaka kwa Mtume (s.a.w.), na Bwana Abu Basiir yupo nyuma yake anamfukuzia ili amfikishe nae alipomfilisha mwenziwe.
Alipofika Madina alijitupa chini ya miguu ya Mtume (s.a.w.), anamwomba amhami na shari ya Bwana Abu Basiir; na Mtume (s.a.w.) akamhami. Baada ya kupumzika akashika njia akenda zake; huku nyuma Bwana Abu Basiir akataka kwa Mtume (s.a.w.) sasa amwache akae Madina. Lakini Mtume (s.a.w.) alikataa katakata kuvunja ahadi yake. Kwa hivyo Bwana Basiir akamwaga Mtume (s.a.w.) akamwambia: “Nakwenda zangu, lakini sitarejea Makka nikadhiliwe na Makureshi, bali nitakwenda mahali pengine ambapo nitaweza kufanya ibada yangu kwa huria kamili. Basi unasemaje, ninayo ruhusa kwenda mahali hapo, nami nisirejee Makka nikapata kudhuriwa?” Mtume (s.a.w.) akamjibu: “Yaliyo katika mkataba wetu ni kutokuachieni kukaa Madina tu, si kukulazimisheni kurejea Makka, ijapokuwa wenyewe hamtaki.”
Bwana Abu Basiir akaondoka akenda zake akakaa karibu na mitaa ya Bani Ghifar na Eani Aslam na Bani Juhayan. Baadhi ya Waislamu wa kabila hizi walimfuata, wakafanya mahali hapo ndipo mtaa wao. Waislamu wengine walikuwa wamefungwa Makka na wazee wao kusikia haya kila mmoja alijitahidi kukata enda akakae mtaa huo. Wakatoroka Waislamu wengi huko Makka wakenda kukaa mtaa huu mpya. Baada ya kujiona tu wamekwisha kuwa wengi, Masahaba walifanya mashauri ya kuipokonya mali misafara ya Kikureshi itakayopita hapo kwenye mtaa wao, Kama wao Makureshi walivyowapokonya mali yao na wakawataabisha katika Makka. Baada ya kuazimia tu shauri hii mara wakaanza kuipitisha. Haukupita msafara wowote baadaye hapo ila waliuvamia na wakayala mali yake ngawira, na wakawatawanya waliokuwa wakiuhifadhi. Mara mbili tatu walifanya hivi. Mwisho Makureshi walipoona vimno tena, walikuja wakubwa wao kwa Mtume (s.a.w.) wakamtaka wavunje shuruti ya 6 ya mkataba, ili apate kuwachukua Madina watu wote wale waliokua Makka, wakatoroka wakawa wanapokonya misafara. Mtume (s.a.w.) akakubali shauri yao, na Makureshi wakaondoka kwenda zao, wanamshukuru Mtume (s.a.w.) kwa wema wake katika kuwasaidia kuhifadhi mali yao na watu wa Mtume (s.a.w.), bali walikuwa wakiwapiga na wenye mali pia.
Baada ya hao Makureshi kuondoka, Mtume (s.a.w.) aliwapelekea barua wale Masahaba waliokuwa nje ya Madina warejee Madina, wakae kwa salama kama wenziwao wanavyokaa. Barua hii ilipofika ilimkuta yule mkubwa wao, Bwana Abu Basiir anakata roho. Wenziwe wakamsomea upesi upesi ile barua, naye alifahamu maana yake na akatii yaliyomo. Walipokwisha kuisoma aliitaka kwa wenziwe wampe aibusu. Nao wakampa. Bwana huyu akaipokea akaiweka mdomoni akaibusu, na pale pale akakata roho.
Yüklə 0,69 Mb.

Dostları ilə paylaş:
1   ...   7   8   9   10   11   12   13   14   15




Verilənlər bazası müəlliflik hüququ ilə müdafiə olunur ©muhaz.org 2024
rəhbərliyinə müraciət

gir | qeydiyyatdan keç
    Ana səhifə


yükləyin